'Nanyi kama mkiona ni vibaya kumtumikia BWANA, chagueni hivi leo mtakayemtumikia;... lakini mimi na nyumba yangu tutamtumikia BWANA'
Maneno haya yapo katika biblia na yalitamkwa na Joshua mbele ya jamii ya waisrael wakati alipoona matendo ya waisraeli yalikuwa ni kinyume na mafundisho ya Mungu.
Waisrael walifundishwa maagizo ya Mungu kwa vizazi mbalimbali, walitendewa miujiza mingi na Mungu wao, waliona faida nyingi za kuishi na kufuata maagizo ya Mungu, faida ya kuwa rafiki wa Mungu. Lakini pamoja na hayo yote waliendelea kumuasi kwa nyakati tofauti tofauti. Wakati huu Joshua hakuona haja ya kuwaeleza Waisrael juu ya ukuu wa Mungu, faida ya kuishi chini ya utawala wa Mungu, kwa namna fulani ni kama alikuwa amechoka kuwakumbusha na kuwaeleza mara kwa mara na akawa amekata tamaa. Ndipo alipowauliza na kuwaambia wana wa Israel, ''Nanyi kama mkiona ni vibaya kumtumikia BWANA, chagueni hivi leo mtakayemtumikia;... lakini mimi na nyumba yangu tutamtumikia BWANA'. Maana aliona hawezi kuendelea kuwakumbusha na kuwafundisha waisrael juu ya umuhimu na faida ya kufuata maagizo ya Mungu kwa vile walikuwa wanajua.
Watanzania tumeishi kwa umoja na upendo na maelewano bila ya kujali tofauti zetu za kidini, za kikabila au kimaeneo. Tulifundishwa juu ya faida ya kuishi kwa namna hiyo. Tukiwa mashuleni tulisoma vitabu vinavyosisitiza umoja na maelewano, tuliimba nyimbo, tukasoma shule za kuchanganishwa, tukafanya kazi kwa kuchangamana, tukahuzunika au kufurahia kwa kuchangamana licha ya kuwa na tofauti kubwa ya imani zetu za kiimani.
Hatukuishia kufundishwa tu bali tulioneshwa faida, na pia kwa upande mwingine tulioneshwa na tukaona hasara, machungu, mateso na misiba ya wenzetu walioamua kukumbatia utengano wa kidini na kikabila. Sisi daima tulikuwa mashuhuda wa faida ya kuishi kwenye jamii isiyofuata misingi ya kidini. Tukatamka kwenye katiba kuwa nchi yetu kama Taifa, haina dini bali tutaheshimu imani ya mtu mmoja mmoja, kila mtu aabudu kadiri dhamira na maamuzi yake yanavyomtuma.
Cha kushangaza ni kwamba pamoja na kuona faida za maisha ya umoja, maisha yanayosimama katika msingi wa maelewano na kuheshimu imani za watu wote, tumeamua kutaka kuonja hasara ya utengano wa kidini. Pamoja na kuona wenzetu wanavyotaabika, wanavyopoteza maisha na mali zao kwa kuendekeza utengano wa kidini lakini bado tumeng'anga'ania kutaka kuwa mashuhuda wa mateso na misiba inayotokana na udini.
Watanzania ni muhimu sana kutafakari, ili kufika hapa tulipo, tumejifikisha au tumefikishwa? Kama tumefikishwa, je tumekuwa wapumbavu wa kiasi gani, tukaacha kutumia hekima ya kukataa nasi tukawa zumbukuku tukakubali kufikishwa hapa? Haya ambayo tayari tumekwishayaona, tunaona yanatosha kutamka kuwa hatutaki kuendelea kubakia tulikofikishwa au bado tuna hamu ya kuingia zaidi chumbani tukashuhudie zaidi? Kama tumefikishwa, je tuna uwezo wa kutoka wenyewe au mpaka tutolewe? Kama tunataka kutoka wenyewe, tutatoka namna gani?
Kwa kuwa tunajua hasara ya udini na faida ya umoja na amani, hatuhitaji kukumbushwa wala kufundishwa, bali wenye hekima na utashi inabidi wasimame na kusema, 'Kama nanyi mkiona ni vibaya kuutumikia umoja na amani, tuambieni vurugu zenu zinataka nini ---- lakini sisi, hata kama serikali itaendelea kulegalega kusimamia amani, sisi daima tutasimama na kuipigania amani na umoja wa Watanzania'. Tukiyatamka haya kwa dhamira, ni dhahiri itakuwa ndiyo mwongozo wetu katika jitihada za kuuvunja udini.
Siku zote katika kutafuta suluhisho la tatizo lolote ni lazima uongozwe na nadharia, dhamira na matendo. Serikali yetu, kuhusu usimamiaji wa amani, inatekeleza zaidi kwa nadharia isiyoambatana na matendo, hasa matendo yale ambayo yanayorutubishwa na usimamizi wa haki na sheria. Nadhani hawajui kuwa nadharia ikishindwa kuendana na matendo, matendo hutengeneza nadharia.
Bart
0 Comments