Katika kipindi cha wiki nne sasa kumekuwa na maandamamo, malumbano na
vurugu kuhusu mradi wa kujenga bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka
Mtwara hadi Dar es Salaam. Mradi huu wa kutandaza bomba la urefu wa
kilometa 542 ni mkubwa sana hapa nchini, na una thamani kubwa zaidi
kuliko miradi mingine yote ya miundombinu iliyopata kutokea hapa
nchini. Mradi huu utajengwa kwa mkopo wa dola za Kimarekani 1.2
bilioni kutoka Benki ya Exim ya China.
Wananchi wa Mtwara kupitia maandamano ya tarehe 27 Desemba 2012
wametaka kujua hatma ya maendeleo ya mikoa wa kusini kutokana na mradi
huu wa bomba la gesi. Serikali imewajibu wananchi hawa kwa kuwaita
wahaini, watu hatari na wasio elewa. Imefika mahali inapotosha madai
yao kwamba hawataki gesi itoke Mtwara.
Kimsingi Serikali haijajibu hoja yeyote ya msingi ya wananchi wa
Mtwara kuhusu mradi wa kusafirisha gesi. Badala yake imekuwa ikijaribu
kupotosha madai ya watu wa Mtwara kupitia mikutano na vyombo vya
habari.
Tangu maandamano haya yatokee, na baadaye mikutano ya hadhara
nahatimaye matukio ya kusikitisha ya kuharibu mali za watu, mauaji ya
watu na majeruhi mbalimbli, Serikali na hasa Wizara yenye dhamana ya
mradi huu, imekuwa ikitoa matamko kwenye vyombo vya habari badala ya
kwenda Mtwara kuzungumza na wananchi, kusikiliza madai yao na kuona
namna ya kutekeleza madai hayo. Kutokana na Serikali kutofanya hivyo,
kusikiliza na kuzungumza na wananchi wa Mtwara, vurugu mbaya sana
zimeendelea mkoani humo.
Mwezi uliopita, Desemba 2012, tatizo lilionekana kuwa ndogo na lenye
kuhusiana zaidi na ukosefu wa kushirikishwa kwa wananchi. Badala ya
kushughulikia tatizo likiwa bado ndogo, Serikali imeona njia pekee ya
kushughulikia suala hili ni kutafuta mchawi na kwa wiki zote hizi
imekuwa ikisemakuwa wanasiasa na makampuni ya uwekezaji ya nje
yanachochea mgogoro huu.
Leo hali iliyopo mkoani Mtwara inasikitisha sana, maana mali za
wananchi zinaharibiwa, nyumba zinachomwa moto na watu wanapoteza
maisha. Tunalaani matukio haya kwa nguvu zetu zote, maana kinachotokea
Mtwara si Utanzania. Tusipowasikiliza wananchi na kutatua mgogoro huu
kwa kuwashirikisha, hali itazidi kuzorota wakati tukitupiana lawama.
Hivi sasa serikali imeona njia pekee ya kushughulikia suala hili ni
kutafuta mchawi na kwa wiki zote hizi imekuwa ikisema kuwa wanasiasa
na makampuni ya uwekezaji ya nje yanachochea mgogoro huu.
Kwanza, Serikali imekuwa ikiaminisha umma kwanza suala hili
limechukuliwa kisiasa. Pili, Serikali imekuwa ikirudia kusema kuwa
baadhi ya makampuni ya uwekezaji nchini na mataifa ya Magharibi
yamekuwa yakichochea wananchi wa Mtwara.
Katika mwendelezo wa mtindo wa Serikali wa 'management by press
conferences' jana Jumamosi Naibu Waziri wa Nishati na Madini ndugu
George Simbachawene aliwaambia wahariri kwamba mimi Zitto Kabwe
ninachochea wananchi wa Mtwara, ninatumiwa, na si mzalendo. Vile vile
alitoa vielelezo kadhaa kuonyesha kuwa mradi wa kujenga bomba la gesi
ni gharama sawasawa. Akasisitiza kwamba mimi ni mwongo.
Katika kipindi chote cha mgogoro wa Gesi Mtwara, sijafika Mtwara.
Sijafanya mkutano wowote na waandishi zaidi ya kuandika mawazo yangu,
kama Mtanzania kuhusu suala hili. Nimeandika makala nne na
zimechapishwa katika magazeti kadhaa hapa nchini na kwenye blogu yangu
(www.zittokabwe.com).
Niliandika: Utajiri wa Gesi Asilia: Tuwasikilize Watanzania wa Mtwara
na Lindi. Nikaandika tena: Tusipuuze mandamano dhidi ya Bomba la Gesi:
Kilio cha Uwajibikaji; Nikaandika tena: Mtwara : Serikali inavunja
nchi kwa kutosikiliza Wananchi; ni baadhi ya makala nilizoandika
kuhusiana na suala la Mtwara.
Sitaki kubishana na Naibu Waziri ama Kiongozi yeyote ya Serikali kwa
sasa. Hatuwezi kuendelea kulumbana, kuzozana, kuzodoana na kurushiana
maneno wakati nchi yetu inaungua. Huu sio wakati wa kutafuta mchawi
bali kutafuta majawabu ya changamoto zilizopo mbele yetu.
Yanayotokea Mtwara ni fundisho kwetu kwa Taifa namna ya kukabili
changamoto za utajiri wa rasilimali, ili kuweka mkakati, mambo haya
yanayotokea Mtwara yasitokee tena Tanzania. Tutaweza kuzuia maafa haya
iwapo tutaweka uwazi katika mikataba, tutashirikisha wananchi kwenye
unyonyaji wa maliasili za nchi, na iwapo tutaweka uwajibikaji.
Rais Kikwete Kikwete ana majibu; ayatoe sasa kwa wana Mtwara
Kwa mujibu wa Mpango Kabambe wa Umeme nchini (Power System Master
Plan), kulikuwa na mradi wa kufua umeme MnaziBay, ambao Rais Jakaya
Kikwete aliagiza utekelezwe mara moja. Serikali ieleze umma kuhusu
mradi huo wa kujenga kituo cha kufua umeme 300MW MnaziBay Mtwara na
kujenga msongo wa umeme wa 300KV mpaka Singida. Umeishia wapi?
Ikumbukwe kuwa mnamo tarehe 12 Oktoba 2012, Rais Jakaya Kikwete
alipokea ripoti ya ujenzi wa mradi huu kutoka makampuni ya China
National Machinery & Equipment Import & Export Corporation (CMEC) ya
China na Siemens ya Ujerumani, ambayo kwa pamoja yalitarajia kujenga
kituo kikubwa cha kuzalisha umeme kutokana na gesi katika eneo la
Mnazi Bay, mjini Mtwara na pia kujenga njia ya kusafirisha umeme ya
kilomita 1,100 kutoka Mtwara hadi Singida. Mradi huu ungegarimu dola
za kimarekani milioni 684 na Rais aliagiza utekelezwe haraka sana. Huu
mradi uliishia wapi? Kwa nini Serikali ipo kimya kuhusu mradi huu
ambao ungejibu kabisa maswali ya watu wa Mtwara? Taarifa ya Ikulu
kuhusu mradi huu imeambatanishwa hapa.
Tufanyeje?
Hapa tulipofikia ni lazima kwanza kabisa kusikia kilio cha wananchi wa
Mtwara ikiwemo kuelewa madai yao. Swali kubwa kubwa la watu wa Mtwara
na Kusini kwa ujumla ni 'tunanufaikaje'? Jibu la swali hili si ahadi
za miradi bali ni vitendo. Hapa ndipo serikali inaposhindwa
kushughulikia suala hili, kutoelewa madai ya wananchi na
kuyapotosha.Viongozi wa kisiasa wenye ushawishi kutoka pande zote,
chama tawala na vyama vya upinzani, waende Mtwara kuzungumza na
wananchi, lakini wawasikilize kwanza.
Lazima viongozi tujenge utamaduni wa kusikiliza wananchi na si
kuwahutubia tu. Wananchi wa Mtwara wana madai ambayo lazima viongozi
tukae kitako kuwasikiliza kisha kufanya nao majadiliano ambayo yatatoa
mwafaka. Rais mstaafu, Ndugu Benjamin Mkapa ameshatoa kauli kuhusu
suala hili. Ni wakati mwafaka sasa kwa viogozi wengine kumuunga mkono
kwa kwenda Mtwara na kukaa na wananchi wa Wilaya zote za Mtwara,
kusikiliza hoja zao na kuona namna ya kupata ufumbuzi wa suala hili.
Wakati hatua hii inachukuliwa, wananchi waombwe kutulia na kuacha
vurugu za aina yeyote ile, na Serikali isimamishe mradi mpaka hapo
suluhu na wananchi itakapopatikana.
Wakati juhudi hizo zinaendelea Serikali iweke wazi mkataba wa ujenzi
wa bomba, kwani ni dhahiri gharama za mradi huu ni kubwa mno kulingana
na uhalisia wa miradi ya namna hii duniani kote. Katika taarifa zote
kwa umma Serikali imekuwa ikisema kwamba mradi utagharimu jumla ya
dola za kimarekani 1.2 bilioni, lakini katika taarifa ambayo Wizara ya
Nishati na Madini imesambaza jana kwa wahariri wa vyombo vya habari
nchini imesema mradi utagharimu dola za kimarekani milioni 875. Usiri
katika mkataba huu unaashiria kwamba Serikali inaficha kitu. Hivyo
njia pekee ni kutaka mkataba uwe wazi kwa wananchi.
Wakati tunawataka wananchi wa Mtwara kuruhusu utulivu, ni vema
Serikali ijiandae kutoa majawabu ya madai ya wananchi hao. Majawabu ya
Serikali yajikite kueleza wananchi wa Mtwara wanafaidikaje na
rasilimali ya gesi asilia kwa maendeleo yao. Wananchi wa Mtwara
wanataka uwajibikaji wa Serikali kwenye utajiri wa nchi, na wamechoka
na porojo za orodha ya miradi isiyotekelezwa.
Viongozi twendeni Mtwara kusikiliza wananchi wetu. Nchi inaungua na
hatuwezi kuendelea kuzozana badala ya kuzima moto huu hatari kama vita
vya MajiMaji. Mimi nakwenda Mtwara haraka na mara baada ya viongozi
wangu wa chama kutoa ridhaa.
ZITTO KABWE
Mbunge, Kigoma Kaskazini (CHADEMA)
Waziri Kivuli wa Fedha
Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni
Source: http://www.wavuti.com/#ixzz2JBJAA2Zq
--
Jobs in Africa - www.wejobs.blogspot.com
International Jobs - www.jobsunited.blogspot.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
0 Comments