[wanabidii] TAMKO LA JUKWAA LA WAKRISTO TANZANIA KUHUSU AMANI NCHINI

Thursday, December 27, 2012
TANZANIA CHRISTIAN FORUM (TCF)
MKUTANO MKUU WA NNE WA JUKWAA LA WAKRISTO TANZANIA (TCF)

TAMKO RASMI 

"ATUKUZWE MUNGU JUU MBINGUNI, NA DUNIANI IWE AMANI KWA WATU ALIOWARIDHIA"

Utangulizi
Katika Mkutano Mkuu wa Nne wa Jukwaa la Wakristo Tanzania, Tanzania Christian Forum – TCF, uliofanyika katika Kituo cha Mikutano na Mafunzo cha Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Kurasini jijini Dar es Salaam, tarehe 6 Desemba, 2012; Wajumbe walitafakari kwa undani juu ya kuzorota kwa mahusiano baina ya Dini mbili za Ukristo na Uislamu nchini Tanzania, pamoja na kutathmini juu ya wajibu wa Kanisa na Utume wake wa Kinabii kwa taifa letu.

Jukwaa la Wakristo Tanzania (TCF) linajumuisha taasisi kuu za Umoja wa Makanisa nchini kama ifuatavyo;-
Jumuiya ya Kikristo Tanzania - CCT
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania - TEC
Jumuiya ya Makanisa ya Kipentekoste Tanzania - PCT
Kanisa la Waadventisti Wasabato – SDA (observers)

Tafakari
Tafakari yetu ilianza kwa kujiuliza yafuatayo:
1. Ni mwenendo gani uliotusibu hivi karibuni kusababisha kukutana kwetu hapa?
Vikundi vya kihalifu vikiongozwa chini ya mwavuli wa waamini wa Kiislamu vimekuwa vikishambulia kwa ukali na kikatili sana imani, mali, majengo na makanisa ya Wakristo kwa jeuri na kujiamini.

2. Kwa mwenendo huo ni kitu gani kilicho hatarini?

Vitendo na mienendo yote ya namna hiyo inahujumu sana Amani, Mapatano na Uelewano kati ya watu wote nchini mwetu. Tunaelewa kwamba ni waamini wachache tu wenye kutenda maovu hayo, lakini mienendo ya kikatili ya namna hii huchochea shari miongoni mwa walengwa wa ukatili husika na kutaka kulipiza kisasi hata kusababisha uvunjifu wa amani.3. Ni athari gani kwa nchi, katika muda ujao, iwapo mienendo hiyo haitadhibitiwa na kukomeshwa kabisa?

Katika nyakati zetu hizi, tunashuhudia fadhaa na migogoro mingi ya kijamii. Kuna hasira kubwa ya chinichini inayotokana na kasoro nyingi za kiutendaji katika mihimili mikuu ya uongozi na utando mkubwa wa ufukara wa kutupwa kwa wananchi wengi usio na matumaini ya kumalizika hivi karibuni. Hatari ya hali hii ni dhahiri kwamba makundi nyemelezi (kisiasa, kiuchumi na kidini), kwa kutumia vikundi halifu vilivyo katika hali ya ufukara na migogoro, yatavielekeza kimapambano na kiharakati kutetea kijeuri ajenda hasimu za wale walio madarakani au washindani wao kwa maslahi ya wanyemelezi. Hali tunayoelezea sio ya kufikirika kwani ndiyo inayotokea huko nchini Nigeria, Kenya na nchi za Afrika ya Kaskazini hivi sasa. Tanzania haina kinga ya kipekee kuiepusha kukumbwa na maovu ya namna hiyo bila utaratibu na vyombo thabiti kuhimili mienendo hasi kama hii. Kutokana na matukio na kauli zinazotolewa na watu mbalimbali hapa nchini, inawezekana tayari wanyemelezi wako kazini wakiongoza vikundi kusukuma ajenda za kutekeleza maslahi yao.4. Masuala yanayotakiwa kufafanuliwa na kudhibitiwa na Dola mapema ili yasiendelee kupotoshwa:

  • Hali ya mahusiano kuzorota pamoja na kashfa dhidi ya Kanisa.

Huu ni wakati wa kukubali kwamba misingi ya Haki, Amani na Upendo katika Taifa letu imetikiswa kwa kiwango kikubwa. Uchochezi, kashfa, matusi na uchokozi wa wazi na makusudi unaofanywa na baadhi ya waamini wa dini ya Kiislamu, ukiendeshwa na kuenezwa kupitia vyombo vyao vya habari vya kidini (redio na magazeti) mihadhara, kanda za video, CD, DVD, vipeperushi, makongamano, machapisho mbalimbali na kauli za wazi za viongozi wa siasa na hata viongozi wa dini husika (ushahidi wa mambo yote haya tunao) pasipo Serikali kuchukua hatua yeyote huku bali imekuwa ikibakia kimya tu. Ukimya huu unatoa taswira ya Serikali kuunga mkono chokochoko hizi. Jambo hili linavyoendelea kuachwa hivi hivi linaashiria hatari kubwa ya kimahusiano siku zijazo.
  • Hadhi ya Baba wa Taifa kuhifadhiwa.

Huyu ni kiongozi aliyetoa maisha yake kwa ajili ya ustawi wa nchi yetu akitetea Watanzania wote bila ubaguzi wowote, akiimarisha umoja wa Kitaifa, amani na upendo kwa watu wote. Kashfa, kejeli na habari za uongo dhidi yake ni kukipotosha kizazi hiki na hata vizazi vijavyo kwa kuondoa moja ya alama muhimu ambazo kiongozi huyo alisimamia kwa ajili ya umoja wa kitaifa.
  • "Memorandum of Understanding" (M.o.U) ya mwaka 1992, kwa ajili ya huduma za kijamii zitolewazo na Makanisa kwa Watanzania wote, ikiwa ni pamoja na huduma za hospitali, vituo vya afya na zahanati na shule mbalimbali zinazoendeshwa na Makanisa nchini kote. Ni vema ikaeleweka wazi kwamba makubaliano hayo (M.o.U) yalikuwa ni kati ya Makanisa ya Tanzania na Makanisa ya nchini Ujerumani ambapo Serikali ya Tanzania ilihusishwa tu, kwa vile raia wake ndio wangenufaika na misaada hiyo ambayo nchi ya Ujerumani ingeitoa kupitia Makanisa hayo. Kanisa limeendelea kujishughulisha na huduma hizi kwa jamii hata kabla ya uhuru na baada ya uhuru pasipo ubaguzi. Ikibidi ni vema kuondoa hali hii, ya Kanisa kuendelea kutukanwa, chuki na kukashifiwa viongozi wake kutokana na huduma hizi kwa jamii yote. Jukwaa la Wakristo Tanzania tunaitaka Serikali itoe tamko la ufafanuzi juu ya M.o.U hiyo, maana yake, makusudi yake na manufaa yake kwa Watanzania wote.


  • Hujuma ya kuchomwa Makanisa na mali za Kanisa, ni tukio la uvamizi na uchokozi wa wazi, ulioyakuta makanisa yetu na waamini wake wakiwa hawana habari na bila maandalizi yoyote. Ni muhimu kuanzia sasa, Wakristo wote wakae macho na wawe waangalifu zaidi.


  • Dhana ya kuwa Tanzania inaendeshwa kwa mfumo Kristo ni potofu na potevu.

Maneno hayo ni ushahidi wa uwepo wa ajenda za waamini wenye imani kali na waliojiandaa kwa mapambano maovu kutetea dhana potovu kinzani na misingi ya demokrasia na haki za binadamu kama ilivyotangazwa na Umoja wa Mataifa na kuridhiwa na Serikali yetu. Jukwaa la Wakristo nchini tunakanusha wazi wazi na kueleza bayana kuwa, nchi hii haiongozwi kwa mfumo Kristo!. Kwa watu walio makini hakuna kificho kuwa viongozi wote waandamizi wa ngazi ya juu Serikalini awamu ya sasa, asilimia 90 ni Waislamu (Rais wa Nchi na Amiri Jeshi Mkuu, Makamu wa Rais, Mkuu wa Usalama wa Taifa, Jaji Mkuu, Mkuu wa Jeshi la Polisi). Kwa mantiki hiyo haiingii akilini kueleza watu kuwa nchi hii inaendeshwa kwa mfumo Kristo! Kwa upande wa Zanzibar asilimia 100 ya viongozi ngazi za juu Serikalini ni Waislamu, na sio kweli kwamba Zanzibar hakuna Wakristo wenye sifa za kuongoza. Kisha, hata uwakilishi wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, theluthi mbili ya wajumbe wake ni Waislamu. Tunayo mifano mingine mingi iliyo wazi, na hii ni baadhi tu. Watanzania wanapaswa kuelewa wazi kuwa, nchi hii inaongozwa kwa misingi ya Utawala wa Kisheria na sio vinginevyo.
  • Matumizi hasi ya Vyombo vya Habari vya Kidini:

Vyombo vya habari vya kidini vinatumiwa na viongozi wa dini ya Kiislam kuukashifu Ukristo na kuwachochea Waislamu hadharani kupitia vyombo hivyo wakiwataka wawaue Maaskofu na Wachungaji, iwe kwa siri au hadharani. Japo Serikali imesikia kashfa na uchochezi huo hatarishi, imendelea kukaa kimya, na kuwaacha wachochezi hao wakiendelea kuhatarisha amani bila kuwadhibiti. Jambo hili linatia mashaka makubwa juu ya umakini wa Dola kuhusu usalama wa wananchi nchini mwao. Imani kali za namna hii huchochea vitendo viovu vya uasi na hujuma sio tu dhidi ya waamini na viongozi wa dini fulani, bali hata na kwa Serikali na viongozi waliopo madarakani, endapo waamini wa dini fulani katika taifa kama Tanzania lililo na waamini wa dini nyingi tofauti, hawataheshimu na kutendeana kiungwana baina yao na wale wasio wa dini na mapokeo yao. Hali hii inapelekea kujiuliza kama je,huu ni wakati mwafaka kwa kila raia au kiongozi wa dini kujilinda yeye mwenyewe na waamini wake dhidi ya wenye imani kali?
  • Matukio yanayosababisha hasira na kutenda maovu:

Tumejionea matukio kadhaa ambayo kwayo vikundi vya watu wenye hasira vilisababisha hujuma na uharibifu mkubwa wa mali za watu wengine. Hivyo ni viashiria tosha vya uchovu na unyonge mkubwa katika jamii yetu, ambamo jambo dogo tu na hata la kupuuzwa, likitendwa na afikiriwaye kuwa hasimu wa watu fulani, wahalifu hujipatia fursa ya kuonesha hasira yao kwa vitendo vya hujuma na shari, wakiharibu hata kuteketeza mali na nyenzo za maisha ya jamii. Suala hili lataka uchambuzi yakinifu na wa kiroho ili kupata majibu na maelezo sahihi na wala sio kwa kutumia nguvu za ziada za kijeshi au kwa majibu mepesi ya kisiasa. Hili ni suala lihusulo tunu na maadili ya jamii yote ya Watanzania katika ujumla wao. Kila mmoja wetu ni mhusika na sote tukitakiwa kuwajibikiana katika ujenzi wa amani iletayo mapatano na uelewano kati yetu.

Mapendekezo:
Kutokana na muono wetu huo tunapendekeza yafuatayo:

  • Tabia na mienendo ya kukashifiana ikomeshwe kabisa na badala yake tujengeane heshima/staha tukizingatia utu wa kila mmoja katika utofauti wetu.
  • Tumwendee Mungu wetu na kumwomba atuongoze sote kufuata utashi wake tukitafuta huruma yake iliyo sheheni upendo wake mkuu, ili atujalie umoja wa kuishi pamoja kwa amani nchini mwetu.
  • Tunaitaka Serikali yetu na vyombo vyake vya usalama, sheria na amani kutenda mara moja na bila kuchelewa, katika nyakati ambazo vikundi halifu kisiasa au kidini vinapoanza uchochezi ili kupambanisha wanajamii. Tabia ya kuachia uchochezi wa kidini kuendelea pasipo hatua mathubuti kuchukuliwa na Dola ni udhaifu mkubwa wa uongozi na uwajibikaji. Ikithibitika kwamba uharibifu uliofanywa ulitokana na kikundi mahususi chini ya uongozi wa dini au chama cha kisiasa au asasi isiyo ya kiserikali, basi taasisi husika iwajibishwe na kulipa fidia kwa uharibifu uliofanywa.
  • Lianzishwe Baraza mahsusi lililo huru lisiloegemea chama chochote cha kisiasa wala dini yoyote na litamkwe na kuwezeshwa kikatiba likiwa na dhumuni kuu la kuilinda na kuiongoza Serikali kuto fungamana na dini yoyote na kuhakikisha kwamba dira na dhana ya utu katika mfumo wa uchumi wenye kujali maslahi ya wote havipotoshwi. Baraza hilo liwe na uwezo wa kuvichunguza vyombo vya sheria na usalama itokeapo matatizo makubwa yaashiriayo uvunjifu wa haki na kuteteresha usalama wa nchi.
  • Na sisi viongozi wa dini za Kikristo, Kiislam, Kihindu na nyinginezo tuwajibike katika kufundisha, na katika majiundo ya waamini wetu, hasa vijana, ili kuwajengea uelewa na utashi wa kuvumiliana kwa upendo. Katika kushuhudia na kuadhimisha imani na ibada zetu sote tutambue , tulinde na kukuza maadili, tunu na desturi za imani za watu wengine wanazo ziheshimu na kuzitukuza. Vikundi vya imani kali na pambanishi kwa kutumia kashfa potoshaji sharti vidhibitiwe kwa weledi mkubwa wa viongozi wa dini husika wakisaidiana na usalama wa taifa. Stahamala [kustahimiliana] ni fadhila inayopaswa kufundishwa na kupenyezwa katika mifumo ya uongozi na maisha ya jamii na ihifadhiwe kwa kufuatiliwa kwa karibu sana.


Hitimisho: 
Kwa sasa Kanisa liko katika vita vya Kiroho, hivyo ni vyema Waamini wote wakakumbuka kuwa, katika mapambano kama hayo Mungu mwenyewe, Mwenye enzi yote ndiye mlinzi wa watu wake na Kanisa lake.
JIBU LITAPATIKANA TU, KWA NJIA YA SALA, KUFUNGA NA MAOMBI!
Hivyo siku ya Jumanne tarehe 25 Desemba 2012, inatangazwa rasmi nchini kote kuwa siku ya sala na maombi kwa Wakristo wote na Makanisa yote nchini, pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuomba kwa imani, amani katika nchi yetu, na kumkabidhi Mungu ashughulikie mipango yoyote iliyopo, ya wazi na ya kisirisiri ya kutaka kuondoa amani ya taifa hili na kuyashambulia Makanisa nchini Tanzania ishindwe na kuanguka pamoja na wale wote walio nyuma ya mipango hiyo.

1. Askofu Bruno Ngonyani (TEC) - Mwenyekiti
2. Askofu Dkt. Israel Mwakyolile (CCT) - Mjumbe (Mwenyekiti Mwenza)
3. Askofu Daniel Aweti (PCT) - Mjumbe (Mwenyekiti Mwenza)
4. Askofu Oscar Mnung'a (CCT) - Mjumbe
5. Askofu Elisa Buberwa (CCT) - Mjumbe
6. Askofu Stephen Mang'ana 
(CCT) - Mjumbe
7. Askofu Dkt. Peter Kitula 
(CCT) - Mjumbe
8. Askofu Alinikisa Felick Cheyo 
(CCT) - Mjumbe
9. Askofu Christopher Ndege 
(CCT) - Mjumbe
10. Askofu Michael Hafidh 
(CCT) - Mjumbe
11. Askofu Charles Salala 
(CCT) - Mjumbe
12. Askofu Dismus Mofulu 
(CCT) - Mjumbe
13. Mchg. Conrad Nguvumali 
(CCT) - Mjumbe
14. Mchg. Ernest Sumisumi 
(CCT) - Mjumbe
15. Mchg. William Kopwe 
(CCT) - Mjumbe
16. Askofu Thaddaeus Ruwa'ichi (TEC) - Mjumbe
17. Askofu Paul Ruzoka 
(TEC) - Mjumbe
18. Askofu Norbert Mtega 
(TEC) - Mjumbe
19. Askofu Severine Niwemugizi 
(TEC) - Mjumbe
20. Askofu Michael Msonganzila 
(TEC) - Mjumbe
21. Askofu Castorl Msemwa 
(TEC) - Mjumbe
22. Askofu Eusebius Nzigilwa 
(TEC) - Mjumbe
23. Askofu Renatus Nkwande 
(TEC) - Mjumbe
24. Askofu Bruno Ngonyani 
(TEC) - Mjumbe
25. Fr. Antony Makunde 
(TEC) - Mjumbe
26. Fr. Sieggried Rusimbya 
(TEC) - Mjumbe
27. Fr. Ubaldus Kidavuri 
(TEC) - Mjumbe
28. Askofu Dkt. Paul Shemsanga (PCT) - Mjumbe
29. Askofu Ability Samas Emmanuel 
(PCT) - Mjumbe
30. Askofu Nkumbu Nazareth Mwalyego 
(PCT) - Mjumbe
31. Askofu Batholomew Sheggah 
(PCT) - Mjumbe
32. Askofu Dkt. Mgullu Kilimba 
(PCT) - Mjumbe
33. Askofu Renatus Tondogosso 
(PCT) - Mjumbe
34. Askofu Emmanuel Mhina 
(PCT) - Mjumbe
35. Askofu O.S. Sissy 
(PCT) - Mjumbe
36. Askofu Jackson Kabuga 
(PCT) - Mjumbe

--
Jobs in Africa - www.wejobs.blogspot.com
nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com
 
DELL LATITUDE D 620 & D30
 
80 GB HardDisk ,CORE 2 DUO , 2.0 GHZ CPU ,1 GB RAM
DVD/CD - RW ,WINDOWS 7 /WINDOWS XP ,WIRELESS , BLUE TOOTH .
 
TSHS : 380,000 , 1 YEAR WARRANTY
 
CALL : 0786 806028
Free Delivery in Dar es salaam
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
 
 

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments