[wanabidii] Ukusanyaji wa Maoni Awamu ya Nne Unaendelea

Thursday, November 15, 2012
Tume ya Mabadiliko ya Katiba inatarajia kuendelea na awamu ya nne na
ya mwisho ya mikutano yake na wananchi wa mikoa sita kuanzia siku ya
Jumatatu, Novemba 19, 2012 hadi Jumatatu, Desema 19, 2012 kwa lengo la
kukusanya maoni yao kuhusu Katiba Mpya.

Mikoa hiyo ni Dar es Salaam, Arusha, Simiyu, Geita, Mara na Mjini
Magharibi na kila siku kutafanyika mikutano miwili, wa kwanza utaanza
saa 3:00 asubuhi – saa 6:00 mchana na kufuatia na mwingine utakaoanza
saa 8:00 alasiri – saa 11:00 jioni.

Taratibu zote za kuanza kazi ya kukusanya maoni katika mikoa
iliyotajwa zimekamilika zikiwemo kuandaa ratiba na kuisambaza katika
ofisi za mikoa, wilaya na Halmashauri za Manispaa na Wilaya husika.
Wajumbe wa Tume na watumishi wa Sekretarieti wamejigawa katika makundi
saba. Kila mkoa utakuwa na kundi moja isipokuwa Dar es Salaam ambao
utakuwa na makundi mawili.

Katika mkoa wa Dar es Salaam Tume imejigawa katika makundi mawili na
siku hiyo ya Jumatatu itaanza na Wilaya za Temeke na Ilala. Katika
wilaya ya Temeke, Tume itaanza na eneo la Keko wakati katika wilaya ya
Ilala itaanza na eneo la Jangwani kwa mikutano itakayoanza saa 3:00
asubuhi. Kwa mikutano ya alasiri, wilayani Temeke mkutano huo
utafanyika Chang'ombe na ule wa Ilala utafanyika Tabata.

Kwa upande wa mkoa wa Arusha, Tume itaanza na Wilaya ya Karatu eneo la
Mbulumbulu wakati mkoani Mara Tume itaanza katika Wilaya ya Tarime
eneo la Bumera. Kwa mkoa wa Simiyu, Tume itaanza na Wilaya ya Busega
eneo la Lamadi na mkoani Geita, Tume itaanza na Wilaya ya Chato eneo
la Kachwamba. Kwa mkoa wa Mjini Magharibi, Tume itaanza katika Wilaya
ya Magharibi.

Tume inawaomba wananchi kuhudhuria mikutano itakayoitishwa na Tume na
kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni yao kwa kuzungumza na pale
wanapokosa nafasi ya kuzungumza, watumie fursa ya kuwasilisha maoni
yao kwa maandishi kwa kutumia fomu maalum zitakazokuwa zinatolewa na
Tume katika mikutano hiyo.

Pamoja na kuwasilisha maoni kupitia mikutano itakayoitishwa na Tume,
wananchi pia wanaweza kuwasilisha maoni yao kupitia tovuti ya Tume
(www.katiba.go.tz) au kwa njia ya posta kupitia anuani za zifuatazo:

Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
Makao Makuu,
Mtaa wa Ohio,
S.L.P. 1681,
DAR ES SALAAM,
Simu: +255 22 2133425,
Nukushi: +255 22 2133442;

Au

Jengo la Ofisi ya Mfuko wa Barabara, Mtaa wa Kikwajuni Gofu, S.L.P.
2775, Zanzibar, Simu: +255 224 2230768, Nukushi: +255 224 2230769

Tume inawaomba wananchi kuhudhuria mikutano itakayoitishwa na Tume na
kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni yao kwa uwazi, uhuru na
utulivu.
Mwisho.

Imetolewa na:

Assaa Rashid,
Katibu,
Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
S.L.P. 1681,
DAR ES SALAAM
+255 (0) 0757 500 800 / 0717 084 252

--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.

Share this :

Related Posts

0 Comments