[wanabidii] Uhalifu unapopewa taswira ya udini!

Wednesday, October 17, 2012

Uhalifu unapopewa taswira ya udini!

Na Mashaka Mgeta

Mimi ni mmoja wa wanaoamini kuwepo dhana potofu ya kushamiri kwa udini, inayoenezwa miongoni mwa Watanzania.

Wapo wanaojinasibu kwa imani zao, wapo watu wanaolalamikia kuporwa haki kwa sababu ya imani zao, wapo watu wanaowalaghai wengine kwa kutumia misingi ya imani ili kutimiza matakwa binafsi.

Dini, imani, mapokeo na mafundisho yake ni mambo yanayohitaji umakini katika kuyajadili, kwa maana yanaweza kuibua tofauti kubwa ama kuziimarisha jumuiya za watu ndani ya taifa lenye serikali isiyotokana na dini kama Tanzania.

Ni ukweli ulio wazi kwamba kunahitajika nguvu kubwa yenye 'sura' ya maajabu kuitumbukiza Tanzania katika mgogoro wa kidini. Kwamba viongozi na waumini wa dini tofauti, watasimama maeneo tofauti, wakitoleana maneno tofauti ili kufanyiana vitendo tofauti, vikilenga kuuathiri upande mwingine.

Ninasema hivyo kwa sababu, asili na muundo wa familia na jumuiya za watu nchini, vimejikita nje ya imani za kidini, ingawa watu wake wanabaki kuwa katika imani wanazoziishi.

Vimejikita nje ya imani za dini kwa sababu, imani ya dini haipewi kipaumbale na mkazo katika kufikia tukio la kijamii, kama kuoa, kuolewa, kujenga urafiki, kutembeleana, kushiriki hafla nakadhalika.

Ndio maana, kwa mfano binti ama kijana wa kiume kutoka familia ya baba na wazee 'waliokubuhu' katika imani ya kikristu, hazuiwi kumuoa ama kuolewa na mwenye kuuishi uislamu.

Watu wa jinsi hiyo wapo wengi katika hesabu yao, wakifunga ndoa kwenye nyumba za ibada ama ofisi za serikali, wakaishi na kutengeneza familia mpya.

Katikati ya hali hiyo, si rahisi kukuta upande wenye kufuata na kuiishi imani fulani, inajenga chuki dhidi ya wale wanaoifuata na kuiishi imani nyingine, kwa maana wote wametokana na 'damu moja'.

Ndivyo inavyoenea kwa upande wanaojenga na kuendeleza urafiki, ujirani, maeneo ya kazi na kwingineko. Dini, imani, mapokeo na mafundisho havipo kwenye orodha ya hitaji kuu la kufikia muunganiko wa kimahusiano, isipokuwa Utanzania na ubinadamu katika ujumla wake.

Kama vile haitoshi, mamlaka za utawala wa nchi, taasisi za kijamii vikiwemo vyama vya siasa, zimekuwa na uongozi usiotokana na misingi ta dini, bali uwezo wa kila mmoja kwa nafasi yake.

Hata pale sehemu ya taasisi hizo zimejikita katika misingi ya kidini, kama mabaraza ya maaskofu, maimamu, masheikh na wengineo, bado wanakutanishwa na chombo kimoja kama ilivyo Kamati ya Amani ya Viongozi mkoani Dar es Salaam.

Kama hali ipo hivyo, tujiulize, kwa nini vurugu zenye sura ya udini zinaibuka na kuathiri mali za wanaoiishi imani nyingine kama ilivyotokea Mbagala jijini Dar es Salaam?

Baada ya Mbagala, mkoani Kigoma pia kumeripotiwa kuwepo tukio la kuchomwa moto kanisa moja! Je, ni udini unaibuka nchini?

Kwa mtazamo wangu, waumini wa dini tofauti hapa nchini wana upeo mpana wa kutambua misingi, mafundisho na mapokeo ya dini zao, ndio maana 'miunganiko' niliyoiainisha hapo awali, ipo na itaendelea kuwepo.

Kwangu binafasi, sitaki kuamini kwamba wakristu wanaoijua misingi, mafundisho na imani yao, wanaweza kuwa sababu ya machafuko hasa pale wasioyaamini hayo wanayoyaishi, watenda kinyume chake.

Hivyo hivyo sitaki kuamini kirahisi kwamba waumini wa kiislamu 'walioiva' katika misingi, imani, mafundisho na mapokeo ya dini yao, wanaweza kufanya kwa kadri nilivyoeleza hapo juu.

Imani kubwa niliyo nayo, ni kwamba makundi hayo, na kutokana na asili yake, yataweka mbele uvumilivu na kuelimishana, hali inayoweza kuwavutia hata wale wasioiamini imani yao, wakaielewa na kuiheshimu zaidi kama si kuifuata na kuiishi.

Hivyo matukio ya vurugu zilizosababisha kuchomwa moto kwa nyumba za ibada na misa takatifu, sitaki kukubali kirahisi kwamba yanatokana na migogoro ya kidini. Itoke wapi? Kwa nani?

Kama jawabu litakuwa sahihi katika hilo, uhalifu uliofanyika na unaweza kufanyika lazima utafsiriwa kwa uhalisi wake, kwamba upo katika sura ya uhalifu wa aina nyingine unaofanyika nchini.

Haiwezekani kukatokea kikundi cha watu wachache, wenye ushawishi unaolenga kufikia matamanio binafsi, wakashiriki uhalifu kisha wajifiche nyuma ya dini! Haiwezekani.

Umahiri wa kuziheshimu na kuziishi imani tofauti ndani ya Tanzania zimechangia kuwajenga Watanzania kuliko ilivyo kwa mifumo mingine.

Hivyo si rahisi kwa mfano mzazo wa kikristu ambaye binti yake amweolewa na kijana wa kiislamu, akawashambulia na kuwajeruhi wajukuu zake, eti kwa sababu tu ni waislamu, walifuata dini ya baba yao!

Vivyo hivyo kwa waislamu ambao vijana wao wameolewa ama kuwaoa wenzao wa kikristu. Sasa inatokea wapi kuamini kwamba muumini halisi anayeishi hali hiyo, atafikia hatua ya kuchoma moto nyumba ya ibada na misa takatifu?

Haingii akilini. Sasa ni vyema ikajulikana kwamba kuupandikiza uhalifu ili uchukue sura ya udini, ni kutaka kutimiza azma chafu ya kuficha ukweli. Wakristu kwa waislamu, kama ilivyo kwa madhehebu  wataendelea kuishi kwa kuziheshimu na kuziishi imani zilizopo.

Hivyo ni wajibu wa mamlaka husika, kufanya uchunguzi wa kina, pasipo kuwaathiri wasiohusika, pasipo kupandikiza dhana potofu isiyoishi katika ardhi ya Tanzania-udini.

Uchunguzi unapokamilika, hatua kali na za haraka zichukuliwe ili kudhibiti uhalifu unaofanyika, lakini zaidi ukihusisha masuala ya dini.

Mashaka Mgeta ni Mwandishi wa Habari za Siasa wa NIPASHE. Anapatikana kupitia simu namba +255 754691540, 0716635612 ama barua pepe; mgeta2000@yahoo.com

Source: Nipashe 17th October 2012

 

--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
 
 

Share this :

Related Posts

0 Comments