TAARIFA
KWA UMMA KUHUSU HATMA YA MWANAHALISI Leo 28 Oktoba 2012
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Bidamu (THRD-Coalition),
wadau wanaounda mtandao huu na mwanachama mwanzilishi wa Mtandao likiwa ni shirika lenye majukumu ya
ya kutetea uhuru wa habari kusini mwa Afrika (MISA-Tan) tunaendelea kwa
pamoja kuonyesha kusikitishwa kwetu kwa kufungiwa kwa gazeti la Mwanahalisi.
Kwa mara kadhaa sasa tunawakutanisha tena lengo likiwa
ni kuendelea kuishawishi serikali ilifungulie gazeti la Mwanahalisi. Kwa vile
hoja yetu ya kutaka kuliona gazeti la Mwanahalisi likiwa mitaani haijatimia
basi na sisi kwa upande wetu kazi yetu bado haijatimia.
Tunatambua umuhimu wa kuheshimu sheria za nchi, lakini
kwa upande mwingine tunaona kwamba ipo haja ya sisi watetezi wa haki za binadamu
kupitia kwenye vyombo vya habari na pia kwenye mashirika mengine yanayounda
mtandao huu kuishawishi serikali kuachana na sheria gandamizi ambazo ni za
kidikteta kama sheria hii ya magazeti ya mwaka 1976 ambayo hukiuka misingi ya
haki za binadamu na utawala bora. Pia kwamba maendeleo ya kiteknolojia na
kisiasa hapa nchini yanaiweka rehani sheria hiyo gandamizi.
Tumebaini kuwa kufungiwa kwa gazeti la Mwanahalisi
siyo tu kwamba kunawaathiri kwa kiwango kikubwa wasomaji wake ndani na nje ya
nchi bali pia kunaathiri uhuru wa kutafuta, kupata na kueneza habari,
kunawaathiri waajiriwa wa gazeti hilo na familia zao na pia kunaiweka katika
hati hati hata kampuni nzima ya Halihalisi ambayo ndiyo mchapishaji wa gazeti
hilo.
Tunaendelea kusisitiza kuwa sababu walizotumia
viongozi wa wizara ya habari kulifungia gazeti la mwanahalisi sio za kweli
kwani kilichoandikwa na Mwanahalisi ni ukweli mtupu ambao hivi karibuni umethibitishwa na tamko la Dr Steven Ulimboka.
Pia, hivi karibuni Dkt Stephen Ulimboka, kupitia kwa
wakili wake Mheshimiwa Nyaronyo Kicheere aliweka wazi kwamba Afisa wa Usalama
wa Taifa Ramadhan Ighondu alihusika katika kutekwa kwake kwa kuwa mazingira yote kabla na baada ya
tukio yanaonyesha wazi kuwa Ramadhani Ighondu ni mdau katika tukio hili.
Kinachoshangaza zaidi ni kwamba baadala ya serikali
kutoa tamko kwamba sasa imepata uhakika kwamba afisa wake alikiuka kanuni za
ajira yake na ingeaza rasmi kuwasaka washirika wa afisa hiyu jambo hilo
halijatokea mpaka sasa huku gazeti hili lililosidia kubainisha ushahidi
likifungiwa. Zaidi, tulitegemea serikali ingemkana afisa huyo kwamba siyo
mwajiriwa wake katika idara hiyo, kama hivyo ndivyo ilivyo, au vinginevyo
tungeitarajia serikali itangaze kwamba inachukua hatua za kisheria dhidi ya
afisa huyo ambaye ametajwa kuhusika katika makosa ya jinai kinyume cha
utaratibu wa mwajiri wake. Pia tungetemea Jeshi la polisi lingetumia fursa hii
kumkamata mshukiwa huyu wa Usalama wa Taifa na kulisadia Jeshi la Polisi
kuwapata wale waliotekeleza udhalimu huu
dhidi ya Dr Steven Ulimboka. Kwa namna yoyote vitendo vya aina hiyo vinaiabisha
serikali na haviwezi kuwa sehemu ya utawala bora ambao serikali yetu imekuwa
ikitangaza kwamba inauzingatia.
Mpaka sasa kumekuwapo na matamko mbali mbali kutoka
kwa wadau, viongozi wa kiroho, mabalozi na hata Baraza la Habari Tanzania (MCT)
likiwa peke yake na hata kwa kushirikiana na wadau wengine wakilaani kufungiwa
kwa gazeti hili lakini serikali imeendelea kuwa kaidi katika hili.
Tunachosisitiza
1.
Kwa Serikali
Tunaendelea kuwasihi viongozi wa nchi waone sasa
umuhimu wa kukutana na viongozi wa Hali Halisi na kujadili namna ya
kulifungulia gazeti hili kwani tayari Dr Steven Ulimboka ameshaweka wazi
kilichoandikwa na Mwanahalisi ni cha kweli kabisa. Serikali itambue kuwa suala
hili sio dogo katika anga za kidemokrasia na haki za binadamu kwani ubabe wa
baadhi ya viongozi serikalini leo unaweza iweka nchi pabaya siku za usoni.
2.
Vyombo vya Habari
Vyombo vya habari pamoja na taasisi mbalimbali katika
tasnia ya habari tuweke tofauti zetu pembeni
na kuungana kwa pamoja katika hili na kuhakisha kuwa ukandamizaji wa
uhuru wa habari kama huu wa wazi wazi haupati nafasi katika enzi hizi za uwazi
na ukweli. Vyombo na taasisi mbalimbali za habari bado mna nafasi na uwezo mkubwa
katika kuhakisha gazeti la Mwanahalisi halipotei katika tasnia ya habari hapa
nchini.
3.
Jumuiya ya Kimataifa
Kwa kuwa mmekuwa wadau wakubwa wa maendeleo na
utekelezaji wa haki za binadamu hapa nchini, tukiwa tunaendelea kuuthamini
mchango wenu, tunawasihi muendelee kuishawishi serikali kwa njia za
kidiplomasia kuhusu suala la kuheshimu kazi za watetezi haki za binadamu na
uhuru wa habari. Nafasi zenu za
kidiplomasia na uhusiano mkubwa
mlionao na nchi ya Tanzania inaweza pia kutumika kushawishi viongozi wa Tanzania walifungulie gazeti la Mwanahalisi.
Kutokana na hali ilivyo ya uvunjifu wa haki za
watetezi wa haki za binadamu ikiwamo
haki ya kutoa habari, MISA-Tan, mwanachama wa THRD-Coalition anaehusika na
uhuru wa habari inaandaa mkutano wa siku moja utakaowakutanisha wadau mbalimbali katika tasnia ya habari ili
kujadili hatma ya gazeti la Mwanahalisi na uhuru wa habari nchini.
Mwisho Tunawasihi wanaharakati, watanzania wote wasichoke wala wasirudi nyuma katika azma hii ya kutetea
haki, uhuru na ulinzi kwa haki na watetezi wake.
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
0 Comments