I: [wanabidii] VIONGOZI AINA YA MCHUNGAJI GETRUDE LWAKATARE NI AIBU KWA TAIFA

Tuesday, October 09, 2012

----- Messaggio inoltrato -----
Da: Abdalah Hamis <hamisznz@gmail.com>
A: Wanabidii <wanabidii@googlegroups.com>
Inviato: Martedì 9 Ottobre 2012 7:55
Oggetto: [wanabidii] VIONGOZI AINA YA MCHUNGAJI GETRUDE LWAKATARE NI AIBU KWA TAIFA

Hivi karibuni Waziri wa Ardhi , Nyumba na Maendeleo ya Makazi Prof.
Anna Tibaijuka na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira)
Dkt. Terezya Huvisa walitoa tamko kwamba nyumba zote zilizojengwa
kando kando ya fukwe za bahari na mito zitabomolewa, bila wamiliki
kulipwa fidia kutokana na kukiuka Sheria za Ardhi na Mazingira za
mwaka 1992, 1995 na 2004.

Kauli hiyo ilitokana na ukweli kwamba imekuwa ni jambo la kawaida kwa
watu wenye nguvu ya fedha kuharibu mazingira kwa makusudi pasipo
kujali athari ambazo zinaweza kutokea sasa na baadae kwa wakazi wa
maeneo husika, jamii inayowazunguka na taifa kwa ujumla! Kwa watu
wengi, kauli ya mawaziri hao ilionekana kama ni hatua muhimu sana
katika kulinda mazingira ya fukwe zetu na jamii nzima hasa kutokana na
umuhimu wa kulinda mazingira katika wakati huu wa athari za mabadiliko
ya tabia-nchi.

Lakini baadhi yetu tuliona kama ni mwendelezo wa kauli za Serikali
ambazo utekelezaji wake ama huwa ni wa mashaka au ukitekelezwa basi
utekelezaji wake hutawaliwa na upendeleo wa hali ya juu kwa watu wenye
fedha na nafasi kubwa serikalini (vigogo).

Moja kati ya nyumba iliyotakiwa kubomolewa imejengwa kwenye viwanja
namba 2019-2020 Kawe Beach, katika fukwe za Bahari ya Hindi. Viwanja
ambavyo vilipatikana kwa ushirikiano wa Mchungaji Lwakatare na tapeli
maarufu wa Ardhi jijini Dar es salaam, anayejulikana kwa jina la Frank
Mushi. Ikumbukwe kwamba katikati ya mwezi Julai, 2012 wananchi
waliojenga nyumba katika maeneo yanayosemekana ni tengefu ya Jangwani
Beach, Mto Ndumbwi na Mto Mbezi walivunjiwa nyumba katika operesheni
iliyoendeshwa na Baraza la Mazingira la Taifa (NEMC), operesheni
ambayo ilihusisha takriban nyumba 15 na kuta ( fences) 8. Katika
nyumba hizo, mojawapo iliyotakiwa kuvunjwa ni ya Mchungaji Getruda
Lwakatare.

Lakini kwa sababu ambazo wahusika, akiwemo yeye mwenyewe na serikali,
wanazifahamu, nyumba yake haikuguswa! Wakati wananchi wanaofahamu
ukweli wa mambo, wakiwa bado wanahoji chinichini juu ya upendeleo wa
kitabaka ulio wazi, hivi karibuni wameshuhudia kupitia njia mbalimbali
za upashanaji habari, ikiripotiwa kuwa Mchungaji Lwakatare (Mchungaji
wa Kanisa la Assemblies of God na Mbunge wa Bunge la Jamhuri wa
Muungano wa Tanzania ) amehamia kwenye nyumba yake mpya. Nyumba ambayo
ilipaswa kuwa imebomolewa kwa sababu imejengwa kwenye viwanja ambavyo
ni kinyume cha sheria kujenga katika maeneo hayo.

Kuvunja sheria kwa uwazi namna hii, huku wengine wakichukuliwa hatua
kwa kuvunja sheria hiyo hiyo, si tu ni 'double standards', bali
kunaweza kutafsiriwa ni kuitia serikali mfukoni. Kitu kibaya zaidi ni
kwamba kiongozi huyo alishataarifiwa tangu mapema juu ya ubatili wa
kujenga katika eneo hilo, kupitia kwa huyo Frank Mushi kabla hata
ujenzi wa nyumba hiyo haujaanza. Ikumbukwe pia kuwa viwanja hivyo
vilipatikana na ujenzi huo kuwezekana baada ya eneo la bahari na mto
kujazwa kifusi na mawe!

Kwa kutambua kuwa kuendelea na ujenzi katika eneo hilo ni kuvunja
sheria za nchi zinazohusu utunzaji wa mazingira kwa manufaa ya jamii
nzima, Mchungaji Lwakatare aliendelea kwa kujiificha nyuma ya mgongo
wa huyo Mushi, akijifanya hahusiki kabisa na kilichokuwa kikiendelea
katika eneo husika. Uthibitisho wa ubatili wa kujenga katika viwanja
husika:

1) Tarehe 4/1/2011 Wizara ya Ardhi kupitia barua yenye Kum. Namba LD/
297571/18 waliandika barua kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa
ya Kinondoni kuhusiana na uvamizi wa kiwanja nana 2019 na 2020 Mbezi
Kawe. Barua husika pamoja na mambo mengine ilibainisha kwamba wizara
imefanya ukaguzi katika viwanja tajwa, baada ya kupata malalamiko juu
ya uharibifu wa mazingira unaoendelea katika eneo hilo. Na kwamba
ukaguzi walioufanya umeonesha kuwa ujenzi unaofanyika katika eneo
husika hauruhusiwi na unakiuka Tangazo la Serikali (GN) No. 76 ya
mwaka 1992. Kupitia barua hiyo, wizara ilimtaka Mkurugenzi wa
Halmashauri kuchukua hatua za kubomoa/kuondoa uendelezaji batili
uliokuwa ukifanyika katika viwanja Na 2019 na 2020 Mbezi Kawe. Barua
hiyo ilisainiwa na Bwana Sadoth K. Kyaruzi, kwa niaba ya Katibu Mkuu
wa Wizara.

2) Uthibitisho mwingine ni barua ya tarehe 30/9/2011 kutoka NEMC
kwenda kwa Bwana Frank Mushi. Barua husika, ilitoa maelekezo kwa Mushi
kuvirudisha katika hali yake ya kawaida, viwanja namba 2019-2020 kwa
mujibu wa vifungu 55(2) (a) (e), (3) na 151 (1) ,(2) (a), (b), (3) ,
(4) (b) na (f) vya Sheria ya Mazingira, sura 191 ya mwaka 2004. Barua
husika inabainisha kwamba timu ya wataalam toka Baraza la Mazingira
(NEMC), Wizara ya Maji, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Halmashauri ya Jiji la Dar es
salaam na Manispaa ya Kinondoni ilitembelea eneo husika kufuatia
malalamiko kutoka kwa viongozi na wakazi wa Kawe Beach.  Timu hiyo
ilibaini kwamba eneo la Mto Ndumbwi, pamoja na bahari lilikuwa
linajazwa mawe na vifusi hali iliyosababisha kupatikana kwa viwanja na
2019 na 2020. Ambapo ndani ya viwanja hivyo lilikuwa linajengwa jumba
kubwa kinyume kabisa na vifungu 55(2)(a) , 55(2) (b) , 55(2)(d) na
55(2)(e) vya Sheria ya Mazingira.

Ilibainika pia kuwa mikoko ilikatwa kinyume na s.63(1) ya Sheria ya
Mazingira. Kwa mujibu wa nyaraka nilizonazo, yafuatayo yalijitokeza

i)  Timu ya wataalam ilibaini kwamba, tayari Wizara ya Maliasili na
Utalii ilishatoa zuio la ujenzi katika eneo husika.

ii)  Manispaa ya Kinondoni, mara kadhaa iliweka zuio la uendelezaji na
kutoa amri kwa 'mmiliki' wa eneo husika kubomoa, lakini mmiliki huyo
alipuuza amri hiyo na kuendelea na ujenzi!

iii)  Ilitolewa amri ya Mahakama, tarehe 5/4/2011 kumtaka Bwana Mushi
asiendelee na ujenzi. Amri hiyo ilipuuzwa na ujenzi ukaendelea.

Baraza la Mazingira lilimwagiza tena, Bwana Mushi:-

2) Kuvunja majengo yote yaliyoko kwenye viwanja vyenye mgogoro.

3) Ndani ya siku saba, tokea amri husika kutolewa (amri ilitolewa
30/9/2011) awe ametoa mawe na vifusi vyote vilivyoharibu mkondo wa
maji na bahari na kuurudisha mto na bahari katika hali yake ya
kawaida.

4) Ndani ya siku 30 chini ya usimamizi wa Wizara ya Maliasili na
Utalii kuhakikisha kwamba mikoko yote iliyokatwa imerudishwa katika
hali iliyokuwa awali. Kwa gharama za Bwana Mushi.

Licha ya amri zote hizo, mazuio yote hayo, matamko ya mawaziri
yaliyotawaliwa na mbwembwe nyingi, ujenzi uliendelea, nyumba
imekamilika. Sasa inatumika. Wakati kigogo huyo amehamia kwenye nyumba
yake kwa matangazo na mbwembwe, Mto Ndumbwi, bahari na mazingira kwa
ujumla yameharibiwa vibaya! Bila kusahau kuwa wananchi wengine
wamebomolewa nyumba zao kwa kutumia sheria hizo hizo. Kwa mujibu wa
Sheria ya Mazingira, Sura 191 ya mwaka 2004, Fungu 57(1) hairuhusiwi
kufanya shughuli zozote za kudumu za kibinadamu ndani ya mita 60
ambazo kwa asili yake zinaweza kuhatarisha au kuathiri vibaya ulinzi
na utunzaji wa mazingira, utunzaji wa bahari, kingo za mto, bwawa au
mwambao wa asili wa ziwa.

Halikadhalika, Sheria ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999 ( Sura 113) Fungu 7
(1) (d) inabainisha kwamba eneo lolote lililo ndani ya mita 60 kutoka
kingo ya mto na bahari linatakiwa kutangazwa kama ardhi hatari au
kuhifadhiwa. Na pale inapotokea kuwa masharti ya sheria moja
yanapingana na masharti ya Sheria ya Mazingira, kuhusu mambo
yanayohusu usimamizi wa mazingira, Sheria ya Mazingira ndiyo hutumika,
kwa mujibu wa Fungu 232 la sheria ya mazingira sura…

Kutokana na hali hii serikali inatakiwa kujinasua katika mwendelezo wa
tafsiri wanayoipata wananchi kuwa imetekwa na kuwekwa mfukoni na watu
wachache wenye uwezo. Maana wanaona kuwa huu ni mwendelezo wa serikali
kuwa na kigugumizi pale sheria zinapovunjwa na vigogo serikalini au
watu wenye fedha wanaoshirikiana na baadhi ya viongozi wa serikali na
chama tawala kufanya ufisadi.

Wameona mambo ya namna hii mara kadhaa, ikiwemo serikali kushindwa
kuwachukulia hatua waliohusika na kashfa kubwa za ufisadi kama 'akina'
Kagoda na wenzake (EPA), Richmond na kashfa nyingine nyingi.

Kwamba sasa inazidi kuonekana dhahiri kuwa kuna watu wako juu ya
sheria za nchi, huku wanyonge wakishughulikiwa.

Ni wakati mwafaka sasa kwa mawaziri wanaohusika na masuala ya ardhi na
mazingira kuwaeleza Watanzania kulikoni wananchi wa hali ya chini
kuvunjiwa nyumba zao kwa kigezo cha kuvunja sheria wakati huo huo
Mchungaji Lwakatare (kigogo) ambaye uharibifu wake ni wa hatari kuliko
hata hao waliovunjiwa akitamba mtaani kwamba yeye yuko juu ya sheria
na hakuna mamlaka yoyote yenye uwezo wa kumzuia kufanya alichofanya!

Ni aibu kwa Taifa kuwa na viongozi wa aina hii!

Viongozi ambao wako tayari kutumia fedha, hila, mamlaka na dhamana za
uongozi walizopewa, kuhalalisha haramu, ni janga kwa mstakabali wa
taifa letu! Waziri Kivuli, Wizara ya Ardhi , Nyumba na Maendeleo ya
Makazi

Imetolewa Dar es Salaam na;
Halima Mdee (MB)
Waziri Kivuli, Wizara ya Ardhi , Nyumba na Maendeleo ya Makazi

--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com  Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.




Share this :

Related Posts

0 Comments