[wanabidii]

Friday, July 01, 2016
FEBRUARI mwaka jana niliandika makala katika gazeti hili kuhusu namna Mwalimu Julius Nyerere, akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1971, pamoja na Waziri wake wa Fedha, Amir Jamal, walivyokataa ushawishi wa kampuni moja ya Uswisi ili eti hatimaye waibe mabilioni ya fedha nchini na kwenda kuyaficha katika benki mojawapo nchini Uswisi.
Kwamba Mwalimu Nyerere alishawishiwa kujiandaa na maisha ya kifahari kama utawala wake ungeingia katika mgogoro na hata kung'olewa, angeweza kwenda kuishi popote duniani huku akitumia 'mapesa' aliyovuna na kuyaficha huko Uswisi.

Katika makala yangu hiyo nilinukuu gazeti la Uhuru la Septemba 3, takriban miaka 45 iliyopita (yaani 1971) kwenye ukurasa wake wa sita ambako ndiko ilikochapishwa barua hiyo maalumu ya siri. Nilieleza bayana kwamba hatua hiyo ya Mwalimu kukataa 'ushawishi huo wa kifisadi' si tukio dogo, bali ni tukio kubwa lenye mafunzo mengi, kwa wakati huo (Februari 2015 nilipoandika makala ile) nilirejea mbinu chafu zilizokuwapo dhidi ya kumtafuta mgombea urais aliye makini na mwadilifu – mwenye hadhi inayofanana na hiyo ya Mwalimu Nyerere ya kukataa kushawishiwa kuwaibia wananchi wake.

Makala ilieleza kwamba barua hizo zilizoandikwa kwa Mwalimu Nyerere na Waziri Jamal, zote za Agosti 5, 1971, zilikuwa na muhuri wa siri, zikimshawishi Mwalimu Nyerere na Jamal, kuingia makubaliano ya siri na kampuni hiyo ya Uswisi ili wafunguliwe akaunti maalumu huko huko Uswisi, kwa ajili ya kufichiwa "mapesa" ambayo wangeweza kukusanya (kifisadi) kutoka Tanzania.

Leo tena naweza kufanya rejea ya tukio hilo la Mwalimu Nyerere na Waziri wake wa Fedha, Jamal, kushawishiwa na kampuni ile ya Uswisi japo si katika muktadha wa kusaka mgombea urais bora, mwadilifu na makini (kama nilivyoandika kwenye makala hiyo ya Februari), bali sasa nitajadili katika mazingira tofauti – mazingira ambayo amekwishapatikana rais ambaye katika miezi yake hii ya awali saba pale Ikulu – si haba, hana suluhu na ufisadi.

Katika hadhi ile ile ya Mwalimu Nyerere kukataa ushawishi wa kugeuzwa fikra ili kuhujumu wananchi wake, sasa namshauri Rais Magufuli aongeze vitisho zaidi. Ndiyo, vitisho halisi dhidi ya majaribio mengine yoyote ya ndani na nje ya nchi yenye kufanana na lile jaribio la kampuni ya Uswisi dhidi ya Mwalimu Nyerere na Waziri Jamal. Vitisho dhidi ya magenge ya uhujumu uchumi kumshawishi akubaliane nao. Hivi si vitisho vya kushika silaha au kutoa amri za kijeshi bali ni vitisho vinavyotokana na nguvu binafsi ya uadilifu wa mtu.

Anachoweza kufanya Magufuli ni rejea tu ya kile alichokifanya Mwalimu, yaani kukataa kuwekwa katika mazingira ya kuchukua tahadhari haramu. Tahadhari ya kuongoza nchi kwa lengo la kujihami na hali binafsi ya kiuchumi baada ya kuondoka madarakani.

Magufuli anaweza tu kurejea uamuzi huo wa Mwalimu Nyerere kukataa ushawishi ule wa kampuni ya Uswisi na akafanya jambo jingine la ziada kwa watu watakaomfuata kwa 'sura' ile mithili ya wale wawakilishi wa kampuni ya Uswisi, kwamba yeye si tu awakatalie lakini awachukulie hatua za kisheria na kisha dunia ijue kwamba Tanzania si nchi tena ya kutuma mawakala wa ufisadi kuja kushawishi viongozi waibe mali ya wananchi na kwenda kuhifadhi kwenye benki zao.

Inawezekana mbinu za kushawishiwa kuibia wananchi kwa sasa zikawa zimebadilika tofauti na ilivyokuwa kwa Mwalimu Nyerere na Waziri wake wa Fedha, Jamal. Inawezekana kwa sasa wizi unafanywa kupitia miradi mikubwa ya kimataifa inayoendeshwa hapa nchini au kupitia mikopo kadhaa ya kimataifa. Inawezekana kuna wizi wa ubia katika miradi ya ubia.

Kwa hiyo, katika mbinu zozote mpya lakini zenye mantiki ile ile ya jaribio lililopata kufanywa dhidi ya Mwalimu Nyerere, Magufuli hana budi kuonyesha kiwango cha juu zaidi cha uadilifu kwa wananchi wake kama ambavyo mara kwa mara amekuwa akijinadi kufanya kazi kwa niaba ya wananchi wote, hasa wananchi masikini.

Hakika, tayari akiwa Ikulu Magufuli anayo rejea muhimu ya kumwongoza na rejea hiyo ni matendo ya uadilifu ya Mwalimu Nyerere, kuanzia hilo la kukataa ushawishi ambao pengine ulifanyika na kufanikiwa kwenye nchi kadhaa si tu za Afrika bali hata katika mataifa mengine nje ya Afrika. Nguvu za uadilifu ndicho kitisho kikuu dhidi ya magenge ya ushawishi wa kifisadi na kwa hiyo, kuna vitisho vyenye manufaa kwa nchi hii, ingawa si vitisho vya silaha nzito au amri za kijeshi.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika

Raia Mwema

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments