[wanabidii] Ukistaajabu ya Profesa Lipumba utayaona ya Chadema

Saturday, July 16, 2016

HAPO zamani za kale, paliibuka msemo maarufu, usemao, "Ukiyastaajabu ya Mussa, utayaona ya Firauni".

Kwa muktadha wa haya yaendeleayo hii leo katika siasa muflisi nchini mwetu, lau kama utaamua kuubadili msemo huo, kwa kuwa akina 'Mtume Mussa' walikwishamalizika duniani, basi pale kwenye jina la 'Mussa' upabadili kwa kuliweka jina la 'Lipumba'.

Walakini kwakuwa Mafirauni yangali yanaishi hadi hii leo, hivyo hapo kwenye jina 'Firauni' unaweza kupaacha vivyo hivyo, ima ukamtafuta Firauni yeyote mashuhuri hapa Tanzania kisha ukambandikia lakabu hiyo.

Kwa mara nyingine tena Chama cha Wananchi – CUF kinaingiwa na tajriba nyingine, baada ya mwanachama wao aliyebingwa wa uchumi duniani, mzalendo wa enzi za BBC (Born Before Computer), mtoto wa mkulima wa Ilolangulu, Profesa Ibrahim Haruna Lipumba, kumwandikia barua Katibu mkuu wa chama chake cha siasa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, akiianika dhamira yake ya kutaka kuurejea wadhifa wake wa Uenyekiti wa chama hicho taifa, alioachana nao baada ya kuamua kujiuzulu takribani mwaka mmoja sasa, na kubakia kuwa mwanachama wa kawaida tu katika chama hicho.

Katika maelezo yake wakati alipokuwa akijiuzulu wadhifa wake, gwiji na galacha huyo wa uchumi alitanabahisha kwamba dhamira yake ilimsuta kuendelea kumuunga mkono Edward Lowassa aliyejiunga na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi-UKAWA ili kugombea urais wa nchi hii.

Msimamo wa Profesa Lipumba wa kutokuwa na imani juu ya Lowassa, aliyetoka CCM na kujiunga na CHADEMA ili agombee urais, haukuchipua tu mithili ya uyoga, bali ulianza siku nyingi tangu kipindi Lowassa angali CCM. Hivyo kudhihirisha maoni yake ilikuwa ni haki yake ya msingi na ya kikatiba. Na kuyasimamia hayo bila ya kutetereka ilikuwa ni ithibati ya ujasiri na kutoyumba kwake. Nani asiyemtaka mwenyekiti kama huyo?

Wanasiasa wengi, hasa wa upinzani, hivi sasa wanalalama kuwa demokrasia inaminywa hapa nchini kutokana na kuzuiliwa kwao kutoa maoni yao kupitia mikutano ya hadhara na makongamano juu ya vile wanavyoviamini na kuvisimamia.

Wanasiasa haohao, ndiyo waliyemshambulia na wanaoendelea kumshambulia mpinzani mwenzao Profesa Lipumba, kwa 'kosa' la kutoa maoni na misimamo yake juu ya kile alichokiamini.

Yaani walimtaka Profesa Lipumba aikalifishe nafsi yake kwa kutokuwa huru kutoa maoni, na misimamo yake ili tu wao wakidhi matlaba zao, halafu na wao wanaloloma kubinywa uhuru wao wa kutoa maoni yao mikutanoni. Ama kweli ukiyastaajabu ya Lipumba, utayaona ya Chadema.

Sasa kwa kuwa uchaguzi ulikwishamalizika, na kwamba Lowassa si mgombea tena, hivyo Profesa Lipumba akaonelea kwamba ili kuendelea kukiimarisha chama chake, ni vyema arejee kwenye kiti chake ambacho kwa yakini kabisa bado kina vumbi tangu alipokiacha kwa kukosa wa kukikalia.

Maajabu yakaanzia hapo; baadhi ya upinzani hasa wasiokuwa wanachama wa CUF, wakaibuka na kujifanya wasemaji wa CUF kwa kumshambulia tena Lipumba kuwa hafai kurejea kitini kwa hoja kwamba Lowassa angali Chadema.

Yaani baadhi ya wafuasi, washabiki, wanachama, wakereketwa, wafurukutwa, na hasa wa Chadema, walioshindwa kumburuza na kumsujudisha kwao Profesa Lipumba ili aisaliti dhamira yake ya kutomkubali Lowassa, leo wanataka kuwaburuza na kuwasujudisha wana CUF wamkane.

Tukumbushane kidogo, hii hofu huja inapoguswa Chadema tu? Aliyewahi kuwa mwanachama wa CUF na Mbunge wa Bukoba, Wilfred Lwakatare, alipokihama chama hicho, na baadaye kujiunga na Chadema, na kuteuliwa kugombea ubunge, mbona hakukuwa na chuki vichwani mwa CUF, na badala yake wakamuunga mkono bila hiyana hadi akaukwaa ubunge?

Haya kama haitoshi, mbona Chadema waliwahi kumpokea mwanachama na kiongozi mwingine wa CUF, Profesa Abdallah Safari, na bado CUF waliidumisha staamala yao bila ya kuisambaratisha UKAWA? Iweje leo CUF ikimrejeshea uenyekiti wake, kiongozi wao aliyejiuzulu, ambaye hadi sasa angali mwanachama wao, iwe nongwa? Amaa kweli ukiyastaajabu ya Lipumba, utayaona ya Chadema.

Akihojiwa na vyombo vya habari kufuatia ombi la Profesa Lipumba kurejea kitini, kiongozi wa Chadema, ambaye pia ni mwalimu wetu wa Kiswahili, Profesa Abdallah Safari, pamoja na majibu marefu, alisema kwamba; "hana imani na Lipumba,"

Nikajiuliza hivi kwanini hii kasumba ya watu wa Chadema kuwasemea semea CUF inataka kushamiri kwa kasi namna hii? Sikupata majibu. Nikajisaili tena; hivi hii 'jeuri' ya kiongozi huyu wa Chadema, dhidi ya Profesa Lipumba, ilikuwa wapi kipindi kile wakati viongozi wenzie tena wa ndani ya chama chake waliopata kutuhubiria hapo awali kuwa Lowassa hafai? Amaa kweli ukiyastaajabu ya Lipumba, utayaona ya Chadema.

Ni Muhali kuwasikia viongozi wa CUF wakiyaingilia na kuyasemea semea mazingaombwe yoyote yale kutoka katika chama chochote kile cha siasa, lakini wanakosa ujasiri wa kuwakemea wale wote wanaoingilia mambo yao ya ndani hasa wakiwa wanatokea upinzani. Sasa nasaha zangu kwa CUF, hebu mtuweke wazi jamani labda wenzetu kuna kifungu kinawabana mbavu kila mnapofikiria tu kujikukurua dhidi ya hulka hii chafu.

Chanzo Rai

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments