[wanabidii] Kitwanga kanyolewa, mliobaki tieni maji

Monday, May 23, 2016

JUZI Rais John Magufuli alitengua uteuzi wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga kutokana kuingia bungeni na kujibu swali linaloihusu wizara hiyo akiwa amelewa.

Suala la mtu mwenye dhamana kubwa kama Kitwanga, la wizara inayogusa usalama wa watu na mali zao, kuingia katika kutumikia wananchi akiwa amelewa ni suala gumu ambalo hata maelezo ya kawaida hayawezi kuleta maana kwa mtu wa kawaida.

Tunasema haiwezi kuleta maana kwa mtu wa kawaida kwa kuwa dhamana aliyonayo mheshimiwa haiendani na tabia ya kunywa wakati wa kazi au kufika kazini ukiwa umelewa.

Katika suala la utumishi wa umma, ofisa au mfanyakazi yeyote kuingia kazini amelewa kiasi cha kushindwa kutekeleza wajibu wake, si tu analeta fedheha katika nafsi yake lakini pia kwa serikali ambayo amedhaminiwa kuifanyia kazi.

Tunapenda kuamini maamuzi ya Rais Magufuli ya kutengua uteuzi wa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga si tu umefuata kanuni za utumishi wa umma ambao unakataza mtumishi kulewa akiwa kazini, bali pia unatuweka sawa, watumishi wote kuondokana na tabia ya kufanya kazi kwa mazoea.

Ufanyaji kazi wa mazoea uliokuwa umefikiwa na wengi wa wenye dhamana umesababisha serikali kukosa heshima, watu wengine kunung'unika na kuona kwamba serikali inalea watumishi wabovu na wenye kiburi.

Hali hiyo ya kiburi inayosababishwa na mazoea kwamba hakuna wa kunichukulia hatua, mimi ni mkubwa, mtu wa karibu na mamlaka, mwenye dhamana inazalisha manung'uniko kwa wananchi ambao huona kwamba serikali haiwajali.

Kwa maneno mengine, Rais amekumbusha watendaji wote nidhamu ya kazi na haja ya kukabiliana na mapungufu ya ufanisi na tija kwa kuondoa watu ambao ni vikwazo wakati wakitakiwa kuwa mfano katika utumishi wa umma.

Kama alivyosema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akitoa ufafanuzi wa maamuzi ya Rais:"Zipo sheria za utumishi ambazo mtumishi hatakiwi kunywa pombe na wala hapaswi kulewa akiwa kazini… mtumishi anapaswa kuwa na akili timamu inayokuwezesha kufanya kazi za Serikali," Waziri Kitwanga amechemka na adhabu aliyoipata inastahili, ya kutenguliwa kwa uteuzi wake.

Kila mtu anayeitakia mema Serikali hii katika juhudi zake za kupambana na ulevi wa madaraka, mali na utendaji wa kazi hatua aliyoichukua Rais Magufuli ni hatua ya kuunga mkono, huku watumishi wakitakiwa kujichekecha kuhusu maadili na utii wa sheria na kanuni za kazi ili kuongeza ufanisi na kuleta tija.

Ulevi wa Waziri Kitwanga ulisababisha hata swali aliloulizwa ambalo hakulijibu vizuri litafutiwe nafasi, ikimaanisha wazi kwamba muda wa juzi alioutumia Kitwanga umepotea bure.

Hili lisibaki kuwa funzo kwa baraza la mawaziri tu kwamba linatakiwa kuchapa kazi, lakini pia watumishi wengine wa umma ambao wamekuwa wakifanya kazi kwa mazoea, wakiendekeza ulevi, kwamba sasa basi, wajifunze kutoka kwa Kitwanga.



Habari Leo

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Related Posts

0 Comments