[wanabidii] Rais Magufuli Urais ni Wako Chukua Hatua

Sunday, April 10, 2016
Kati mijadala iliyochukua muda wa wengi hapa katika majukwa mengi ni:

Je, Tanzania inaweza kujitegemea ghafla leo baada ya kuwa tegemezi kwa miaka yote?

Ukifuatilia utagundua kuwa watu wengiwasio na Elimu ya uchumi ndiyo wamekuwa mstari wa mbele kuelezea kuwa Tanzania ina uwezo wa kujitegemea kwa 100% hata kuanzia leo. Lakini wataalam wa uchumi na viongozi wa serikali wameeleza kuwa Tanzania bado tunahitaji kusaidiwa ili kuweza kusimama kwa miguu yetu kwa 100%. Baadhi ya wachumi na watendaji wa serikali wamelisema hilo wazi na wengine wamenyamaza kimya kwa kukosa ujasiri wa kutamka kile wanachokijua kuwa Tanzania haina uwezo wa kujitegemea kwa 100% kwa ghafla, japo uwezo huo upo kwa siku za mbeleni kama tutakuwa na mipango thabiti.

Magufuli alipozungumzia kuhusu kujitegemea alitoa kauli tata, alisema Tanzania ina uwezo wa kujitegemea, na ilistahili kuwa donor country, hakusema tunaweza kujitegemea kuanzia sasa. Hakusema tutakuwa donor country kuanzia sasa. Na nina uhakika Magufuli kamwe hatathubutu kutamka kuwa Tanzania tayari tunaweza kujitegema kuanzia sasa, japo uwezekano upo.Tafsiri yangu ni kuwa alimaanisha kuwa uwezo huo tunao japo hatujitegemei, na je ni lini tutajitegemea, na kwa mipango ipi? Ndiyo jambo tulilostahili hasa kulijadili.

Miongoni mwa hatua za kuelekea kujitegemea ni hiyo ya kusimamia ukusanyaji wa kodi, kuongeza uwekezaji, kufanya kazi kwa bidii, kuwa na matumizi mazuri ya fedha za serikali, uwajibikaji, kujenga mifumo na utengenezaji wa sera zinazolenga kujitegema. Hayo hayatokei kwa kulala na kuamka.

Kujitegemea ni process, siyo kila siku unasaidiwa katika kila kitu: barabara unajengewa, maji unaletewa, wagonjwa wako wote wa HIV wanapewa ARV na wageni, uzazi wa mipango unasaidiwa, huduma ya Mama na Mtoto unalipiwa, umeme unajengewa, madaraja unajengewa, mafunzo ya watendaji wako unagharamiwa, mafunzo ya majeshi unasaidiwa, silaha za kivita unanunuliwa, n.k., halafu uamke tu na kusema kuwa kuanzia kesho najitegema. Utakuwa kichaa! Mwenye hekima lazima atatuambia kuwa katika process ya kujitegemea, tunaanza kujitegemea na nini. Tunatarajia tuambiwe kuwa katika mwaka huu wa fedha barabara zetu zote tunazijenga wenyewe, mwaka mwingine atatuambia maendeleo ya sekta ya kilimo yanagharamiwa na sisi wenyewe, n.k.

Ni ukweli huu ndiyo unaofanya wataalm wote wa uchumi au kukaa kimya au kuishia tu kusema, tunasikitishwa kukatiwa misaada, tunatarajia watoaji wa misaada watafikiria upya uamuzi wao, na wengine kuamua kukaa kimya. Ila wale wasiojua hata A ya uchumi kama wanabaki wanapiga kelele za kujifurahisha kuwa tunaweza kujitegema kuanzia sasa.

Zimbabwe ilikuwa na uchumi imara zaidi ya mara 10 ya uchumi wa Tanzania.

Zimbabwe inachimba madini mengi kuliko Tanzania. Zimbabwe ina migodi ya kisasa ya precious metals kama gold, na ilikuwa nayo hata kabla ya Tanzania. Inachimba base metals kama Nickel, Copper, Zinc na Lead. Tanzania hatuna migodi ya madini hayo, copper kidogo inatoka pale Bulyanhulu kama by-product.

Zimbabwe ni nchi inayoongoza katika uchimbaji na uuzaji wa madini ya Lithium katika Afrika.

Zimbabwe inachimba industrial minerals kama limestone, dolomites na phosphates.

Zimbabwe ni nchi ya pili Duniani katika uchimbaji na uuzaji wa madini ya platinum (white gold).

Zimbabwe ina viwanda vya aina mbalimbali vinavyozalisha bidhaa zaidi ya 6,000.

Ni kutokana na uchumi huo imara wa Zimbabwe, Mugabe alifanya jeuri, akiiamini uchumi wake imara ungeweza kusimama wenyewe bila ya kuyategemea mataifa ya Ulaya Magharibi na Amerika akijidai kuwa maumuzi ya kuwanyang'anya ardhi walowezi alikuwa analinda uhuru wa Taifa lake. Zimbabwe hata wananchi wa vijijini walikuwa hawajui kununua nyanya zilizowekwa barabarani kwenye mchanga kama Tanzania, walikuwa wananunua kwenye super markets zilizokuwa zimeenea nchi nzima.

Leo Zimbabwe haina hata sarafu yake yenyewe, inatumia dola ya marekani na Randi ya Afrika Kusini. Je hapo sasa Zimbabwe imekuwa na uhuru zaidi au imepoteza uhuru wake? wananchi wake, tena wasome waliishia kuuwawa huko Afrika Kusini walikokuwa wameenda kubangaiza maisha. Nilipokuwa Afrika Kusini nilizungumza na baadhi ywa hudumu (waiters) wa mahoteli ya Afrika Kusini, wengi walikuwa Wazimbabwe, wengine ni walimu wa sekondari, wengine ni wauguzi, walikuwa clinical oficcers, wanaona aheri wakafanye kazi ya uhudumu wa hoteli Afrika kusini kuliko kufundisha sekondari au kutibu wagonjwa nchini Zimbabwe.

Hivi kwa Zimbabwe kuamua kutumia sarafu za wale wale uliosema wanakuingilia uhuru wako, ni uhuru zaidi? je, Watanzania tunataka tufike huko? Namsihi Rais Magufuli azisikie sauti zetu hizi, watanzania wana asili ya unafiki wanapoongea na mkubwa, watakusifia hata pale unapokosea.

Watanzania tuna ule msemo kuwa mwenzio akinyolewa wewe tia maji, tusijifanye ni Vinjekitile tunapigwa risasi tunakufa ndugu wanaotuona tunakufa wanasema risasi hizo zimegeuka maji na damu inayomwagika ni maji. Binadamu mwenye akili hujifunza kupitia makosa ya mwenzake. Tusiwe kama nyumbu ambao wanaona aliyetangulia anaingia kwenye mto, analiwa na mamba mmoja, na yeye anaamini hatakamatwa kwa sababu yule mamba ameshiba kwa kumla yule nyumbu wa kwanza bila ya kujua mto una mamba wengi.

Tanzania nchi maskini kabisa, tena kwa mbali ukilinganisha na Zimbabwe haina uwezo wa kushindana na haya mataifa makubwa kwa kiburi, yatubidi tuwe werevu, twende nao kwa urafiki na uelewano, huku tukiendelea kujenga uwezo wetu wa kujitegemea. twende kwenye uhalisia, tusipelekwe na sifa au mihemuko ya kisiasa.

Tunataka utawala wa Magufuli ufanikiwe, kufanikiwa kwa utawala wake ni unafuu kwa watanzania na kufanikiwa kwa Tanzania kama taifa. Tunakuomba Magufuli, fanya jitihada zako zote, ujenge uhusiano wa karibu na ulio imara na jamii ya kimataifa. Tofauti ya kuwa na mahusiano mazuri na mahusiano mabaya gharama yake ni kubwa mno. Zimbabwe kimaendeleo imerudi nyuma zaidi ya ilivyokuwa miaka 20 iliyopita. Mpe maelekezo Waziri wako wa Mambo ya nje kuwa tunataka mahusiano mazuri na jamii ya kimataifa, tunataka misaada yote iliyosimamishwa tuipate ili itupe nguvu ya kuweza kujitegemea haraka, tuitumie misaada hiyo kama mbegu tukijua kuna siku itatoweka.

Msambichaka Mkinga

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments