[wanabidii] Prof. Shivji: Tuwe makini na ubeberu wa Marekani kupitia MCC

Monday, April 11, 2016
Raia Mwema: Profesa hatua ya MCC kusitisha msaada wake kwa Tanzania inatupa somo gani kama taifa?

Shivji: Somo moja ambalo hatua hii inatukumbusha tena ni umuhimu wa kujitegemea hasa katika kuchukua maamuzi yetu sisi wenyewe. Na hii ndiyo hasa ilikuwa falsafa ya Mwalimu (Baba wa Taifa Julius Nyerere), falsafa ya kujitegemea, siyo kwamba unaweza kujitegemea kwa maana kwamba hutataka mahusiano na watu wengine hapana, isipokuwa kujitegemea maana yake ni kwamba katika uhusiano ule kunakuwa na usawa, hilo moja.

Pili kunakuwa na kuheshimiana na tatu bado unabaki na uhuru wako wa kufanya uamuzi wako. Hiyo ndiyo maana hasa ya kujitegemea. Pale ambapo uchumi wako unakuwa tegemezi kabisa ndiyo unapoteza uhuru wako wa kisiasa. Kwa hivyo nafikiri jambo hilo lilivyotokea linatufundisha tena, kwamba je, tumepotea wapi njia kiasi kwamba leo jambo kama hili linapotokea taifa zima na kila mtu anazungumzia kana kwamba hatutaweza kuishi bila msaada huu?

Nafikiri ni nafasi nzuri kama taifa kuanza kufikiria upya tena mwelekeo wetu na falsafa yetu hasa kama tukitaka kulinda uhuru wetu wa kisiasa. Jambo la pili ambalo ningependa kulisisitiza kwamba hakuna msaada wowote unaotolewa, uwe umetoka Magharibi au Mashariki, hakuna msaada unaotolewa bila ya maslahi ya wale wanaotoa msaada, hilo lazima tuelewe, tusiseme kwamba ni fadhila tu, kuna maslahi yao.

Ni wazi kabisa kwamba MCC wana mkakati wa kuhakikisha wanakuwa na ushawishi katika sekta ya nishati. Ukiangalia takwimu nchi za Magharibi hususani Marekani wameanza kutegemea sana nishati kutoka Afrika hasa kutokana na tatizo na migogoro ya nchi za Mashariki ya Kati. Kwa hiyo wana interest (maslahi) yao, na watafikia maslahi hayo kwa njia mbali mbali ikiwemo hiyo ya kutupatia msaada wanapoona kuna maslahi yanalindwa na kusitisha misaada hiyo wanapoona maslahi yao yana walakini.

Kwa hiyo tusichukue sababu zinazotolewa (na MCC) kwa juu juu tu tuliangalie suala hili kwa undani wake. Jambo jingine ningependa kulisisitiza ni kwamba mambo yetu sisi wenyewe tutatue wenyewe, siyo kwa shinikizo siyo kwa kulazimishwa, tusione kwamba kama tukishangiliwa na mtu mwingine ndiyo tunafanya jambo jema, na tukilaaniwa na mtu mwingine basi tunafanya jambo baya, la hasha, lazima sisi tujitegemee na kufanya mambo yetu, hilo ni jambo muhimu sana.

Chanzo Raia Mwema

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments