[wanabidii] Dk. Slaa: Kama wewe si fisadi, unamchukia Magufuli kwa lipi?

Saturday, April 02, 2016
RAIA MWEMA: Hii ni mara yako ya kwanza kufanya mahojiano rasmi na chombo cha kitaifa cha habari hapa nchini tangu ulipoenda masomoni.Labda, kwa faida ya wasomaji,ungesema uko wapi hivi sasa na unafanya nini?

SLAA: Itoshe tu kusema kwamba kwa sasa niko nchini Canada kwa masomo na Mungu akinijalia ninategemea kumaliza mwezi Septemba mwaka huu. Kwa wale ambao hawakuwa na taarifa, ninasoma Pyschology (Saikolojia) na kujikita hasa katika Psychotherapy na Psychoanalysis.

(Psychotherapy ni aina ya tiba wanayotoa wanasaikolojia kwa matatatizo yanayowahusu wanadamu kutokana na misongo ya mawazo. Psychoanalyisis ni masomo yanayoweza kumsaidia mtu kujitambua, kufahamu kuhusu mahusiano na namna watu wanavyotakiwa kuishi duniani. Mhariri)

Kwa wale wanaofahamu vizuri historia yangu, nilisoma mambo ya saikolojia kama sehemu ya falsafa wakati nikiwa mwanafunzi katika Seminari ya Kibosho kati ya mwaka 1971 hadi mwaka 1972.

Hivyo sasa ninajikita katika baadhi ya mambo ambayo wakati nasoma sikuyaingia kwa undani, na isitoshe nilisoma zaidi ya miaka 40 iliyopita hivyo kuna mambo mengi mapya.

Elimu inakua kila siku. Ndio maana wahenga husema Elimu haina mwisho.

RAIA MWEMA: Nani anagharamia masomo yako hayo?

SLAA: Hoja ya nani anagharimikia masomo yangu haina msingi. Ni Watanzania wangapi wanasoma nje ya nchi na hawalipiwi na serikali?

Niliwaeleza naenda sabbatical (likizo ya kitaaluma) na kwa faida ya watu wanaotaka kujiendeleza kielimu, kuna programu nyingi zinazogharimia masomo kama mtu unazo sifa stahiki, ikiwa ni pamoja na gharama ya familia kama itahitajika.

Hata ukienda kwenye balozi mbalimbali jijini Dar es Salaam, unaweza kupata hizo scholarships.

RAIA MWEMA: Ndiyo kusema umeamua kuachana na siasa na kujikita kwenye mambo hayo ya kitaaluma?

SLAA: Suala la kuacha au kubaki kwenye siasa nadhani ni tafsiri tu. Nilisema sitakuwa kwenye party politics (siasa za vyama), lakini nitakuwa mwanasiasa kwa kuzungumzia masuala yenye maslahi kwa taifa langu. Hakuna wa kunifunga mdomo kwenye hili.

Katika wakati huu, malengo yetu makubwa ni kujenga uchumi imara na mifumo sahihi ya utawala katika kipindi hiki na kukosoa pale panapohitaji marekebisho.

RAIA MWEMA: Katika siku za mwanzo za urais wa Rais John Magufuli kulikuwa na madai kutoka kwa vyama vya upinzani kwamba "ameiba sera zao". Una mtazamo gani kuhusu dhana hii ya 'kuiba sera'?

SLAA: Ni vema tukakumbushana malengo makubwa ya Upinzani. Mosi ni kuleta daima mawazo mapya kwa lengo la kuondoa madarakani chama tawala.

Hili litafanyika kwa upinzani kuja na mawazo mbadala ya kumnufsisha mwananchi na mawazo hayo mapya ndiyo yatakayowashawishi wananchi wakati wa uchaguzi kuchagua upinzani ili wanufaike na sera, ilani na dira inayotolewa nao kwa kulinganisha na chama kilichoko madarakani.

Kwa kufanya hivyo, wapinzani hawatabaki kuwa wasindikizaji au wapoteze kabisa maana. Mfumo wa vyama vingi unashindanisha sera, ilani na programu za vyama mbalimbali.

Pili, licha ya Lengo la msingi la kuondoa chama tawala madarakani, mawazo mapya yanayozalishwa na upinzani yana lengo la kumnufaisha mwananchi. Hii ndio faida pekee ya mfumo wa vyama vingi, kwani mfumo wowote wa kisiasa usio na lengo la kumnufaisha mwananchi hauna manufaa yeyote, bali hugeuka wa kibinafsi kwa manufaa ya viongozi husika tu.

Serikali iliyoko madarakani ina haki daima kuyachukua mawazo yoyote bora kutoka popote na kwa yeyote yanayozalishwa na wadau mbalimbali kwa manufaa ya umma (ikiwa ni pamoja na vyama vya siasa) na kuyatekeleza bila hata kuhitaji ridhaa ya aliyeyazalisha.

Serikali makini zinazokuwa sikivu na kutekeleza mawazo hayo mazuri, huviweka vyama vya upinzani kuwa daima wasindikizaji kwa kutekeleza kila wazo jipya wanalotoa.

Wakati wa uchaguzi wanaweza kujikuta wamefilisika kama hawatakuwa na ubunifu mkubwa na kuwa kiwanda cha kuzalisha mawazo mapya kila wakati.

Hii ni changamoto kubwa kwa vyama vinavyofikiria kuwa wanayo hati miliki ya mawazo yaliyoko kwenye hadhara yaani public domain).

RAIA MWEMA: Rais Magufuli amekuwa madarakani kwa takribani miezi minne sasa. Una maoni gani kuhusu utawala wake kwa muda huo?

SLAA: Kwanza, kwa dhati kabisa, napenda kumpa pongezi Rais Magufuli kwa kutembea kwenye ilani aliyoihubiri na ahadi zake binafsi alizozitoa wakati wa kampeni za kutafuta urais.

Wakati naeleza msimamo wangu kuhusu nani anafaa kupigiwa kura sikuficha msimamo wangu. Nilieleza kuwa kwa mtazamo wangu naona JPM (Magufuli) anaonyesha dhamira ya kweli ya kupiga vita ufisadi. Nadhani Taifa linashuhudia jitihada kubwa katika utekelezaji wa ahadi hiyo.

Tatizo mmoja kubwa, ambalo Watanzania tumelipigia kelele kwa zaidi ya miaka 20 ni tatizo la ufisadi. Tumeeleza mara kadhaa kuwa nchi yetu ni tajiri lakini wananchi wake wengi ni masikini wa kutupwa. Si kwa sababu nchi haina rasilimali bali utajiri wa taifa unaishia mikononi mwa kundi la watu wachache.

Tangu Serikali Kuu hadi Halmashauri zetu na hata Serikali za Mitaa na Vijiji; watu wachache wanajinufaisha wakati umati mkubwa unakondeana mahali pengine hata mlo wa siku ni wa shida.

Japo siko Tanzania na napata taarifa nyingi kutoka huko kupitia magazeti, mitandao ya kijamii na marafiki wanaonijulisha mambo mbalimbali yanayoendelea, naamini taifa zima, isipokuwa kundi la watu wachache ambao ama ni wanufaika wa ufisadi na wizi wa mali ya umma au wananufaika kisiasa na ajenda hizo ambazo zina mvuto kwa wananchi –japo wao waliisha kuikimbia ajenda ya ufisadi tangu walipowakaribisha mafisadi miongoni mwao. Wote ni mashahidi wa hatua kubwa zinazochukuliwa katika vita dhidi ya ufisadi.

Ili funufaike na rasilimali za Taifa kuna hatua kadhaa muhimu kama vile kufunga mianya yote ya ufisadi na wizi wa mali ya umma. Hili limefanyika bandari, TRA, Idara mbalimbali na taasisi za serikali. Hii kazi imefanyika kwa kiasi kikubwa, japo mianya bado inajitokeza hapa na pale.

Bunge nalo halijasalimika. Wengine tulikwisha kumtaka CAG afanye ukaguzi maalum wa Bunge letu ambalo kama ilivyoonekana katika Bunge la 10, lilikuwa pipa la kupitisha mali za umma kwa matumizi mabovu ya chombo chenyewe kilichopaswa kuisimamia serikali.

Wabunge, hasa wa upinzani, wamekuwa wakipiga kelele, lakini inapofikia mabilioni ya pesa waliyayotumia wenyewe kwa matumizi ya " hovyo" ikiwemo dalili za ufisadi wa wazi utadhani wanakuwa wamepigwa sindano ya ganzi. Wote kimya na au kupitisha hoja inayowahusu kwa sauti kubwa ya ndiyoooo. Hii ni hatari sana.

Ni marais wachache sana duniani wenye ujasiri wa kuwagusa wabunge, tena kama taasisi. JPM ameonyesha ujasiri wa ajabu hivyo anahitaji kupigiwa makofi ya kumtia moyo huyu shujaa asiyejali hata maslahi yake. Binafsi, nimemvulia kofia Rais wangu !

Najua watu watasema maneno mengi. Namshauri Rais azidi kumtumaini Mungu wake na dhamira yake imuongoze. Mahitaji ya kuondoa umaskini wa Watanzania yamuongoze na mapenzi ya Mungu kwa taifa letu yawe ndiyo dira yake.

Hakuna Taifa Mungu ameliumba liwe maskini, mwandishi mmoja mashuhuri aliwahi kusema; "Viongozi wenu wa Afrika ndiyo wamewafanya maskini na si mapenzi ya Mungu". Wizi na ufisadi uliokuwepo ulikuwa wa kimfumo, hivyo hauwezi kuisha bila kugusa mizizi yake.

Kupiga vita dhidi ya ufisadi na wizi wa mali ya umma vinahitaji mshikamano, dhamira ya kweli, hatua za makusudi na za dhati. Ni vita vya taifa zima kwani tuwe chama tawala, tuwe upinzani tunachopigania ni maslahi ya taifa.

Kama tuna nia ya kweli na hilo ndilo lengo kuu basi tutatofautiana katika njia za kufikia hilo lengo kuu lakini vita ni vyetu wote. Na wala hakuna uadui kati ya chama na chama au mtu na mtu. Tutasimamia misingi yaani principles.

Hatua ya pili ni kuwachukulia hatua wale wote wanaohusika kwa kuwasimamisha kupisha uchunguzi. Wanaoonekana na dalili za kuhusika kufikishwa kwenye vyombo vinavyohusika vya kiutawala na vya kisheria. Hali hiyo imefanyika na inaendelea kufanyika nchi nzima.

Kwa wote tuliokuwa tumevalia njuga vita dhidi ya ufisadi hii ni hatua ya kupongezwa na kuungwa mkono kwa nguvu zote. Hata maeneo ambayo kwa muda mrefu yamekuwa hayaingiliwi, yameguswa.

Haiangaliwi sura ya mtu mapambano yanaongozwa na maslahi mapana ya taifa, kama yalivyoidhinishwa na wananchi kwa njia ya kura zao wakati wa uchaguzi.

Hapa ndipo penye kelele nyingi na wengine tulizitegemea kwani ukiisha kuingilia chakula cha watu ujue kuwa wanufaikaji wote, mmoja kwa mmoja au wale wanaonufaika kwa njia yao ( indirect beneficiaries) au hata " fuata bendera" wanaoburuzwa kwa ushabiki tu.

Hata hivyo, kamanda anayejua ahadi yake kwa wananchi, wajibu wake kwa Mungu wake, kwa taifa lake na dhamira yake hatatishwa na kelele hizo. Kikubwa ni kwa mheshimiwa Rais na watendaji wake asiwe na dhamira ya wazi ya kumnyanyasa mtu bila sababu.

Hatua hiyo ni dhahiri pia itakumbwa na majungu mengi, umbeya, kusingiziana na kuchafuana. Ni kweli katika hatua hiyo wako wachache watakaokumbwa na mtego wa panya ambapo huingia wahusika na wasiohusika.

Lakini huwezi kuacha kuchukua hatua kwa ajili hiyo. Wahenga husema, 'Uamuzi lazima uchukuliwe, tena kwa wakati unaofaa hata kama baadaye utaonekana ni mbaya, utarekebishwa! Hii ndiyo hali tuliyonayo. Mfumo ulikuwa umeoza, ni lazima maamuzi magumu yafanyike, na wakati wa maamuzi magumu siyo wa kubembelezana.

Hatua kubwa ya tatu ni kurekebisha watendaji wakuu wa zile taasisi za ufuatiliaji na za kichunguzi kama PCCB ( Takukuru). Mara ngapi tulipiga kelele kuwa TAKUKURU yenyewe inahitaji kuundiwa TAKUKURU ya kuichunguza?

Hali hiyo ilikuwepo tangu ngazi ya taifa hadi ngazi ya Halmashauri za Miji, Manispaa na Wilaya. Ilihitaji ushujaa mkubwa kuigusa TAKUKURU ili Raisi asiwe pia mpelelezi wa mashauri ya rushwa na wizi wa mali ya umma.

Japo kwa kiwango kikubwa Polisi, Usalama wa Taifa, Idara ya DPP na Mahakama hawajuguswa sana ni imani yangu kuwa punde kutakuwa na "shake-up" (safisha-safisha) kubwa pia ili mifumo ianze kufanya kazi.

Kuna baadhi ya watu walianza kupiga kelele tangu siku ya kwanza baada ya JPM kuanza kuchukua hatua. Ni kweli katika uwanja wa mpira wako ambao kazi ya ni kushangilia sana, wako ambao wanaweza kumpiga jirani teke kwa kuwa mchezaji alikuwa karibu na goli na badala ya kufunga akapaisha mpira juu !

Ebu huyo mtaalamu wa kupiga kelele na kuwasema wenzake apewe mpira na aachiwe goli bila hata kipa tuone kama ataweza kufunga bao.

Namuomba Magufuli asikatishwe tamaa na hao wanaoponda kila analofanya. Tunawajua kwa vile wao –katika wakati muhimu sana waliwakumbatia mafisadi.

Leo wana lipi la kumuambia shujaa wa Watanzania? Mimi namuambia Magufuli kaza moyo au kaza buti wasemavyo vijana.

Ni imani yangu kuwa muda mrefu hautapita kabla nafasi zilizo wazi katika ngazi zote zipate watendaji waadilifu na waliochujwa vizuri kufanya kazi za umma.

Mfumo haujengwi hewani, bali kwa kutumia watu waadilifu, wanaoaminika na wanaowajibika. Kwa kuwa uadilifu, uaminifu na uwajibikaji ni tunu adimu sana iliyoachwa kutekekezwa kwa muda mrefu, unatakiwa uangalifu mkubwa sana katika kuwapata vinara wa kujenga mifumo mbalimbali itakayorudisha taifa letu kwenye reli.

Kwenye miezi yake minne ya kwanza, Rais ameingilia tatizo kubwa linalofanana na kansa katika taifa letu. Tatizo la dawa za kulevya. Mwenye macho au masikio haambiwi tazama au sikiliza.

Kwa muda mfupi, Serikali ya Awamu ya Tano imeingia mpaka kwenye kiini cha tatizo hilo. Magazeti na mitandao ya kijamii ni mashahidi wa idadi kubwa ya watu waliokamatwa katika siku hizi chache.

Na haya yamefanyika kimyakimya. Hakuna kelele. Hivi ndivyo namna ya kupambana na mtandao huu wenye fedha nyingi, silaha na ' network' pana.

RAIA MWEMA: Aliyekuwa mgombea urais wa Chadema na Ukawa, Edward Lowassa, amezungumzia serikali ya Magufuli na kusema haina dira (vision). Unadhani yuko sahihi?

SLAA: Kwanza lazima tukubaliane kuwa Magufuli, japo anafanya kazi kama Magufuli, ni lazima afanye kazi ndani ya mfumo mpana wa CCM. Hivyo Dira ya Msingi ni ileile ya Chama Cha Mapinduzi.

Wengi tunakubali kuwa Tanzania ina mzigo wa maandishi mazuri katika makabrasha ya serikali. Tatizo letu la msingi lilikuwa ni kukosa jemadari shupavu, mwenye ujasiri wa kuchukua hatua hata kama kwa muda itawaudhi baadhi ya watu. Mtu huyu sasa amepatikana na ndiyo maana wengi tumeweka matumaini yetu kwa Magufuli.

Unaweza kuwa na gari jipya, zuri sana lenye 4WD lakini kama huna dereva shupavu hutaweza kuvuka wala kufikisha abiria salama.

Tanzania imebarikiwa kati ya nchi nyingi, siyo tu Afrika, bali duniani kuwa na dereva shujaa na shupavu, dereva asiye na ubinafsi , dereva asiyeangalia na kupima umaarufu wake anaposemwa au anayetafuta sifa kwa kusemwa vizuri tu.

Magufuli ni binadamu na ni dhahiri kwamba kama binadamu yeyote inamtia moyo anapopongezwa na kumtakia heri na mafanikio. Ni kweli wengi wanalalamikia udikteta, lakini katika hatua zote alizochukua sijamwona hata mmoja anayesema kavunja sheria hii au ile.

Aidha katika uozo uliokuwepo kiasi fulani cha udikteta lazima kiwepo lakini kidhibitiwe na Bunge. Check and Balance ni kazi ya Bunge. Watu wanaomkosoa Magufuli wanatakiwa kufanya hivyo kwa kutoa mifano hai na si bla bla.

Hatua ya pili ni mtazamo wake Magufuli kama mtu na Rais. Hilo Magufuli hataki mnyonge anyanyaswe. Anataka rasilimali za taifa zishuke chini kumnyanyua Mtanzania wa kawaida. Ebu tuwe wakweli, kuna vision gani watu wanataka zaidi ya hayo!

Hicho ndicho siku zote, tukiacha wakati wa Mwalimu, kimewashinda viongozi wote waliofuata. Taifa likageuzwa kuwa 'Shamba la Bibi'. Watanzania hawana shida na nadharia kwani ziko nyingi. Wanataka sasa utendaji wenye manufaa kwao.

Na Magufuli ameeleza siyo tu dhamira yake kubadilisha hali hiyo, bali ameanza kuchukua hatua stahiki; elimu ya bure hadi kidato cha nne na anaitekeleza kwa bajeti aliyoikuta.

Bajeti yake na mwelekeo wake halisi tusubiri bajeti yake ya kwanza katika Mkutano wa Bunge ujao. Lakini dalili ya awali imeonekana na amefanya hivyo bila kuongeza kodi kwa mwananchi wa kawaida, bali amesimamia tu mapato halisi ya serikali kwa kutumia sheria za kodi zilizoko.

Magufuli ameelezea kukerwa na hali ya barabara na usafiri Dar na kwenye miji yetu mbalimbali. Hatua zimeanza kuchukuliwa kwa kutengeneza barabara ya kilomita nne alizookoa kutoka yaliyokuwa maadhimisho ya siku ya Uhuru.

Ebu piga hesabu sherehe zote, semina zote alizofuta, safari za nje za mawaziri na wabunge alizofuta au kuzidhibiti! Hatua hii ya kuokoa fedha kutoka kwenye matumizi ya anasa kwa peke yake ni hatua ya kinidhamu ya hali ya juu, lakini pia ni vision ya pekee kuelekeza fedha zinazookolewa kwenye "huduma za jamii.

Mimi binafsi nimefurahi sana kwani miaka mingi, na niko on record japo nilichekwa na kukejeliwa kuwa sitahudhuria sherehe yeyote ile ya ulaji na kujenga personality cult bali niko tayari kushiriki Maadhimisho ya Kitaifa .

Sikuwahi kuhudhuria sherehe wala dhifa yeyote, kwani dhamira yangu ilikataa ulaji- sikuhudhuria bali nilisisitiza kuwa nitashiriki yanayosherehekewa kwa kufungua miradi ya maji, Afya, barabara za vijijini, shule mbalimbali.

Kuna wakati huwa ninajiuliza, hivi hawa viongozi waliomtangulia Magufuli kweli walikuwa na mioyo ya nyama au walikuwa wakibeba mawe kwenye vifua vyao? Mtu na akili zako na dhamana yote uliyobeba, unafanyeje sherehe ya Siku ya Ukimwi kwa ulaji wa masaa tu wenye kugharimu mabilioni?

Tulifanya hivyo wakati ndugu zetu walioathirika hawana dawa za kurefusha maisha (ARV) ambazo ni muhimu kurefusha maisha yao, au kuwapatia chakula ili kupambana na nguvu ya dawa ambayo miili yao iliyodhoofu haiwezi kuhimili tena !

Tulikosa siyo tu vision, bali busara ya kawaida, upendo kwa Watanzania wenzetu na kutazama zaidi matumbo yetu. Tazama nani mlalahoi hualikwa kwenye sherehe hizo za ulaji kama siyo wafunga tai? Sawa, sherehekeeni kwa hela zenu lakini siyo kwa gharama ya uhai wa Watanzania.

Tutafakari, ni ng'ombe wangapi, mayai mangapi huchangishwa kwa nguvu kutoka kwa wananchi ambapo wengine hulala rumande au kufungwa kwa kushindwa kutoa mchango huo ambao kimsingi hauko kisheria?

Lakini wanapokeshea Mwenge kreti ngapi za bia huteketezwa kwa usiku mmoja tu?? Ni mwananchi gani hupewa hata soda kama siyo hukesha kwa kuimba na kucheza ngoma zao wakati wenzao wakijichana?

Huu ulikuwa ni uwendawazimu tu. Anayesema kufuta haya siyo vision yeye ana vision ipi au turudi kwenye kamusi kutafuta maana halisi ya neno " Vision"?

Magufuli siyo tu, amefuta sherehe bali fedha zote zinaelekezwa kwenye miradi inayomgusa mwananchi. Kama hatuna la kusema jamani au kama ametufilisi basi ni bora kunyamaza tu kuliko kufanya upotoshaji.

Serikali ya Awamu ya Tano tayari inazungumzia fly- overs Dar, barabara pana ( six lane), reli ya kisasa, kupunguza ofisi za serikali katikati ya mji na kujenga satelite cities (miji ya pembezoni). Hii haiwezi kuja kama hakuna vision. Marehemu Mzee Abeid Karume, Rais wa SMZ aliweza wakati ule kujenga nyumba kwa ajili ya Walalahoi ambazo ziko hadi leo.

Kwa ulafi wetu sisi tumegeuza hata shirika letu la NHC kuwa mrija kwa ajili ya wenye uwezo. Mabadiliko haya ndiyo kinachoitwa vision kama kuna aliyekuwa hafahamu.

Aidha vision pia hutafsiriwa kwa njia ya bajeti na kwa kuwa sijaona bajeti ya Magufuli siwezi kuizungumzia. Lakini naamini mifano hiyo michache ni kielelezo cha kutosha kuwa Rais wetu anayo vision anayoitekeleza.

RAIA MWEMA: Wakati ukiwa kinara wa siasa za upinzani, mlikuwa maarufu kwa kuibua kashfa na uozo serikalini ambao sasa umepachikwa jina jipya la majipu. Siku hizi, Magufuli na viongozi wa chama tawala ndiyo wanaotumbua hayo majipu.

Ili upinzani uendelee kuwa imara hapa nchini, unadhani nini wanatakiwa wafanye maana kwa majipu tayari serikali inaonekana kufanya kazi hiyo?

SLAA: Sidhani ni wakati mwafaka kwangu kushauri upinzani. Watanzania wanajua kwanini niliondoka Chadema. Nilishikilia principles za msingi ! Hizo principles zinabaki na kila ninapopata nafasi nitaendelea kuwapiga vita mafisadi popote watakapokuwa, iwe kwenye Upinzani au Chama Tawala.

RAIA MWEMA: Uliwahi kuwa mgombea urais wa upinzani mwaka 2010 na watu walitaraji pengine ungekuwa mgombea wa Ukawa mwaka 2015 kabla ya ujio wa Lowassa.

Kama ungewania urais mwaka jana na kushinda, kuna mambo gani ambayo ungeyafanya tofauti na anavyofanya Magufuli sasa?

SLAA: Kama ningelikuwa mimi Rais wa Tanzania ningelifanya nini tofauti? Watanzania wengi wanajua vision na mtazamo wangu tangu mwaka 2010 na hata kwenye ziara zangu mikoani na vijijini kuanzia mwaka 2011 hadi 2015.

Nimezunguka nchi nzima mijini na vijijini. Watanzania wanajua nilisimamia nini na bado nasimamia nini. Kwa Kuwa Rais wangu anayatekeleza na mengine ambayo hata mimi sijayasema, wajibu wangu sasa ni kumpa nafasi ya kutekeleza hiyo vision yake kwa manufaa ya Watanzania.

Patakapohitaji niwe mkosoaji nitafanya hivyo kwa uhuru kamili, kwa kuwa mimi sifungamani na chama chochote. Yeyote atakayesimama upande wa Watanzania nitamwunga mkono, kwani dhana ya vyama vingi siyo kutengeneza cartel (makundi ya kimaslahi) bila sababu za msingi.

Chama cha siasa kije na sera zake na tukiona ni sera nzuri kwa manufaa ya taifa hatutaogopa kuziunga mkono bila kujiunga na chama chenyewe. Ule msemo wa kuwa "Tutafanya mkataba na shetani, kama mkataba huo utatufanya kuindoa CCM". Mimi siyo wa jamii hiyo.

Nawatakia Watanzania kila la kheri katika safari ya ukombozi wa taifa letu

Raia Mwema

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments