[wanabidii] Wanasiasa hawa wachukuliwe hatua za kinidhamu

Saturday, November 21, 2015
WALIOWAHI kushika nyadhifa kubwa serikalini wanapotosha vijana wetu katika majukwaa ya kisiasa kwa manufaa yao binafsi ya kisiasa.Hakika taifa letu limepata ufa mkubwa wa kimaadili kutokana na lugha mbalimbali zinazotolewa na viongozi wastaafu wa taifa ambao tulitarajia kuwa wao ndiyo kioo au dira ya taifa kwa kushika nyadhifa kubwa kama Uwaziri Mkuu.

Taifa linapofikia mahala kiongozi aliyewahi kuwa Waziri Mkuu anasimama jukwaani na kuthubutu kuudanganya umma na hasa vijana wetu wenye umri wa miaka kati ya 18-30 ili ajinufaishe kisiasa kwa kutarajia kupata wafuasi wengi atakaonufaika nao kwa kuwatumia kupata kura nyingi katika chaguzi za kitaifa na hasa nafasi ya urais, ni dalili za uvunjifu wa amani nchini kwani vijana wetu wenye umri huo 35 wengi wao hawaijui vizuri historia ya taifa hili hivyo ni rahisi kuwadanganya.

Lakini wewe kama mzazi mwenye umri wa miaka zaidi ya 60 unapothubutu kuwadanganya watoto wa wenzako ambao wengine ni mayatima au wengine hawawajui baba zao hawakupata bahati ya kulelewa na wazazi wao wa pande mbili, je, unawajenga au unawabomoa watoto hao kwa mujibu wa maadili ya taifa, kama unathubutu kuwadanganya watoto hao basi mbele ya mwenyezi unafanya makosa, pia unahatarisha maisha ya watoto hao kwa kuwa wanaweza kuchukua uamuzi ambao hawajui madhara yake na baadaye wakajuta kwa sababu umewadanganya.

Kwa mfano, kama Waziri Mkuu mstaafu aliyewahi kuitumikia nafasi hiyo nyeti kwa miaka 10 kama Frederick Sumaye na kusema kuwa Serikali ya CCM haijafanya kitu chochote cha maendeleo kwa muda wa miaka zaidi ya hamsini (tangu uhuru 1961 ? 2015) na Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashifa ya Richmond, Edward Lowassa na mmoja kati ya wazee wanaoijua vizuri historia ya TANU/CCM mzee Kingunge Ngombale Mwiru wapo jukwaani wamekaa kimya kuushuhudia uongo huo wa wa Fredrick Sumaye bila kumkemea, badala yake wanamshangilia hii ni ishara mbaya kwa Tanzania.

Sumaye amekuwa Waziri Mkuu kwa muda wa miaka kumi kuanzia 1995 ? 2005 chini ya Rais Benjamini Mkapa katika utawala wa awamu ya tatu na kuvunja rekodi ya mawaziri wakuu wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kukaa na cheo hicho kwa muda mrefu kuliko mawaziri wakuu wote tangu uhuru wa Tanganyika /Tanzania (1) Mzee Rashid Kawawa, Edward Sokoine, Cleopa Msuya, Joseph Warioba, John Malecela, Salim Ahmed Salim, Edward Lowassa na sasa Mizengo Pinda, cheo cha uwaziri mkuu ni cheo kikubwa kwa kuwa wewe ndiye bosi wa mawaziri wote na mshauri mkuu wa rais katika masuala yote yanayohusu serikali.

Sumaye huyu huyu amekuwa akitoa kashfa nyingi kwa Serikali ya CCM kuwa haijafanya kitu kwa miaka 50 madarakani akijumlisha na miaka yake kumi akiwa Waziri Mkuu wa Serikali ya CCM, aliongoza kama Waziri Mkuu chini ya Mkapa, wakiwamo katika baraza la mawaziri rais aliyemaliza mihula yake madarakani, Jakaya Kikwete kwa wakati huo akiwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Lowassa akiwa Waziri wa Aridhi na wizara zingine katika serikali ya awamu ya tatu.

Sumaye katika kipindi cha Uwaziri Mkuu wake ndiye aliyechangia kwa kiasi kikubwa kuanza kwa ufisadi wa mali za umma na kusababisha Watanzania wengi kukosa ajira kwa kuziuza NBC, ATC na mashirika mengi. Kuwakaribisha makaburu wa Afrika Kusini kuja kumiliki uchumi wetu na kuvuruga kwa kuliipiza kisasi kwa Tanzania kuwasaidia wapigania uhuru wa nchi za kusini mwa Afrika, kwa mfano Shirika la Ndege la Tanzania (ATC), shirika hili lilikuwa likifanya vizuri kibiashara katika awamu ya kwanza ya MwalimuJulius Nyerere, Waziri Mkuu akiwa Sokoine na mzee Ali Hassan Mwinyi, awamu ya pili na mawaziri wakuu Warioba, Malecela na Msuya.

Katika kipindi ambacho serikali ya awamu ya kwanza na ya pili, shirika hilo lilikuwa na ndege zaidi ya sita zilizokuwa zikiruka hapa nchini na nje ya nchi, Sumaye alipokuwa Waziri Mkuu ndiye aliyeanza mchakato wa kuliuwa shirika hilo kwa kuanza kufanya mazungumzo na Ami Mpungwe aliyekuwa balozi wetu Afrika Kusini na kufanya mazungumzo na viongozi wa South African Airways lililokuwa chini ya makaburu katika nyadhifa zote za uongozi wa juu.

Baada ya makaburi kufanikiwa kununua hisa nyingi za shirika hilo kupitia kwa Fredrick Sumaye akiwa Waziri Mkuu, wakati huo Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi akiwa Profesa Mark Mwandosya, Katibu Mkuu wake akiwa Salim Msoma, Mwenyekiti wa bodi Balozi Abbas Sykes na Mkurugenzi Mtendaji Mkuu, Emmanuel Kimaro, hapo ndipo makaburu walipoanza rasmi kuliua shirika hilo kwa kuiamuru menejimenti ya Air Tanzania kupunguza wafanyakazi wake na hasa marubani na mafundi, wakalazimishwa kupunguza marubani 15 na wahandisi 30, makaburu wakishirikiana na Sumaye na Ami Mpungwe wakaiamuru tena ATC iuze ndege zake Boeing na fokker huo ndiyo ukawa mwisho wa ATC kufanya vizuri katika sekta ya anga.

Kwa kuwa Sumaye ameitukana Serikali ya CCM kipindi cha kampeni za Uchaguzi Mkuu, kuwa ni dhaifu, legelege na haijafanya kitu kwa zaidi ya miaka hamsini, viongozi niliowataja bahati nzuri wako hai, waitwe chini ya Profesa Mwandosya na mzee Abbas Sykes watoe taarifa rasmi juu ya suala la ATC/NBC na mashirika mengine nyeti kwamba yamedhoofishwa na Sumaye akiwa Waziri Mkuu. Itakumbukwa kwamba NBC ilileta tafrani kubwa ya kuuzwa kwake kwa kuwa ilikuwa ikijiendesha kwa faida na pia ilikuwa ndiyo benki yetu ya taifa ya biashara, hakukuwa na sababu ya kuuiuza kwa bei ya kutupa kwa makaburu wa Afrika Kusini ambao, inawezekana, walimrubuni Sumaye kwa nguvu ya ushawishi wowote ili wainunue benki hiyo na kuisambaratisha kama walivyofanya kwa ATC, Sumaye akiwa Waziri Mkuu wa Serikali ya CCM anayoitukana katika majukwa ya siasa.

Sumaye huyu huyu amejinyakulia mashamba makubwa na ranchi za mifugo katika sehemu mbalimbali za nchi kwa manufaa yake na familia yake, ana sahau kuwa CCM ilimpa nafasi ya Uwaziri Mkuu akiwa na elimu ndogo kama Form Six na Shahada ya Afisa Kilimo wa ngazi ya kawaida na pia ametoka kwenye familia maskini huko Hanang Arusha na amesomeshwa na Serikali ya TANU/CCM bure hadi kidato cha sita wazazi wake hawakuwa na uwezo wa kumlipia ada.

Kwa kuwa anamtukana baba wa taifa na viongozi wote waliokuwa madarakani wakati huo yeye akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi na sekondari, usalama wa taifa waende Hanang wakapate taarifa rasmi ya maisha yake na utajiri aliokuwa nao baada ya kuwa Waziri Mkuu katika Serikali ya CCM anayoitukana leo bila haya.

Sumaye huyu hajijui kuwa katika mawaziri wakuu wastaafu yeye ndiye mwenye sifa ya kupungukiwa hamasa ya fikra (Mr. O), amekuwa akiropoka kama kasuku alichoongea asubuhi, jioni ataongea kitu tofauti bila ya kuwa na kumbukumbu ya matamshi yake mwenyewe. Mzee Benjamini amembeba kwa miaka kumi kwa upendeleo wa hali ya juu bila ya kujali lawama na ushauri aliokuwa akiupata kwa viongozi mbalimbali kuwa ambadilishe huyo anakuharibia serikali yako lakini mzee Mkapa aliweka pamba masikioni kumlinda Sumaye katika wadhifa huo ambao haukulingana na akili yake.

Sumaye hajui hata historia ya Tanganyika/Tanzania kwa masuala ya maendeleo ya kuleta uhuru na Muungano, kuondoa udini/ukabila na umoja wa kitaifa, kushiriki kikamilifu kulikomboa bara la Afrika kutoka mikononi mwa tawala za kidhalimu barani Afrika kuanzisha East African Community, kuanzisha SADC, kuwasaidia ndugu zetu waliokuwa chini ya utawala wa kidhalimu wa Idd Amin Dada aliyefanya mauaji mengi kwa Waganda wasiokuwa na hatia na hasa wasomi, Serikali ya CCM imeunda jeshi imara na lenye uadilifu chini ya marehemu Edward Sokoine akiwa Waziri wa ulinzi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yeye ndiye aliyemshauri Mwalimu Nyerere kuanzishwa kwa majeshi ya Anga na Majini MAJINI (AIRFORCE/NAVY) kwa ajili ya ulinzi wa anga na bahari na makombora ya masafa marefu.

Sumaye kaa chini tafakari juu ya maisha yako tangu utotoni hadi ulipo sasa hivi ulitoka wapi na ulikuwa na maisha gani huko nyuma kabla ya kuanza kutukana na kujitukana bila ya kujijua, elewa kuwa hata wanao kama wana busara watakudharau tu.

Wewe ulipokuwa CCM na Lowassa ulikuwa unamkashifu sana Lowassa kuwa ni fisadi mkubwa na wenzake kadhaa na ukatishia kwamba endapo CCM itamsimamisha Lowassa kuwa mgombea urais wake utakihama chama hicho, na kuelekea sehemu nyingine ambayo haiwakubali mafisadi kama Chadema, lakini kinyume chake, bila ya aibu kwa Watanzania unamkumbatia Lowassa na kumsifu kuwa anafaa kuwa rais eti apatiwe kura kura nyingi atawaondolea umasikini Watanzania, sisi kama watu wazima na akili zetu tukueleweje?

Fredrick Sumaye, Lowassa uliyekuwa unamsema kuwa fisadi mkubwa na mla rushwa ni Lowassa mwingine au yule yule?
Fredrick Sumaye hustahili kuaminika hata kidogo mbele ya jamii, umeweka mbele maslahi yako na wala siyo maslahi ya taifa kwa jumla au ya chama hufai kuwa mwanasiasa kwa kuwa wewe ni hatari, unaweza kuliingiza taifa katika matatizo makubwa, serikali iwapige marufuku wanasiasa wenye tabia kama za Sumaye, kwani hata CCM hakuondoka kwa kupenda bali ni kwa sababu ya kutopendekezwa jina la mgombea urais wa CCM wa 2015, hii ndiyo ilikuwa sababu kubwa ya Sumaye kuondoka CCM na kuanza kuwatukana CCM na viongozi wake kuanzia Mwalimu Nyerere hadi Jakaya Kikwete.

Binafsi hadi sasa, nadhani Rais bora zaidi kuwahi kutokea Tanzania ni Mwlaimu Julius Nyerere na Waziri Mkuu bora zaidi kuwahi kutokea hadi sasa ni Edward Sokoine. Lakini vile vile, Waziri Mkuu anayeweza kudharaulika miongoni mwa mawaziri wakuu wote ni Frederick Sumaye.

Mwenyezi Mungu ibariki TANZANIA

Mwenyezi Mungu ibariki AFRIKA

Mwandishi wa makala haya Japhet Mwandimo ni Mwanajeshi mstaafu wa Jeshi la Anga la Wananchi wa Tanzania. Anapatikana kwa simu 0785 042078

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Related Posts

0 Comments