Ndugu zangu,
Kubwa linalozungumzwa mitaani kwa sasa ni jina la Waziri Mkuu ajaye. Hakuna ajuaye, ni John Magufuli anayetembea nalo mfukoni jina hilo. Na Afrika Rais kumteua Waziri Mkuu ina maana ya kumteua mtu atakayemwamini katika kumtanguliza mbele. Ina maana ya rais kulitafuta ' tingatinga' lake. Mtu wa kuwa tayari kujitoa muhanga au kutolewa kafara, inapobidi.
Waziri Mkuu ambaye, anayoyafanya yana baraka ya Rais,, yakipokewa vizuri na wananchi, asiwe waziri Mkuu anayejipeleka mbele kuzisomba sifa na kumfunika Rais wake. Awe Waziri Mkuu jasiri na mnyenyekevu pia, kwa rais na wananchi. Asiwe mtu anayefikiria kuwa Waziri Mkuu na kisha awe Rais, kazi hiyo itamshinda. Na lazima awe mwadilifu na asiye na tamaa ya kujilimbikizia mali.
Mwalimu Nyerere alipong'atuka alipata kumwelezea rafiki yake Rashid Kawawa. Alitamka; " Huyu Rashid huyu sidhani kama kuna mtu mwingine anayeweza kufanana naye."
Mwalimu alimmwagia sifa nyingi Rashid Kawawa ikiwemo moja kubwa ya uvumilivu. Rashid Kawawa ama maarufu kama ' Simba wa Vita' alipata kuwa Waziri Mkuu wakati wa uongozi wa Mwalimu.
Ndio maana ya kusema pia, kuwa Afrika cheo cha Uwaziri Mkuu ni sawa na binadamu kugeuzwa ' Tingatinga', tena lenye mabawa. Kazi ya tingatinga ni kutangulia mbele kusafisha njia. Waziri Mkuu hutangulia mbele. Atakayofanya yakiwa mema hachelewi kutamka; " Jamani haya yote yanatokana na hekima na busara za Kiongozi Mkuu" - Na Afrika hakuna anachofanya Waziri Mkuu bila Kiongozi Mkuu kujua na zaidi kutoa baraka zake.
Na mambo yakienda kombo?
Waziri Mkuu anapaswa kuyakabili madongo na mawe yote yatakayorushwa. Ahakikishe kuwa Rais haguswi na madongo hayo. Waziri Mkuu asiwe ni mtu mwenye kusubiri shukrani. Na hakika, historia ni mwalimu mzuri. Nimekumbushia hilo mara kwa mara. Kwenye tawala za Kifalme, Mfalme au Malikia ndio wenye kulindwa na yote, Waziri Mkuu ndiye mbeba lawama.
Kabla ya kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Winston Churchill alipata kuwa waziri wa masuala ya majini ( Marine Minister). Ilikuwa ni wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Winston Churchill ambaye pia alikuwa askari mwanamaji, aliacha ofisi yake na kuongoza vikosi vya wanamaji katika vita hivyo. Na hata baada ya vita kwisha, Churchill akafanywa kuwa 'Waziri wa Vita' ( Defence Minister). Baadae, Winston Churchill akaja kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza.
Pamoja na ukweli, kuwa Winston Churchill aliiongoza vema Uingereza na hata kuweza kufanikisha ushindi katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia, bado, Waingereza hawakumchagua Winston Churchill katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1945. Inaweza kusemwa, kuwa wapiga kura wa Uingereza hawakuwa na shukrani. Kwamba wapiga kura wa Uingereza hawakumpima Churchill kwa historia bali kwa yatakayokuja. Kuna cha kujifunza.
Yumkini shingo zetu wanadamu ni ndefu, lakini maisha yetu ni mafupi sana. Ndio, muda wetu wa kuishi humu duniani ni mfupi sana. Na historia itabaki kuwa hakimu kwa tunayoyafanya sasa. Maana, wengi wetu tunaishi na kuziacha nchi zetu tulizozaliwa hata kabla hatujatimiza miaka 80 humu duniani. Lakini nchi tulizozaliwa tunaziacha zikiwa na wanadamu wenzetu. Ni watoto wetu, ni wajukuu zetu. Na sisi Waafrika tumekuwa ni watu wabinafsi sana. Ni watu tunaoishi bila kufikiria sana ya kesho na kesho kutwa. Tunajiangalia sisi tu.
Sehemu kubwa ya matatizo ya nchi zetu hizi yanatokana na ubinafsi huo. Na bahati mbaya kabisa, baadhi ya viongozi tuliowapa dhamana za uongozi ndio wenye kuongoza kwa matendo yenye kutanguliza maslahi yao binafsi. Kwetu sisi Watanzania hali yetu ya kiuchumi bado duni mno. Ufisadi unalitafuna taifa letu. Tuna lazima ya kukumbushana ukweli huu, maana, tukifanya masihara taifa letu liko katika hatari ya kuingia katika hali ya machafuko makubwa. Ili kuunusuru uchumi wetu usiyumbe zaidi tuna lazima ya kutumia fedha na rasilimali zetu kwa busara kubwa. Kuna busara ya kutomuiga tembo kwa lolote lile. Mengine afanyayo tembo yanatokana na ukumbwa wa maumbile yake. Tunahitaji Waziri Mkuu wa watu, ambaye si mpenda makuu na mwenye ujasiri wa kufanya anayoyaamini ni ya maslahi kwa umma.
Maggid,
Unapokea Email hizi kwa sababu umejiunga na Jukwaa la 'Mabadiliko'.
Kuchangia mada tuma kwenye Email hii: mabadilikotanzania@googlegroups.com
For more options, visit this group at:
http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania?hl=en?hl=en
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Mabadiliko Forum" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to mabadilikotanzania+unsubscribe@googlegroups.com.
To post to this group, send email to mabadilikotanzania@googlegroups.com.
Visit this group at http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania.
To view this discussion on the web visit https://groups.google.com/d/msgid/mabadilikotanzania/CAMD-ye71TKiv5o06hXUaJrLWbSd2Q_SSR33iQcUUoxs4sZUsBA%40mail.gmail.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 Comments