[Mabadiliko] HONGERA UKAWA MPEIPA NCHI SOMO

Friday, November 06, 2015
HONGERA UKAWA MPEIPA NCHI SOMO

Na Ananilea Nkya

Baada ya uchaguzi mkuu kukamilika, Watanzania wote wanaopigania mabadiliko ili kila baada ya uchaguzi nchi yetu ipate uongozi uongozi utakaowezesha mamilioni ya Watanzania wanaoteseka kwa umaskini kuondokana na umaskini wao, bila shaka watavipongeza vyama vinanyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi UKAWA.

UKAWA wametoa somo kubwa kwa nchi yetu kuhusu changamoto kuu zinazokabili nchi yetu kufikia uchaguzi huru na wa haki kama nitakavyoeleza katika makala hii.

Aidha wanachama na viongozi wa CCM ambao waliamua kuchukua maamuzi magumu kuondoka katika chama hicho na kuungana na UKAWA katika kupigania mabadiliko nao wanastahili pongezi kubwa.

Miongoni viongozi hao ni Edward Lowassa aliyekuwa mgombea Urais CHADEMA –UKAWA ---ambaye ushawishi wake wa kisiasa umeacha historia ya aina yake katika uchaguzi wa vyama vingi Tanzania.

Wengine Mzee Kingunge Ngombale Mwiru, Waziri Mkuu mstaafu Mheshimiwa Fredrick Sumaye na Waziri wa Mambo ya Ndani mstaafu Lawrence Macha.

Viongozi hawa wamejitoa mhanga kukubali kujishusha na kuwa sehemu ya harakati za wananchi kutafuta mabadiliko ya kunufaisha walio wengi.

Tena wamejitoa bila kujali kudhalilishwa kwa matusi na kunyanyaswa na vyombo vya dola kama wanavyonyanyaswa wananchi wa kawaida.

Ninaamini ni watu wasioitakia mema Tanzania na wasiojali maslahi ya Watanzania wengi ndio pekee watawabeza viongozi hawa kutokana na uamuzi wao wa kuungana na wana mabadiliko.

Lakini Watanzania wanaoelewa vema mchango wa uongozi katika harakati za ukombozi watawapongeza na kuwatia moyo viongozi hawa waliojitoa mhanga na kuthamini mchango wao katika kupigania maslahi ya Watanzania walio wengi maana bila viongozi kujitolea ili kuleta mabadiliko, mabadiliko hayawezi kupatikana.

Zaidi ya yote vyama vinavyounda UKAWA ambavyo ni NLD, NCCR-Mageuzi, CHADEMA Nna CUF vinastahili pongezi kubwa kwa sababu umoja wao katika uchaguzi wa mwaka huu umetoa somo jipya katika siasa za vyama vingi Tanzania.

Jambo moja kubwa ambalo UKAWA wamewathibitishia Watanzania ni kwamba vyama vya upinzani vikishirikiana kwa dhati na kujiandaa vema kupata viongozi makini na wenye dhamira ya kweli ya kuleta mabadiliko kweli ya kunufaisha mamilioni ya Watanzania maskini, wanashinda uchaguzi kwa kura nyingi.

Jambo muhimu zaidi sana ambalo UKAWA wametoa somo kwa Watanzania katika uchaguzi huu ni kwamba nchi yetu bado ina safari ndefu kufikia uchaguzi HURU NA WA HAKI unaowesha mshindi kutangazwa mshindi na si vinginevyo. Je amani inaweza kutamalaki kwenye jamii yetu kama uhuru na haki kwenye uchaguzi vitaendelea kuchezewa kwenye uchaguzi?

Swali hili msingi wake ni mgogoro ulipo sasa kuhusu kutotangazwa kwa matokeo ya mshindi katika uchaguzi wa Urais Zanzibar na UKAWA kutokukubali matokeo ya Urais.

UKAWA katika uchaguzi huu wametoa somo kwamba kuna matatizo makubwa matatu yanayokwamisha uchaguzi huru na wa haki Tanzania. Mambo hayo ni haya:
1) Walioko madarakani kutokuwa na dhamira ya dhati (political willingness) kuona mfumo wa siasa za vyama vingi ukistawi na kuleta manufaa kwa mamilioni ya Watanzania wanaoteseka kwa umaskini nchini. Dhamira inakosekana kutokana walioko madarakani kunufaika na kuwepo kwao madarakani.
2) Mifumo ya kisheria na kitaasisi iliyokuwa inatumika kutawala wakati wa mfumo wa chama kimoja cha siasa kuendelea kutumika katika mfumo wa vyama vingi hivyo kunufaisha chama kilikuwa madarakani.
3) Vyombo vya dola kutumika kisiasa kunyanyasa wananchi wanapodai haki ya uchaguzi huru na wa haki.

Hivyo matatizo haya yasipotafutiwa ufumbuzi wa kikatiba kabla ya uchaguzi mwingine 2020 tbila shaka idadi ya wapiga kura ikapungua sana uchaguzi ujao kutokana na wanachi kukata tamaa kwamba uchaguzi hauna manufaa yoyote kw amaisha yao.

Lakini kibaya zaidi tusishangae umaskini ukiongezeka mara dufu miongoni mwa mamilioni ya Watanzania tuendako maana hata kama serikali ya Rais John Magufuli itafanya kazi kubwa na kuweza kukuza uchumi kutoka asilimia saba (7%) ilivyo sasa na kufikia asilimia kumi na tatu (13%) huenda uchumi huo usiwanufaishe Watanzania wengi wanaoteseka kwa umaskini.

Hii ni kutokana Katiba na mifumo ya kiutawala iliyopo nchini hivi sasa kutoa mwanya kwa watawala kujitajirisha zaidi wao wenyewe kwa fedha na mali za za nchi huku mamilioni ya Watanzania wakibaki maskini wa kutupa.

Kwa hiyo kazi kubwa aliyonayo Rais Dr John Magufuli, UKAWA, vyama vingine vyote vya siasa na Watanzania wote ni kutafakari hatma ya mamilioni ya Watanzania wanaoteseka kwa umaskini kwa kuzingatia hayo matatizo matatu niliyoyaainisha hapo juu. Mungu Ibariki Tanzania.

Note: Ninaridhia anayetaka kuchapisha andiko hili afanya hivyo lengo likiwa ni kujifunza tuijenge nchi yetu nzuri Tanzania.






Ananilea Nkya
 E-mail:ananilea_nkya@yahoo.com

--
Unapokea Email hizi kwa sababu umejiunga na Jukwaa la 'Mabadiliko'.
Kuchangia mada tuma kwenye Email hii: mabadilikotanzania@googlegroups.com


For more options, visit this group at:
http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania?hl=en?hl=en
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Mabadiliko Forum" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to mabadilikotanzania+unsubscribe@googlegroups.com.
To post to this group, send email to mabadilikotanzania@googlegroups.com.
Visit this group at http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania.
To view this discussion on the web visit https://groups.google.com/d/msgid/mabadilikotanzania/1962723928.787313.1446818393904.JavaMail.yahoo%40mail.yahoo.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Related Posts

0 Comments