Lula wa Ndali Mwananzela
MOJAWAPO ya mambo ya kutisha zaidi kutoka katika historia ya kisiasa ya nchi yetu ni hii hamasa ambayo baadhi ya ndugu zetu wamekuwa nayo ya kumshabikia Lowassa wengine wakiapa kabisa kuwa wanataka awe Rais wetu.
Tunaaminishwa kuwa sasa harakati za mabadiliko zimepata kiongozi anayeweza kuziongoza kweli kweli na kuwa kiongozi huyo siyo tu anaweza kuziongoza bali pia anapaswa kuziongoza. Na katika hili ndugu zetu hawa wanajaribu kuwaaminisha kuwa nafasi pekee ya mtu huyo kutuongoza ni urais na katika hili wanaonekana wametia pamba masikioni.
Ndugu zetu hawa wanatushangaa inakuwaje sisi wenzao ambao wengine tulijipambanua kuwa ni watu tunaotaka mabadiliko sahihi, makini na ya kweli leo hatujadandia hili treni na hatujatoroka twende huko aliko na sisi tuwepo. Wanatushangaa – hawashangai tunavyowashangaa wao kutushangaa – ati imekuwaje leo "nafasi" hii ya mabadiliko imetokea na sisi ambao tulidai sana mabadiliko hatuirukii na kuishangilia.
Jibu lake mojawapo ni kuwa hawataki kuamini kuwa sisi tunatambua au tumetambua ulaghai ulipojitokeza. Tumeelewa siasa katika kipeuo chake cha chini kabisa – ulaghai wa kisiasa. Tumetambua kuwa nafasi ya mabadiliko ya kweli imepoteza pale ambapo watu tuliowaamini kuongoza harakati hizi walipoamua kugeuka na kubinafsisha mabadiliko kiasi kwamba tunaogopa kama Lowassa akishinda chama kitakachoongoza kitakuwa ni Chadema au Lowassa.
Dalili zote zinaonesha (nazilionesha mapema tu) kuwa Lowassa siyo kiongozi wa kuweza kusimamiwa na chama cha siasa. CCM pamoja na nguvu zake zote na uwezo wake wote ilishindwa kumsimamia Lowassa na kumdhibiti kiasi kwamba ilibidi itumie kichinjio maalumu kummaliza kisiasa na kuwaachia wengine wahangaike naye.
Wenye kuamini kuwa Chadema chenye udhaifu wa uongozi sasa kitapata shida sana kuweza kumdhibiti mtu ambaye hata hivi sasa tu kampeni yake inaonekana kuwazidi nguvu kuisimamia. Kuna tetesi kuwa ni watu wa
Lowassa hasa ndio wenye kuisimamia kampeni hiyo na hata wakongwe wa chama wakitaka baadhi ya mambo inabidi wawapitie watu hawa. Fikiria itokee ashinde uchaguzi; kuna wana Chadema watakuja mbele ya wananchi na machozi kutuambia "tulifanya makosa tulipoisaliti damu isiyo na hatia". Wakati huo itakuwa wamechelewa.
Lakini kwa vile tunawapenda ndugu zetu wa Chadema na hasa wale ambao wameshiriki kwa kiasi kikubwa kuchochea mabadiliko ushauri wangu kwa Watanzania wapiga kura na wanaotaka kweli kuisaidia Chadema na wanaompenda sana Lowassa awaongoze basi wafanye jambo makini na la lazima na mimi nitawaunga mkono – wampe Lowassa uongozi wa
Chadema kwa kumkatalia Ikulu ili akiongoze chama hicho.
Kwa vile watu wanaamini Lowassa kweli amekuwa ni mtu wa mageuzi na amekubali ajenda za mabadiliko njia pekee ya kumpima itakuwa ni kumpa uongozi wa chama cha siasa akijenge na kukiandaa kwa kufuata maono yake (tunaambiwa anajua matatizo yote ya Watanzania na ana utatuzi wake). Sasa ili tuweze kumuamini njia nzuri ni kumpa uongozi wa Chadema kwa kumkatalia Ikulu.
Na kwa vile Freeman Mbowe mwenyekiti wa sasa wa Chadema anamuamini sana kiasi kwamba aliamua kummilikisha Lowassa harakati za mabadiliko basi njia nzuri ya kuonesha imani hii ni kuwa baada ya Lowassa kushindwa tu itabidi ajiuzulu ili ampishe Lowassa Uenyekiti – sidhani kama Lowassa atakubali kuwa Katibu Mkuu; na Mbowe achukue nafasi ya Dk. Slaa kuwa Katibu Mkuu na pamoja waijenge tena Chadema (wakisaidiwa bila ya shaka na wake zao ambao leo ni wanaharakati).
Watanzania na wanachadema wenye kuwaamini viongozi hawa wanapaswa kumchagua mgombea mwingine (sijali sana kama atakuwa Magufuli) ili Lowassa aoneshe huo umahiri wa uongozi wake kwenye kukiongoza chama. Ni kweli anaweza kuwa kiongozi wa chama na Rais kwa wakati mmoja kama alivyo Kikwete lakini hapo atakuwa anatumia urais kuiongoza Chadema. Akinyimwa urais ndio wana Chadema watajua ni kwa kiasi gani Lowassa aliwapenda sana na kuungana nao.
Wazo la yeye kujiuzulu baada ya kushindwa Uchaguzi Mkuu wiki ijayo itabidi likataliwe na wana Chadema wote na ikibidi maandamano yafanyike nchi nzima kumuomba awaongoze Chadema kwa miaka mitano ijayo.
Ndugu zangu akiiongoza Chadema kwa miaka mitano ijayo na ikaimarika na kuponywa majeraha ya kujitakia ya mwaka huu nina uhakika akigombea mwaka 2020 hata mimi nitampa kura yangu na kumuunga mkono kwani atakuwa amethibitisha kweli yeye alifanya uamuzi wa kuingia Chadema kwa ajili ya kuongoza harakati za mabadiliko na nina uhakika ataonesha uongozi ambao utaiinua Chadema kwa miaka mitano ijayo kuliko uongozi wa watu wengine waliokuwepo kwa muda mrefu. Hata mimi nitamwombea kura 2020.
Bila kumjaribu na kumpima katika chama tunaweza vipi kumpa uongozi wa nchi tukaamini kuwa chama kitaweza kumdhibiti wakati tunajua jinsi gani alisumbua na kuvuruga chama chake ambacho ni tawala tena akiwa mbunge tu?
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 Comments