HAKUNA mwanasiasa wa upinzani katika miaka ya karibuni aliyefikia umaarufu wa Augustine Lyatonga Mrema wakati alipohama kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kwenda NCCR Mageuzi, Februari mwaka 1995.
Mikutano yake na wananchi, mabomu ya machozi yaliyokuwa yakipigwa, khanga zilizokuwa zikitandikwa na akina mama ili atembee juu yake wakati akipita na mambo mengine.
Tangu kuruhusiwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, Tanzania ilikuwa haijawahi kuona mwanasiasa wa upinzani mwenye nguvu na ushawishi kama Mrema.
Lakini, ilikuwaje kwa mtu aliyekuwa na wadhifa wa uwaziri na kwa kipindi kifupi akiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Ndani, akaja kujikuta katika kambi ya upinzani?
Katika mazungumzo yake nami wiki hii, Mrema alisema jambo lililomfanya ahame kutoka CCM kwenda NCCR-Mageuzi lilikuwa vita dhidi ya ufisadi ambayo leo bado ni ajenda kuu ya vyama vya upinzani.
Wakati huo, anasema, taifa lilikuwa na mafisadi lakini hakupata ushirikiano kama ambao baadhi ya vyama na wanasiasa wanapata hivi sasa.
"Nilikuwa napinga ufisadi. Kuna suala la mfanyabiashara Chavda ambaye alichukua fedha za serikali na badala ya kuendeleza mashamba ya mkonge kule Tanga akazila. Kuna watu niliwakamata na dhahabu lakini wakaachiwa.
"Wakati huo nilionekana kero kwa wenzangu ndani na nje ya serikali. Nikajiuliza binafsi, sasa naendeleaje katika mazingira kama haya? Nilitaka ufisadi uwe historia. Nilitaka kurejesha nidhamu ndani ya serikali. Lakini watu wakawa wananipiga vita waziwazi.
"Nikasema kwamba haiwezekani kubaki humu. Bora niende nikawe mpinzani labda huko naweza kuleta mabadiliko. Hiyo ndiyo sababu kubwa iliyonifanya nijiunge na upinzani na hasa NCCR Mageuzi," anasema.
Kujiunga na NCCR Mageuzi
Wakati Mrema alipohama CCM, karibu vyama vyote vilivyopata usajili nchini vilimwomba ajiunge kwao. Kila chama kilikuwa na uhakika wa kuongeza idadi ya wanachama endapo vingempata mwanasiasa huyo.
Mmoja wa watu waliohusika na jitihada za kumhamishia Mrema kutoka CCM kwenda NCCR-Mageuzi alikuwa ni Msafiri Mtemelwa ambaye wakati huo alikuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa chama hicho.
"Mrema alikuwa anatisha wakati huo. Kabla hajajiunga na chama chetu, tulikuwa chama kizuri lakini hatukuwa na wafuasi kabisa. Nakumbuka kuna mikutano ya hadhara tulikuwa tunafanya na unakuta hujapata hata watu kumi tu.
"Sisi NCCR tulikuwa na ngome yetu kule Kongowe, Dar es Salaam. Kule angalau tulikuwa tukifanya mikutano tunapata washabiki kidogo. Kwa hiyo kama kuna mkutano wetu na tunataka waandishi wa habari waje na wapate picha nzuri, ilibidi twende Kongowe.
"Alipokuja Mrema hali ikabadilika ghafla. Siwezi hata kukwambia tulikuja kupata wanachama wangapi baadaye kwa sababu watu walikuja wengi sana kwa kweli. Hata sisi wenyewe hatukutaraji kama Mrema alikuwa na watu wengi kiasi hicho," anasema.
Wakati Mrema alipovuliwa nyadhifa zake Dodoma, Mtemelwa aliandaa vijana wa chama hicho kwa ajili ya kumpokea atakapoingia eneo la Ubungo. Hata hivyo, kwa mshangao wao, wakati wakiwa wako Ubungo tayari, waliambiwa kwamba mwanasiasa huyo alisharejea Dar es Salaam usiku wa siku iliyotanguliwa.
Kwa mujibu wa Mtemelwa, kuna kila dalili kwamba Mrema aliondolewa Dodoma na Serikali kupitia Idara ya Usalama wa Taifa mapema baada ya taarifa kufika kwenye vyombo vya dola kuwa ameandaliwa mapokezi na upinzani atakapofika Dar es Salaam.
"Asubuhi sana vijana wa NCCR na wengine ambao hawakuwa hata wanachama wetu tukajisogeza hadi Ubungo kumsubiri Mrema apite. Ilipofika mchana tukaona kimya, tukaanza kuulizana, imekuwaje tena "Mzee haonekani. Unajua mawasiliano ya simu wakati huo hayakuwa kama sasa. Ndiyo tukapata taarifa baadaye kwamba Mrema yuko Dar tayari. Tukachoka na mapokezi yakaishia hapo," anasema Mtemelwa.
Mtemelwa anakumbuka kwamba baada ya kubaini Mrema yupo Dar, NCCR ikaamua kupeleka ujumbe maalumu nyumbani kwake, Masaki jijini Dar es Salaam, kumwomba ajiunge na chama hicho.
"Nakumbuka waliokwenda kumuona ni aliyekuwa Mwenyekiti, Mabere Marando, James Mbatia, Dk. Masumbuko Lamwai, Dk. Ringo Tenga aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama na Anthony Komu.
"Walipofika nyumbani kwake, walikutana na aliyekuwa Mwenyekiti wa TLP, Leo Herman Lwekamwa, ambaye taarifa tulizozipata wakati huo zilikuwa zikidai kwamba alikuwa amelala nyumbani kwa Mrema akimshawishi ajiunge na chama chake," anasema Mtemelwa.
Marando, ambaye kwa sasa ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, alizungumza na Raia Mwema wiki hii na anaeleza namna tukio la kukutana na Mrema kwa mara ya kwanza lilivyokuwa.
Uamuzi wa kumtafuta na kumpata Mrema ulikuwa wa Kamati Kuu ya chama. Sisi tulitumwa kumtafuta na kuhakikisha tunampata Mrema ndani ya chama chetu.
"Tulipofika pale tulikutana naye. Alitukaribisha vizuri na tukafanya naye mazungumzo. Alisema mambo mawili makubwa; Mosi alitaka vyama vyote vya upinzani viungane na yeye ndiyo awe mgombea wa upinzani na la pili lilikuwa kutaka apewe Uenyekiti wa NCCR.
"Wakati huo kulikuwa na kitu kinaitwa Umoja wa Demokrasia Tanzania (UDETA) ambayo kwa sasa naweza kuufananisha na Umoja wa Katiba ya "Wananchi (UKAWA). Ulikuwa muungano wa vyama vya upinzani ingawa hata hivyo haukudumu. Hili suala la mgombea halikuwa na shida sana maana Mrema alikuwa na nguvu kubwa sana kisiasa. Lakini la Uenyekiti ilibidi liamuliwe kwenye chama.
"Tukaondoka na kwenda kujadiliana. Nadhani tulikutana pale Leader's Club, Kinondoni na wenzangu na mimi nikakubali kuachia ngazi ili Mrema awe Mwenyekiti. Dk. Tenga naye akajiuzulu Ukatibu Mkuu ili mimi nichukue nafasi yake," anasema Mrema.
Mbatia, ambaye sasa ndiye Mwenyekiti wa NCCR, anakumbuka tukio hilo kama vile limetokea jana. Katika mazungumzo yake na gazeti hili, naye anaeleza maneno hasa yaliyotamkwa na Mrema kwenye mkutano huo.
"Mrema alisema, 'sasa tunaenda kwenye Uchaguzi Mkuu. Kama msiponipa uenyekiti na mimi urais nikakosa, nitakuwa mgeni wa nani? Watanzania wanamtaka Mrema wao na kwa hilo hamuwezi kuzuia'. Nikishindwa urais, basi nirudi kuwa Mwenyekiti," Mbatia anakumbusha Mrema alivyosema.
Baada ya Kamati Kuu kuamua, vijana wanne wa NCCR walipewa barua iliyosainiwa na Marando iliyoeleza kuhusu maamuzi ya Kamati Kuu ya NCCR. Kwamba wamekubali Mrema awe Mwenyekiti wa chama hicho na pia mgombea Urais.
Vijana hao, anakumbuka Mtemelwa, walikuwa ni yeye, Blasius Loloma, Kezia Makoyo, Lugiko Kamnyabale na Komu. Hawa ndiyo waliopewa kazi ya kupeleka majibu ya barua yao.
Mtemelwa anasema kwamba walipofika kule, walipewa taarifa kwamba Edwin Mtei, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wakati huo, naye alikuwa ameenda kumuona Mrema kumwomba ajiunge na chama chake.
Mpaka siku ambayo kina Mtemela wanapeleka barua kwa Mrema, kwa mujibu wa Marando, tayari Lyatonga alikuwa amechukua kadi ya chama cha TLP ya Lwekamwa.
Si ajabu kuwa akina Mtemelwa walipewa jibu tofauti na walilolitarajia baada ya kumkabidhi Mrema barua yake.
"Alituambia kwamba vyama vyote vya upinzani vinatakiwa kufunga safari hadi Moshi mkoani Kilimanjaro ambako ndiko amepanga kutangaza atajiunga na chama gani. Hivyo, hakutupa jibu la ndiyo au hapana. Ilikuwa kazi ngumu kweli.
"Tukapata taarifa kuwa Mtei alimpa Mrema ofa ya kuwa Katibu Mwenezi wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini. Ilijulikana kuwa waziri huyo wa zamani alikuwa na nguvu sana katika kanda ya ziwa. Hivyo, tulikuwa tukifahamu tayari kuwa ofa yetu sisi ni kubwa kuliko CHADEMA.
"Tukaanza maandalizi ya kwenda Moshi. Nakumbuka ilikuwa ni mwezi Machi hivi lakini sikumbuki tarehe. Wakati huo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro alikuwa Omar Mahita ambaye baadaye alikuja kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP).
"Tulipofika Moshi, Mahita akatuambia haturuhusiwi kufanya mkutano wa kisiasa pale. Hoja aliyoitumia ni kwamba
Mrema amehama CCM na hajajiunga na chama chochote cha siasa. Sasa anakwenda Moshi kufanya mkutano wa hadhara kama chama gani? Hii ndiyo hoja ambayo ilitumiwa kuzuia mkutano wa Moshi.
"Ndipo hapo sasa tukamwambia Mrema na akaamua kujiunga na NCCR. Tulimwambia ya kuwa NCCR ilikuwa na wanasheria wengi na kwa wakati ule wangemsaidia sana kwa vile serikali ya CCM ilikuwa inamfuatafuata sana," anakumbuka Mtemelwa.
Nilimuuliza Mrema ni kwa nini aliamua kuwasumbua viongozi wa upinzani namna ile?
"Mimi nilikuwa hot cake bwana. Sasa ukiwa hot cake si lazima uringe jamani? Wakati huo Watanzania ulikuwa huwezi kuwaeleza kitu kuhusu Mrema wao. Ilibidi pia nijihakikishie kuwa chaguo ninalolifanya ni sahihi," aliniambia Mrema.
Hatimaye, Machi, 1995, Mrema alitangaza rasmi kujiunga na NCCR katika tukio lililotetemesha nchi. Mwenyewe, ananiambia, alikuwa "amewasha moto."
Kwa siku tatu mfululizo tangu Mrema ajiunge na NCCR, tulitoa kadi nyingi kwa wanachama wapya kuliko kawaida. Maombi yalikuwa mengi kiasi kwamba tulikuwa tukitoka ofisini tumechelewa sana.
"Kwa maoni yangu, nadhani kilichotokea wakati ule kinaweza kisitokee tena. Niko kwenye siasa za upinzani tangu vyama vingi viruhusiwe na sijaona mwanasiasa aliyependwa kuliko Mrema.
"Niseme bila unafiki hapa kwamba Mrema ni sehemu ya upinzani hapa Tanzania, tutake au tusitake. Bila yeye, upinzani usingefika hatua hii. Hebu tujiulize leo, ni wana CCM wangapi waliowahi kushika wadhifa kama wa Mrema na halafu wakahama na kujiunga upinzani?
"Miaka michache iliyopita, tulisikia taarifa za kutaka kuundwa kwa chama cha CCJ na kundi la vigogo kutoka CCM lakini walipofikiria maisha ya taabu watakayoishi bila posho za serikali, wakaamua kubaki kwenye chama chao.
"Lakini Mrema aliondoka CCM katika kipindi ambacho upinzania haukuwa na nguvu kabisa. Akaacha mambo yake yote na kujiunga na upinzani. Mrema ana makosa lakini huwezi kuzungumzia upinzani hapa nchini pasipo kumzungumzia," anasema Mtemelwa.
Kwenye mazungumzo yangu na Mrema, namuuliza nini kilichofanya NCCR yake ipendwe kuliko vinavyopendwa vyama vingine vya upinzani kwa sasa.
"Ni rahisi sana. Wananchi wa Tanzania walikuwa wakimjua Mrema nje na ndani. Waliniona wakati nilipokuwa Naibu Waziri Mkuu na walikuwa wakijua utendaji kazi wangu.
"Vyama vingi vya upinzani hapa nchini vina watu ambao hawajulikani uwezo wao. Sasa mtu hajawahi kuwa hata Katibu Tarafa au Mkuu wa Wilaya tu angalau halafu anakuja kwa Watanzania na kutaka Urais. Sasa huyo mtu atapigiwaje kura? Atashindaje? Atapendwaje kama Mrema?
"Mimi na Maalim Seif tuna nguvu kwa sababu wananchi wetu walituona wakati tulipokuwa madarakani. Wanajua wakituchagua watapata nini. Wapinzani wengine ni majina tu.
Mwisho wa Mrema NCCR
"NCCR walinitafuta kwa sababu walitaka kuingia Ikulu. Walijua bila Mrema Ikulu ingekuwa ndoto kwao. Tanzania kulikuwa hakuna mali inayouzika kama Mrema. Kulikuwa na msemo, 'Urais ni Mrema Piga Ua'.
"Sasa baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, NCCR ikakosa kuingia Ikulu. Wale jamaa wakaona chama nimeshawajengea na sasa sifai. Wakaanza kupanga njama za kuniondoa.
"Wakaamua kunifanyia vitimbi vya kila aina. Mwishoni kuna watu wakataka kuniua kwenye Mkutano wa Halmashauri Kuu kule Raskazone, Tanga. Niliponusurika nikasema sasa hawa wataniua.
"Walifanya hivyo kwa kusaidiwa na serikali. Polisi wakawa wanakung'uta mabomu kila ninapokwenda. Ruzuku ikawa inapelekwa kwa akina Marando na mimi sikupewa. Mahakama nayo ikawa inanishughulikia. Kesi kila siku zikawa haziishi mahakamani.
"Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nayo ikawa shingoni kwa Mrema kila siku. Lakini mimi nilikuwa mpinzani mstaarabu. Sikuwahi kuua hata kuku kwenye mikutano yangu ya hadhara.
"Siku hizi wapo viongozi wa CCM ambao wananifuata na kuniambia Mrema afadhali wewe ulipokuwa mpinzani. Ulikuwa mzalendo na mstaarabu. Wapinzani wengine siku hizi hawana hata uzalendo.
"Nikawaambia mlikosea wenyewe. Mnavuna mlichopanda. Mimi nilikuwa mpinzani lakini upinzani wangu ulikuwa unajali maslahi ya Taifa. Kwa wema wangu mkaamua kunishughulikia kila kukicha. Sasa leo mmekutana na madume ya kenge. Mtakula jeuri yenu sasa. Watu wanapoteza maisha kwenye mikutano ya siasa siku hizi. Ni siasa gani hizi jamani?" anahoji Mrema.
Mrema anajutia nini kwenye maisha yake ya siasa?
"Sikufanya hesabu zangu sawa sawa wakati nikitoka CCM kwenda NCCR. Ningejitahidi walau kuondoka na vigogo walau watano hivikutoka katika chama hicho. Labda na viongozi wa chama wa mikoa na hata mabalozi.
"Sasa mimi niliondoka mwenyewe. Peke yangu. Nilipoona umati wa watu unajaa katika mikutano yangu ya hadhara na wanawake wanatandika khanga kila ninapopita, nikajua nimemaliza kazi.
"Hebu fikiria, mimi peke yangu nilipata kura milioni 1.8 mwaka 1995. Levy Mwanawasa, alipata kura kama hizo kwenye uchaguzi wao nchini Zambia na akapata urais.
"Hivi ningeondoka na watu pale CCM unadhani ningepata kura ngapi? CCM kweli wangeweza muziki wangu? Kwenye siasa zangu, kwa kweli hapo ndiyo mahali pekee nadhani nilifanya makosa.
"Inawezekana wananchi walikuwa wanajiuliza, sawa, Mrema anafaa kuwa Rais lakini je, Waziri Mkuu wake atakuwa nani? Mambo ya Nje? Mambo ya Ndani? Sikuwa na watu wanaofahamika kama viongozi. Kama ningelifanya hilo, pengine ningeweza kuingia Ikulu," anasema Mrema.
Swali moja tu najiuliza kila wakati, hivi ingekuaje kama Tanzania ingepata Rais anayeitwa Augustime Lyatonga Mrema?
0 Comments