Ndugu zangu,
Kuna waliopoteza dira njiani kwenye safari ya kisiasa. Naziona ishara za wazi wazi.
Safari ya kisiasa inahitaji mwelekeo. Anayesafiri kisiasa anahitaji ramani na dira. Ramani ni miongozo na taratibu, lakini dira hujengeka kiitikadi.
Dira ina maana ya compass kwa kimombo. Uchaguzi unahusu pia kuchagua unachokiamini. Anayetaka kuongoza watu ni lazima aikamate sawa sawa dira. Akichezesha mikono na mwelekeo pia utachezacheza.
Wanaoongozwa wanataka kujua kiongozi wao anadhamiria kuwapeleka wapi. Hivyo, kiongozi asiye na ramani wala dira mkononi hutiliwa mashaka. Uchaguzi unahusu imani. Kuchagua unayemwamini.
Tofauti na Ujamaa, ubepari umejengeka katika mtaji. Bepari hayuko tayari kuitumia risasi ya mwisho kwa maslahi ya wengi.
Swali, inakuwaje basi jamii inapobaki na risasi moja ya mwisho?
Babu yangu amepata kunisimulia, kuwa katikati ya njaa kali, ikafika siku ikabaki risasi moja. Alihitajika mbogo ( nyati) aangushwe ili kitoweo kitoshe kwa wengi.
Kijijini akatafutwa mlenga shabaha mahiri kuliko wote. Akapewa jukumu la kwenda kumwangusha nyati porini.
Kijiji kizima kikabaki kimya kusubiri kishindo cha risasi kutoka mbugani.
Kikasikika. Wanakijiji walipofika porini wambebe nyati wakamsikia mlenga shabaha yule mahiri akitamka;
" Jamani, ilibaki kidogo tu, nimemkosa!"
Naam, na jamii katika hali zake hutokea ikawa kwenye hali inayofanana na kubaki na risasi moja ya mwisho. Jamii ya namna hiyo haipaswi kuongozwa kwa ushabiki na jazba katika kufanya maamuzi ya nani wa kumkabidhi gobore na risasi ya mwisho.
Ni vema mtu huyo atakayepewa jukumu hilo awe ni mtu asiye na mzaha, mtu mwenye uwezo, hekima na busara. Mtu ambaye, hata baada ya kuchaguliwa, atakuwa ni mwenye uwezo wa kuwaunganisha wa ndani ya chama chake wakawa kitu kimoja, pia kuwaunganisha watu wake wakawa kitu kimoja.
Ndio, awe ni mtu makini na mwenye kuweza kuikamata dira bila kuitingisha.
Hapo, jamii hiyo inaweza kuuona kwa usahihi, mwelekeo wa njia ya safari yao, kama taifa.
Ni Neno La Leo.
Maggid.
Iringa.
Unapokea Email hizi kwa sababu umejiunga na Jukwaa la 'Mabadiliko'.
Kuchangia mada tuma kwenye Email hii: mabadilikotanzania@googlegroups.com
For more options, visit this group at:
http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania?hl=en?hl=en
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Mabadiliko Forum" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to mabadilikotanzania+unsubscribe@googlegroups.com.
To post to this group, send email to mabadilikotanzania@googlegroups.com.
Visit this group at http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania.
To view this discussion on the web visit https://groups.google.com/d/msgid/mabadilikotanzania/CAMD-ye6Fv6-AkSHAE%3DU9Nz8reRWA5pgwW2TFbWM3cgzx%2BUJs%3Dw%40mail.gmail.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 Comments