JONSON Mbwambo ni kati ya waandishi wa habari wa siku nyingi. Ameifanya kazi hii ya uandishi kuanzia wakati wa Rais wa Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere hadi sasa ambapo Serikali ya Awamu ya Nne ya Jakaya Kikwete inafikia ukingoni na kuashiria kuja kwa Rais mpya wa Awamu ya Tano.
Mbwambo amekuwa akiandika katika mazingira ya nchi yetu ilipokuwa inatawaliwa na mfumo wa chama kimoja mpaka sasa ambapo kuna vyama vingi vya kisiasa na baadhi ya vyama hivyo vikionekana kama 'Saccos' au kampuni za kifamilia au za watu wa eneo fulani.
Mbwambo ni kati ya waandishi ambao wanalitanguliza taifa kabla ya nafsi zao. Kila mara anasema taifa kwanza. Yamkini Mbwambo ameathirika na utofauti huu wa mihula ya utawala, lakini anabakia kuwa mwandishi muhimu sana katika jamii ya Watanzania ambayo inahitaji kuambiwa habari zilizo za ukweli.
Mbwambo sio mwandishi kanjanja na anaandika mara zote akizingatia misingi ya uandishi wa habari. Aidha, Mbwambo haandiki kwa kufuata mkumbo au katika hali ambayo inaweza kutiliwa mashaka kwamba labda kapewa bahasha ya kaki kama wanavyofanyiwa baadhi ya wanaoshika kalamu.
Mwandishi huyu hawezi kufananishwa na akina Hassan Ngeze wa Rwanda aliyekuwa akiandikia Gazeti la Kangura na kutangazia Radio ya Milles Collines na ambaye uandishi wake ulisababisha mauaji ya kimbari ya mwaka 1994. Huwezi kumfananisha Mbwambo na Arap Sang, mwandishi wa Kass FM ya Kenya aliyetumia kalamu yake kuchochea vurugu za kikabila baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2007.
Nchini kwetu Tanzania kwa sasa hivi na hususani wakati huu tunapoelekea Uchaguzi Mkuu, tunao waandishi wengi wa aina ya akina Hassan Ngeze na Arap Sang ambao wanaandika ili wapate mkate wao wa kila siku bila kujali mustakabali wa nchi yetu baada ya Uchaguzi Mkuu.
Johnson Mbwambo kwa wakati huu anaandikia gazeti ambalo limejijengea heshima kubwa katika jamii ya Watanzania wa rika zote na hapana shaka mwandishi huyu haegemei upande wowote wa kisiasa. Njozi za Mbwambo kwamba Chadema ingekuwa Chama Kikuu cha kupambana na CCM zilizimwa baada ya chama hicho kumpokea Edward Lowassa na kumpa nafasi ya kugombea Urais. Tofauti na Mbwambo, wapo waandishi ambao wanakuambia wazi kwamba kula Ukawa na kulala CCM, lakini wapo wengine wanaosema maisha ni popote bora mkono unakwenda kinywani. Wasomaji wa makala hii watajiuliza ni kwa nini naandika makala haya nikianza na wasifu wa mwandishi huyu.
Nimefanya hivyo kwa sababu nafahamu kwamba vyombo vingi vya habari, wahariri na mitandao mingi ya kijamii inatumiwa na baadhi ya wanaogombea ama ubunge, udiwani au urais. Waandishi wa vyombo vya habari na hasa vile vya watu binafsi wamekuwa wakionyesha wazi kwamba ama wamenunuliwa au wameahidiwa mambo makubwa na baadhi ya wagombea. Hilo silioni kwa Mbwambo na wale wanaofanana na yeye. Anaandika kuihabarisha jamii na kuitahadharisha kwamba suala la Uchaguzi Mkuu sio la kuchukuliwa kwa mzaha kwa sababu uchaguzi ni maisha yetu. Tusiyachezee kwa kumshabikia Lowassa na mgombea mwenza wa kubandikwa Juma Haji Duni.
Hivi karibuni katika 'tafakuri jadidi', Mbwambo aliandika katika gazeti la Raia Mwema kwamba Edward Lowassa hafai kuwa Rais wa nchi hii na Watanzania wasitarajie mabadiliko makubwa kama watamchagua kuwa Rais. Washabiki wa Lowassa walimjia juu Mbwambo na kumwelezea kama mtu mwenye chuki binafsi na mgombea wao, Lowassa. Washabiki au wapambe hawa hawakufikiria wala kuhoji kama Lowassa alitokea wapi, ni kwa nini alikatwa CCM, ni kwa nini anang'ang'nia kuwa Rais, ni nani anampa fedha ambazo anazigawa kama njugu, atazilipaje akiingia Ikulu na hawakujiuliza pia kwamba Lowassa atafanya nini kama chama kilichompokea hakitashinda katika uchaguzi huu.
Mimi nimeshaandika makala nyingi za kuonyesha Chadema Chama kisichotabirika na kilipoamua kumpokea Lowassa niliandika makala kuionya jamii ya Watanzania kwamba kama haijitambui na itakubali Lowassa kuwa Rais wao, Tanzania isitarajie mabadailiko yoyote. Nilieleza kwamba mabadiliko yanayotarajiwa na Watanzania yanaweza kupatikana ndani ya CCM na sio nje ya chama hicho kama baadhi ya wapiga debe wa Lowassa wanavyojaribu kuwaaminisha Watanzania. Mabadiliko yanawezekana na yatapatikana ndani ya CCM na Lowassa analifahamu hilo. Lowassa hawezi kutumia Ilani ya vyama vinne kuleta mabadiliko.
Johnson Mbwambo na wengine wanaofanana naye, wanaandika uhalisia wa Lowassa. Wanafahamu kwamba Lowassa sasa sio mwanasiasa wa kawaida bali amejengwa kama taasisi iliyoundwa na wanasiasa walioshindwa kuishi ndani ya CCM kwa sababu ya tamaa zao kwa upande mmoja na kwa upande mwingine, taasisi hiyo inaundwa na wafanyabiashara ambao wanaamini kwamba Lowassa akiingia madarakani watavuna na watatafuna utajiri wa nchi hii kama wanavyotaka.
Wafanyabiashara hawa wanachagizwa na wanasiasa ambao wanawaambia toeni fedha zenu Lowassa aingie madarakani kwa sababu fedha zenu zitarudi na Lowassa hatawaangusha. Wapo wafanyabiashara ambao watakwenda hata kwa waganga wa kienyeji kuhakikisha kwamba mgombea wa CCM hapiti. Wanamwogopa.
Nimekuwa nikisoma falsafa ya watenda makosa ya aina nyingi hata ya wizi wa kawaida kwamba mara zote hawawezi kuficha alama zote za makosa yao. Sasa hivi Lowassa anajinasibisha na watu wa tabaka mbalimbali, anakwenda Tandale sokoni, anakunywa maziwa kwa mama lishe, anapanda daladala na anatumia maneno ya kuwavutia wale wenye shida na dhiki kwamba yupo tayari kuishi na walalahoi.
Nina uhakika kwamba Lowassa ambaye tuna umri unaolingana, hajawahi kuishi maisha haya ya kuigiza, hajawahi kuishi na watu wa chini tangu alipozaliwa. Lowassa amezaliwa kwenye familia inayojiweza na amesoma na kufanya kazi nzuri zenye maslahi ya wazi kwake kama Ofisi ya Waziri Mkuu Kitengo cha Maafa na Wizara ya Ardhi alipohakikisha kwamba kila ndugu yake anapata kiwanja mahali anapopataka, ana maisha ya starehe, lakini leo kwa sababu anautaka Urais, yupo tayari kwenda Tandale kuwauliza wachuuzi kama wanayaonaje maisha haya. Anawakejeli, lakini hawana la kufanya au kumwambia kwamba aache kuwasanifu.
Hali hii ndio anayoiona Mbwambo kwamba huu ni usanii ambao kwa bahati nzuri Lowassa ameusomea katika Shahada yake ya Kwanza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, sanaa ya maonyesho na sasa anataka kuitumia katika kupata nafasi ya kisiasa, tena nafasi kubwa kabisa ya kuongoza dola. Sawa, pengine Lowassa ana nia nzuri na Watanzania wa ngazi ya chini. Moyo alionao sasa ni wa kutiliwa shaka kwa sababu katika umri wake wa miaka 62 sasa hajawahi kuonyesha huruma anayoionyesha wakati huu.
Inawezekana tabia anayoionyesha sasa inatafsiri kile ambacho baadhi ya wafuasi wake wamesema yeye ni kama Mtume Muhammad Astaghafirallah' na yeye ni chaguo la Mungu kwa Watanzania. Kama kweli ni hivyo na anataka kuosha vidonda vya wanyonge kama alivyofanya Yesu, namshauri aendelee, lakini aende pia kwenye gereza la Keko, Segerea au Ukonga. Akutane na wafungwa, ale nao na alale huko angalau kwa siku moja kama alivyofanya aliyekuwa Mbunge wa Arusha kwa tiketi ya Chadema Godbless Lema, ambaye kwa sababu zisizo wazi anapenda kulala jela pamoja na wafungwa.
Mwandishi Johnson Mbwambo pamoja na waandishi kama yeye wamekuwa wakitumiwa sms za matusi na kashfa kwamba wana chuki binafsi na Lowassa. Mimi binafsi na waandishi wengine wanaoandika juu ya Lowassa, naamini sina hata chembe ya chuki naye ila ninaandika kuihabarisha jamii ya Watanzania isije ikaingia au ikaangukia kwenye mikono isiyo salama kwa sababu Lowassa alivuka daraja hata kabla hajalifikia.
Itakumbukwa kwamba hata kabla bwana huyu hajaenda Dodoma kwenye mchakato wa kilichokuwa chama chake CCM kutafuta mgombea Urais, alishasema ni yeye tu anayefaa kuteuliwa kugombea Urais na mpango wa kushindwa hakuwa nao. Yeye alikuwa ni kushinda, kushinda na kushinda tu. Kwake mchakato au utaratibu wa kumtafuta mgombea wa CCM haukuwa na maana.
Chama chake, CCM ambacho aliapa kwamba hawezi kutoka na wale wasiompenda watoke wao, hakikumteua kwa sababu kiliona kwamba hafai. Mtu anayeifahamu vyema hulka ya Lowassa anapoandika kwamba mtu huyu hafai kama alivyosema Dk. Slaa kwenye mkutano wake na waandishi wa habari. Wapo wanodandia hoja na kutoa majibu ya haraka kuwa 'huyu katumwa, amenunulika anatumiwa na CCM na maneno mengine yanayowafariji wana UKAWA, lakini yenye ukakasi kwa Watanzania wanaojitambua. Siamini kama Mbwambo naye aliandika kwa kutumwa au kununuliwa. Huyu anasimamia ukweli hata uwe mchungu kiasi gani.
Wapo watu wanaoandika juu ya afya ya Lowassa kwamba ni mbaya, anatembea kwa shida, hawezi kuzungumza kwa muda mrefu na hata akizungumza kauli yake ina katikakatika kuashiria kwamba afya yake ina mgogoro. Mke wake mama Regina Lowassa ambaye naye ninamfahamu sio mzungumzaji mzuri, amesimama hadharani na kusema kwamba mume wake yuko 'fit' na anayetaka kujua afya ya mumuwe amuulize yeye Regina.
Kauli ya mama Regina ilinikumbusha majibu ya Rais wa kwanza wa Kenya, Mzee Jomo Kenyatta kwa wazee wa Mombasa alipowaambia kwamba kama wanataka kujua afya yake ilivyo wamuulize Mama Ngina ambaye alikuwa mke wake kwa wakati huo miezi michache kabla ya kufariki mwaka 1978. Kifo kitamkuta kila mtu na hutokea mzima akafa na mgonjwa akapona na kwa imani yangu hiyo suala la afya ya Lowaasa, kama vile ambavyo Mbwambo hajalihusisha na mimi sitaki kulifanya hoja ya kujadili kwa sababu hilo litaamuliwa na Mungu wake mwenyewe.
Wakati naanza kuandika makala haya, Dk. Slaa alikuwa hajazungumza na waandishi wa habari kuhusu chama chake cha Chadema na ujio wa Lowassa katika chama hicho. Nilichokisikia kutoka kwa Dk. Slaa kilinifariji sana na nikatamani kumwambia Mbwambo aendelee kuandika na kusimamia ukweli kwa sababu haugawanyiki na kwamba wapo wachache wenye uchungu na nchi hii kama yeye. Hata hivyo, kama nilivyosema katika para zilizotangulia, kati ya waandishi waliohudhuria mkutano wa Dk. Slaa wapo ambao wanafanana au wamezidi kiwango cha Arap Sang na Hassan Ngeze.
Ni waandishi wa habari ambao walimuuliza Dk. Slaa maswali ya kejeli na ambao baada tu ya mkutano walikuwa wa kwanza kuandika kwenye mitandao ya kijamii kwamba Dk. Slaa ametumwa ili kuiangamiza Chadema na Ukawa.
Nasaha za Dk. Slaa alizitoa kwa vijana wa Chadema kwamba wasipige kura kwa ushabiki bali wafanye uamuzi sahihi ni vema zikaelekezwa kwa vijana wote kwa sababu kama alivyobainisha Dk. Slaa wapo viongozi ambao ninaamini kwamba sio waadilifu, lakini wanataka kuchukua taifa letu. Viongozi wa aina hiyo ni pamoja na Edward Lowassa akipambwa na wafanyibiashara na wanasiasa wengine wasio na nia njema na nchi yetu.
Nimesema kwamba akina Mbwambo na sasa akina Slaa waendelee kutetea ukweli kwa sababu mara zote ukweli utashinda. Kitu ambacho napenda kuwatahadharisha watanzania ni kwamba waelewe kuwa kauli ya Dk. Slaa haikuwafurahisha wale wote wanaomuunga mkono Edward Lowassa. Kauli zilizotolewa na baadhiya viongozi wa Chadema ni kwamba Dk. Slaa alishaonywa na Mwenyekiti wao Freeman Mbowe kwamba afunge mdomo wake, lakini sasa ameufungua na amesema hatanyamaza.
Tafakuri ya kumalizia makala haya ni kwamba je, Mbowe ataendelea na juhudi zake za kumnyamazisha Slaa na kama ile hoja ya Dk. Slaa kutumiwa inakinzana vipi na kutumiwa kwa mke wake wa zamani, Rose Kamili. Ee Mungu, tunakuomba utuvushe salama kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015.
Chanzo Raia Mwema
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 Comments