
Ndugu zangu,
Kwangu mimi, mmoja wa wanasiasa wanaoacha pengo katika mbio za Urais za mwaka huu ni Profesa Ibrahim Lipumba.
Ni kwa vile, uchumi ni moja ya ajenda zinazopaswa kuwa sehemu ya mijadala muhimu katika kupima uwezo wa wagombea. Ni katika kutafuta majibu ya ni kwa namna gani wagombea wamejipanga kimikakati katika kutuambia sio tu watafanya nini , bali ni kwa namna gani, kwenye kututoa hapa tulipo na kwenda kwenye hali bora zaidi kiuchumi, kama taifa.
Nakumbuka, kwenye Uchaguzi wa mwaka 2005, Vyombo vya Habari vilikazana kuandika habari za JK na Freeman Mbowe. Ikawa ni habari za CCM na CHADEMA kila kukicha. Vikasahau, kuwa kulikuwa na mgombea wa urais aliye kwenye mbio na mwenye umuhimu pia, maana, kuna wengi walimkubali. Yawezekana jambo hilo lilifanywa na media yetu kwa bahati mbaya au kwa makusudi. Kumsahau Profesa Ibrahim Haruna Lipumba wa Chama Cha Wananchi ( CUF).
Kwangu mimi, mwaka ule wa 2005, katika wote walioshiriki mbio za Urais, Prof. Lipumba ndiye alikuwa mwenye uzoefu zaidi wa njia ya urais ambayo wenzake na yeye walikuwa wanaimbilia.
Ikumbukwe, Profesa Lipumba ana uzoefu wa kinyang'anyiro cha urais tangu mwaka 1995. Ilikuwa ni kwenye Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi.
Ikumbukwe, Lipumba alishiriki mdahalo wa kwanza wa wagombea urais.
Ni Profesa Lipumba aliyeibuka wa pili kwenye mdahalo ule. Mdahalo uliomwacha Ben Mkapa akiongoza na Mrema akiambulia nafasi ya tatu, huku John Cheyo akikamata mkia. Hata hivyo, bado mashirika ya habari ya kigeni yalimpa Prof. Lipumba alama za juu zaidi.
Ndio, Lipumba ni mpiganaji mahiri. Mwaka 1995 aliingia kwenye mbio za Urais kama ' Profesa'. Hilo lilikuwa kosa, akalirudia tena mwaka 2000. Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, Profesa Ibrahim Lipumba alionekana zaidi kama ' Ibrahim Lipumba'. Profesa aliamua kushuka chini, kuwa na watu na kuongea lugha yao.
Nakumbuka kukutana na Profesa Lipumba ana kwa ana kwa mara ya kwanza mwezi Oktoba 2005, wiki kadhaa kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu. Ni pale Isimila Hotel, Iringa. Ni Hotel ya kawaida kabisa. Ndugu yangu Saed Kubenea alikuwa kwenye msafara wa kampeni wa Profesa Lipumba, na ni Saed Kubenea aliyefanya maandalizi ya mimi kukutana na Profesa Lipumba.
Ilikuwa siku ya Alhamisi, nilifika pale Isimila Hotel kunako saa tatu asubuhi. Aliponiona, Profesa Lipumba alinijia akiwa mwingi wa tabasamu;
" Kumbe, ndiye wewe Maggid!" Alitamka huku akionyesha furaha. Mkono wa kushoto alikamata jarida la Rai na chupa ya 'Maji Afrika'. Saed Kubenea alisimama kando, mbali kabisa kupisha mazungumzo ya Profesa na mimi.
Kwenye mazungumzo yetu nilimwona Profesa Lipumba kuwa ni mtu wa kawaida sana. Tukiwa tumesimama, kuna wakati kwenye mazungumzo yetu, Lipumba alikuwa akipukuta vumbi kwenye suruali yake kwa kutumia gazeti la Rai.
Mwanasiasa huyu Lipumba anaongea kwa mpangilio na kwa kutulia. Kushiriki kwake katika uchaguzi wa 1995, 2000 na 2005 kumempa uzoefu zaidi katika vinyang'anyiro vya urais. Lipumba ana uwezo na kipaji cha kufafanua mambo magumu yakaeleweka kwa mtu wa kawaida.
Mwaka ule wa 2005, kuna wakati nilimsikia Lipumba akitoa mfano wa ajira elfu moja zenye uhakika kwa vijana zinavyoweza kuathiri maisha ya mama mwuza vitumbua. Profesa Lipumba alitamka;
" Ndugu zangu, bila ya vijana hawa kuwa na ajira na kipato , mama huyu atashinda na vitumbua vyake vikimtazama !."
Hakika, Lipumba ana uwezo pia wa kutengeneza sentesi fupi na zenye kishindo; Mwaka ule 2005 nilimsikia akitamka;
"Wananchi nikopesheni kura zenu, nitawalipa maendeleo!" Hizi ni baadhi tu ya nguvu za Ibrahim Lipumba katika rethorik, sanaa ya kuzungumza.
Kampeni za Profesa huwa na sura za mikakati ya kijeshi. Mwaka 2005 tulimwona Lipumba akianza kampeni kwa kuanzia nakule ambapo aliamini kuna matumaini ya kupata ushindi, matumaini ya kuvuna kura.
Itakumbukwa, Lipumba alianza kampeni zake kwenye 'ngome' ya CUF kwa wakati huo, na hata hii leo. Ni mikoa ya Kusini; Lindi na Mtwara. Huko Profesa 'alipiga kambi' ya zaidi ya juma moja akifanya kampeni.
Baada ya kule kusini, tulimwona Profesa akichagua maeneo ya kwenda. Na kila alikokwenda kulikuwa ni kule ambako, CUF ilionekana kuungwa mkono.
Mwaka 2005, staili ya kampeni ya Profesa Lipumba ilibadilika pia. Profesa Lipumba alionekana kuwavutia zaidi wasikilizaji na watazamaji kwenye hotuba zake. Lipumba baada ya kuongea majukwaani alishuka chini na kuongea na wapiga kura akiwa karibu nao sana. Kila mahali alipofika, aliunganisha masuala makubwa na yale ya mahali hapo. Aliachana na staili ya kutumia muda mwingi kukishutumu Chama Cha Mapinduzi bila kuwafafanulia wapiga kura yeye akiingia madarakani atafanya nini na kwa namna gani. Hivyo, kwa mwaka ule wa 2005, Profesa Lipumba alisisitiza zaidi nini angekifanya, yeye na chama chake, na kwa namna gani. Kile ambacho CCM wameshindwa kukifanya.
Kabla ya mikutano ya hadhara, Profesa alifanya jitihada za kuikaribia jamii ya mahali hapo. Mathalan, Profesa Lipumba alikwenda sokoni . Huko aliongea na wananchi, aliuliza bei za vyakula. Kule Musoma tukamwona Profesa akipima nguo kwa fundi cherehani, alitaka fundi huyo amshonee suti yake. Pale Bunda Lipumba akamtembelea nyumbani kwake Mzee Raphael, mwanachama wa CUF wa miaka mingi. Kule Geita tulimwona Lipumba akizungumza na wachimbaji madini wadogowadogo akiwa kwenye machimbo yao.
Ndio, tulimwona Lipumba akibeba mawe kuweka chini ya tairi na hata kusukuma gari lake kule Kondoa . Ni wakati msafara wake ulipokwama njiani. Tulimwona Lipumba akishiriki shughuli ya mazishi kule Mafia na Kagera. Kwamba kila alipokwenda kukampeni, Profesa Lipumba alitafuta habari kuhusiana na mahali hapo, ikiwamo pia habari mbaya kama misiba. Kwenye misiba kuna wapiga kura.
Hii nayo ni staili ya kampeni aliyoionyesha Lipumba katika uchaguzi mwaka 2005. Kushuka chini kwa watu. Mgombea usijikite tu kwenye kukusanya watu, unapaswa pia kuonekana iliko mikusanyiko ya watu, kuongea nao katika hali za kawaida, na si za maonyesho.
Na bila shaka, nguvu za Profesa Lipumba za mwaka 2005 na mavuno makubwa ya kisiasa aliyovuna yeye na chama chake, hayakutokana na Profesa peke yake.
Profesa hakusita kuniambia, kuwa alijivunia pia nguvu za chama chake, CUF. Kwamba kimejitahidi sana kuweka mizizi chini waliko watu. Chama cha CUF kiliundwa Mei 28, 1992. Ni chimbuko la kuunganishwa kwa Chama cha kutetea haki za Wananchi (Civic Movement) kwa upande wa bara na chama cha KAMAHURU cha Zanzibar.
CUF imetokana na vuguvugu la mageuzi nchini. Ingawa NCCR-mageuzi kilikuwa ni chama cha kwanza cha upinzani, CUF kilikuwa chama cha pili kusajiliwa katika mfumo wa vyama vingi baada ya CCM. Hii ilitokana na sura yake ya muungano kuonekana dhahiri. Hii ni moja ya nguvu kubwa za CUF. Hakuna anayejisumbua kuweka hadharani, ukweli kuwa, kwa sasa, CUF ni chama pekee cha upinzani, chenye uhakika wa kuwa na wawakilishi bungeni kutoka Unguja, Pemba na Bara. Na kwa upande wa Bara, Profesa Lipumba, kutokana na kuaminika kwake, amekuwa mhimili muhimu wa kuhakikishia CUF viti upande wa Bara.
Chadema, na NCCR, pamoja na umaarufu wao Bara, vyama hivi viwili, havijapata kuwa na hakika ya kuvuna viti vya Ubunge Unguja na Pemba. Na siku ikitokea, hiyo itakuwa ni habari kubwa.
Naam, miaka kumi imepita tangu nikutane na na kuongea na Profesa Lipumba. Mengi yametokea, ikiwamo ya yeye mwenyewe Profesa kuachia ngazi ndani ya CUF. Nitapenda nikutane tena ana kwa ana na Profesa, nizungumze nae, ni katika kuendelea kujifunza, hata kwangu.
Maggid,
Iringa.
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 Comments