KILA nikitafakari yanayotokea katika nchi yetu Tanzania naingiwa na shaka na hofu kubwa kwamba tusipochukua hatua tunaweza kutumbukia kule ambako taifa la Mexico limezama hivi sasa. Nimepata huko nyuma kuifananisha nchi yetu Tanzania na taifa la Mexico, na sitachoka kufanya hivyo, kwa sababu woga na hofu yangu hiyo bado iko pale pale, na imeongezeka zaidi katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25.
Kwa karibu miongo mitatu sasa Mexico imekuwa ikipigana vita ya kukomesha biashara ya madawa ya kulevya, lakini badala ya biashara hiyo kupungua imekuwa ikishamiri mwaka hadi mwaka. Tanzania nayo imekuwa ikiendesha vita dhidi ya ufisadi kwa miaka kadhaa sasa, lakini tunachokiona ni kwamba ufisadi unaongezeka mwaka hadi mwaka.
Katika Mexico, kila rais mpya aliyeingia madarakani aliapa kupambana na biashara hiyo, lakini hakuna aliyefanikiwa. Hata Rais wa sasa, Enrique Pena Nieto, licha ya kusaidiwa mno na Marekani, yaelekea vita hiyo inamshinda.
Tanzania nako hali ni hiyo hiyo. Kila rais – kuanzia Mwinyi, Mkapa hadi Kikwete waliahidi kupambana na ufisadi lakini hakuna aliyefanikiwa. Zao zimebakia, mpaka sasa, kuwa ni ahadi hewa. Hata wagombea urais wetu wa sasa – Magufuli na Lowassa wanajitutumua majukwaani kuwa wakiingia Ikulu watapambana na rushwa na ufisadi, lakini hakuna dalili za uwepo wa dhamira za kweli katika kauli zao hizo. Jambo muhimu kwa wasomaji wangu kulifahamu ni kwamba katika Mexico biashara hiyo ya madawa ya kulevya ilianza kidogo kidogo. Na ingawa umma ulipiga kelele ukisaidiwa na vyombo vya habari, lakini watawala waliziba masikio.
Katika Tanzania, kwenye janga la ufisadi, hali ni hiyo hiyo. Wanaharakati, wanataaluma mbalimbali na wananchi wa kawaida wamepiga kelele wee, lakini hakuna hatua madhubuti zinazochukuliwa mbali ya maneno matupu.
Tumefika mahali hata mgombea urais anayetuhumiwa miaka mingi kwa ufisadi (Lowassa) naye sasa kwenye kampeni anajipa ujasiri wa kutamka kuwa akiingia Ikulu atapambana na rushwa na ufisadi!
Tumefika mahali mgombea urais wa CCM, Magufuli naye anatamba kwamba akiingia Ikulu ataanzisha mahakama maalumu kwa ajili ya mafisadi; kana kwamba tatizo letu la sasa ni uhaba wa mahakama za kuwashitaki!
Ni nani asiyejua kwamba tatizo si upungufu wa mahakama nchini; bali tatizo ni utamaduni wa kijinga wa Serikali ya chama tawala CCM wa kutowakamata na kuwashitaki mafisadi (impunity culture)?
Tukirudi Mexico, kidogo kidogo mashamba ya kulima mimea inayotengeneza madawa ya kulevya yakaongezeka vijijini. Ikafikia hatua kikaanzishwa kikundi cha kiharamia cha kusimamia biashara hiyo haramu, lakini bado watawala waliendelea kulaza damu. Na kwa sababu hiyo, sasa biashara hiyo katika Mexico imekuwa zimwi kubwa ambalo halikamatiki. Kutoka katika kuwa na kikundi kimoja tu cha kiharamia kinachosimamia biashara hiyo, sasa kuna vikundi (cartels) vikubwa visivyopungua sita. Baadhi ya vikundi hivyo vya kiharamia, kama kile kinachoitwa Sinaloa Cartel, kinachoongozwa na Joaquim "El Chapo" Guzman, kimefikia hata hatua ya kuwa na jeshi lake kwa ajili ya kupambana na vikundi vingine kugombea maeneo na ruti za biashara hiyo, na pia kwa ajili ya kupambana na polisi au vikosi vya serikali.
Watawala wa Mexico walipozinduka na kuanza kupambana na biashara hiyo, wakakuta zimwi limeshakuwa kubwa. Hivi sasa, si tu kwamba vikundi hivyo vina majeshi yake, lakini pia vina mtandao mkubwa kiasi kwamba vimechomeka 'watu wao' ndani ya serikali – kuanzia kwenye polisi na majaji hadi kwenye wanasiasa na watawala serikalini. Lakini si hivyo tu; kwani mafisadi hao baada ya watu wao kukamata dola, walianza kuyatumia mabilioni ya mapesa wanayoyavuna katika biashara hiyo kupelekea maendeleo katika baadhi ya maeneo! Pale ambako hapakuwa na barabara, kina "El Chapo" wakajenga barabara. Pale ambako hapakuwa na shule au hospitali, kina "El Chapo" wakajenga hospitali.
Kwa maneno mengine, pesa chafu inayotokana na madawa ya kulevya ikatumika kuwarubuni wananchi kwa kuwajengea vitu hivyo vya maendeleo. Na kwa sababu hiyo, kina "El Chapo" wametokea kupendwa mno katika baadhi ya maeneo ya Mexico kuliko wanavyopendwa viongozi wa serikali! Ndugu zangu, hiyo ni Mexico. Ni hali ambayo namwomba Mungu isitokee Tanzania. Na hatari hiyo ipo. Wakati ambapo vita ambayo Mexico inapigana nayo ni dhidi ya biashara ya madawa ya kulevya, hapa Tanzania vita ambayo tunapigana nayo ni dhidi ya ufisadi ambao humo ndani imo pia biashara hiyo!
Kwa karibu miongo miwili sasa tangu ufisadi ukithiri nchini, hakuna mafanikio yoyote ya maana dhidi ya janga hilo. Kama Mexico, nasi tumebadilisha marais lakini hakuna rais aliyefanikiwa kushinda vita hiyo. Kama Mexico, nasi tumeimarisha TAKUKURU yetu lakini hakuna dalili za mafanikio. Kama Mexico, nasi tumefanya mabadiliko katika sheria zetu kadhaa na hata kutunga mpya (kama hii ya kudhibiti matumizi ya pesa wakati wa uchaguzi), lakini hakuna mafanikio ya wazi yanayoonekana.
Isitoshe, sasa tumefikia hatua mbaya kabisa ambapo fedha chafu za mafisadi zinatumika kutuchagulia viongozi wa kututawala. Tumefika mahali ambako hata mtuhumiwa wa miaka mingi wa ufisadi (Lowassa) sasa tunaona ndiye anayefaa kuwa rais wetu! Na tunamshabikia kwa maelfu kama ambavyo Mexico wanawashabikia kina 'El Chapo' wao! Ni kwa nini vita hii ya ufisadi inaelekea kutushinda Watanzania? Nauliza hivyo, maana hata Chadema ambacho kilikuwa mbele katika vita hiyo sasa kimeitosa! Nahisi jibu ni kama lile lile la Mexico; nalo ni kwamba tumechelewa kujitosa katika uwanja wa mapambano, na tulipoamua kufanya hivyo tukakuta mtandao wa ufisadi umeshakuwa mkubwa mno na unaogusa kila sekta. Ni dhahiri kwamba kama tukiendelea kuupuuza utafanikiwa kukamata dola.
Hilo likitokea – yaani wakifanikiwa kukamata dola (Ikulu), basi 'timu' ya mtandao wa ufisadi katika Tanzania (Mafioso and Mafisadi United - MMU) itakuwa imepata ushindi mkubwa, na inaweza kutuchukua miaka 50 kufanikiwa kuuondoa Ikulu! Kwa maoni yangu, utawala wao utakuwa wa hovyo mno kuliko huu wa sasa wa CCM. Naweza kubashiri nini kitatokea kama 'timu' ya Mafioso and Mafisadi United itakamata Ikulu. Kitu hicho ni kwamba watu wao watakamata karibu kila sekta muhimu za uchumi katika Tanzania.
Lakini si hivyo tu. Kila sekta ya kiutawala watajaza watu wao. Yaani kuanzia makamanda wa polisi, JWTZ hadi Usalama wa Taifa watachomeka watu wao. Watachomeka pia mahakimu wao, majaji wao, mawaziri wao, madaktari wao, watu wao katika mabenki (ikiwemo BOT), watu wao kwenye bureau de change, na hata waandishi wao wa habari nk! Yaani Tanzania itakuwa kama Mexico.
Kama ilivyo katika Mexico, mtandao wa mafisadi katika Tanzania nao ukikamata dola utakuwa huru kutumia pesa chafu zilizopatikana kwa njia za kifisadi (kama ten percent za mikataba ya vitalu vya gesi asilia na mafuta) kuwaletea wananchi 'maendeleo' katika majimbo ya wabunge wao! Na ndiyo maana nasema ya kuwa itakuwa vigumu mno kuwaondoa madarakani wakishakamata dola. Kama ilivyo Mexico, itakuwa vigumu kwa wanavijiji Tanzania watakaonufaika na visima, zahanati na shule zilizojengwa kwa pesa chafu za mafisadi hao kufanya uasi wa kutowapigia kura za urais, udiwani na ubunge katika chaguzi zitakazofuata kila baada ya miaka mitano.
Ndo maana nasema yaweza kutuchukua miaka 50 kuiondoa Ikulu 'timu' ya Mafioso and Mafisadi United–MMU; hata kama kila baada ya miaka mitano uchaguzi mkuu utafanyika nchini kama kawaida.
Ndugu zangu, nimetumia mfano wa Mexico kujenga hoja kuhusu hatari ya kweli itakayotukabili Tanzania kama tutawaacha mafioso na mafisadi wakamate dola kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25. Hivi sasa wafanyabiashara na mabilionea kadhaa (si wote) katika Tanzania wanaounda 'timu' hiyo ya MMU wamehamishia nguvu zao Chadema baada ya Edward Lowassa kuhamia huko na kupewa nafasi ya kuwania urais!
Wana Chadema wenyewe wanatamba kwamba hiyo haijalishi; ilimradi tu 'timu' hiyo ya MMU inawasaidia kuing'oa CCM madarakani! Ukweli ni kwamba Chadema ya sasa siyo tena kile chama makini, adilifu na kilichouchukia ufisadi. Hiki (Chadema) cha sasa kimegeuka na kuwa chama chenye viongozi wenye uroho wa pesa na wa kutaka madaraka ya haraka haraka, na ndiyo maana hivi sasa kinakimbiliwa na mafisadi kadhaa waliokuwa CCM; hasa baada ya kuitosa ajenda yake ya vita dhidi ya ufisadi.
Sasa, ikizingatiwa ukweli kwamba afya ya Lowassa siyo nzuri sana kuweza kuendesha nchi kwa ufanisi kama akiwa rais, ni dhahiri kutakuwa na ombwe la uongozi na mkanganyiko wa hali ya juu katika 'serikali tarajiwa' ya Chadema.
Nionavyo, ni katikati ya mkanganyiko huo wa uongozi 'timu' ya Mafioso and Mafisadi United - MMU itafanikiwa kupachika watu wao katika kila sekta muhimu ya uchumi nchini ili iweze kufanikiwa vilivyo na maliasili za Tanzania. Ni katikati ya mkanganyiko huo tarajiwa tunaweza kushuhudia wafanyabiashara mabilionea ndani ya MMU wakigawana vitalu vya gesi asilia na mafuta kana kwamba si mali yetu sote! Watagawana vitalu hivyo ili wapate kuvifanyia ukuwadi kwa makampuni ya Wazungu (rejea kitabu cha Prof Chachage – Makuwadi wa Soko Huria).
Hebu jiulizeni: Ni kwa nini wafanyabiashara hao mabilionea wanamwaga mapesa yao kumsaidia Lowassa kukamata dola? Je, ni kwa sababu tu ni rafiki yao na wanampenda? Je, ni kwa sababu wanawapenda Watanzania na wanawaonea huruma kwa jinsi wanavyopigika kimaisha? Sijui wewe unafikiriaje, lakini mimi naamini wanafanya hivyo kwa sababu (Lowassa akiwa rais) wanaiona fursa ya kweli na ya uhakika ya kujitajirisha zaidi na maliasili za Tanzania. Na kwa sasa, ni gesi asilia na mafuta; maana ndizo maliasili pekee za uhakika tulizosalia nazo baada ya migodi ya madini (kama tanzanite) kuanza kukauka huku tukiachiwa mashimo!
Ndiyo maana ni wajibu wetu sote kuzinusuru maliasili hizi pekee za uhakika tulizosalia nazo zisiangukie mikononi mwa 'timu' ya Mafioso and Mafisadi United -MMU inayotaka kuzitwaa ikishakamata dola. Nilisema hapo mwanzo kwamba utawala mbovu wa CCM ndani ya kipindi cha miongo mitatu umeifanya nchi yetu Tanzania kufanana na Mexico; yaani tumejenga utamaduni wa kutowakamata na kuwashitaki mafisadi (impunity culture). Katika hilo, niongeze kwamba hali itakuwa mbaya zaidi kama Chadema hii ya sasa na mgombea urais wake watakamata dola.
Kwa nini nasema hivyo? Ni kwa sababu baadhi ya watuhumiwa hao wa ufisadi ndani ya CCM wamehamia na wataendelea kuhamia katika chama hiki kilichokuwa alama ya vita dhidi ya ufisadi nchini – yaani Chadema. Baadhi yao ndiyo watakaounda serikali mpya (mawaziri, ma-RC, ma-DC nk) kama Chadema kikishinda uchaguzi.
Je, ufisadi nchini utapungua au utaongezeka kama Chadema kikitwaa dola chini ya taswira yake ya sasa ya kuwakumbatia watuhumiwa wa ufisadi kutoka CCM waliohamia katika chama hicho kumfuata Edward Lowassa? Je, mtuhumiwa wa jana wa ufisadi ambaye hakuwahi kusafishiwa tuhuma hizo na mahakama anaweza leo kuwa championi wa vita dhidi ya ufisadi? Au ndo ule msemo wa Kiswahili – Mchawi mpe mwanao akulelee?! Majibu unayo mwenyewe.
Ndugu zangu, naiona hatari ya kweli ya nchi yetu kuzidi kuelekea iliko Mexico ya sasa kama Chadema kitakamata dola kikiwa na taswira yake ya sasa. Naiona pia hatari ya kweli inayokabili vitalu vyetu vya gesi asilia na mafuta kama Chadema kitakamata dola kikiwa na taswira yake ya sasa. Yaani Chadema yenye mwelekeo tofauti kabisa na wa huko nyuma.
Nihitimishe kwa kusisitiza tu kwamba wengi tulijenga imani na chama hiki (Chadema) kwamba ndicho ambacho kingekuwa mbadala wa CCM katika kuirudisha nchi yetu kwenye reli sahihi. Sasa si hivyo tena. Kwa usaliti kilioufanya wa kuwakaribisha watuhumiwa wa ufisadi kutoka CCM kugombea nafasi za uongozi ikiwemo ya urais, sitatokwa na machozi Oktoba 25 itakapodhihirika kwamba kimepigwa tena mweleka na CCM licha ya kuungwa mkono na 'timu' nzima ya MMU!
Kwa hakika nitafurahi. Nitafurahi kwa sababu gesi yetu asilia na mafuta vitakuwa vimesalimika kuangukia mikononi mwa mabilionea wa 'timu' ya Mafioso and Mafisadi United - MMU. Yaani maliasili zetu hizo zitasalimika wakati tukiendelea kutafuta chama kingine cha upinzani mbadala wa Chadema kukiingiza Ikulu kuchukua nafasi ya CCM. Kwangu mimi itakuwa ni wakati mwafaka wa kutafuta chama kingine mbadala cha Upinzani ambacho kwacho nitajenga upya matumaini yangu ya kuondolewa CCM madarakani na kuingizwa chama kipya kilicho bora zaidi. Ndoto hiyo itaishi, haifi.
Labda nihitimishe kwa kusema kwamba, mpaka sasa, chama cha upinzani mbadala wa Chadema kinachoanza kunivutia kwa umakini wake na sera zake nzuri ni ADC Wazalendo cha Zitto Kabwe. Licha ya kwamba hakijatimiza hata umri wa mwaka mmoja, ADC Wazalendo kimeibuka na hati muhimu inayoitwa Azimio la Tabora. Azimio hilo ambalo ndilo dira ya chama hicho linaihuisha siasa ya Ujamaa na Kujitegemea ya Mwalimu Nyerere kulingana na mazingira ya sasa.
Ni siasa hiyo ndiyo inayoweza kuwahakikishia Watanzania kupata 'mgao' unaoridhisha wa keki ya taifa. Siasa hiyo ndiyo pia inayoleta matumaini ya kupunguzwa kwa pengo kati ya matajiri na masikini - pengo linalokua kwa kasi nchini.
Si hivyo tu. Licha ya kwamba ADC Wazalendo hakijafikisha umri wa mwaka mmoja, kimeibuka na ilani nzuri ya uchaguzi kuliko ya Ukawa ambayo inajumuisha vyama vinne kikiwemo Chadema!
Na mwisho, licha ya kwamba uhai wake ni wa miezi michache tu lakini ADC Wazalendo kimeweza kusimamisha wagombea ubunge 219 kati ya majimbo 265 nchini; ilhali Chadema, licha ya umri wake mkubwa, kimeweza kusimamisha wagombea 139 tu. Kwa ufanisi huo kiliouonyesha ndani ya kipindi kifupi cha uhai wake, kwa nini nisiamini kwamba miaka si mingi chama hicho cha Zitto Kabwe kitakuwa mbadala wa Chadema katika siasa za Tanzania? Tafakari.
0 Comments