Wasomi na CCM: Tutimize wajibu wetu mwaka 2015!
Imeandikwa na Dkt. Hamisi Kigwangalla.
Makala, Raia Mwema, Septemba 2, 2015.
Kuna mtu amesema uchaguzi wa mwaka 2015 ni kipimo kikubwa kupata kutokea nchini cha imani ya watanzania juu ya chama hiki kikongwe, chenye sura ya kitaifa, chenye historia ya kusimamia ukombozi wa nchi nyingi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara kutoka kwenye mikono ya kidhalimu ya wakoloni, na chenye historia ya kuasisiwa kutokana na vyama vilivyopigania uhuru wetu.
Chama Cha Mapinduzi, CCM, kimegusa kwa namna moja ama nyingine maisha ya watanzania wote katika nyakati mbali mbali. Ni mtu mwenye uchu wa madaraka, asiyejitambua ama anayefuata upepo tu atakayekana ukweli huu.
Hebu tuwaangalie kwa umakini viongozi vinara wa upinzani na kama hawajawahi kuguswa ama kufaidika na CCM – hakuna. Kuanzia waliosomeshwa na serikali ya CCM bure, walioajiriwa na serikali ya CCM, waliowekewa mazingira rafiki wakafanya shughuli za kilimo na biashara vizuri wakatajirika mpaka wale waliopewa uhuru wa kuanzisha vyama vyao binafsi vya siasa na kuanza kuitukana serikali ya CCM kwa uhuru uliopitiliza bila kuadhibiwa.
Wote hawa ni wanufaika halali kabisa wa CCM na sera na maamuzi yake katika nyakati mbalimbali.
Hata hivyo, CCM haipaswi kujitapa kwa haya, maana itavimba kichwa visivyo, maana ni yenyewe iliamua kutanua demokrasia kwa kuruhusu mfumo wa vyama vingi kinyume na matakwa ya wananchi – kwa kuwa wananchi walisema (kwa asilimia 80 kabisa!) kuwa wanataka mfumo wa chama kimoja ubaki kama ulivyo, na pia kwa sababu toka mwaka 1977 CCM ilipoanzishwa hakukuwa na chama kingine zaidi yake, na haya mambo yalipaswa kufanywa na chama cha siasa, na hakukuwa na namna nyingine yangefanyika nje ya mfumo uliokuwepo.
Sisi wasomi tuliopata fursa ya elimu tuna wajibu wa kuilinda CCM kwa kueleza ukweli popote pale tulipo, kuwa bila CCM madhubuti, bila CCM madarakani, nchi yetu itayumba. Hivi kiukweli kwa sasa kuna chama gani cha siasa chenye itikadi inayoeleweka na kuaminika kwa wananchi zaidi ya CCM? Ni kweli kuna vyama vya siasa, lakini bado vichanga sana na vinahitaji muda wa kukua kabla ya kuaminiwa na umma kushika dola.
Ni lazima tujiulize na tuchambue, kama kweli kuna chama kingine chochote cha siasa chenye sura ya utaifa zaidi ya CCM, ama kwa usawa na CCM, ama chama kilicho imara kitaasisi – kimuundo, kisera na kiitikadi zaidi ya CCM…kama hakipo je tuko radhi kishike dola chama kingine chochote kisicho na sura na sifa hizo ama chenye sura ya ukabila, ukanda ama udini?
Tufikirishe mbongo zetu jamani, walau kidogo tu; tuamke tuitazame nchi yetu kwa jicho la kizalendo zaidi. Tutoke kwenye ndoto za mchana kuwa tunaweza kupata mabadiliko kwa haraka na kwa uhakika zaidi tukiwa na chama cha upinzani ambacho kinaundwa na watu waliodumu kwenye mfumo wa Chama Cha Mapinduzi maisha yote kwa kuwa tu leo wamehamia upinzani?
Je tunasahau kuwa CCM inaleta usawa, udugu, umoja na mshikamano wa kitaifa? Tunu ambazo zinatusaidia kudumisha amani, upendo na utulivu wa Taifa letu? Tunu ambazo ni nguzo ya jamii yoyote yenye kusonga mbele kwenye nyanja zote za maendeleo?
Nchi yoyote ile baada ya kufanikiwa kudumisha demokrasia; kuimarisha mfumo wa kutoa haki kwa watu wake; kudumisha amani, upendo, umoja na mshikamano, inabaki na wajibu mmoja mkubwa mbele yake – kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo. Tanzania ya miaka ya 60 ilijenga misingi ya maendeleo ya jamii iliyotupeleka mpaka miaka ya 90, ambapo tulitanua wigo wa demokrasia na kujenga mfumo mpya wa uchumi unaotokana na soko huria. Japokuwa si kwa utashi wetu, lakini ilikuwa ni uamuzi sahihi wa kufanya kwa nyakati hizo.
Mfumo wa uchumi wa soko huria tulioufuata miaka ya mwanzoni mwa 90, kufuatia uamuzi usio maarufu sana wa 'Azimio la Zanzibar' unakuja na mambo yafuatayo; kwanza, bei hazipangwi na serikali bali nguvu ya soko inaamua wauzaji na wauziwa watauzaje na watanunuaje kwa makubaliano yao, pili, njia kuu za uzalishaji zinatoka kwenye mikono ya serikali na kwenda kwenye mikono ya watu ama taasisi binafsi, na tatu, kwa uwepo wa hali hizo hapo juu ni lazima tutegemee uwepo wa ushindani mkali baina ya watu na taasisi binafsi kwenye Nyanja zote za uchumi na jamii kwa sababu aina hii ya uchumi inatia motisha ya ushindi na mafanikio kwa atakayepigana zaidi na kwa umahiri kuliko mwingine.
Lakini pia, aina hii ya uchumi inaleta matabaka baina ya watu wenye nacho na wasio nacho, na iliwafanya watu waliokuwa na ahueni ya kimaisha wakati tunaingia kwenye mfumo huu, ama waliokuwa na elimu na ajira wakati huo, kuwa kwenye nafasi nzuri zaidi kuanza kupigana kuutafuta ushindi na mafanikio kuliko wenzao. Pia hali hii, kwa kuwa ilikuwa haijazoeleka, na kulikuwa na wengine ambao hawakuwa na pa kuanzia, kwa hakika walishikwa na mduwao na hawakujua la kufanya, wengine mpaka leo bado hawajaelewa nini kilitokea na wanapaswa kufanya nini. Bahati mbaya sana serikali yetu na chama chetu hakikuwaandaa.
Na mpaka leo bado wapo wasioelewa nini cha kufanya. Wote hawa wanarusha lawama kwa CCM na serikali yake. Saa nyingine lawama hazina msingi, saa nyingine si lawama za kweli, lakini CCM na serikali yake haiwezi kukwepa lawama hizi. Mzigo wa shida, kero na ndoto za watanzania ni wa CCM na haiwezi kuukwepa.
Walau sisi tunaoelewa nini kilitokea na nini kinaendelea kwenye mfumo wa maisha ya jamii ya watanzania, pengine sababu ya kupata elimu na kuwa kwenye uongozi, tuna wajibu wa kufanya – tunalazimika kuwaelimisha watanzania kilichotokea na kuwahamasisha wajue nini cha kufanya kwenye uchumi mpya wa kushindana. Waelewe kwamba sasa elimu ni ya kulipia na kwamba serikali inawajibika kuandaa taasisi bora za kutoa elimu na wananchi wanaoitaka elimu ni wajibu wao kuigharamia – japokuwa hatujafika huko na kwamba bado serikali inagharamia kwa kiwango kikubwa, bado tunalazimika kuchangia.
Wananchi wana haki ya kuelimishwa kuwa huduma za afya si za bure tena kama ilivyokuwa kabla ya miaka ya 90, tunalazimika kuchangia na kwamba wajibu wa serikali ni kujenga taasisi bora za kutoa huduma ya afya, na kwamba serikali itawajibika kutoa huduma hizi bure kwenye makundi maalum tu kama wazee wenye umri zaidi ya miaka 60, wanaoishi kwenye mazingira magumu, akinamama wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano.
Yote haya hayawezi kueleweka kirahisi kwenye vichwa vya watanzania tuliolelewa kwenye nchi iliyokuwa na mfumo wa kutuhudumia kwa kila kitu bure.
Leo hii watanzania watalalamika kuwa CCM na serikali yake imeua viwanda, watakumbuka kuwa Mwl. Nyerere alijenga viwanda vingi na watasema viongozi wa sasa wameviua – usemi huu si sahihi kwa mtu anayeelewa kwamba viwanda hivi viliuzwa kwa sababu ya kuiondoa serikali kwenye dhima ya kumiliki njia za uzalishaji mali na kuvihamishia kwenye sekta binafsi, na kule, kwa matakwa ya sera hizi serikali lake jicho tu, mikono mbali! Hiyo sasa ni mali binafsi na serikali haiingilii shughuli za watu binafsi – jukumu lake ni kuleta amani na kuacha wananchi wajenge uchumi wao, na serikali ibaki kukusanya kodi tu na kujenga miundombinu ya kuwezesha ustawi wa watu wake kutokea.
Kwenye mfumo wa uchumi wa namna hii ni lazima watu tufanye kazi kwa bidii ili kuleta maendeleo yetu binafsi na ya taifa, serikali ituwezeshe tu kufikia matamanio na matarajio yetu. Serikali itupe ulinzi wa kisheria na wa kiusalama, kazi ya maendeleo ni yetu wananchi.
Huu mwaka wa uchaguzi, mengi yatasemwa – nasikitika kuwa, wapinzani wa CCM watarundika kila aina ya lawama na mapungufu kwa CCM, ni sawa, maana ni haki yao kufanya hivyo, lakini je, wao wakiingia madarakani watakuwa na jipya? Kutoka wapi kwa mfano!
Kila mtanzania anatakiwa kufanya kazi kwa bidii kukuza uchumi wake na wa Taifa kwa ujumla. Serikali imetekeleza majukumu yake ya msingi kiasi cha kutosha, ndiyo maana tuna watanzania siku hizi wanahesabiwa miongoni mwa watu tajiri zaidi Afrika, wametajirikaje? Si kwa kulala na kusubiri serikali iwape kila kitu – wakati huo ulipita zamani, bali kwa kutumia fursa zilizopo kujenga uchumi wao na wa Taifa letu.
Tupige siasa zetu ndiyo, lakini tuseme ukweli. Kwa sisi tuliopelekwa shule na CCM na serikali yake tukumbuke wajibu wetu – kuusema ukweli kwa faida ya nchi yetu.
Mwandishi wa makala hii ni Daktari, Mbunge Mstaafu wa jimbo la Nzega aliyebobea kwenye Uchumi wa Afya na Afya ya jamii. Ni mwandishi wa Kitabu cha Kigwanomics na Tanzania Tuitakayo na makala mbali mbali.
Hamisi A. Kigwangalla, MD, MPH, MBA
P.O.Box 22499,
Dar es salaam.
Tanzania.
Phone No: +255 754 636963
+255 782 636963
website: www.peercorpstrust.org or www.hamisikigwangalla.com
Email: hamisi.kigwangalla@peercorpstrust.org or info@hamisikigwangalla.com
Skype ID: hkigwangalla
Blog: blog.hamisikigwangalla.com
Unapokea Email hizi kwa sababu umejiunga na Jukwaa la 'Mabadiliko'.
Kuchangia mada tuma kwenye Email hii: mabadilikotanzania@googlegroups.com
For more options, visit this group at:
http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania?hl=en?hl=en
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Mabadiliko Forum" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to mabadilikotanzania+unsubscribe@googlegroups.com.
To post to this group, send email to mabadilikotanzania@googlegroups.com.
Visit this group at http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania.
To view this discussion on the web visit https://groups.google.com/d/msgid/mabadilikotanzania/CAGnhviCtDjbze6doexgA%3DrjG0PFURDeGLxD-TOC%2BcB2meb_j-Q%40mail.gmail.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 Comments