[Mabadiliko] CCM WANAJIDANGANYA

Friday, September 18, 2015
CCM WANAJIDANGANYA

Na Ananilea Nkya

Chama cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake wanapaswa wasijidanganye kwamba kwa kumteua Dr John Magufuli kuwa mgombea wa Urais chama hicho kimekuwa kisafi na na hivyo kinaweza kuwatumikia wananchi na kuondoa umaskini unaoumiza mamilioni ya wananchi nchini hivi sasa.

Hakuna chama chochote cha siasa duniani kimeweza kujisafisha kikiwa madarakani.

Zaidi siyo dhambi wala aibu kwa chama cha siasa kushindwa uchaguzi. Ni jambo la kawaida na ni heshima pia kama chama cha siasa kinakubali kushindwa uchaguzi ikiwa imetokea hivyo.

Chama cha siasa kinaposhindwa uchaguzi na kukubali kushindwa kinastahili kupongezwa na kuheshimiwa.

Hivyo hakuna mamtiki yoyote kwa CCM kutumia propaganda kwamba kwa mgombea wake wa Urais kupata watu kwenye mikutano ya kampeni basi tayari kimeshinda kwa asilimia 69.3. Huku ni kujidanganya na kudanganya umma.

Kama umati wa watu ndicho kigezo cha ushindi wa CCM takwimu hizi zinapingana na hiki kigezo kwa sababu viko vyama vingine pia ambavyo vimekuwa vikipata umati mkubwa wa watu kwenye mikutano—tena wanaokwenda kwa hiari na gharama zao.

Je vyama hivi na vyenyewe vikifanya propaganda na kutangaza kwamba kutokana na wingi wa watu wanaohudhuria mikutano yao vinaweza kushinda kwa asilimia 80 nchi itakuwa imewekwa katika hatari kiasi gani baada ya uchaguzi ?

CCM na serikali yake inapaswa kutambua kuwa siasa za ushindani katika nchi zikiendeshwa vema bila chama chochote kuendesha propaganda kwa lengo la kubaki madarakani hata wakati kimekataliwa na umma ni kuvuruga amani na kuongeza umaskini katika nchi.

Imetokea katika nchi kadhaa duniani vyama vilivyotawala muda mrefu vimeondoka madarakani na nchi hizo zikabaki salama na kupiga hatua kubwa ya kimaendeleo.

Mfano nchi jirani za Kenya na Zambia vyama vikongwe vimeshindwa na vyama vingine vimepewa ridhaa na wananchi wan chi hizo na vimeendesha nchi bila matatizo yoyote na maisha ya wananchi yanasonga mbele.

Vyama vingi vinawezesha chama kinachopewa ridhaa kikishindwa kutekeleza ahadi zake kupunzishwa kwa muda ili kujipanga upya nan a kwa kufanya hivyo kinalazimika kuacha jeuri dhidi ya wananchi, uzembe , ufisadi na rushwa.
Chama cha siasa kikishapunzishwa kwa muda na kujisafisha, hulazimika kubuni sera nzuri za maendeleo na mikakati ya kuzitekeleza na chaguzi zinazofuata kikiomba tena ridhaa kwa wananchi na kinakubaliwa.

Hapa ndipo mfumo wa vyama vingi unakuwa na manufaa kwa nchi husika. Kuondoa umaskini miongoni mwa wengi na kuiletea nchi maendeleo.

Vinginevyo rasilimali za nchi zinabaki kunufaisha watawala wachache na wawekezaji wa nje katika zama hizi za utandawazi wizi, soko holela na utandawaziwizi wa zama za ukoloni mpya kibepari duniani unaofukarisha mafukara mamilioni ya wananchi.

Wanaoitetea CCM ibaki madarakani wanapaswa kujiuliza : Ni kwa nini CCM ing'ang'anie madaraka na isipewe muda wa kupunzika, kujitafakari, kujisafisha na kupata nguvu na maono na sera ya mapya za kuongoza nchi yetu ili Tanzania ipae kimaendeleo?

Ni kwa nini nchi yetu iendelee kuongozwa na CCM ilichochoka kiasi kwamba sera zake kila uchao zinazaa mamilioni ya wananchi maskini wa kutisha wakiwepo wanachama wengi wa CCM na huku viongozi wakiwa matajiri wa kutishwa kutokana na ufisadi, rushwa, uzembe, uvivu na watawala kutafuna fedha za wananchi kwenye miradi ya umma na kujipangia safari za nje ya nchi tena kwa kupanda ndege daraja la kwanza kwenda kuomba misaaada kama neti za mbu au kuchukua digrii ya heshima?

Hebu fikiria kwa mfano Mwenyekiti mwenza wa UKAWA, James Mbatia ameweka bayana kwamba Rais Jakaya Kikwete katika kipindi ccha utawala wake amesafiri nje ya nchi mara 409 na safari hizo ziligharimu shilingi trilioni 4.5.

Maana yake angalao kila mwaka Rais alisafiri nje ya nchi mara 40 akipoteza siyo tu fedha alizotumia kwa safari hizo bali pia muda mwingi wa kuwatumikia Watanzania.

Mbatia alisema safari hizo za nje zingepunguzwa kwa asilimia 80 zingepatikana fedha ambazo zingetosha kujenga vyuo vikuu 80 nchini kila chuo kikigharimu shilingi bilioni 50.

Aidha fedha hizo zingeweza kujenga vyuo vya ufundi 200 nchi nzima kila chuo kikigharimu bilioni 20. Kadhalika fedha hizi zineweza kujenga hospitali 100 na kila hospitali ikigharimu bilioni 30.

Je kwa hali hii kuna Mtanzania hata awe mwana CCM mwenye akili timamu na anayeipenda Tanzania kwa dhati kabisa na anayeweka mbele maendeleo ya nchi yetu na mamilioni ya watu wake ambaye atatelea CCM iendelee kuongoza nchi yetu miaka mingine mitano kuanzia tarehe 25 Oktoba mwaka huu 2015?

Ni mwanaCCM wa aina gani asiye na huruma na mamilioni ya Watanzania wanaoteseka kwa umaskini ambaye atataka CCM iendelee kuwa madarakani huku watawala wakijinufaisha kwa kusafiri nje ya nchi kwa fedha ambazo zingeweza kutoa elimu bora hadi chuo kikuu, huduma bora za afya maji safi na salama au kujenga barabara au viwanda vya kutoa ajira ?

Mbona hata CCM wenyewe wanajua kuwa sera za chama chao hakiuziki katika uchaguzi wa mwaka huu na ndiyo sababu badala ya kuuza chama na sera zake wanauza mgombea wao wa urais Dr John Magufuli?

Hata hivyo wananchi wanafahamu kuwa makubaliano ya uongozi wa nchi ni kati ya chama/vyama vinavyoomba uongozi wa nchi na wananchi na siyo kati ya mgombea Urais wa chama fulani na wananchi.

Hii ina maana kuwa mwisho mwa siku ni chama/vyama husika vinavyoomba ridhaa ya kuongoza nchi ndivyo vitawajibika kutekeleza ahadi zake kwa wananchi. Ahadi zisipotekelezaka uchaguzi unaofuata wananchi wanachukua maamuzi sahihi kupitia sanduku huru la kura.

CCM isijidanganye kuwa Dr Magufuli ndiye CCM maana CCM ni taasisi ni chama cha siasa na kwa taratibu za uchaguzi makubaliano ya kuongoza nchi hufanyika baina ya vyama vya siasa na wananchi na siyo baina ya mgombea Urais na wananchi.

Makubaliano ya kuongoza nchi yanakuwa ni kati ya vyama vya siasa na wananchi kwa sababu mgombea kama binadamau anaweza kuondoka katika chama kwa sababu mbali mbali lakini chama cha siasa kama taasisi kinabaki, hakiondoki na hivyo kitakuwa kitadaiwa utekelezaji wa ahadi zake kwa wananchi.

Hebu fikiria kama vyama vinavyounda UKAWA vingekuwa vimeingia makubaliano na mtu mmoja mmoja mfano CUF (Prof Ibrahim Lipumba) au CHADEMA (Dr Wilbroad Slaa). Je leo hii UKAWA ingekuwa ipo na kuendelea kufanya kazi nzuri ya kisiasa kwa maendeleo ya nchi yetu kama ambavyo imekuwa ikifanya hadi sasa?

Kwa hiyo ni vema wanaCCM na viongozi wa CCM katika uchaguzi wa mwaka huu 2015 wakaanza kujiandaa kisaikolojia kwamba CCM inaweza ikashindwa au ikashinda kwenye uchaguzi badala ya kufanya propaganda zinazoashiria kuwa hakiko tayari kuondoka madarakani hata kama kitakuwa kimekataliwa na wananchi kwenye sanduku huru la kura.

Aidha ni muhimu hasa viongozi waandamini ndani ya CCM na serikali yake kutambua kuwa katika siasa za vyama vingi maendeleo ya nchi yanapatikana kwa haraka zaidi na umaskini miongoni mwa wananchi walio wengi unapungua kwa kasi endapo uchaguzi unafanyika kwa uhuru na haki.

Kadhalika watambue kuwa ni kawaida na ni afya kwa nchi kama chama kilichokaa madarakani muda mrefu kikishindwa kukubali kushindwa bila kulazimisha ushindi kwa goli la mkono.

Vile vile watambue kuwa kitendo chochote cha CCM na watawala wa serikali ya CCM kuzuia chama kingine cha siasa kisiongoze nchi yetu katika kipindi cha miaka mitano ijayo, hata pale wananchi watakapokuwa wameamua hivyo ni sawa na kukwamisha maendeleo ya Tanzania na kutaka mamilioni ya Watanzania wanaoishi kwa umaskini waendelee na umaskini wao kwa miaka mingine mitano.

Hiyo haitakubalika. Itakuwa ni sawa na kuanzisha vurugu zenye lengo la kuitumbukiza nchi yetu katika vitendo vya kusababisha kuvunjika kwa amani.
Ni pale tu demokrasia ya vyama vingi inapofanya kazi bila hila kwa Tume ya Uchaguzi kufanya kazi kikamilifu, ubunifu bila upendeleo, chama kilichopo madarakani kuacha kuendesha kampeni kwa kutumia lugha za vitisho, dharau kwa vyama vingine, giliba, rushwa, uchakachuaji na ubabe ndipo wananchi na nchi inaponufaika na mfumo wa vyama vingi vya siasa kwa kutokomeza umaskini.

Mwaka 2011, Rais Kikwete aliwahi kuulizwa na mwanahabari mmoja kutoka nje ya Tanzania kuwa ni kwa nini Tanzania ni maskini ili hali ina rasilimali nyingi za asili zinawezeza kutumika kutajirisha Watanzania wote na alimjibu kuwa hajui.

Hata hivyo, Rais Kikwete anapaswa kutambua kuwa moja ya sababu zinazochangia umaskini kuitafuna Tanzania ni CCM kutokukubali kwa dhati mfumo wa vyama vingi vya siasa ufanye kazi inavyotakiwaili hali chama hicho kimeshaacha falsafa ya Ujamaa iliyoendana na mfumo wa chama kimoja nabadala yake imebeda falsafa ya ubepari inayoendeana na mfumo wa vyama vingi.

Kuthibitisha kuwa CCM bado haijakubali mfumo wa vyama vingi ufanye kazi, Rais mstaafu Benjamini Mkapa akipiga Kampeni kule Bukoba katika uchaguzi wa mwaka huu 2015 alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema kuwa vyama vya upinzani havistahili kupewa dhamana ya kuongoza mpaka vifikishe umri wa miaka 50.

Wananchi wanajiuliza ni kwa nini CCM isubiri hadi vyama vya upinzani vizeeke ndipo vipewa ridhaa ya kuongoza nchi?

Hii kauli ya Mkapa inatukumbusha Watanzania zama za ASP na TANU vilipokuwa vinapigania uhuru kutoka kwa wakoloni mbapo mwishoni mwa miaka ya 50 ambapo wakoloni kama anavyofanya Mkapa walikuwa wanadai kuwa ASP na TANU vilikuwa bado ni vyama vichanga hivyo havikustahili kupewa ridhaa ya kuongoza Tanzania (Zanzibar na Tanganyika).

Lengo la wakoloni lilikuwa ni kuchelewesha uhuru. Hata hivyo TANU NA ASP vilikaza buti na viliwapuuza wakoloni na uhuru wa nchi yetu ulipatikana bila kuchelewa kama walivyotaka wakoloni.

Hivyo watawala wa CCM wanaotaka CCM iendelee kuongoza nchi wanapaswa kujiuliza ni kwa nini Watanzania wakubali kuacha mali za nchi yao zikiwa zinatajirisha watawala wachache na wawekezaji kutoka nje ya nchi ili hali mamilioni ya Watanzania wakiwepo wanachama wa CCM wengi wakiendelea kubaki maskini na mafukara?

Ni kwa nini CCM isipumzishwe kwa miaka mitano kiweze kujitafakari na kujipanga upya kama kweli kimekubali mfumo wa vyama vingi kwa dhati kabisa na kwa kutambua kuwa siasa za vyama vingi zikiendeshwa kwa uhuru ndipo nchi yetu itaweza kukomesha uzalishaji wa mafuriko ya wananchi maskini katika nchi yetu ili hali nchi yetu ni tajiri wa mali asili—madini, gesi, maji, misitu an ardhi yenye rutuba?

Nadhani Rais mstaafu Mkapa alitoa kauli hiyo au kwa vile hajatafakari vema manufaa ya siasa za vyama vingi na umuhimu CCM kukubali kushindwa uchaguzi kwa uhuru na haki kwa kusikiliza na kuheshimu maamuzi ya umma .

Vinginevyo alitoa kauli hiyo kwa sababu hajaishi maisha wanayoishi Watanzania walio wengi ambao wanateseka kwa umaskini.

Hata hivyo ni vema Rais mstaafu Benjamin Mkapa akatambua kuwa wajibu wake kama Rais mstaafu kwa taifa hii kwa sasa siyo kulinda maslahi ya watawala wachache wa CCM ambao wanadhani kwa CCM kuondoka madaraka Tanzania itaharibikiwa.

Mkapa pia anapaswa kuwaonya baadhi ya viongozi wa CCM wanaopanda majukwaani na kuweweseka kwa kusema kuwa CCM kamwe haiwezi kuviachia vyama vya upinzani kuongoza nchi.

Wanaoweweseka na kusema CCM haiwezi kuviachia vyama vya upinzani kuongoza nchi wanathibitisha kuwa serikali ya CCM inaendesha mfumo wa vyama vingi kama geresha lakini watawala wa serikali ya CCM hawako tayari kuona CCM inaondoka madarakani kwa amani hata kama wananchi watakuwa wameamua hivyo kupitia sanduku huru la kura. Hii haikubaliki.

Ndiyo sababu baadhi ya wananchi wanajiuliza: Je CCM na serikali ya CCM yake mwaka huu 2015 watatumia kwa 'goli la mkono' kuzuia maamuzi ambayo wananchi wa Tanzania watakuwa wamefanya kupitia sanduku huru la kura kuhusu hatma ya uongozi wa nchi yao ?

Kama serikali ya CCM watafanya hivyo, watakuwa wamejidanganya na kudanganya Watanzania na ulimwengu kuwa Tanzania nchi nchi ya vyama vingi vya siasa.

Badala yake Tanzania itakuwa inaendelea kuwa nchi ya chama kimoja cha siasa maana vyama vingi vya siasa havitaweza kuendeshwa kwa uhuru na ufanisi unaopaswa bila kuwekwa misingi ya kuondoa umaskini nchini --misingi ambayo itawekwa na Katiba Mpya inayotokana na maoni ya wananchi haitaandikwa.

Lakini zaidi CCM na serikali yake watakuwa wamejidanganya kwa sababu watakuwa wamefanya maamuzi mabaya ya kutaka kuendelea kutengeneza bomu la mamilioni ya Watanzania maskini na kikundi kidogo cha watawala matajiri wa kutisha hali ambayo itahatarisha zaidi amani na utulivu wa Tanzania tuendako.

Tukifika hapo wawekezaji wa kigeni na wafadhili (wakoloni wa zama hizi mpya za utandawazi wizi ) watachekelea sana maana watakuwa wamepata mwanya mpya wa kuibia zaidi Tanzania . Mungu ibariki Tanzania tusifike huko

Note: Naruhusu anayetaka kuchapisha Makala hii afanye hivyo. Lengo tuelemishane kwa manufaa ya nchi yetu na wananchi wote.

Ananilea Nkya
 E-mail:ananilea_nkya@yahoo.com

--
Unapokea Email hizi kwa sababu umejiunga na Jukwaa la 'Mabadiliko'.
Kuchangia mada tuma kwenye Email hii: mabadilikotanzania@googlegroups.com


For more options, visit this group at:
http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania?hl=en?hl=en
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Mabadiliko Forum" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to mabadilikotanzania+unsubscribe@googlegroups.com.
To post to this group, send email to mabadilikotanzania@googlegroups.com.
Visit this group at http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania.
To view this discussion on the web visit https://groups.google.com/d/msgid/mabadilikotanzania/1442593614.54616.YahooMailBasic%40web163901.mail.gq1.yahoo.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Related Posts

0 Comments