[wanabidii] ‘Lowassa-mania’ na ya mpiga filimbi wa Hamelin!

Thursday, August 27, 2015

'Lowassa-mania' na ya mpiga filimbi wa Hamelin!


  Tumesahau ya Augustine Mrema 1995?

NIKIRI kwamba katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, mtu unahitaji ujasiri wa hali ya juu kukikosoa Chadema na mgombea urais wake, Edward Lowassa.


Kwa wiki tatu hizi nimejaribu kufanya hivyo, na mrejesho ni wingi wa sms za matusi na vitisho kutoka kwa baadhi ya wafuasi wake. Sitaki kuamini ya kwamba Chadema ya sasa imejaa watu wa namna hiyo – wanaokimbilia kwenye matusi badala ya kujibu hoja kwa hoja.


Nyerere alipata siku moja kumwambia mzungumzaji mmoja ukumbini: Urgue, don't shout (jenga hoja, usipige tu kelele). Nami nawahimiza mashabiki hao wa Lowassa wajibu hoja kwa hoja si kukimbilia kwenye matusi na vitisho. Wasumbue kidogo akili zao kufikiri badala ya kukimbilia matusi.


Kinachonishangaza, hata hivyo, ni kwamba hata wale marafiki zangu wachache ninaowaheshimu kitaaluma ambao ni wanachama wa miaka mingi wa Chadema nao sasa huwaambii kitu dhidi ya Edward Lowassa! Linapokuja suala la Lowassa hawataki kufikiri sana na kujibu hoja kwa hoja.


Hata baadhi ya waandishi maarufu wa safu za magazeti ambao huko nyuma walikuwa mstari wa mbele kuandika kuhusu tuhuma za ufisadi zinazomwandama Lowassa sasa nao wamegeuka. Wanaimba wimbo ule ule wa Freeman Mbowe kwamba eti sasa 'tatizo ni mfumo si kina Edward Lowassa'! Hii ni sawa na kusema Tanzania kuna ufisadi lakini hakuna mafisadi! Kuna lojiki kweli hapo?


Hata hivyo, nitakuwa mjinga kama sitatambua na kukiri kwamba Edward Lowassa amezoa wafuasi wengi nchini kama ilivyokuwa kwa Lyatonga Mrema mwaka ule wa 1995 alipoondoka CCM 'dakika za mwisho na kuhamia NCCR Mageuzi kugombea urais.


Sina haja ya kuwakumbusha hapa wasomaji wangu kilichomkumba Mrema katika uchaguzi ule, na wala sina haja ya kuwakumbusha wasomaji wangu taswira ya sasa ya Mrema na chama chake kichovu cha TLP.


Na wala siyasemi haya nikiimanisha ya kuwa Lowassa ataishia alikoishia Mrema. La hasha. Nayasema haya ili kukumbushana tu historia. Tukiikumbuka historia ya Mrema labda tutakumbuka pia kwamba rais huchaguliwa kwa kura, na si maandamano ya kishabiki ya umati wa watu!


Niseme tu hapa kwamba kuna gonjwa linaitwa 'Lowassamania' ambalo limewakumba baadhi ya Watanzania kiasi cha kuwafanya washindwe kufikiri sawa sawa. Ni gonjwa lile lile lililotukumba baadhi yetu enzi zile za Mrema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995.


Hebu yatafakari maneno kama haya yaliyotamkwa hivi karibuni na

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kuhalalisha Lowassa kujiunga na chama hicho ambacho kwa miaka kadhaa kilimtuhumu kuwa ni fisadi, na hata kuweka jina lake kwenye ile orodha maarufu ya watuhumiwa papa wa ufisadi (orodha ya fedheha):


"Chadema haimzuii mtu kujiunga kwani Chadema kuna kila aina ya wanachama – kuna vibaka, majambazi, wezi, wachawi, wala rushwa, mafisadi na wengineo. Hiki ni chama cha siasa. Kinajumuisha watu wengi. Siwezi kusimama na kusema ya kuwa wanachama wote ni wasafi, na hivyo anayetaka kujiunga na chama chetu anakaribishwa"!


Kwa mtazamo wangu, hayo ni maneno ya hovyo kupata kutamkwa hadharani na kiongozi wa juu kabisa wa chama cha siasa duniani. Kwa ufupi, tafsiri ya kauli hiyo ni kwamba Chadema si chama makini na kinapokea yeyote anayetaka kujiunganacho bila kujali ni jambazi, mwizi, mbakaji, lodi wa biashara ya madawa ya kulevya, fisadi, mchawi, tapeli nk.


Hivi ni mtu gani makini na aliyestaarabika duniani angependa kujiunga na chama cha aina hiyo? Ingawa ni kweli Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere alipata kukishutumu CCM kwamba kimegeuka kokoro kwa kuingiza kila aina ya wanachama, lakini sikumbuki kama kuna kiongozi yeyote wa chama hicho aliyesimama hadharani na kuwakaribisha wezi, majambazi, mafisadi nk kama alivyofanya Mbowe kupitia matamshi yake hayo ya Julai 21, 2015.


Ni Mbowe huyo huyo ambaye kabla Lowassa hajahamia Chadema aliwahi kumchanachana hivi wakati ule Lowassa akigombea kuteuliwa na CCM kuwania urais:


"Hao wanaomtaka Lowassa ni wale wanaojua kuwa watanufaika binafsi akipita kwenye urais lakini kimsingi huyu jamaa ni dhaifu sana na hafai kuongoza Tanzania ya sasa yenye changamoto lukuki. Wapambe wake wanasema si msemaji bali ni mtendaji, hivi nani atakubali porojo hizo wakati tunajua akiwa Waziri Mkuu hakufanya lolote kukemea wizi, ubadhirifu na ufisadi? Richmond ilikuja akiwa wapi?"


Huyo ndiye Mbowe ambaye sasa anammwagia Lowassa sifa kibao! Je, tuamini maneno yake ya jana au tuamini maneno yake ya leo? Vyovyote vile, mtu asiyeweza kusimamia maneno yake mwenyewe hastahili kuaminika hata kidogo. Ukigeugeu wa namna hiyo ni ishara ya ubabaishaji wa hali ya juu.


Angalau Lowassa ana shahada ya sanaa za maonyesho; sina hakika kama Mbowe anayo lakini wakifanyacho wote ni usanii mtupu!

Ndugu zangu, ninaposema kwamba gonjwa hilo la Lowassamania limetufanya tushindwe kufikiri sawa sawa maana yangu ni hiyo. Mbowe tuliyemfahamu miaka mingi Chadema hawezi kuwa ndiye Mbowe yule yule aliyeyatamka hadharani maneno hayo hovyo ya kukishusha hadhi Chadema! Ni Lowassamania hiyo!


Katika wiki hizi mbili nimekuwa nikukutana na marafiki zangu kadhaa ambao ni wanachama wa Chadema na safari zote wamekuwa wakinisihi niache kuandika mambo hasi kuhusu Lowassa na Chadema. Baadhi yao walioko mikoani wamekuwa wakinipigia simu na kuzungumza nami kwa muda mrefu wakinisihi jambo hilo hilo.


Katika mawasiliano hayo niliitumia fursa hiyo kutaka kujua kutoka kwao kitu ambacho wanakiona kwa Edward Lowassa ambacho labda mimi sikioni. Yaani nilijaribu kupata maelezo kutoka kwao ni kwa nini ugombea urais wa Edward Lowassa umevuta hisia zao. Yaani kwa nini nao Lowassamania imewakumba.


Maana; kama ni uchapakazi, mbona siuoni uchapakazi uliotukuka wa

Edward Lowassa katika kipindi cha miaka miwili aliyokuwa waziri mkuu? Kama ni utetezi wa wanyonge, mbona hatujamsikia bungeni akisema lolote? Kama ni misimamo yake murua ya kiitikadi, kisera na kimaono, mbona hatujaiona wala kuisikia?


Na kama ni uadilifu, ndio hivyo tena – yeye ni mtu ambaye amekuwa akiandamwa na kashfa ya ufisadi kwa miaka mingi. Kwa ufupi, hakuna anayejua kwa uhakika ni kwa nini anautaka urais kwa udi na uvumba. Wanamfuata tu Lowassa bila kujiuliza kama walivyokuwa wakifuata kikombe cha Babu Loliondo kwa maelfu bila kujiuliza!

Kwa hiyo, nilizungumza kwa muda mrefu na marafiki zangu hao ndani ya Chadema kupata majibu ya maswali hayo, na hasa nini wenzangu wanakiona kwa Edward Lowassa ambacho labda mimi sikioni.


Nilichogundua kutoka kwa marafiki zangu hao wa Chadema ni kwamba hawaamini katika uadilifu wa Edward Lowassa kwa sababu wanakiri kuwa ana nakisi katika hilo. Hawajui pia itikadi, sera au maono yake ya kiuongozi; bali wanaamini tu ya kwamba anaweza kuwasaidia kuiondoa CCM madarakani. Kwao, kama wasemavyo wazungu, the end justify the means.


Kwa mtazamo wao, kuiondoa CCM madarakani ni jambo muhimu na la lazima kuliko uadilifu wa serikali mbadala itakayoingia madarakani. Kwao, hata angejitokeza shetani mwenyewe na kuwaahidi kuwa atawang'olea CCM madarakani, wangemfuata huyo shetani na kumpa heshima ya kuwa mgombea urais wao!


Kwa mtazamo wao ni kwamba, tunapaswa kwanza kuiondoa CCM madarakani kwa njia yoyote na mbinu yoyote ile, na kisha mengine yatafuata baadaye! Na hapo ndipo ninapotofautiana na marafiki zangu hao ndani ya Chadema.


Kweli siipendi CCM (CCM yangu ni ile ya Mwalimu Nyerere) lakini siichukii

CCM kiasi cha kuhalalisha chama nilichokipenda (Chadema) kuivunja hata demokrasia kinayojaribu kuijenga kwa kumteua 'dakika za mwisho' (bila hata kumshindanisha na wengine) mtu ambaye kwa miaka kadhaa kilimwita fisadi – mtu ambaye haijui katiba ya hicho chama wala itikadi yake na maono yake.


Kama alivyoandika mdogo wangu Deus Bugaywa katika toleo la Raia Tanzania la Agosti 13, ni ujinga kuunganisha tu nguvu kwa malengo ya kutaka kwenda Ikulu bila kuwa na kanuni na misingi inayoweza kwenda kusimamia mabadiliko ya kweli ya wananchi wanayoyataka.


Kwenda Ikulu kwa ajili tu ya kwenda Ikulu siyo kiu ya mabadiliko ambayo wengi wetu tunayataka. Mahatma Gandhi (rejea seven social sins) alipata kuandika ya kwamba moja ya mambo yanayochangia kusambaratisha jamii ni kujitosa katika siasa sizizo na mipango au misingi (politics without principle). Na kwa Lowassa ni hivyo hivyo; maana yeye anachotaka ni kwenda Ikulu tu!


Kwa hiyo, mimi nakataa kujiunga na treni la kumshabikia Edward Lowassa na Chadema yake ya sasa. Nakataa kufanya hivyo kwa sababu sitaki kufananishwa na wale panya au watoto katika ile simulizi maarufu ya kale ya Mpiga Filimbi wa Hamelin (Pied Piper of Hamelin).


Wanaoifahamu simulizi hiyo ya Lower Saxony ya Ujerumani ya kale watakumbuka jinsi maelfu ya panya na baadaye mamia ya watoto wa

Hamelin walivyomfuata mpiga filimbi yule kwa kuvutiwa na mlio wa filimbi yake. Walimfuata bila kujiuliza na bila kutafakari na mwisho wake 'safari ya matumaini' ikawa ya maangamizi makubwa kwao! Hapana, mimi nakataa kumfuata mpiga filimbi wa Hamelin bila kwanza kujiuliza na kutafakari sauti na mlio wa filimbi yake!


Lakini kabla sijahitimisha ujumbe wangu wa leo, napenda kusisitiza jambo moja. Jambo hilo ni kwamba siwalaumu maelfu ya Watanzania wenzangu wanaomfuata na kumshabikia Lowassa bila kwanza kutafakari na kujiuliza. Siwalaumu kwa Sababu wao ni waathirika tu wa utawala mbovu wa CCM ambao tumekuwa nao miaka nenda rudi.


Utawala huo mbovu wa miaka mingi wa CCM umewafanya maelfu kwa maelfu ya Watanzania waishi maisha magumu na ya kukata tamaa. Katika hali hiyo ya kukata tamaa, akitokea yeyote na kupiga filimbi ya kuwaahidi kuing'oa serikali hiyo madarakani ni lazima watamfuata kwa mamia. Baadaye maelfu watafuata mkumbo. Ilikuwa hivyo kwa Mrema mwaka 1995 na ndivyo ilivyo sasa 2015 kwa Edward Lowassa.


Historia inatukumbusha pia kuwa ilikuwa hivyo kwa dikteta Adolph Hitler wa Ujerumani (soma kitabu chake Mein Kampf – Mapambano yangu). Ndugu zangu, kukata tamaa ya maisha ni kitu kibaya mno kwa jamii yoyote duniani. Kwenye kukata tamaa mtu utarukia behewa lolote bila kwanza kujiuliza linakupeleka wapi!


Kwa hiyo, siwalaumu waliokumbwa na Lowassamania! Hata hivyo, wasichokijua maelfu ya vijana nchini wanaomfuata Lowassa (kama mpiga filimbi ya Hamelin alivyofuatwa na wale watoto), ni kwamba mgombea urais huyu (Lowassa) hawawakilishi wao – yaani walalahoi na masikini; bali anawakilisha kundi la matajiri (kina Rostam, Manji, Mengi, makampuni ya simu, madini, mafuta na gesi, vitalu vya uwindaji nk), na hivyo akiingia Ikulu hao ndo atawasikiliza kwanza na si walalahoi au wasionacho waliompigia kura.


Mzee Joseph Warioba na kijana Zitto Kabwe walipata kutamka kwa nyakati tofauti ya kwamba uchumi wa Tanzania unashikiliwa na mabilioni 40 tu nchini! Huhitaji kuwa msomi kujua ya kwamba watu wengi ni masikini nchini kwa sababu uchumi wa nchi umeshikwa na watu hao wachache tu!


Kwa hiyo, swali la kujiuliza ni hili: Hivi Lowassa akiingia Ikulu anaweza kuleta mabadiliko ya kisera na ya kiuchumi kuusambaza utajiri wa hao mabilioni 40 ili kupunguza pengo kati ya walionacho na wasionacho? Atakuwa na ubavu huo wa 'kugawana ka-sungura' ilhali mapesa ya hao mabilionea ndiyo yaliyomweka madarakani?


Ni nani asiyejua ya kwamba katika mfumo wa kibepari matajiri wataendelea kuwa matajiri na masikini watazidi kuwa masikini? Wale wanaomshabikia Lowassa (ilhali tiketi yake ya urais ni tiketi ya matajiri) kama wangelitafakari hayo pengine wasingelimkimbilia kama wale watoto walivyomkimbilia mpiga filimbi wa Hamelin. Wangetafakari kwanza. Nashukuru Mungu mimi si mmoja wao!


Nihitimishe kwa kusisitiza tena kwamba sina chuki binafsi na Lowassa. Ni hofu tu ya mustakabali wa nchi yangu Tanzania ndo unaonisumbua.


Vinginevyo sina chuki binafsi na Lowassa kama ambavyo mwaka 1995 sikuwa na chuki binafsi na Mkapa (CCM) nilipofanya kosa la kumkimbilia Mrema (NCCR) bila kwanza kutafakari.


Ndiyo, Mrema huyu huyu ambaye leo amekuwa mpinzani mkubwa wa Upinzani Tanzania - japo anaongoza chama kinachoitwa cha Upinzani! Tatizo letu Watanzania ni kwamba historia haitufundishi chochote.Tafakari


Chanzo Raia Tanzania

Toleo la 419

19 Aug 2015

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Related Posts

0 Comments