Katika hili la maadili, nawaunga mkono Butiku, Polepole na Warioba
Kwa siku kadhaa sasa kumekuwa na mijadala imekuwa ikiendelea kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii hasa baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu na kulazimishwa kujiuzulu kutokana na kashfa ya Richmond, Edward Lowasa kujiondoa CCM na kujiunga na CHADEMA ambako ameteuliwa kuwa mgombea Urais kupitia chama hicho na UKAWA.
Baada ya Lowasa kwenda CHADEMA, kama ilivyotabiriwa, ameondoka na wale watu ambao walikuwa kifua mbele kuhakikisha anakuwa mgombea ndani ya CCM. Ni watu hao ndio waliokuwa wanamvimbisha kichwa Lowasa aonekane kuwa anakubalika na kila mwana CCM hali iliyomfanya atoe maneno ya kejeli na jeuri eti hakuna mwenye ubavu wa kumkata. Miongoni mwa watu hao ni pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga, Hamisi Mngeja na aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Mgana Msindai. Pia wamo Apson Mwang'onda na wengine ambao wengi wao wametimkia huko kutokana na kushindwa kwenye kura za maoni ndani ya CCM.
Hata hivyo, kitendo cha CCM kumkata Lowasa kimepokelewa kwa heshima kubwa na watu wengi. Miongoni mwao ni Jaji Joseph Sinde Warioba ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Joseph Butiku wa Mwalimu Nyerere Foundation na Humphrey Polepole aliyewahi kuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Hoja kubwa wanayoshikilia ni maadili. Kwamba, CCM iliharibiwa na watu waliokosa maadili kama Lowasa na hivyo kukifanya chama kuwatumikia watu hao badala ya kuwatumikia wananchi.
Sasa CCM imezaliwa upya. Safari hii hawakuangalia watu usoni. Ndo maana akina Polepole, Warioba na Butiku ambao walionekana kuichoka CCM kuanza kufufua penzi lao kwa chama hicho.
0 Comments