[wanabidii] Hofu Ukawa kuvunjika yatanda

Friday, August 21, 2015
MWENYEKITI mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), James Mbatia, amewataka viongozi na wanachama wa umoja huo kuheshimu makubaliano yaliyomo kwenye mwongozo waliotiliana saini mwaka jana.

Mbatia alitoa angalizo hilo baada ya kuwepo kwa viashiria kwa baadhi ya vyama ndani ya umoja huo kwenda kinyume na walichokubaliana hasa kuachiana majimbo kwa wagombea wabunge na udiwani.

Wiki hii kumekuwapo taarifa katika baadhi ya majimbo kwamba kuna vyama ndani ya Ukawa vimeweka wagombea kila kimoja tofauti na makubaliano yalivyokuwa awali.

"Ukawa si mali ya vyama vya siasa peke yake bali ni umoja wa Watanzania wanaounga mkono Rasimu ya Pili ya Katiba iliyowasilishwa bungeni na Jaji Joseph Warioba," alisema.

Alisema Oktoba mwaka jana viongozi wa NCCR Mageuzi, NLD, Chadema na CUF walikubaliana kwa maandishi kushirikiana.
Alisema changamoto zinazojitokeza kwa sasa ni mambo madogo yanayoweza kutatuliwa na kuwaomba viongozi kuyahubiri malengo yao na kuyatekeleza kwa vitendo.

Mbatia aliyasema hayo kutokana na kuwapo kwa taarifa kwamba wapo viongozi wenzake ndani ya NCCR ambao hawajaridhishwi na mwenendo ndani ya Ukawa hasa baada ya chama hicho kupewa majimbo machache.
Jana kulikuwa na hofu kwamba Mbatia angetoa tamko zito ambalo lingetikisa Ukawa, lakini alipozungumza na waandishi wa habari, alikanusha kufikiria kuiondoa NCCR ndani ya Ukawa.

Akizungumzia baadhi ya changamoto zinazojitokeza majimboni kwa sasa, Mbatia aliwaomba viongozi wenzake hasa ngazi ya wilaya kutekeleza makubaliano ya Ukawa.

Alisema wagombea watakaojitokeza kuwania majimbo kinyume na makubaliano ya Ukawa, hatawanadi hata kama ni wa NCCR.

"Kama tutafanya kampeni Jimbo la Ilala ambalo liko chini ya Chadema, mimi Mbatia nitahakikisha ninamnadi mgombea aliyesimamishwa na Chadema na si vinginevyo.
"Vivyo hivyo, Mbowe atakapokwenda Ileje (Mbeya), atafanya kampeni kwa mgombea wa NCCR Mageuzi aliyependekezwa ndani ya makubaliano ya Ukawa na si vinginevyo. Changamoto nyingine tutajadili kwa mazungumzo. Tutekeleze yale tuliyokubaliana na si ujanja ujanja," alisema Mbatia.

Awali akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa NCCR Mageuzi ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Ndelakindo Kessy, alisema NCCR imeongezewa majimbo ya ubunge kutoka 14 hadi 19.

Kwa mujibu wa Ndelakindo, majimbo ya NCCR sasa ni Kasulu Vijijini, Kasulu Mjini, Bunyungu, Muhambwe, Kigoma Kusini, Manyoni, Vunjo, Mwanga na Mufindi Kusini.
Majimbo mengine ni Mbinga Mjini, Ileje, Serengeti, Mufindi Kusini, Gairo, Mpwapwa, Kibakwe, Mtera, Mtera Mjini, Nkenge na Ngara.

Chanzo Raia Tanzania

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments