[wanabidii] KESI YA KUGOMBEA MIRATHI YA MWANDISHI WA HABARI YAUNGURUMA TENA ARUSHA .

Wednesday, July 08, 2015





Mwandishi wetu,Arusha

Kesi ya kugombea mirathi ya mwandishi wa habari mkongwe nchini marehemu,Betty Luzuka juzi imeendelea katika mahakama ya mwanzo ya Maromboso ambapo shahidi mwingine katika kesi hiyo Michoro Christopher alitoa ushahidi wake mbele ya mahakama hiyo.

Kesi hiyo ya mirathi inayovuta hisia za watu mbalimbali jijini Arusha  ipo katika mahakama ya mwanzo ya Maromboso  yenye nambari 222 ya mwaka 2013 inaitaka  mahakama hiyo ipitie hukumu yake iliyotolewa Septemba 27 mwaka 2013  na hakimu Prince Gideon iliyompa  ushindi kaka wa marehemu.
 
Kaka wa marehemu aitwaye, Ssarongo Luzuka alifungua kesi hiyo akimtuhumu mke wa aliyekuwa ofisa mwandamizi wa jumuiya ya Afrika Mashariki ,Phil Makini Kleruu aitwaye Hilda kujimilikisha mali za marehemu bila kufuata utaratibu wa kifamilia na kimahakama mara baada ya marehemu kuaga dunia Agosti mwaka 2013 katika hospitali ya Shreee Hindu ya jijini Arusha baada ya kuugua kwa muda mrefu.
 
Hatahivyo,upande wa mdaiwa umepinga  kutokuridhishwa na hukumu hiyo kutokana na madai  kuwa ana wosia halali alioachiwa na marehemu uliomilikisha mali zake zote  ambazo ni nyumba tatu zilizopo maeneo ya Njiro,Olmatejoo na Pemba road,mamilioni ya fedha zilizopo katika akaunti mbalimbali  pamoja na shamba lenye ukubwa wa zaidi ya ekari 3 lililopo eneo la Mkonoo mkoani Arusha .
 
Shahidi huyo aliieleza Mahakama hiyo kuwa mbali na kufamahamiana na marehemu tangu mwaka 2003 pia alikuwa rafiki wa karibu ambapo alikuwa akitunza funguo za nyumba za marehemu iliyopo maeneo ya Pemba road jijini Arusha.

Shahidi huyo aliiambia  mahakama ya kwamba siku marehemu amefariki dunia katika hospitali ya mkoa ya Shree Hindu daktari wa hospitali hiyo alimwambia akatafute shuka nyeupe kwa ajili ya kumfunika marehemu ambapo alifika nyumbani kwa marehemu na kufungua chumba chake lakini cha ajabu alikuta chumba hicho kimevurugwa.

Martin,mbele ya hakimu anayesikiliza kesi hiyo,Moka Mashaga alisema kuwa mbali na kushuhudia chumba hicho kuvurugika pia alikuta funguo za kabati la nguo za marehemu zimeshamishwa mahala zinapokuwa jambo ambalo si la kawaida.

Alisema kuwa mara baada ya kufungua kabati la nguo za marehemu kwa lengo la kutoa shuka hilo alikuta begi la marehemu lililokuwa linahifadhi vyeti vyake vya shule,mikataba ya nyumba,hati za nyumba pamoja na fedha mbalimbali  halionekani na ndipo alipoingiwa na mashaka na kuhisi huenda limeibiwa.

Shahidi huyo alienda mbali zaidi na kusema kuwa mara baada ya kufanikiwa kupata shuka la kumfunika marehemu ndipo alipomtafuta kaka wa marehemu,Ssarongo na kumweleza kuhusu tukio hilo ambapo alipojibiwa kuwa suala hilo litazungumziwa katika kikao cha familia.

Hatahivyo,shahidi huyo aliiambia mahakama hiyo kwamba mbali na tukio hilo pia  aliwahi kushuhudia siku marehemu akiwa nyumbani enzi za uhai wake akipokea kadi mbili za pongezi kwa siku yake ya kuzaliwa kutoka kwa familia ya  Kleruu na mkewe.

Shahidi huyo alisema kuwa katika kadi mojawapo mke wa ofisa huyo(Hilda) aliandika ujumbe wa kuomba kukopeshwa na marehemu kiasi cha sh,milioni 4 na kwamba atazirudisha ikibidi anaweza kufika nyumbani kwa ajili ya kuandikishiana jambo ambalo marehemu hakulitekeleza.

Mara baada ya kusikiliza ushahidi huo hakimu anayesikiliza kesi hiyo aliamua kuihairisha hadi mnamo Julai 13 mwaka huu ambapo ataita pande mbili katika kesi hiyo kuja kukamilisha ushahidi wao kabla kupanga tarehe ya hukumu.

Mwisho.


 




 









(Piichani chini ni mwandishi wa habari mwandamizi marehemu Betty Luzuka aliyefariki mwezi Agosti mwaka 2013 jijini Arusha)











Share this :

Related Posts

0 Comments