Mwandishi Wetu
SASA kumekucha, jogoo limekwisha wika Dodoma, kada wa CCM apewe kura za ndiyoooo! Najiuliza kama angekuwa, John Damiano Komba angeimba kwa furaha wimbo huu baada ya John Pombe Magufuli kuibuka kuwa ndiye mgombea urais wa chma hicho mwishoni mwa wiki iliyopita.
Naandika makala haya nikiwa na faraja tele moyoni mwangu. Faraja hii haitokani na uteuzi wa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano uliofanywa na CCM, hasha!
Faraja hiyo inatokana na chama hicho kikongwe barani Afrika na dunia kwa ujumla kumteue mgombea wake wa chama kuliko ambavyo kingemteua mgombea wa watu fulani.
Kuna watu, kwa maelfu tu, ndani ya CCM, walitaka chama hicho kiteue mgombea wao wa urais, atakayepeperusha bendera yao hao, atakayenadiwa na kuuzwa na wao mbele ya Watanzania.
Watu hao fulani, walitaka mtu wao huyo ateuliwe na CCM ili hata kesho na kesho kutwa awe rais wao na si rais wa chama wala rais wa Watanzania wote pindi atakapochaguliwa (kama ingekuwa hivyo) Oktoba mwaka huu.
Hii haikuwa mara yao ya kwanza kufanya hivyo, hapana. Hii ilikuwa ni mara ya pili watu hao kutaka iwe hivyo. Walifanya hivyo mwaka 2005 ikawa, sasa walitaka na mwaka huu wa 2015 wafanye hivyo pia. Wenye CCM yao, safari hii wamekataa!
Jakaya Mrisho Kikwete alifanikiwa mwaka 2005, ile ilikuwa ni bahati yake. Lakini kura zake zilipungua.
Watu wale wale wa mwaka 2005, kwa sababu tu walifanikisha kufyeka pori na kupata njia aliyopitia Jakaya hadi Magogoni, basi wakataka pia safari hii na wao wapitie njia ile ile aliyotumia Jakaya kupita.
Wahenga wanasema; bahati ya mwenzio usiilalie mlango wazi. Tena wanasema; si kila mtu anayo bahati ya mtende! Lakini pia, wahenga hao wanasisitiza kwamba; ukiona vinaelea, vimeundwa.
Ni ujinga wa hali ya juu kwa mtu kuilalia mlango wazi bahati ya Jakaya. Huyu alikuwa na bahati yake ya mtende iliyoanza kuonekana tangu mwaka 1995 alipoingia ndani ya tatu bora ya makada wa CCM bila hata kufanya maandalizi yoyote ya kuutaka urais!
CCM ni taasisi iliyo kamilika. Ni chama cha siasa ambacho mwasisi wake ni Julius Kambarage Nyerere. Chama hiki kipo, kinaendelea kuelea katika utawala wa nchi hii kwa sababu kiliundwa na mwasisi mwenye heshima zake kwa Watanzania na walimwengu kwa ujumla.
Misingi iliyokijenga chama hicho na kukifanya kiendelee kupendwa na Watanzania walio wengi, sasa na hata kwa miaka ijayo, ni uadilifu tu.
Uadilifu wa Kambarage, moyo wake wa kujali, kuwatetea na kuwapigania wanyonge, ndio unaokifanya chama chake hicho kiendelee kuaminiwa na sehemu kubwa ya umma wa wananchi.
Kamwe chama hiki hakiwezi kukabidhiwa kwa kundi la watu wasiokuwa walio na uadilifu wenye kutiliwa shaka, wasiokuwa na huruma kwa umma wa Watanzania hata kama vinywa vyao vinasema maneno kadhaa ya huruma, huku wakikumbatiana na matajiri ambao wamevuna kutoka katika migongo ya Watanzania.
Wenye CCM yao, wanaojaribu kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa vitendo vyao hata kama si kwa asilimia 100, safari hii wamegoma chama chao kutekwa na wenye nia ovu ya kukiondoa chama hicho kwenye misingi yake ya asili ya kuwa chama cha wanyonge, chama cha wakulima na wafanyakazi.
Nilikuwa Dodoma kwa takriban wiki nzima kufuatilia mchakato huo wa uteuzi ambao hatimaye ulimwibua Magufuli. Harakati zilizokuwa zinaratibiwa na makundi mbalimbali ya watu hao katika maeneo mbalimbali ya mji huo wa Dodoma, hasa maeneo ya St. Gasper, Dodoma Hotel na Nam Hotel, kwa hakika kabisa zilidhihirisha dhamira zao ovu kwa CCM!
Walikosea sana.
Naamini, kama harakati zile na nyingine, nguvu zao kubwa za fedha walizozitumia kabla na wakati wa mchakato huo wangezitumia wakiwa katika chama kingine cha siasa, mfano wa UMD, kwa vyovyote vile iwavyo, asingekuwepo wa kuwazuia kuingia Magogoni.
Walichokosea, ni kutaka kupitia njia ile ile ya CCM waliyopitia mwaka 2005, kabla ya baadaye wenye chama chao kuwashitukia na kuwataka wajivue magamba yao kama wanataka kuendelea kuwa salama, kama wanataka kuheshimiwa, kama wanataka kuendelea kuwa na majina mazuri mbele ya umma wa Watanzania.
Dalili za kukwama kwa watu hawa, zilianza kujionyesha mapema tu. Katikati ya wiki iliyopita nilishituka kumuona Mzee Kingunge
Ngombale-Mwiru akishuka kutoka ndani ya gari lake, kiasi cha saa 8:00 hivi mchana, kwenye lango kuu la kuingilia jengo la White House, zilipo ofisi za wakuu wa CCM, kwa maana ya Mwenyekiti, Makamu na Katibu Mkuu.
Pole pole nilijivuta kutoka nilipokuwa hadi nikamfikia Kingunge. Kulikoni Mzee Kingunge eneo hili, muda huu, siku hii ya leo Ijumaa na tarehe hii ya Julai 9? "Aah nina 'appointment' na Katibu Mkuu, ameniita!" Nikajisemea kimoyomoyo, kazi imekwisha.
Sijakaa sawa, wakati Kingunge akiwa bado yuko ofisini kwa Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana, nikamuona mtu mwingine muhimu katika kundi hilo, Hamis Mgeja, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga naye akienda ofisi hiyo hiyo.
Sijakaa sawa, wakati Mgeja akisubiri Kingunge atoke ili naye aweze kuingia, nikamuuna mtu muhimu mwingine, Rugarabamu, Mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa, akiwa amekaa kwenye benchi nje la mlango wa kuingilia ofisi za Kinana.
Nilipomsogelea huyu naye na kumuuliza kulikoni eneo hilo muda huo, siku hiyo na tarehe hiyo, akiwa katika hali ya unyonge mkubwa tofauti na nilivyzoea kumuona siku zote alijibu: "Nilitaka kumuona Kinana nikavunjevunje hoja zao, lakini kwa bahati mbaya sikufanikiwa. Ameniambia nimtafute baadaye...vipi bwana wewe, mbona sikuelewi? Kwanini hutaki kutafuta fursa ya maisha yako ya baadaye kwa kujiunga na timu ya ushindi? Shauri yako, baki huko huko utakufa masikini!"
Si Kingunge wala Mgeja aliyetoka ndani ya ofisi ya Kinana akiwa na uso unaoakisi safari njema ya matumaini. Wote hao, watu muhimu kabisa katika iliyokuwa kambi yao, walitoka katika ofisi ya Kinana wakiwa na nyuso za kujikatia tamaa.
Siku hiyo ya Ijumaa ya Julai 9, ambayo ilitarajiwa vikao vyote muhimu katika mchakato huo vifanyike kwa mfululizo, kwa maana ya Kamati ya Usalama na Maadili, Kamati Kuu na Halmashauri Kuu, iliweza kutoa picha kamili ya hali halisi ilivyo katika kambi hiyo.
Kilipomalizika kikao cha Kamati Kuu usiku wa siku hiyo, katika hali isiyotarajiwa, niliwashuhudia Jerry Silaa, Adam Kimbisa na Sophia Simba wakizozana katika hali iliyoonyesha uchungu wa kujikatia tamaa.
Baadaye, akaibuka mwanasiasa kijana, aliyekuwa akionekana kujijengea heshima ya kipekee ndani ya CCM, Emmanuel Nchimbi, akajitokeza mbele ya waandishi wa habari na kuwaambia wamsubiri atakuwa na neno la kuwaambia baada ya dakika kama 20 hivi zijazo.
Na kweli, baada ya muda huo, Nchimbi akajitokeza mbele ya waandishi wa habari na wapiga picha yakamtoka yaliyomtoka. Akasema Kamati Kuu imevunja katiba ya chama, kwa hiyo, yeye na wenzake, Sophia na Kimbisa hawakubaliani na uamuzi wa uteuzi wa majina matano yaliyotoka Kamati Kuu kwenda Halmashauri Kuu!
Nchimbi, kada aliyekuwa akionekana kama kada na moyo wa CCM kutokana na uzoefu wake mkubwa ndani ya chama hicho, anaweza kuungana na Kingunge kuumba rais wa kikundi cha watu badala ya rais wa chama chake na Watanzania kwa ujumla? Niliusemea moyo wangu, CCM imeingiliwa!
Chaguo wanalo wao, kukiri hadharani dhambi yao hiyo ya usaliti kwa chama chao, au kusubiri na kujaribu tena baadaye 2015, lakini kwa mwaka huu wa 2015, jogoo la CCM ni John Pombe Magufuli! Kingunge aliapa, dunia ikamsikia, kwamba nje ya Edward Lowassa, CCM haitabaki salama. Tusubiri tuone
Raia Mwema
Toleo la 414
15 Jul 2015
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 Comments