[wanabidii] Ubunge Hai:Mbowe apita kwa itifaki

Wednesday, June 24, 2015
Ubunge Hai:Mbowe apita kwa itifaki

Paul Sarwatt, Moshi.
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika jimbo la Hai, mkoani Kilimanjaro kitatumia "itifaki" kumpitisha Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe, kuwa mgombea pekee wa ubunge katika jimbo hilo katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu. Mbowe kwa sasa ni mbunge wa jimbo hilo, baada ya kurudi bungeni katika uchaguzi wa mwaka 2010, na ameshatangaza nia ya kutetea kiti chake katika uchaguzi wa mwaka huu.

Mbunge huyo aliingia bungeni kwa mara ya kwanza katika uchaguzi wa mwaka 2000 na mwaka 2005 aligombea nafasi ya Urais na kuwa miongoni mwa wagombea walioshindwa na Rais Jakaya Kikwete.

Taarifa zilizopatikana kutoka jimboni humo wiki hii zinaeleza kuwa, hadi mwanzoni mwa mwezi huu, hakuna kada yoyote wa Chadema jimboni humo aliyeonyesha nia ya kutaka kupimana "ubavu" na Mbowe katika mchakato wa kura za maoni. Mmoja wa wanachama wa chama hicho Wilaya ya Hai aliiambia Raia Mwema kuwa wanachama wenye nia wameshindwa kujitokeza kutokana na hofu kuwa si rahisi kushinda kura za maoni ndani ya chama kutokana na "uzito" wa Mbowe kisiasa na unafiki wa viongozi wa ngazi ya wilaya na Mkoa.

"Si kwamba hakuna wanachama wanaotamani kugombea, tatizo ni hofu ya kutoungwa mkono na viongozi wa chama pamoja na wanachama ambao wanamwogopa Mbowe,"alidai.
Hata hivyo Katibu wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema, alipuuza madai hayo na kufafanua, hatua ya wanachama wa jimbo hilo ya kumwachia Mbowe inatokana na heshima aliyojijengea mbele ya jamii na wananchi wa jimbo la Hai.

"Mbowe katika jimbo lake anaitwa kaka, na wana Chadema pamoja na CCM, wanampenda sana, kama kuna mtu anataka kushindana na kaka basi atakuwa anashindana na wana Hai wote,"alisema Lema.

"Kama wana Chadema wamempa Mwenyekiti wao heshima kuna ubaya gani?"Mbowe ni kiongozi wa kitaifa heshima anayopata si ya bahati mbaya, inatokana na mchango wake mkubwa katika harakati za kuleta mageuzi ya kisiasa nchini,"aliongeza Lema.
CCM wamponda: Diwani wa CCM Kata ya Weru Weru Adris Mandray, alidai katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa Mbowe kama Mbunge hakuwahi kutetea maslahi ya wananchi wake, ndani na nje ya Bunge.

"Baada ya uchaguzi wa mwaka 2010, Mbowe alihama jimbo, robo tatu ya shughuli zake za kisiasa akawa anafanyia nje ya Hai na alikuwa anazungumzia masuala ya kitaifa zaidi akitumikia cheo chake cha Uenyekiti wa chama chake badala ya kuzungumzia masuala yanayohusu jimbo la Hai,"alisema Diwani huyo. Diwani huyo anadai kuwa pia Mbowe ni "mbaguzi" kutokana na tabia yake ya kutowajali wananchi wanaoishi maeneo ya tambarare katika jimbo hilo ambao hawana huduma muhimu kama barabara, maji na shule zenye hadhi.

"Kwa mfao Rais Kikwete alipotembelea Hai mwaka jana, Mbowe alipewa nafasi ya kuzungumza, alimwomba Rais serikali iwajengee barabara ya kiwango cha lami urefu wa kilomita 3 kutoka Masama-Machame ambako ni nyumbani kwake, badala ya kuomba ujenzi wa barabara ya kilomita 25 kati ya Boma Ng'ombe-Kikafu Chini ambayo haipitiki kabisa,"alidai Mandray. Aliongeza katika kipindi hicho cha miaka mitano, Mbowe hakuwahi kusimamia chochote kuhusiana na maendeleo ya jimbo hilo isipokuwa msaada wa magari mawili ya wagonjwa ambayo ameyatoa katika mwaka wa mwisho wa uongozi wake hatua inayoashiria kuwa lengo ni kujipigia kampeni ili achaguliwa tena.

Makada CCM wajitokeza:
Hata hivyo, pamoja na hatua hiyo ya wana Chadema kumwachia Mbowe apite bila ya kupingwa, makada saba wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamejitokeza kuwania jimbo hilo iwapo watapita katika mchujo wa kura za maoni.

Miongoni mwa makada waliotajwa ni pamoja na aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo hilo kati ya mwaka 2006-2010, Fuya Kimbita, ambaye pia ni Mjumbe wa NEC wilaya ya Hai, Dustun Mallya ambaye ni Mkurugenzi wa wilaya ya Meru Mkoani Arusha na Rajab Nkya ambaye ni Diwani wa Kata ya Machame Chini. Makada wengine ni Ally Mwanga ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Hai, Robert Swai na Martine Munisi ambaye ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UV-CCM) Wilaya ya Arusha Mjini.

Taarifa zinaeleza kuwa tayari makada hao wameshaanza harakati za kujinadi katika makundi mbalimbali ndani ya chama kutafuta kuungwa mkono ili kushinda kura za maoni na kukabiliana na nguvu ya Mbowe.Wakati makada hao "watunishiana misuli" kwa kutumia nguvu ya fedha kuwashawishi wanachama, kivutio katika harakati hizo imeelezwa ni hatua ya Mwenyekiti wa UV-CCM Martine Munisi kutumia usafiri wa baiskeli na pikipiki (boda boda) kuwafikia wapiga kura.

"Huyo kijana amevuta hisia za watu wengi kutokana na uwezo wake katika kujenga hoja na amekuwa kivutio kutokana na tabia yake ya kutumia usafiri wa kawaida, na wakati mwingine hutembea kwa miguu kutafuta kuungwa mkono na wanachama tofauti na watangaza nia wengine ambao hutumia magari hata ya kifahari,"anaeleza moja wachama wa CCM jimboni humo.
Habari zaidi zilizopatikana kutoka ndani ya CCM wilayani humo zinaeleza kuwa mchuano mkali baina ya makada hao CCM ni kati ya Munisi, Mallya na Kimbita ambao wanapewa nafasi kubwa ya kuibuka washindi.
Munisi pamoja na changamoto ya kutokuwa na ukwasi wa kutosha anaelezwa kuungwa mkono
na makundi ya vijana na wanawake kutokana na hoja zake zilizojikita katika kutafuta ufumbuzi wa matatizo mbalimbali yanayowakabili.Aidha Kimbita ambaye hata hivyo hakupatikana kupitia simu yake ya mkononi, amejenga msIngi wa kampeni zake kwa kuegemea zaidi kwa makada na wanachama waliomwunga mkono wakati alipochaguliwa kuwa mjumbe wa NEC na alipokuwa mbunge.

Katika mazungumzo yake na Raia Mwema, Munisi alithibitisha kuwa anawania nafasi hiyo kupitia chama chake cha CCM, na yupo tayari kukabiliana na changamoto zinazojitokeza kuanzia ndani ya chama na nje ya chama. "Naelewa changamoto za kutafuta nafasi kama hii nyeti ya ubunge hasa kwa vijana ambao kwanza ndiyo tunaanza safari ya maisha, lakini nimejizatati kukabiliana nazo na ninawafikia wanachama na wananchi kwa njia rahisi zaidi"anaeleza."Nafahamu fika kuwa kuna baadhi ya wapiga kura ndani ya chama changu na wale wa nje ya chama wanaodhani kuwa wakati huu ni wakati wa "mavuno" kwa kuchukua rushwa ndogo ndogo, mimi kwanza ninachofanya ni kuwaelimisha watu wa aina hiyo juu ya umuhimu wa kuchagua kiongozi bora katika jamii,"alisema.

"Ujumbe wangu umefika mbali sana, vijana wengi wameanza kuelewa juu ya umuhimu wa kuwa na kiongozi au mwakilishi atakayepeleka mawazo yao ndani ya Bunge na atakayesimamia ajenda muhimu za kimaendeleo katika jimbo,"aliongeza. Mwenyekiti huyo wa vijana alisema kati ya maeneo muhimu atakayoyatilia mkazo iwapo atachaguliwa ni kusimamia ujenzi wa bwawa la maji la Bolotti ambalo linaweza kuhudumia nusu ya vijiji vya jimbo hilo kwa kilimo cha umwagiliaji.

"Bwawa hili kwa sasa limejaa tope na ni kama halitumiki tena na mbunge aliyepo (Mbowe) kwa sababu anaishi nje ya jimbo lake hana muda wa kusimamia ukarabati wake, sasa utaona pia changamoto ya kuwa na kiongozi anayefanya shughuli zake nje ya jimbo analoongoza,"alisema Munisi. Kada mwingine aliyezungumza na Raia Mwema ni Dustun Mallya ambaye alithibitisha kuwa anaweza kuingia katika mbio za kumwondoa Mbowe katika nafasi hiyo ya ubunge muda utakapofika.

"Nimefuatwa na makundi mbalimbali ya kijamii, yakiniomba niingie katika kinyang'anyiro cha ubunge, wahenga wanasema "Sauti ya Wengi ni Sauti ya Mungu," hivyo tutakaporuhusiwa rasmi na chama chetu nitatathmini maombi yao,"alisema. Katibu wa Mbowe ajibu hoja:
Juhudi za kumpata Mbowe hazikuweza kufanikiwa mwishoni mwa wiki kutokana na simu ya kuita bila ya kujibiwa, lakini Katibu wake Totinan Ndonde akijibu hoja za wakosoaji wa mbunge huyo alisema wananchi hawakumchagua ili wamwone bali asimamie maendeleo yao.

"Wanaodai kuwa mbunge haonekani jimboni wamefilisika kifikra, pamoja na wajibu wake wa kibunge, Mbowe ni kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, ni Mwenyekiti wa chama kikubwa cha upinzani nchini hivyo huduma yake inahitajika Watanzania wengi zaidi tofauti wanavyofikiri watu wa CCM katika jimbo la Hai,"alieleza.

Akizungumzia suala la maendeleo, Ndonde alisema katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa Mbowe, jimbo hilo limepiga hatua muhimu katika sekta kama afya,elimu na miundo mbinu.
"Kwa upande wa afya, mbunge ametimiza ahadi yake ya kutoa magari mawili ya wagonjwa kwa Hospitali ya Wilaya pamoja na Hospitali Teule ya Machame na tayari yamekabidhiwa,"alisema Ndonde.

Aliongeza kuwa mbunge huyo ametumia fedha za mfuko wa jimbo kukarabati madarasa katika shule kadhaa za msingi pamoja na kuboresha miundo mbinu katika vijiji na vitongoji vya jimbo hilo kwa asilimia 80. "Mheshimiwa Mbowe amenunua greda kwa ajili ya kufanyia ukarabati wa barabara za jimbo hilo hasa zile za ukanda wa tambarare na mashine hiyo iko katika ofisi za jimbo kwa sasa,"aliongeza.


Alisema katika kipindi cha miaka mitano, pia Mbowe amesimamia upandaji wa miti ya aina mbalimbali ipatayo 700.000 hivyo kuboresha mazingira ya jimbo hilo kuwa kijani zaidi ifikapo mwaka 2025. Jimbo la Hai ni kati ya majimbo yenye vuguvugu la siasa za mabadiliko, ambapo tangu kuanza kwa chaguzi za mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1995, CCM na upinzani wamekuwa wakipokeza kuongoza jimbo hilo kwa vipindi tofauti.

Chanzo raia mwema

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Related Posts

0 Comments