PHILEMON Ndesamburo, Mbunge wa Moshi Mjini, ni miongoni mwa wabunge walioijadili Taarifa ya Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza Mchakato wa Zabuni ya Kuzalisha Umeme wa Dharura ulioipa ushindi Richmond LLC ya Houston, Marekani 2006, iliyosababisha, aliyekuwa waziri mkuu, Edward Lowassa, kujiuzulu.
Ndesamburo aliliambia Bunge, "…nchi za wenzetu kama za China, wahujumu wa namna hii si kwamba wanajadiliwa, wananyongwa hadharani."Mafisadi wananyongwa China. China ilimhukumu kunyongwa Liu Han Februari 2015. Han alikuwa na shilingi trilioni 10. Gazeti la Telegraph la Uingereza la Februari 9, 2015 liliripoti kuwa Han alikamatwa 2013 na kunyongwa baada ya kupatikana na hatia ya ufisadi.
Opereshini Fox Hunt; maana yake ni operesheni Kamata Mbweha, ni maarufu sana nchini China.
Kamata Mbweha imefanikisha kukamatwa watuhumiwa wa ufisadi 680 waliokimbilia Marekani, Canada, Australia na kwingineko. Walirudishwa China kujibu mashitaka ya ufisadi. Waliopatikana na hatia tayari wamekwishakunyongwa. China haitaki porojo.
Dk. Harrison Mwakyembe, Mwenyekiti wa Kamati, aliwasilisha taarifa ya Richmond bungeni Februari 6, 2008. Kamati ilimtuhumu Lowassa, pamoja na mambo mengine, kuvunja sheria kwa kushinikiza Tanesco kupokonywa jukumu la kutafuta kampuni ya kufua umeme.Waziri wa Nishati na Madini, alimwandikia Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Julai 13, 2006, kuwa, "Nimezungumza tena na Waziri Mkuu (Lowassa) leo, juu ya bei ya mitambo ya Aggreko. Msimamo (wa Lowassa) ni ule ule niliokueleza awali na ameagiza…achukuliwe Richmond."
Februari 7 2008 Spika, Samuel Sitta, alimpa Lowassa nafasi ya kujitetea. Lowassa alikuwa na saa zaidi ya 14 kujipanga kujibu. Badala ya kijitetea Lowassa alijiuzulu. Alifahamu kuwa asingeweza kuwababaisha kisanii wabunge makini kama akina Mwakyembe?
Lowassa anadai kuwa alitaka kuvunja mkataba wa Richmond. Si kweli. Magazeti yalianika bayana kashfa hiyo. Lowassa anadai kuwa alitaka kuvunja mkataba wa Richmond akiwaeleza wenzake "kuhusu habari za magazeti." Alihisi mambo yamemkalia vibaya siyo?
Lowassa, na wapambe wake, anajitahidi kujionyesha kuwa yeye ni mtu wa uamuzi mgumu. Anatamani umma uamini kuwa Jakaya Kikwete ndiye aliyekuwa na mamlaka ya kuvunja mkataba wa Richmond. Alipoona kuwa Kikwete havunji mkataba kwa nini hakujiuzulu? Mtu wa "uamuzi mgumu" asingesubiri Kamati Teule ianike uozo wa kashfa ili kujiuzulu.
Jitihada za Lowassa kujinasua katika kashfa ya Richmond iliyotia taifa hasara ya zaidi ya shilingi milioni 152 kwa siku kwa miaka miwili zitagonga mwamba. Anadai alionewa. Wakuonewa Lowassa? Wajumbe wa kamati hiyo wako hai. Wabunge waliokuwa wakali wa CCM wakati huo kama Christopher Sendeka, Lucas Selelii, James Lembeli, Anna Malecela mpo? Dk. Slaa na wapinzani wenzake waliokuwa bungeni Februari 6 na 7, 2008 watanyamaza?
Vita ya Richmond ina wapiganaji wengi. Hivyo acha niandike mambo mengine muhimu. Kwanza, uadilifu wa Lowassa unatiliwa shaka na watu wengi. Septemba 15, 2007 pale Mwembe Yanga, Temeke, Dar es Salaam na kwa ujasiri mkubwa Dk. Slaa alimtaja Lowassa katika orodha aliyoita ya "mafisadi." Na kwa jinsi Lowassa anavyotamani kuwa rais, japo kwa saa chache tu, angekimbilia mahakamani kama angekuwa msafi. Hakudiriki!
Wahariri wa baadhi ya vyombo vya habari waliokutana na Lowassa Dodoma hivi karibuni nao pia waliutilia shaka na kuhoji utajiri wake. Lowassa aliwajibu kuwa eti ana "ng'ombe kati ya 800 na 1,000. Kwetu Umasaini unapokuwa kiongozi unapewa ng'ombe ili usipate taabu kwa ajili ya kuwakarimu wageni wanapokuja." Huu ni uongo. Hakuna kitu kama hicho Maasaini.
Lowassa anadiriki kuwakashifu wazalendo wanaopinga wizi wa mali za umma. Alisema, "...kudanganya watu kwamba nikiwa masikini ndiyo nafaa kuwa kiongozi ni ujinga." Hili ni tusi la nguoni kwa wanaopambana na ufisadi. Utajiri usio na maelezo ni batili. Hakuna anayewachukia matajiri waliopata fedha zao kwa juhudi na njia halali, wanaolipa kodi na hawajawahi kupora ofisi za umma.
Bilionea Philemon Ndesamburo, kwa mfano, ni kipenzi cha watu. Hakuna anayeutilia shaka utajiri wake. Anamiliki hadi chopa. Bilionea mwingine anayeheshimika ni Dk. Reginald Mengi.
Mengi anamiliki hadi vyombo vya habari. Haiwezekani kuwaorodhesha hapa matajiri wasafi Tanzania. Ni wengi sana. Nani mwenye mgogoro nao? Pili, kinyume cha majigambo yake na wapambe wake kuwa eti ni mchapa kazi na mwenye kuchukua uamuzi mgumu Lowassa ni adui mkubwa wa sheria na utawala bora.
Gazeti la Mwananchi la Mei 26, 2015 lilimnukuu Lowassa akiuelezea uviziaji wake wenye shaka, "Chini ya uongozi wa Rais (Benjamin) Mkapa tukagundua hawa jamaa (City Water) ni matapeli...tulifanya kikao saa tisa alasiri, tukachukua kibali cha kumkamata yule Mzungu wa City Water na tukamfukuza akaondoka siku hiyo hiyo kwa ndege kurudi kwao, tulifanya saa tisa alasiri ili asiende mahakamani kupata zuio, kwa hiyo tulivizia muda huo ili asije kwenda kupata zuio." Huo ni uviziaji wa kimafia. Mzungu huyo hakupewa haki ya asili ya kusikilizwa. Si ajabu walimvizia asije akafungua mkoba wa mabaya.
Tatu, Lowassa alikuwa kinara wa mtandao wa uliomwingiza Kikwete madarakani mwaka 2005. Kikwete aliposhinda alimteua Lowassa kuwa Waziri Mkuu; kuthibitisha majigambo ya Lowassa kuwa yeye na Kikwete "hawakukutana barabarani." Waliuhadaa umma kwa maneno matamu kama vile "ari mpya," "nguvu mpya," "kasi mpya" na porojo nyingine kama "maisha bora kwa kila Mtanzania." Ni wazi kuwa ahadi za Kikwete zimebaki hivyo; ahadi. Shilingi imeporomoka. Gharama ya maisha imepanda.
Lowassa asivyojali hayo leo anajipitisha badala ya kuomba radhi kwa kuudanganya umma.
Nne, baadhi ya waandishi wa habari na wamiliki wa vyombo vya habari, wanajitahidi kumsafisha sana Lowassa, lakini Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, anawaonya Watanzania dhidi ya genge hili, "Hao wanaomtaka Lowassa ni wale wanaojua watanufaika binafsi (Lowassa akiwa Rais)."
Mwisho, ni rahisi samaki kuishi nchi kavu kuliko Lowassa kuhamia vyama vya upinzani hasa vile vinavyounda Ukawa. Kwanza, hadiriki! Pili, hatakiwi kule. Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema, ameshasema Lowassa "hafai kuongoza Tanzania." Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti CUF, nae amekaririwa mara kadhaa akisema kuwa "Lowassa ni msanii."
CCM, kwa vyovyote vile, haina sababu ya kumwonea haya achilia mbali kumwogopa Lowassa.
Raia Mwema
Toleo la 411
24 Jun 2015
--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 Comments