Mwitikio wa wananchi na vyombo vya habari umekuwa mkubwa sana kiasi kwamba wananchi na vyombo vya habari ni kama wamesahau kuwa kuna matukio mengine yanaendelea nchini, ikiwamo Bunge la Bajeti mjini Dodoma, ambalo kwa kawaida, huvuta msisimko kuliko tukio lolote lingine la kitaifa.
Somo kubwa ninaloliona ni ule ukweli kuwa pamoja na mawaa yake, bado Watanzania wengi, wenye vyama na wasio na vyama, wanaitazama na kuitumainia CCM kwa uongozi wa nchi. Ukweli huu unaakisi ile nasaha ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuwa "Rais wa nchi yetu anaweza kutoka Chama chochote cha siasa, lakini Rais bora wa Tanzania atatoka CCM".
Hadi sasa, CCM ni chama pekee ambacho kimeweza kubeba haiba na taswira ya utaifa na Chama chenye hazina ya viongozi, demokrasia pana na mifumo. Pengine ndio sababu wananchi na vyombo vya habari hawaonyeshi shauku hiyo hiyo kwa michakato inayoendelea ndani ya vyama vya upinzani ikiwemo vile vinavyounda Ukawa, maana vina wigo finyu wa demokrasia ya ndani ya vyama hivyo na isitoshe wagombea wake ni wale wale wa siku zote. Na wengine wanapoonesha nia huundiwa zengwe na kufukuzwa.
Jambo ambalo halina mjadala ni kuwa Watanzania wanahitaji mabadiliko ambayo yatawatoa katika lindi la umasikini na ufisadi. Pamekuwepo na chambuzi mbalimbali hapo nyuma zikihitimisha kwamba kiu hiyo ya Watanzania ya mabadiliko ilimaanisha kuchoshwa na CCM, ama kuitoa CCM madarakani. Tofauti na chambuzi hizo, tunachokishuhudia ni wananchi kuendelea kuamini mabadiliko haya yanaweza tu kutokea na kuletwa na CCM na si nje ya CCM.
Matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Desemba mwaka jana yanatupa fundisho kubwa. Kwa matarajio ya wapinzani, kufanyika kwa uchaguzi ule baada ya Bunge la Katiba kukamilisha Katiba Inayopendekezwa tuliyoambiwa imechukiza wananchi, na kufuatiwa na mjadala wa Bunge wa sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow, CCM ingeanguka katika uchaguzi wa serikali za mitaa. Pamoja na yote hayo, CCM ilipata asilimia 84 ya kura ikilinganishwa na wapinzani waliopata 16.
Ukiachana na picha ya jumla inayoonyesha kuwa asilimia za ushindi kwa wapinzani zilipanda kutoka asilimia nne mwaka 2009 hadi 16 mwaka 2014, ukifanya uchambuzi wa kina wa maeneo waliyoshinda wapinzani, utaona kwa kiasi kikubwa, pale wapinzani walipoongeza viti, ushindi wao ni matokeo zaidi ya hujuma zilizosababiswa na teuzi za ndani za CCM kuliko jitihada na mkakati wa ushindi wa upinzani.
Ndio sababu kuna mtawanyiko wa viti walivyoshinda wapinzani ndani ya kata, wilaya na mikoa ambao ukiujumlisha haukupi uhakika wa kusema kata, jimbo au wilaya fulani imechukuliwa na upinzani. Kwa kifupi, ushindi wa upinzani hauonekani kuwa ushindi wa kimkakati.
Kabla ya CCM kutangaza ratiba yake ya uchaguzi, kulikuwepo na manung'uniko na lawama kutoka kwa wananchi tena wengi wasio wanachama wa CCM kuhusu kuchelewa kutangazwa kwa ratiba ya uchaguzi wa CCM. Binafsi, haikunishangaza sana kutokana na ukweli kuwa, kwa ukubwa wake na dhamana yake, CCM si ya wana CCM peke yao bali inamhusu kila Mtanzania.
Ndio kusema, yale maneno ya Baba wa Taifa ya mwaka 1995 kuwa CCM ikishatangaza mgombea ni kama imeshatangaza Rais wa nchi yetu bado yangali mujarabu hadi sasa.
Katika uhai wake, Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere alishauri kutokana na ule uhalisia kwamba upinzani wetu bado ni dhaifu, na kusababisha mgombea wa CCM ndiye awe Rais, ni muhimu kwa mgombea urais CCM akajulikana mapema zaidi, ikiwezekana mwaka mmoja.
Aliamini kwa kufanya hivyo, wananchi wote, hasa wale walio nje ya CCM watapata pia muda wa kutosha kumjua na kumpima, maana ndiye mwenye uwezekano mkubwa wa kuwa Rais wao. Utamaduni huu wa Chama kutangaza mgombea wake mwaka mmoja hutumika pia na jirani zetu wa Msumbiji.
Utaratibu huo wa kumtangaza mgombea wa Chama mapema zaidi unasaidia kukilazimu Chama kuchagua mgombea muadilifu maana, wananchi wanakuwa na muda mrefu wa kumjua tofauti na utaratibu wa sasa ambapo hutangazwa muda mfupi na kuingia katika Uchaguzi Mkuu. Salama pekee katika utaratibu wa sasa uko katika uthabiti wa mifumo na vikao vya Chama katika kuhakiki, kuchuja na kuchagua mgombea. Kwa lugha nyepesi, tumewekeza matumaini na imani yetu kwa wajumbe wa CCM wasiozidi 2,300 kutuchagulia Rais wa Tanzania, na sisi kubaki na jukumu la kumthibitisha tu.
Katika zama hizi ambazo tunasikia kuwa wajumbe wa vikao hivyo hupata nafasi hizo kwa fedha, na hivyo pia kununulika na wagombea kwa fedha, kuna shaka kuwa wale wasio waadilifu wanaweza kununua njia yao ya kwenda Ikulu. Maana unachotakiwa kufanya ni kuwanunua wajumbe wasiopungua 1,500 tu. Ni kwa sababu hii, kumekuwepo na hofu kubwa miongoni mwa wananchi kwamba vikao vya Chama vinaweza kuteleza na kuchagua mgombea urais kwa vishawishi vingine nje ya sifa za mgombea, mahitaji ya wakati na mahitaji ya nchi.
Hofu hiyo ya vikao vya Chama kutumika kupitisha wagombea wasio wasafi imetulizwa na kauli ya Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete. Wana CCM wengi na wananchi wamefarijika na kauli ya Mwenyekiti kuwa Chama na vikao vyake havitayumba katika kumchagua mgombea wa urais wa CCM. Muhimu zaidi ni pale aliposema kuwa CCM haina nafasi kwa yule anayenunua uongozi kwa fedha, au yule ambaye mienendo, matendo na haiba yake haviakisi uadilifu na anachukiza wapiga kura ambao wengi wao si wana CCM.
Kauli ile ilituliza mioyo ya wengi maana kulianza kuwepo shaka ya kuwepo nafasi kubwa kwa wenye fedha chafu na tuhuma za kifisadi kupitishwa, hasa kwa tambo zao za kukiweka Chama mfukoni au kutaja idadi wa wajumbe ambao wapo katika daftari lao la malipo.
Kufunguliwa kwa pazia la uchaguzi wa ndani ya CCM kumefufua matumaini mapya kwa Watanzania wote. Kujitokeza kwa watangaza nia wengi tena waliosheheni sifa kumeondoa ile hofu iliyokuwa imetanda kuwa yuko mtangaza nia mmoja ambaye tayari amekwishashinda na amekuwa akisubiri tu kukamilisha ratiba ya chama atangazwe. Maana tumeshuhudia wenyeviti wa CCM na wajumbe wa Halmashauri Kuu na Kamati Kuu ya CCM wakisimama nyuma ya kila mtangaza nia aliyejitokeza.
Tunachokiona katika mchakato huu wa kutangaza nia ndani ya CCM ni ushahidi kuwa hakuna mwenye hatimiliki ya kugombea urais wala mwenye uhakika wa ushindi. Zaidi, tumeona kuwa ndani ya CCM hakuna ukame wa viongozi wenye uwezo wa kumrithi Rais Kikwete kama tulivyokuwa tunaaminishwa na kikundi fulani. Hii inaendelea kudhihirisha ubora wa CCM kama chama kilicho imara kushinda mtu na kuwa hakuna mwana CCM maarufu kushinda Chama.
Haitashangaza pia, kwa wingi huu wa waliojitokeza, hapatakuwa na ugumu wa kupata wagombea walio safi zaidi. Maana wingi wa watangaza nia unaondoa ile sababu ya kufumba macho na kumpeleka kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu mgombea hata yule asiyefaa kwa kisingizio aidha cha uchache wa wagombea wenye sifa, au uchache wa wagombea waliojitokeza. Wana CCM na wananchi hawatarajii kuona mgombea mwenye madoa mengi miongoni mwa wale watakaopita katika mchujo wa kwanza wa Kamati Kuu, maana walio safi na wenye sifa wamejitokeza wengi wa kutosha hadi sasa.
Macho, masikio na mioyo ya Watanzania imeelekezwa CCM. Ni matumaini ya Watanzania kuwa CCM haitawaangusha. Watanzania wanatamani CCM iendelee kuwa madhubuti, maana wanaamini, bila CCM madhubuti nchi yetu itayumba.
--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 Comments