Ndugu zangu,
Mada hii kuhusu sanaa ya kuhutubia, ama kujieleza mbele ya watu inazidi kupata wafuatiliaji zaidi. Nami, naingiwa na ari zaidi ya kuliandikia jambo hili, hususan pale ninapopokea simu kutoka kwa Mtanzania anayefikiria kuwania Udiwani na ananiomba nimshauri juu hili la sanaa ya mawasiliano.
Leo tujikite kwenye eneo la sauti. Wagiriki wa kale waliita ' Prosodi'. Duniani hapa kuna sauti nyingi kama ilivyo wingi wa wanadamu. Sauti zina midundo yake. Kuna sauti nene, nyembamba, nzito, na hata ya mikwaruzo. Mzungumzaji ni vema ukajijua una sauti ya namna gani.
Wengi hupuuzia umuhimu wa sauti unapoongea mbele ya hadhara. Katika hili, Rais aliye madarakani, Jakaya Kikwete yuko makini sana. Anaelewa umuhimu wa sauti.
Kuna mtu ameniambia, kuwa JK husisitiza sana uwepo wa vifaa vya kutoa sauti vitakavyomfanya asikike vema.
Sauti ni muhimu sana kwenye hotuba. Mzungumzaji anaweza kupangilia hoja zake vema lakini akaangushwa na sauti, ama kutoka vifaa vya kupazia sauti vilivyopo, au yeye mwenyewe kutokuwa makini juu ya namna ya kutumia vema sauti yake.
Sauti hufanyiwa mazoezi pia. Unaweza kwenda bustanini au kando ya bahari na kuifanyia mazoezi sauti yako. Usimame tu na kuongea kwa sauti kama vile unaongea na watu wengi. Fanya mazoezi kujua wapi unaweka vituo. Kasi ya sauti yako na mengineyo. Mazoezi si ya mpira tu, hata sauti kwenye hotuba. Kuna misuli ya koo yenye kuhitaji mazoezi. Na mapafu pia. Usipoyafanyia mazoezi ndipo hutokea mzungumzaji akaonekana kuishiwa hata pumzi za kuongea. Hotuba nayo huathiriwa.
Mzungumzaji sharti ajue, kuwa ni sauti gani atumie kulingana na anachokiongea. Kuna mahali kwenye hotuba unatakiwa uweke sauti ya msisitizo. Kuna mahali iwe nzito kidogo. Kuna mahali iwe ya unyenyekevu, kwa maana laini kidogo. Kuna mahali unatakiwa kuongea kwa sauti ya huzuni.
Huwezi kupewa kipaza sauti utangaze tukio la msiba ukaanza na kutamka kwa sauti; : Jamani ee, jamaa yetu ndio keshakufa tena, sasa tujipange kwa taratibu za mazishi!" Hivyo sivyo wanavyotarajia kusikia waombolezaji.
Hapa Julius Nyerere ni mfano mzuri wa kutumia sauti husika kwa tukio husika. Alasiri ile ya Aprili 12, 1984, siku shujaa wa Watanzania, Edward Sokoine alipofariki kwa ajali ya gari, mimi nilikuwa natembea kwa miguu nikitoka shuleni Tambaza Sekondari. Pale maeneo ya Kinondoni ' A' nikasikia wimbo wa taifa ukipigwa. Enzi hizo ukisikia wimbo wa taifa unapigwa redioni mchana ni lazima ufuatile kujua kuna nini. Nikasogea kwenye redio kwenye moja ya maduka.
Wimbo wa taifa ulipomaliza ikasikika sauti ya Julius Nyerere, Rais wa Nchi. Kutoka sekunde ya kwanza aliongea kwa sauti ya pole pole na iliyochanganyika na huzuni.Tuliomsikiliza tukafahamu Rais ana habari mbaya kwa Taifa. Nakumbuka alianza kwa kutamka..:
" Ndugu zangu Watanzania, leo kunako majira ya saa..."Kilichofuatia ni sehemu ya historia yetu.
Huu ni mfano wa kutumia sauti muafaka kwa tukio husika.
Ni muhimu saa pia, kuwa unapokuwa jukwaani, sauti iendane na lugha ya mwili. Unapozungumza jambo la huzuni, basi na sura nayo ionekane hivyo, hupaswi kuonyesha sura ya kuchangamka. Au kuweka mikono mfukoni ( Kama mwenyekiti wenu hapo pichani). Hupaswi wala kurusharusha mikono. Hapo ni mahali hata pa kukunja mikono yako kifuani.
Mada hii ni endelevu..
Kwa ushauri wa bure, namba yako hiyo chini..
0754 678 252
Maggid
Unapokea Email hizi kwa sababu umejiunga na Jukwaa la 'Mabadiliko'.
Kuchangia mada tuma kwenye Email hii: mabadilikotanzania@googlegroups.com
For more options, visit this group at:
http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania?hl=en?hl=en
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Mabadiliko Forum" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to mabadilikotanzania+unsubscribe@googlegroups.com.
To post to this group, send email to mabadilikotanzania@googlegroups.com.
Visit this group at http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania.
To view this discussion on the web visit https://groups.google.com/d/msgid/mabadilikotanzania/CAMD-ye4Fy9xBTjrmNbzGi2NrD-Uk78Zp3vjJHhUvMjLUtVaYCw%40mail.gmail.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 Comments