[wanabidii] MAGESA MWITA - NAACHANA NA SIASA ZA KIHAFIDHINA ZA CHADEMA

Tuesday, April 21, 2015

NAACHANA NA SIASA ZA KIHAFIDHINA ZA CHADEMA

Wakosoaji wangu mara kadhaa wamenitaka kuonyesha upande niliopo kisiasa sijui ni kwanini lakini kwa mwenendo wa comments zao inaonekana ni kwa kutaka kujua namna watakavyokuwa wanajibu hoja zangu. Inaonekana kwao hoja sio issue, issue ni uko upande gani. Mwanzoni sikuona swala hili kama ni la msingi kwa kuwa mimi naamini nchi haijengwi na chama kimoja. Nikawa tayari na bado niko tayari kuunga mkono wazalendo wa kweli kutoka vyama vyote ikiwemo CCM, Chadema, CUF, NCCR, ACT n.k. Nitapinga siasa zote zenye lengo la kufifisha demokrasia, ubinafsi na zisizolenga mabadiliko ya kweli. Hivi karibuni nimejaribu kuungana na wote ambao kwa gharama yoyote ile tulitaka kuona umoja zaidi katika vyama vya upinzani na sio ubaguzi. Juhudi hizi zimekwama kwa kuwa tu eti viongozi wakuu wa Chadema na wafuasi wao hawataki! Mwenendo wa Chadema makao makuu kwa siku za hivi karibuni umegubikwa na sura kuu mbili:

1. Kuzimishwa kwa demokrasia ambayo ndio msingi mkuu wa chama. Lipo genge linalokubaliana nje ya mfumo rasmi wa chama juu ya nani wawe viongozi wakuu wa chama na kuleta kwenye vikao vya chama kama utaratibu tu. Ukitofautiana na genge hili basi utaitwa msaliti. Demokrasia ndani ya chama inataka watu wote kupewa haki sawa katika kugombea uongozi, kuchujwa kwa vigezo na watakaopita mchujo kupigiwa kura. Demokrasia haiwapi haki viongozi wakuu waliopo kukaa pembeni na kukubaliana nani wawe viongozi na kutaka wote tufuate hivyo, hii ni kwa sababu dhana hii inaleta mgongano wa kimaslahi. Kwa mfano Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na Wakurugenzi wa makao makuu ni rahisi kumpendelea Mwenyekiti aliyepo (aliyewapendekeza/aliyewateua) kwa kuwa kuchaguliwa kwake ni kujihakikishia kuteuliwa kwao tena. Huku ni kulindana na kunakinyima chama fursa ya kutumia vipaji bora zaidi vilivyopo ambavyo bado vipo nje ya utawala wa uliopo. Pili inaleta hofu na woga kwa wanachama na hivyo wanachama wenye mawazo mbadala hukaa kimya na mawazo yao mwisho wa siku chama kinakuwa na ufinyu wa mawazo.

2. Ajenda ya Mabadiliko ndani ya Chadema haina nguvu tena! Ajenda imekuwa ni fitina dhidi ya mtu au watu, hoja ya USALITI ndio ajenda kuu ya Chadema. Na hapa kuna dhana mbili, ya kwanza ni waraka wa mabadiliko wa akina Kitila Mkumbo unaoitwa mpango wa mapinduzi, wenye akili waliishajibu kuwa hakuna mapinduzi kwenye uchaguzi utakaopigiwa kura. Pili ni propaganda kuwa Zitto Kabwe alinunuliwa na CCM, hili formaly hali exist kwa kuwa hakuna kikao au ngazi yoyote ndani ya Chadema ambapo Zitto aliwahi kutuhumiwa, kushitakiwa au kuhukumiwa juu ya jambo hili, kimsingi halipo kwenye chama. Ni wahuni tu walilianzisha baada ya kuona hoja yao ya waraka wa kimapinduzi haina mashiko.

Mimi naamini demokrasia ya kweli ndani ya chama ni ishara ya kutupa uhakika kuwa hata chama hicho kikishika dola nchi itakuwa na demorasia ya kweli, uhuru na haki za wananchi vitalindwa, uchaguzi huru na wa haki, uwazi katika shughuli za serikali n.k. Kufifisha demokrasia ndani ya chama ni ishara ya wazi kuwa chama hicho kikishika dola kitafifisha pia demokrasia ndani ya nchi.

Wananchi wetu wapo katika hali ngumu, hali ya umasikini wa kipato, hudumu za kijamii bado haziridhishi, safari ya utawala bora bado ni ndefu, n.k. Hoja ya mabadiliko lazima ituonyeshe masuluhisho juu ya masuala hayo niliyoyataja, chama kinapoimba tu mabadiliko kama ngonjera tu bila kutuonyesha mipango ya masuluhisho haitoshi. Labda kikishinda ndio kutakuja na mpango, sawa lakini sasa hii siyo ajenda kuu cha Chadema, ajenda imekuwa ni propaganda juu ya mtu. Huku ni kutoka kwenye hoja iliyokifanya kuwa chama kikuu cha upinzani. Tuelewe lengo sio kushinda uchaguzi eti tu kwa kuwa CCM imechokwa lah! Lengo ni kushinda kwa kuwa chama kina masuluhisho ya matatizo yaliyopo.

Nawatambua makamanda wengi waliovuja jasho kuijenga Chadema na Tanzania kwa dhamira ya kweli, katika masuala ya kujenga nchi bado tupo pamoja kama nilivyo pamoja na wazalendo bila kujali vyama walivyomo. Katika siasa za vyama naachana kabisa na siasa za Chadema, siasa za propaganda, siasa za kukumbatia madaraka kwa hila, siasa za kuua demokrasia, siasa za kificho kificho, siasa za majungu fitina na matusi.

Mwisho, nitamke wazi kuwa tangu sasa nafuatilia kwa karibu siasa za ACT – Wazalendo. Asanteni.




--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments