[wanabidii] Maswi asimamishwa kazi kwa muda

Wednesday, December 24, 2014
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Yohana Sefue, amemsimamisha kazi kwa muda Ndugu Eliakim Maswi, Katibu Mkuu ya Wizara ya Nishati na Madini, ili kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yake, kama ilivyoelekezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.

Balozi Sefue amemsimamisha kazi Ndugu Maswi kuanzia leo, Jumanne, Desemba 23, 2014, kwa kutumia madaraka aliyonayo kama Mamlaka ya Nidhamu kwa Watumishi wa Umma wanaoteuliwa na Rais, wakiwemo Makatibu Wakuu.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Balozi Sefue mjini Dar es Salaam imesema kuwa amechukua hatua hiyo "Kwa mujibu wa Kifungu 4(3) (d) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Na. 8 ya mwaka 2002 (kama ilivyorekebishwa)" ambapo "Katibu Mkuu Kiongozi ndiye Mamlaka ya Nidhamu kwa Watumishi wa Umma wanaoteuliwa na Rais, wakiwemo Makatibu Wakuu."

Badala yake, Balozi Sefue amesema kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Ngosi C. Mwihava atakaimu nafasi ya Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, hadi uchunguzi dhidi ya Ndugu Eliakim C. Maswi utakapokamilika.

Taarifa hiyo ya Balozi Sefue pia imekariri kauli ya Rais Kikwete katika hotuba yake kwa Taifa jana, Jumatatu, Desemba 22, 2014 ambako Rais alisema:

"Kuhusu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, kwa vile ni Mtumishi wa Umma, anatawaliwa na Sheria na Kanuni za Utumishi wa Umma, hivyo nimeshaelekeza Mamlaka kuchunguza tuhuma zake na hatimaye ikibainika ana makosa hatua za kinidhamu zitachukuliwa."

Ndugu Maswi, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Ndugu Frederick Werema pamoja na Mawaziri wawili walituhumiwa wakati wa Kikao cha Bunge kilichopita kuhusiana na Akaunti ya Tegeta Escrow.

Wakati huo huo, Rais Kikwete ameelekeza kuwa pamoja na hatua nyingine zinazochukuliwa, Shirika la Umeme (TANESCO) waendelee na majadiliano na IPTL kuhusu uwezekano wa kushusha tozo la uwekezaji (capacity charge) zaidi ya punguzo la awali lililopatikana kupitia Kituo cha Kimataifa cha Kusuluhisha Migogoro ya Kimataifa (ICSID).

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu – Dar es Salaam.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Related Posts

0 Comments