[wanabidii] MAMBO SABA YA KUJIULIZA KABLA YA KUKOPESHA

Friday, November 14, 2014

MAMBO SABA YA KUJIULIZA KABLA YA KUKOPESHA 
MWANANCHI - 13/11/2014 - UKURASA 18

Kukopesha ni kitendo cha kumpa mtu, kikundi cha watu au taasisi kiasi fulani cha fedha au mali kwa makubaliano ya kurejesha fedha hizo baada ya muda zikiwa pamoja na riba au kama jinsi zilivyo. Kukopesha huleta ladha nzuri ya mafanikio kifedha wakati wale wanaokopeshwa wanapokuwa waaminifu kurejesha fedha hizo kwa wakati. Kutorejeshwa kwa fedha hizo za mkopo ndani ya muda mliokubaliana na mkopeshwaji huleta ishara ya aidha kutolipwa kabisa fedha hizo au kulipwa nje ya muda ambapo thamani yake itakuwa imeshuka tofauti na mlivyokubaliana hapo awali.

Kukopa harusi, kulipa matanga ndio msemo unaoweza kukupa taswira nzuri ya mambo gani ujiulize kabla ya kukopesha. Wengine hujifariji kuwa mdaiwa hafungwi, kwa hiyo wanaweza wasikulipe na wasipate madhara yoyote kisheria. Usipokuwa makini kabla ya kukopesha unaweza ukajikuta unafirisika, unagombana na watu, ndoa yako inavunjika, undugu unaisha na urafiki uliodumu kwa muda mrefu unavunjika. Hii ni kwa sababu tu umeshindwa kujenga mazingira mazuri ya uwajibikaji kisheria kati yako na yule unayemkopesha. Hii haijalishi unamkopesha nani na kiasi gani unachokopesha. Mali bila daftari hupotea bila habari. Fedha haina undugu, ujamaa, kujuana wala urafiki. Ukitaka kufanikiwa kifedha na kudumisha mafanikio yako, lazima ujenge misingi imara ya kisheria itakayolinda fedha zako.

Kwanza jiulize, je kuna mkataba wa maandishi kati yako na yule unayemkopesha? Hii ina maana usimkopeshe mtu kwa makubaliano ya mdomo tu. Hii haijalishi unamuamini kiasi gani. Katika maswala ya kifedha usimuamini mtu kupita kiasi, atakuja kukushangaza atakapokugeuka na kukuliza. Pili jiulize je, mkataba huo umeshuhudiwa na wakili au shahidi mwingine yeyote? Ni muhimu kuwa na mtu wa tatu kama shahidi katika mkataba wenu, atasaidia kuutetea mkataba huo. Tatu jiulize, je mtu huyo anayeingia mkataba huo ana mamlaka kisheria ya kuingia mkataba huo na je ndiye atakayewajibika katika urejeshwaji wa mkopo huo? Usije ukaingia mkataba na mtu mwingine na ukatarajia ulipwe na mtu mwingine, utakwama.

Nne jiulize, unafahamu anwani sahihi ya huyo unayemkopesha kwa maana ya anapoishi, ofisi yake, mawasiliano yake, mjumbe wake na mengineyo? Tano jiulize, je mtu huyo ana uwezo wa kulipa fedha hizo alizokopa ndani ya muda mliokubaliana? Usimkopeshe mtu kwa kumhurumia ili atatue shida zake, kopesha kwa maslahi ya kibiashara. Sita jiulize, je mtu huyo ana dhamana yoyote ya mkopo huo au kuna mtu amejitolea kumdhamini ambaye asipolipa yeye ana uwezo wa kulipa deni hilo? Kukosekana kwa dhamana au mdhamini ni kuhatarisha ulinzi na usalama wa fedha zako. Saba jiulize, endapo mtu huyo akifariki, akipata ulemavu wa kudumu au tatizo na hivyo kushindwa kurejesha mkopo huo utawezaje kurejesha fedha zako?

Haya ni mambo ya msingi sana ya kujiuliza na kuyapatia majibu kwanza kabla hujatoa fedha zako kumkopesha yeyote yule. Ukiona huna majibu sahihi ya maswali hayo usithubutu kumkopesha mtu fedha. Bora lawama kuliko fedheha. Hata kama utalaumiwa lakini fedha zako zitakuwa salama. Kwa taasisi zinazotoa mikopo ni muhimu kupata vibali vinavyokuruhusu kufanya hivyo na pia kulinda haki za mteja kisheria kwa kutomdharirisha, kumnyanyasa na kumfanyia fujo kwa sababu tu ameshindwa kuleta marejesho. Kumbuka kudaiwa hakumuondolei mtu haki zake za msingi kisheria.


--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Related Posts

0 Comments