Leo nimeamka na aya hizo hapo chini katika rasi yangu, naomba nianze kuzichezesha kindumbwendumbwe kisicholia, yaani, kisicho na ukelele. Nitazichezesha nitakavyo na nipendavyo ili mradi kwa kufanya hivyo nisichupe mipaka tuliyopewa waja katika kuchunguza mambo yanayotuhusu, hususani yale yanayotuhusisha na muumba wetu.
Kimsingi si vibaya hata kidogo kuchunguza na kuyatafakari yale yanayosemwa ni siri ya uumbaji na pumzi zinazotawala hizo siri, sema hawa wajitao wenye mamlaka juu yetu, yaani miungu, hawaishi kututisha kila tunapojaribu kuchunguza siri za uungu wao, wanachotaka si kingine, bali tusijue udhaifu wao na wala upumbavu wao, ili wapate kututawala milele, ila yule aliyesema sisi tu mfano wake si punde atasanda kama si kusalimu amri.
"Na hii ndiyo Njia ya Mola wako Mlezi Iliyo nyooka. Tumezipambanua Aya kwa watu wanao kumbuka." Qur-an 6:126
"Na kwa hakika hii ndiyo Njia yangu Iliyo Nyooka. Basi ifuateni, wala msifuate njia nyingine, zikakutengeni na Njia yake. Haya amekuusieni ili mpate kuchamngu." Qur-an 6:153
"Njia ya ulio waneemesha, siyo ya walio kasirikiwa, wala walio potea." Qur -an1:7
"Yesu…..Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi" Yohana 14:6
"Yesu…mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi , ajapokufa atakuwa anaishi." Yohana 11:25
Ukisikia neno "njia" katika vifungu hivyo ni MFUMO WA MAISHA, mfumo ambao unaathiriwa na sheria za kiuchumi na kimaumbile. Sheria za kiuchumi ni sheria zile zinazotokana na uwepo wa mahitaji ya mja yaso na ukomo sanjari na uwepo wa rasilimali zenye ukomo katika upatikanaji wake. Sheria za kimaumbile ni zile zinazosimamia maumbile ya vitu mbalimbali na nguvu zinazolinda uwepo wa maumbile hayo katika maeneo yake yaliyopangiwa na muumba. Sheria za kimaumbile ndio inayifanya dunia kuwa sayari ya tatu kutoka katika jua na binaadamu kula na kwenda haja.
Si lengo la andishi langu kuzungumzia jinsi sheria za kimaumbile na zile za kiuchumi zinavyoathiri mifumo mbalimbali ya maisha, bali lengo la andishi langu kuelezea kwa namna gani tunaweza kutambua mfumo sahihi, na kwa namna gani tunaweza kuishi na watu walio nje ya mfumo sahihi pasina hata kuathiri haki zao za msingi, haki ambazo zinaheshimu silika za kimaumbile na si vinginevyo!
Tumekuwa tukikhitilafiana juu ya mfumo upi ni sahihi wa maisha kama waja, lakini kwa Mungu mifumo ya maisha iko mingi, lakini katika hiyo mifumo mingi, kuna mfumo mmoja tu ambao ni sahihi, na yeyote atakayekwenda kinyume na mfumo huo basi atakuwa ni mwenye hasara leo na kesho pia.
Kama kulivyokuwa na miungu mingi, basi pia kuna mifumo ya maisha iko mingi pia, na kila mungu ameumba mfumo wake ambao inabidi waja wake waufuate, na kila mungu anaona mfumo wake wa maisha ndio sahihi, na kila mungu anaona mfumo wa mungu mwenzake si sahihi, na kikubwa zaidi kila mungu anamuona mungu mwenzake ni shetani, yaani ibilisi. Baadhi ya miungu maarufu ni Yesu, Allah[s.w], JEHOVA, Budha, Krishina, Mzimu, Jua, Mwezi, Ardhi, Anga, na Ng'ombe.
Ibilisi ndiye shetani maarufu na gumegume, na ukichunguza kwa makini utagundua kuwa kila mungu niliyemtaja hapo juu wakati fulani ndio huwa shetani. Hii inatokana ukweli kwamba kila mungu hujiona kuwa yuko sahihi, na kila mungu anamtuhumu mungu mwenzie ni shetani, na ya kwamba atakaye mfuata shetani ataangamia na atakayemkataa ataongoka. Ndio kusema mungu wako wewe msomaji kwa wengine ni shetani, utake ndivyo na usitake ndivyo.
Kuna miungu inayoamini kuwa, kuna vitu havijawahi kujiita mungu, bali ni watu wameamua kuvifanya na kuviita hivyo vitu "mungu". Allah[s.w] na JEHOVA kwa pamoja wanaamini kuwa Yesu, Ngo'mbe, Budha, Ardhi, Mwezi, Jua, Anga, na Krishna hawajawahi kujiita mungu, bali binadamu kutokana ujahili wao wameamua kuwafanya kuwa miungu. Allah[s.w], JEHOVA na Yesu wanaitazama miungu ya Afrika kwa jicho gani? Mizimu ya Afrika inatazamwa kwa jicho baya na hawa wajiitao miungu ya kweli na yenye nguvu.
Uislamu ulipoingia Afrika ulikuta dini na miungu yetu, haraka sana mungu wa waislamu akaingia wivu kwa miungu yetu, wivu huu ndio uliopelekea mizimu[miungu] yetu kuitwa mashetani, matambiko[ibada] zetu kuitwa upuuzi na kafara zetu kwa mizimu yetu kuitwa ni utumishi wa kijahilia, wanasema miungu yetu ni vitu visivyoweza kutusaidia wala kutupigania. Wakati mungu wa waislamu akisema haya, waifrika tayari walikuwa wamenufaika na mambo chungu mno toka kwa miungu yao. Jamani babu zetu walikuwa hawapati mvua mara baada ya tambiko la mvua kufanyika?
Ukristo ulivyoingia, haukuvunja misingi mizuri na imara ya dini zetu tu, bali pia na mfumo wetu wa utawala na utamaduni wetu kwa ujumla wake. Uislamu ulivunja mfumo wetu wa utawala, lakini si kwa kiwango kikubwa kama cha ukristo. Mungu wa ukristo ndiye aliyekuja na mbwembwe za mwanamke kuzaa pasina kumjua mume. Mungu wa ukristo waliwaita miungu yetu ni mapepo wachafu na waafrika ni watu waliolaniwa. Mungu huyu anasema kuwa alitufanya kuwa weusi kutokana na dhambi tulioifanya ya kumuua Habili. Je, sisi wafrika tunamjua huyo Habili? Huu si kama upuuzi ni kitu gani?
Ukichunguza kwa makini katika sinema zenye uwepo wa muhusika shetani, basi muhusika huyo hufanywa kuwa mweusi. Kwa ujumla katika michoro au sinema shetani huwa mweusi na mungu huwa mweupe. Hizi ni propaganda makhususi kwa kubomoa na kuvunja misingi ya dini za kiafrika na uafrika wenyewe. Ndio maana leo hii sishangai kitendo cha watu weusi kujichubua, eeh, nani anapenda kufanana na shetani? Kwahiyo wazungu wametengeneza mawigi, dawa za kubadili nyewele na dawa za kujichubua ili kumfanya mwafrika atoke katika ushetani na aingie katika ustaarabu. Kwa hili hawa watu hawana adabu, tena shenzi zao kila wakihema wao na miungu yao!
Na wale waumini wa miungu hii ya kigeni, sijui mara baada ya kupewa matango pori na miungu yao, wamekuwa wakipigana vikumbo wao kwa wao, na baadhi yao wamefikia hata kuuana na kuumizana kisa tu ulevi wa ubinafsi unaotokana na matango pori. Ubinafsi wa sisi tuko sahihi na nyinyi ni maqafiri, sisi tumeokoka na nyinyi mmepotea, sisi suni na nyinyi mashia, sisi tunaiheshimu sabato na nyinyi mnaihalifu, ubinafsi umbao umekuwa kama panga lenye ukali kuwili, upanga ambao hauna macho hata ukaona huyu ni binaadamu mwenzangu, au baba yangu, au mama yangu, au mtoto wangu, nk. Upanga unakata, wallahi unatutenganisha na kutugawa. Rejea yanayotokea Nigeria na hata mgawanyiko wa bunge la katiba juu ya mahakama ya kadhi.
Wakati yote hayo yakijiri, yaani hayo ya bw Upanga na kibarua chake cha kufitinisha, miungu iko pembeni imetulia tuli, jamani haina macho? Yametobolewa? Haina masikio? Yamezibwa? Haina ndimi? Zimekatwa? Ngoja nisifike mbali, kwani nachelea kusema hivi "eeh, bila shaka iko faraghani ikicheka kwa kejeli wazifanyazo kwa waja."
Miungu hii ndio inayowafanya wawaite wenzao ni watoto wa shetani, na wao ni watoto wa mungu, ili hali sote tunajua, tumezaliwa mara baada ya mama zetu kulala na baba zetu, haijalishi usiku au mchana, kichakani au kitandani, kwenye busati au kwenye ngozi ya mnyama, sote ni matokeo ya ngono, iweje umwite mwenzio ni mtoto wa shetani? Je mama yake alilala na shetani hata akamzaa yeye? Na iweje wewe ujivike utukufu wa kujiita mtoto wa mungu? Je, mungu alilala na mama yako hata ukazaliwa wewe?
Au ni miungu yenu ndio iliyowalisha matango pori hata mkapata kibli ya kuwaita wenzenu ni watoto wa shetani? Je miungu yenu ndio iliyowaambia kuwa nyinyi ni watoto zake? Jamani tusibaguane, jamani tupendane, kumwita mwenzio mtoto wa shetani ni jambo baya sana. Na wewe kujiita mtoto wa mungu si jambo jema pia. Sisi sote wafrika ni ndugu na letu ni moja, ni jambo la kijahili sana kwa kukubali kugawanywa kwa misingi ya kidini, tena dini zenyewe za kigeni, dini zilizokuja kutufanya tuwe watii kwa watawala badala ya kuwa watii kwa uafrika wetu, kwa wahenga wetu na mizimu yetu.
Baada ya pwampwa za hapo juu, naona ni vema nirudi katika lengo kuu la tasnifu yangu ya leo. Kila mfumo wa maisha unaotwaliwa na imani za kiungu ni sahihi na unahitaji kuheshimiwa. Ni kweli iso shaka kuwa, kwa kiwango kile ambacho mtu anaona mfumo wa mwenziwe si sahihi, basi ajue kuwa ni kwa kiwango hicho hicho mfumo wake pia waonekana si sahihi na watu wa mifumo mingine. Kukubalika kwa mfumo anoufuata mtu kuwa ni sahihi inategemea na mtu huyo atakavyoweza kujenga hoja zenye mashiko juu ya kile anachokiamini.
Kila mfumo ni sahihi midhali uko katika mifumo ya maisha, na kila mfumo sahihi ni lazima ufike mahala uwe na utaratibu wa kuishi na watu wenye mifumo isiyo sahihi. Mfano, uislamu unauona ukristo si mfumo sahihi, lakini ukamilifu na sahihi wa uislamu utapimwa kwa kuangalia ustahamilivu wa dini hiyo katika kuishi na mfumo wa ukristo ndani ya chumba kimoja na dola moja. Pia ukamilifu wa ukristo na mifumo mingine itapimwa kwa mtindo huu. Dini za kiafrika ni sahihi endapo tukitumia kigezo hicho.
Kwa kigezo hicho pia uislamu uko sahihi, kwani wenyewe una utaratibu wa kuheshimu mifumo mingine ya maisha. Waislamu wote wasioheshimu mifumo mingine ya kimaisha wajue wanapingana na sheria za kiislamu. Pamoja na kwamba uislamu unaheshimu mifumo mingine, lakini uislamu hauko tayari kuchokozwa na kufanyiwa istizai. Uislamu unaishi na mifumo mingine pasina tatizo lolote.
"Wala msiwatukane hao wanao waomba badala ya Mwenyezi Mungu, wasije na wao wakamtukana Mwenyezi Mungu kwa jeuri bila ya kujua. Namna hivyo tumewapambia kila umma vitendo vyao. Kisha marejeo yao yatakuwa kwa Mola wao Mlezi, naye atawaambia waliyo kuwa wakiyatenda" quran 6:108
Aya hiyo inawakataza waislamu kutukana miungu mingine na mifumo ya hiyo miungu.
"Wale ambao wametolewa majumbani mwao pasipo haki, ila kwa kuwa wanasema: Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu! Na lau kuwa Mwenyezi Mungu hawakingi watu kwa watu, basi hapana shaka zingeli vunjwa nymba za wat'awa, na makanisa, na masinagogi, na misikiti, ambamo ndani yake jina la Mwenyezi Mungu linatajwa kwa wingi. Na bila ya shaka Mwenyezi Mungu humsaidia yule anaye msaidia Yeye. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu Mtukufu" qur-an 22:40
Aya hiyo inakataza waislamu kuvunja nyumba za ibada za mifumo mingine.
Hata ukristo unahimiza watu wake waishi vizuri na watu wa mifumo mingine, ndio maana inasemwa ukipigwa shavu la kushoto basi geuza na la kulia pia.
HITIMISHO.
.Njano5.
0715845394/0762845394/0784845394Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 Comments