Tumeendelea kushuhudia majanga yakiliandama Jeshi la Polisi nchini kwa baadhi ya vituo vyake kuvamiwa na majambazi na kuporwa silaha, huku askari wake wakiuawa na wengine kujeruhiwa.
Mapema mwezi huu, askari wawili walipoteza maisha na wengine watatu kujeruhiwa baada ya majambazi kuvamia Kituo cha Polisi cha Bukombe, mkoani Geita na kupora silaha.
Tukio hilo lilitanguliwa na jingine la Juni, mwaka huu katika kituo kidogo cha polisi cha Mkamba, wilayani Rufiji, ambapo askari mmoja aliuawa na wengine wawili kujeruhiwa, baada ya majambazi kuvamia kituo hicho na kupora silaha na risasi. Matukio ya aina hiyo hakika yamezoeleka, kwani yamekuwa yakitokea katika sehemu mbalimbali nchini.
Hata hivyo, tukio la juzi mjini Songea ambapo askari polisi wawili mkoani Ruvuma waliokuwa katika doria walijeruhiwa baada ya kurushiwa bomu na watu wasiofahamika ni la aina yake.
Tunasema ni tukio la aina yake kwa kuwa tukio kama hilo halijawahi kutokea nchini.
Hatuamini kama waliofanya kitendo hicho walikuwa majambazi, bali raia ambao pengine walikuwa na uhasama na Jeshi la Polisi, kwa maana ya kulipa visasi. Ndiyo maana tukio hilo limeliweka jeshi hilo katika mfadhaiko mkubwa kutokana na kutofahamika kwa lengo na nia ya watu waliofanya kitendo hicho.
Kinachozidisha utata ni kwamba kama waliofanya kitendo hicho walikuwa majambazi wangewapora askari hao silaha au wangevamia kituo chochote cha polisi.
Lakini mazingira yanaonyesha waliofanya kitendo hicho walitaka tu kuwaua askari hao, ingawa bado ni kitendawili kama watu hao walikuwa na uhasama tu binafsi dhidi ya askari hao au Jeshi la Polisi kwa jumla.
Kwa kuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Isaya Mngulu tayari yuko kwenye eneo la tukio, wananchi watarajie kwamba pengine watapata undani wa tukio hilo katika muda siyo mrefu.
Tumezungumzia suala hili kwa uchungu mkubwa kutokana na unyeti wa Jeshi la Polisi.
Kwa sababu jeshi hilo ni roho ya nchi, tungetarajia kila mmoja wetu aliunge mkono badala ya kulidhuru, hata kama baadhi ya askari wake wamepotea njia na kuharibu taswira yake kwa kujikita katika vitendo vinavyolitia doa. Kwa mfano, tafiti zote zimeonyesha kwamba jeshi hilo ni kinara wa vitendo vya rushwa.
Hata hivyo, siyo siri kwamba kutokana na matukio ya kihalifu yanayoendelea kuikumba nchi yetu, tunalihitaji Jeshi la Polisi pengine kuliko wakati mwingine wowote.
Ndiyo maana tunashangazwa na Serikali kutotenga fedha za kutosha kwa ajili ya kuliimarisha jeshi hilo kwa kila hali. Lazima tukubali kwamba tusipowalinda polisi, kamwe nao hawatatulinda.
Tusiendeleze lawama, uhasama na visasi kwa jeshi hilo, kwani kufanya hivyo hakutatusaidia iwapo hatutaliimarisha kwa kuhakikisha lina askari wenye weledi na maadili.
Kuendelea kuitumia FBI kwa matukio ya uhalifu hapa nchini siyo mkakati endelevu. Kinachohitajiwa ni kulipatia mafunzo na nyenzo za kisasa kupambana na uhalifu.
Changamoto kwa jeshi hilo ni kujitathmini na kuwaondoa askari ambao vitendo vyao vimechafua taswira yake mbele ya jamii. Kaulimbiu yake iwe 'haki sawa kwa wote na ulinzi wa raia na mali zao'.
Serikali iwe na dhamira ya kuondoa unyonge wa askari wetu kiuchumi. Hayo yote yamo ndani ya uwezo wetu. Kinachohitajika ni dhamira na utashi.
http://www.mwananchi.co.tz/uchambuzi/Tusipowalinda-polisi-nao-hawatatulinda/-/1597604/2458324/-/item/1/-/63dbkbz/-/index.html
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 Comments