KANSA MBAROUK NA UENYEKITI WA CHADEMA TAIFA.
Nimeona nami niseme kitu baada ya kaka, rafiki na mlezi wangu wa kisiasa kuchukua fomu kuomba ridhaa ya wanachadema ili awaongoze katika kipindi cha miaka mitano ijayo katika nafasi ya mwenyekiti wa chama Taifa!!
Binafsi baada ya kumsikia kwa kitambo kidogo Ndg Kansa Mbarouk katika siasa za mkoa wa Tabora, ni mwaka 2011 ndipo nilipoanza kuwa naye karibu zaidi. Hii ni baada ya kuchaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha tano na sita katika shule ya sekondari ya wavulana Tabora. Toka kipindi hicho mpaka leo amekuwa ni mwalimu wangu mzuri wa siasa. Tulikuwa naye pamoja katika uchaguzi mdogo wa Igunga baada ya kujiuzulu Rostam Aziz, na kwa hakika japo Chadema ilishindwa katika uchaguzi ule lakini kazi iliyofanywa na Ndg Mbarouk ilikuwa kubwa sana na ya kusifiwa na kila mpenda mabadiliko wa nchi hii!!
Nafasi anayoomba ya uenyekiti wa chama Taifa pia inatetewa na Freeman Mbowe ambaye amekuwa kwenye nafasi hiyo tangu 2004.
Kwanza kabisa binafsi ninaamini ndg Mbarouk anatosha kabisa kwa nafasi aliyoomba na ameonyesha uthubutu na kuondoa kile kilichokuwa kinaandaliwa cha kumfanya Mbowe apite bila kupingwa kama ilivyokuwa 2009 baada ya wazee kumuomba Zitto Kabwe ajitoe kugombea nafasi hiyo na kumuachia Mbowe. Nimekuwa nikiikosoa hatua hiyo ya wazee wa chama kwani iliinyima nafasi demokrasia ya kuchaguana ndani ya chama kinachojinasibu kuwa ni cha kidemokrasia!!
Kwa nini ninaamini kuwa Mbarouk ndiye anafaa kuwa Mwenyekiti wa chama kwa wakati huuu!!??
1. Huyu ni mtu ambaye anakifahamu chama kindakindaki akiwa ni miongoni mwa wanachama wa mwanzo kabisa kujiunga na Chadema mwaka 1992 kipindi inatafuta wadhamini. Amekuwa kiongozi kati ngazi mbalimbali za chama kama vile Katibu wa chama wilaya ya Tabora, Katibu wa Chadema mkoa wa Tabora, Mwenyekiti mkoa wa Tabora na mjumbe wa Kamati kuu kwa miaka mingi! Uzoefu alionao katika uongozi ndani ya chama sio wa kubezwa, amekuwa ni kiongozi wa chama katika ngazi mbalimbali toka chama kinaanzishwa mpaka kilipofika leo. Hivyo anatambua changamoto za kiuongozi na anajua jinsi ya kukabiliana na changamoto hizo bila kukigawa chama, ni kiongozi anayekubali kukosolewa pale anapokosea hukuakitambua uongozi ni dhamana ya muda tu na si kitu cha kudumu!!
2. Kuingia kwa Mbarouk kwenye ofisi ya Mwenyekiti wa Chadema Taifa kutasaidia kuondoa ile dhana iliyojengeka vichwani mwa watu kuwa Chadema ni chama cha kikabila, kikanda na kidini. Hii itasaidia sana kuzima hoja hizo ambazo kwa kiwango kikubwa sana zimekuwa kikwazo kwa chama kukubalika kwa watu wa baadhi ya kada hapa nchini kwetu.
3. Mbarouk ni mtu ambaye anafahamu umuhimu na wa kushusha ruzuku kwa ngazi za chini na kudhibiti matumizi ya fedha za walipa kodi wa nchi hii zinazoingia Chadema kama ruzuku na pia michango ya watu wengine wenye mapenzi mema na Chadema.
Anafahamu ni ugumu gani wanaopata viongozi wa chama ngazi ya chini katika uenezi wa chama kwa kukosa pesa za uendeshaji wakati chama kinapata ruzuku na inaishia makao makuu ya chama. Naamini anaweza kusimamia haya kwani ameanzia nafasi ya chini kabisa, hivyo anajua umuhimu wa kushusha ruzuku mpaka ngazi ya chini kabisa!!
Ni mwanasiasa ambaye ana msimamo usioyumba katika kusimamia anachoamini, anatambua kuwa katika siasa hakuna rafiki wala adui wa kudumu bali kunakuungana mkono kwa hoja inayokuwepo kwa muda husika. Hii imemfanya awe karibu na viongozi wenzake wa chama kwa ngazi zote.
Huyu ni rafiki yake na Freeman Mbowe toka kipindi yeye akiwa katibu wa chama wilaya ya Tabora na Mbowe ni mwenyekiti wa BAVICHA Taifa, amekuwa karibu na Zitto Kabwe tangu kipindi Zitto yuko chuo kikuu cha Dar es Salaam, amekuwa karibu na Dr. Slaa kwa miaka mingi. Hoja yangu hapa ni kuwa Mbarouk mtu anayeweza kukirudisha chama katika umoja wake wa awali, huyu ni kiongozi anayeweza kuponya maumivu na kuondoa makovu ya makundi yaliyotokana na uchaguzi wa 2009 ndani ya chama.
4. Ni kiongozi ambaye wanachadema hawatajuta kumpa ridhaa awaongoze, baada ya uongozi wa Mzee Mtei, Marehemu Makani na Mbowe sasa ni wakati wa mtu mwingine kupokea kijiti cha uongozi. Baada ya chama kuonekana kudumaa kwa muda na kuanza kupoteza imani ya wananchi ni wakati wa kuruhusu mawazo na fikra mpya ziongoze chama!!
Hivyo ninaamini ndg Kansa Mbarouk ni chaguo sahihi kwa wanachadema katika nafasi ya mwenyekiti wa chama, najua atakumbana na vikwazo na vitimbwi vingi katika safari yake ya kutimiza adhima yake ya kuleta mabadiliko ndani ya chama!
Najua atakutana na mashambulizi yaliyozoeleka kwa kila anayesimama kumpinga Mbowe kuwa ni msaliti, mamluki, pandikizi na majina yote yanayodhi na kukera lakini hapaswi kukata tamaa.
Atashambuliwa sana na baadhi ya watu ambao wanaamini kina Mbowe mi Sacred na hawapaswi kupingwa kwa lolote lile, atakumbana na vitisho vya kila namna lakini hapaswi kukata tamaa kwani kwa sasa amebeba matumaini ya watanzania wengi wanyonge wenye matumaini na chadema mpya!!
Chadema mpya isiyo na ubaguzi, Chadema mpya ambayo ni chama dola chenye misingi na si chama cha kudandia hoja na kila hoja moja inapochuja wanahaha kutafuta hoja nyingine ya kukipandisha juu chama.
Mbarouk ni mtu wa kuja kukitoa chama kutoka makao makuu mpaka ngazi ya chini kabisa ya msingi, tofauti na sasa ambapo chama hakijui kina misingi mingapi nchi nzima na kama kuna idadi nina uhakika wa asilimia mia moja kuwa data hizo ni za uongo. Haya yakiwa ni matokeo ya kuleana ndani ya chama kwa viongozi wanaosema yes kwa mwenyekiti na katibu mkuu kwa kila kitu.
Mwisho nimtakie heri kaka yangu, rafiki na mlezi wangu kisiasa kwa uthubutu aliouonyesha na si kufanya maigizo kama ya Mbowe eti kuchukuliwa fomu na wazee kutoka nyumbani kwao na hasimu wake wa kisiasa, ukiwa ni muendelezo wa siasa zile zile za chuki, siasa za kitoto na siasa zisizo na dira wala maono!!
Wanachadema wasipomuelewa leo watamuelewa miaka mingi ijayo wakiwa wameshachelewa sana, wakati wa mabadiliko ni sasa!!
John Patrick,
LL. B.
UDSM
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 Comments