[wanabidii] CUF:TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI - 9/11/2014

Thursday, September 11, 2014

CUF:TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

11/0/2014

Kifungu 21 cha Azimio la Haki za Binaadamu duniani kinatamka kwamba "Matakwa na utashi wa watu utakuwa ndio msingi wa mamlaka ya Serikali, matakwa haya yatathibitishwa na uchaguzi ndani ya vipindi mbali mbali. Uchaguzi huo utakuwa sawa kwa wote na kutoa haki ya kuchagua na utafanywa kwa kura ya siri au kwa utaratibu mwengine ulio huru"
Kifungu hiki kinaweka kanuni ya msingi ya usawa wa kuchagua (kupiga kura) au kupata uwiano wa uwakilishi na ndio msingi mmoja kati ya misingi ya kuwepo kwa mipaka ya majimbo ya uchaguzi duniani kote.

Mamlaka ya Tume

Tume ya uchaguzi Zanzibar ndio chombo kilicho na mamlaka ya kusimamia chaguzi zote za Wananchi na kura ya maoni zinazofanywa Zanzibar. Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, toleo la mwaka 2010 Tume imepewa mamlaka na vigezo vya kuzingatia katika kuongeza au kupunguza majimbo ya uchaguzi kwa kutilia maanani sababu mbali mbali. Kifungu cha 120 cha Katiba hiyo kinasema:- 
1) Bila ya kuathiri masharti ya kifungu hiki, Zanzibar inaweza kugaiwa katika majimbo ya uchaguzi yenye majina na mipaka kama yatakavyoelezwa na Tume.

2) Baraza la Wawakilishi linaweza kuweka kisheria, idadi ndogo kabisa ya majimbo ya uchaguzi yasiyopungua 40 na idadi kubwa kabisa ya majimbo yasiyozidi 55.

3) Majimbo yote yatakuwa karibuni na wakaazi sawa sawa kama itakavyoonekana na Tume, lakini Tume inaweza kuepuka shuruti hii kwa kiwango kile kinachofikiria kuwa inafaa kwa ajili ya kuzingatia:


a) idadi ya watu na zaidi katika kuhakikisha uwakilishi unaofaa katika miji mikubwa na miji ya mashamba yenye idadi ndogo ya watu;
b) ukuaji wa idadi ya watu;
c) njia za usafiri;
d) mipaka ya sehemu ya utawala, na kwa madhumuni ya kifungu hiki idadi ya wakaazi wa sehemu yoyote ya Zanzibar itahakikishwa na ripoti ya kuhesabu watu ya karibuni sana ambayo imefanywa kwa mujibu wa sheria.

4) Katika kipindi cha miaka 8 hadi 10 au wakati wowote Tume itachunguza idadi ya mipaka na majina ya majimbo hayo kwa kiwango kile ambacho inahisi ni wajibu kuangaliwa upya, na inaweza kwa kutoa tangazo, kubadili idadi, mipaka na majina ya majimbo hayo.


5) Iwapo hesabu ya idadi ya watu imeshafanywa kwa mujibu wa sheria, au iwapo mabadiliko yamefanywa katika mipaka ya sehemu yoyote ya Utawala, Tume inaweza ikachunguza suala hilo na kuweka mabadiliko hayo katika kiwango kile ambacho Tume inahisi ingefaa kufanyiwa mabadiliko hayo.

Kwa kutumia Mamlaka iliyotajwa hapo juu, Tume ya Uchaguzi Zanzibar imepitia na kuyagawa upya Majimbo ya Uchaguzi Zanzibar katika vipindi tofauti vya muda. Kwa Mfano Kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, mwaka 2000 Majimbo ya Malindi, Mkunazini na Makadara yaliyokuwemo katika orodha ya Majimbo ya Wilaya ya Mjini yalifutwa na badala yake Tume ikaanzisha Majimbo Mapya ya Mji Mkongwe, Chumbuni na Dole.

Kwa kutumia kigezo cha Sensa ya mwaka 2002, ambapo Zanzibar ilikuwa na idadi ya watu 981,754, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ilifanya upitiaji upya wa majimbo ya uchaguzi mwaka 2005, ambapo katika zoezi hilo baadhi ya majimbo yalibadilishwa majina na mipaka mipya kuongezwa. Majimbo ya Mwera, Muembemakumbi, Mlandege, Utaani, Vitongoji, Wingwi na Pandani yalifutwa, na Majimbo mapya ya Magogoni, Bububu, Fuoni, Kiembesamaki, Mtoni, Mwanakwerekwe, Mpendae na Wete yakaanzishwa.

Wakati Tume ikifanya zoezi hili ilizingatia kigezo cha idadi ya watu pekee na kuacha kuzingatia vigezo vingine vya kikatiba kama inavyotakiwa na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Aidha, kigezo hiki cha idadi ya watu kinaonekana kutumiwa kwa utashi wa kisiasa kwani wakati wa zoezi hilo kilitumika katika kuyagawa majimbo ya baadhi ya wilaya mfano majimbo ya wilaya ya Wete, na kuacha kutumiwa katika wilaya nyengine kama vile majimbo ya wilaya ya Kaskazini 'A'

Upitiaji huo wa Majimbo ya uchaguzi Zanzibar ulioshindwa kuzingatia vigezo vya kikatiba ulisababisha
i. Kuwepo kwa uwakilishi usio sawa. Hii ilitokea pale wakati wa upunguzaji wa majimbo zaidi kwani kura za waliokuwa wakishinda huenda zikapotea baada ya jimbo lao kuondolewa na tume. Mfano ubadilishaji wa mipaka ya Jimbo la Kikwajuni mwaka 2000 kwa kuliongezea baadhi ya shehia nje ya jimbo hilo (shehia ya Miembeni) kwa ajili ya kukisaidia Chama Tawala ulipelekea kutokea kwa tatizo hilo.


ii. Sauti za kura au maamuzi ya wapiga kura kutokuwa na thamani. Mara nyingi kura huwa ni kielelezo cha maamuzi ya watu kupata kiongozi wao au kufanya maamuzi katika maendeleo ya jamii yao. Ugawaji na ukataji wa majimbo uliofanywa na Tume ya uchaguzi kwa miaka iliyopita uliegemea mrengo wa kisiasa na hivyo kufanya kura za watu fulani au kundi fulani zisionekane athari yake katika maamuzi husika.

iii. Kuondoka kwa ushawishi na mchango wa chama ambacho mawazo yake hayazingatiwi katika maamuzi ya uendeshaji wa chaguzi. Kila kundi ndani ya jamii lina nafasi yake katika kukuza demokrasia na Maendeleo ya siasa na uchumi. Mfumo usio makini uliotumika katika mchakato wa kuongeza au kupunguza ama kubadili mipaka ya majimbo kwa lengo la kusaidia kundi fulani, umepelekea kudumaa kwa siasa za ushindani na hivyo kudumaza maendeleo na ustawi wa watu katika baadhi ya majimbo ya uchaguzi.

SABABU ZA KUKUTANA NA WANAHABARI

1.CUF-Chama Cha Wananchi kinatambua mchango mkubwa unaotolewa na waandishi wa habari katika shughuli za maendeleo, vyombo vya habari katika ulimwengu wetu wa leo vimekuwa ni kiunganishi kikubwa kati ya jamii na taasisi mbali mbali.


2. Katika siku za hivi karibuni, Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi Zanzibar amesikika akisema kwamba ni Wananchi tu ndio ambao wametoa maoni juu ya zoezi la upitiaji na ugawaji wa majimbo. CUF imeamua kukutana na wanahabari kuwaeleza kwa uwazi kwamba iliwasilisha nyaraka mbili ambazo zinajitosheleza kimaelezo juu ya upitiaji, ugawwaji na ubadilishaji wa majimbo na wadi za uchaguzi kwa namna ambayo kwa namna ambayo itasaidia ugawaji bora wa majimbo ya uchaguzi Zanzibar.


3.CUF-Chama Cha Wananchi kimelazimika kukutana na wananhabari kuelezea wasi wasi wake juu ya taarifa za Tume ya Uchaguzi Zanzibar kujenga mazingira ya kuhalalisha kutumia maoni ya chama tawala katika ugawaji na upitiaji wa majimbo kinyume na utaratibu wa sheria na hivyo kuwa mwanzo wa uvurugaji wa uchaguzi mkuu wa 2015.

UDHAIFU WA TUME YA UCHAGUZI YA ZANZIBAR KATIKA MAPITIO NA UGAWAJI WA MAJIMBO MIAKA ILIYOPITA

Katika ugawaji wa mipaka ya majimbo ya uchaguzi uliofanywa na Tume mwaka 2000 na 2005 kasoro zifuatazo zilijitokeza:
i.Kuzingatiwa kwa kigezo kimoja cha idadi ya watu na kutotilia maanani vigezo vingine vya kikatiba. Mfano kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 toleo la 2010 Tume ya uchaguzi imetakiwa, pamoja na mambo mengine, kuhakikisha uwakilishi unaofaa katika miji mikubwa na miji ya mashamba yenye idadi ndogo ya watu.

Ugawaji wa majimbo mwaka 2005 kwa kiasi kikubwa ulishindwa kuzingatia kigezo hicho. Majimbo ya wilaya za Wete, Chake chake, na Micheweni yaliyofutwa yalikuwa na sifa za miji ya mashamba.

ii.Kuzingatiwa kwa baadhi ya vigezo kwa baadhi ya majimbo na kupuuzwa katika majimbo mengine. Mfano, kwa mujibu wa sensa ya watu na makaazi ya mwaka 2002, Mkoa wa kaskazini Unguja ulikuwa na idadi ya watu 136,639 na kupaswa kuwa na majimbo saba, lakini Tume iliamua kuweka majimbo nane ya uchaguzi katika wilaya hiyo.

Kwa mujibu wa gazeti la Nipashe toleo namba 0578232 la Jumatano septemba 10, 2014, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jecha Salim Jecha, alisema kuwa yapo baadhi ya majimbo yana idadi kubwa ya wakaazi na yanastahili kukatwa na kuwa majimbo mawili tofauti na majimbo mengine yana idadi ndogo ya wakaazi yanastahili kukatwa mfano majimbo mawili kufanywa jimbo moja.

Aidha, Mkurugenzi wa tume hiyo, Salum Kassim Ali, alitaja majimbo kama vile Dimani lenye idadi ya wananchi 58,000, Fuoni lenye Wananchi 65,000 na Dole lenye wananchi 39, 000 kuwa ni majimbo yanayoongoza kwa na idadi kubwa ya watu na majimbo ya Mgogoni lenye idadi ya watu 17,000, Chambani lenye idadi ya watu 15, 000 na Raha Leo lenye idadi ya watu 16,000 kuwa ni majimbo yenye idadi ndogo ya watu.

Taarifa za Tume ya uchaguzi Zanzibar juu ya idadi ya watu katika majimbo ya uchaguzi, kama zilivyochapishwa na vyombo vya habari, ni za upotoshaji na zinazokwenda kinyume na taarifa mbalimbali za serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kwa mujibu wa sensa ya watu na makaazi ya mwaka 2012, jimbo la Mgogoni lina idadi ya watu 21, 649 badala 17,000, Chambani kuna wakaazi 15, 909 badala ya 15, 000 na Dole lina watu 38, 775 badala ya 39, 000 kinyume na madai ya Mkurugenzi wa Tume ya uchaguzi Zanzibar.

Mbali ya kupewa mamlaka ya kutumia vigezo mbalimbali kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar, Tume imekuwa ikitumia zaidi kigezo cha idadi ya watu katika kuyagawa majimbo ya uchaguzi Zanzibar. Kigezo hiki hakitokuwa na mantiki ya kutumika kwa sasa. Kwa mujibu wa Takwimu za sensa ya watu na makaazi ya mwaka 2012 hakuna ushahidi wa kupungua kwa idadi ya watu katika wilaya na mkoa wowote wa Zanzibar, bali ongezeko kubwa la idadi ya watu katika maeneo hayo.

Aidha, sensa ya mwaka 2012 ilifanyika baada ya miaka kumi (2002-2012) kinyume na sensa ya mwaka 2002 ambayo ilifanyika baada ya miaka 14 (1988-2002), hivyo kulinganisha ongezeko la idadi ya watu na kugawa majimbo kwa kigezo cha idadi ya watu kwa kutumia sensa hizi mbili hakutakuwa na mantiki ya msingi.

Kuwepo kwa idadi ya majimbo yenye watu wengi na hivyo kukosekana uwiano sawasawa wa uwakilishi wa wananchi katika majimbo ya uchaguzi kutoka jimbo moja hadi jingine, kama inavyoelekezwa na katiba, kunatokana na mfumo mbaya ulioshindwa kuzingatia vigezo vya kikatiba na kimazingira katika kuyagawa majimbo ya uchaguzi katika miaka iliyopita kwa lengo la kukihakikishia chama tawala ushindi.

Aidha maelezo ya Tume ya uchaguzi yanathibitisha uwepo wa lengo la kugawa majimbo ya uchaguzi kwa kuzingatia kigezo cha idadi ya watu na kupuuza vigezo vyengine vya msingi vya kikatiba kama vile uwiano wa uwakilishi wa miji mikubwa na miji ya mashamba yenye idadi ndogo ya watu, njia za usafiri na mipaka ya sehemu ya utawala kama ilivyojitokeza katika ugawaji wa majimbo ya uchaguzi katika miaka iliyopita.

Kama ilivyoainishwa, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imepewa mamlaka ndani ya katiba kuhakikisha uwakilishi unaofaa katika miji mikubwa na miji ya mashamba yenye idadi ndogo ya watu. Hichi ni kigezo kimojawapo ambacho Tume inaweza kukizingatia kwa kutengua shuruti ya uwakilishi sawa sawa wa idadi ya watu katika kuyagawa majimbo na mipaka yake. Majimbo yanayoelezwa na Tume ya uchaguzi kuwa na idadi ndogo ya watu, kama ilivyochapishwa na vyombo vya habari, yana kidhi haja na sifa ya kubaki kama yalivyo kutokana na kuwa na sifa ya kuwa ni majimbo ya mashamba kama inavyotakiwa na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, toleo la 2010.

Kufutwa kwa majimbo yanayodaiwa kuwa na idadi ndogo ya watu kwa kuchanganywa na kuwa jimbo moja, kutapelekea kupunguza uwiano wa uwakilishi wa Wananchi katika vyombo vya uwakilishi na maamuzi. Uzoefu unaonesha wazi kwamba Tume ya Uchaguzi mara zote imekua ikiegemea hoja ya idadi ya watu na kusahau hoja nyengine zilizomo ndani ya mamlaka iliyopewa kwa mujibu wa katiba.

Upitiaji wa mipaka ya Majimbo uliofanywa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar mwaka 2005 na kupelekea kufutwa kwa majimbo ya Mwera, Utaani, Vitongoji, Wingwi na Pandani kwa kigezo cha idadi ya watu bila ya kuzingatia kwamba ni majimbo ya miji ya shamba yenye tofauti kubwa na miji mikubwa.

Aidha, maelezo ya Tume yanadhihirisha muendelezo wa mpango wa ukiukwaji wa sheria na utendaji wa upendeleo kama inavyothibitishwa na matokeo mbalimbali ya uvizaji wa demokrasia nchini. Mfano wa karibu wa kuthibitisha jambo hili ni matukio yaliyojitokeza baada ya zoezi la uandikishaji na uwekaji wazi wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Baada ya kumalizika kwa mara ya pili kwa zoezi la uandikishaji wa wapiga kura, Tume kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi ya Zanzibar ya mwaka 1984, kifungu cha 25 (i), ilitangaza ruhusa ya pingamizi kwa walioandikishwa bila ya kukidhi sifa na vigezo vya haki ya kuandikishwa.

Mfano wa mipango ya uchafuzi wa uchaguzi mkuu wa 2015 unadhihirika katika jimbo la Tumbatu ambapo katika malalamiko ya pingamizi 288 yaliyoripotiwa katika Tume ya uchaguzi katika jimbo hilo, ni watu 12 tu ndio waliyoondoshwa katika daftari kama inavyoonekana katika jadweli lifuatalo:
Nam

Shehia

Pingamizi zilizowekwa

Pingamizi zilizosikilizwa

Pingamizi zisizosikilizwa

Waliofutwa katika daftari

waliobaki
1.

Pale

225

91

134

2

223
2.

Mto wa pwani

63

19

44

10

53


JUMLA

288

110

178

12

276

Kutokana na kasoro hizo na dalilili mbalimbali zilizojitokeza kama ilivyoelezwa, The Civic United Front (CUF-Chama Cha Wananchi) kinaitaka Tume ya uchaguzi kuzingatia matakwa ya kikatiba na kuweka kwa uwazi uwiano wa kimajimbo ili kuhakikisha uwakilishi bora wa wananchi katika vyombo vya maamuzi na kutunga sheria kwa kuweka asilimia ambayo jimbo linaweza kutofautiana na jimbo jengine (percentage of deviation) kwa idadi ya watu.

Aidha, CUF inaitaka Tume ya uchaguzi ya Zanzibar kuzingatia kuwa kumekuwepo na malalamiko ya muda mrefu ya wadau wa uchaguzi juu ya utaratibu mbovu wa ugawaji wa majimbo Zanzibar kulikopelekea uvunjifu wa amani kulikotokana na kutokuridhika kwa baadhi ya wananchi.

Ili kuiepusha nchi na watu wake kurudi katika zama za khasama, chuki na mifarakno, CUF-Chama Cha Wananchi kinaishauri Tume kuzingatia matakwa ya Katiba na kufanya kazi zake kwa uadilifu na kutopokea maagizo yoyote nje ya mamlaka yake katika kusimamia zoezi la uongezaji au upunguzaji au ubadilishaji wa mipaka ya majimbo ya uchaguzi ili kuimarisha ustawi wa demokrasia ndani ya Zanzibar.

Kutokana na maelezo yaliyoainishwa hapo juu, The Civic United Front (CUF-Chama Cha Wananchi) kinaitaka Tume ya uchaguzi ya Zanzibar kuzingatia mazingira ya amani na maelewano yaliyopo na kutokuwa taasisi ambayo itakuwa chanzo cha vurugu na mifarakano katika nchi.

IMETOLEWA NA:


MH. NASSOR AHMED MAZRUI
NAIBU KATIBU MKUU CUF- ZANZIBAR


--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Related Posts

0 Comments