MCHANGO Prof. Mgongo Fimbo KWENYE MDAHALO WA CHAMA CHA WANASHERIA, TANGANYIKA, UBUNGO PLAZA, TAREHE 2 AGOSTI 2014
Kwa hali ilivyo, mimi sijadili Mkwamo, ninajadili kinyume chake, yaani MUAFAKA.
Mpaka sasa makundi mawili ya BUNGE MAALUM LA KATIBA, yaani, UKAWA na TANZANIA KWANZA hayajafikia muafaka kuhusu Muundo wa Jamhuri ya Muungano. Mkwamo unahusu ubishi wa Madaraka. UKAWA wanataka muundo wa Serikali Tatu uliopendekezwa na TUME YA MABADILIKO YA KATIBA wakati TANZANIA KWANZA wanapendelea muundo waliouzoea wa Serikali Mbili. Hali hii imekuwa hivyo kwa sababu hawajampata Mpatanishi mwenye weledi na upeo wa kutosha.
Kwa kuzingatia kichwa cha Mdahalo huu. mimi ningeshauri ifuatavyo:
. UKAWA wafikirie kuafiki wazo la Bunge la Tanganyilka (kwa jina au utaratibu wowote ule) kusimamia mambo yasiyokuwa ya Muungano kama inavyopendekezwa na TANZANIA KWANZA.
. UKAWA na TANZANIA KWANZA wafikirie kuafiki uwepo wa Mkuu wa utawala wa Tanganyika (ambaye siyo Rais) mwenye mamlaka kamili kwa mambo yasiyokuwa ya Muungano. Huyu mkuu wa utawala asaidiwe na Baraza la Mawaziri kushughulikia mambo yasiyokuwa ya Muungano na awajibike kwenye Bunge la Tanganyika.
. UKAWA na TANZANIA KWANZA wafikirie kuafiki uwepo wa Mfuko wa Hazina wa Tanganyika.
. UKAWA na TANZANIA KWANZA wafikirie kuafiki uwepo wa mamlaka ya Mahakama za Tanganyika – Mahakama Kuu na Mahakama za Mahakimu.
. UKAWA na TANZANIA KWANZA wafikirie kuafiki uwepo wa mamlaka za serikali za mitaa Tanganyika.
. UKAWA na TANZANIA KWANZA wafikirie kuafiki uwepo wa usimamizi wa Ardhi na Rasilimali Asilia za Tanganyika.
TUME YA MABADILIKO YA KATIBA ilitarajia kuwa mambo haya yote yangeingizwa kwenye Katiba ya Tanganyika; kwa hiyo hayamo kwenye RASIMU YA KATIBA ingawa sisi wananchi tuliwapelekea mapendekezo kamili.
Kama UKAWA na TANZANIA KWANZA wataona kuwa mambo haya ni mazito basi wanialike kuwa MSULUHISHI WAO bila malipo. Hapa majuzi kuna mwandishi aliandika kuwa Msuluhishi hateuliwi, hujitolea mwenyewe.
Iwapo mambo haya yanazungumzika, basi Bunge Maalum la Katiba liahirishwe mpaka muafaka upatikane. Iwapo muafaka utapatikana, makundi yote mawili yatakuwa Washindi.
HALAFU SURA moja au mbili hata tatu ziandikwe na Wataalamu na kuongezwa kwenye RASIMU YA KATIBA. Mapendekezo ya wananchi juu ya masuala haya yapo, yaliwasilishwa kwenye TUME YA MABIDILIKO YA KATIBA.
Hatua hizi hazipingani kamwe na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba; hatua hizi ni kuboresha RASIMU YA KATIBA wala siyo kupingana na misingi yake.
NIONGEZE, UKAWA na TANZANIA KWANZA wafikirie kuafiki mawazo kuwa:-
i. Ili kukinga ubinafsi ndani ya Bunge Maalum la Katiba, Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba hatagombea, kuchaguliwa au kuteuliwa katika nafasi ya kisiasa hadi utakapopita muda wa miaka mitano tokea kuacha nafasi ya Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba kwa kujiuzulu au maisha ya Bunge Maalum la Katiba kukoma. Mjumbe atakayejiuzulu kabla ya Bunge Maalum la Katiba kufanya uamuzi kwa kupiga kura juu ya SURA yoyote ya Rasimu ya Katiba hatabanwa na masharti haya.
ii. Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba yuko huru kujiuzulu kwa kutoa taarifa iliyoandikwa na kutiwa saini kwa mkono wake na kuiwasilisha kwa Katibu wa Bunge Maalum la Katiba.
Mawazo haya hapo juu yanaweza kutekelezwa bila kubadili Sheria yo yote.
Mwisho
Haya yangu Mimi Zitto
Bahati mbaya sana watu wameziba masikio yao na kuweka misimamo yao. Mawazo haya ya wazee wetu yangeweza kuondoa mkwamo uliopo hivi sasa.
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 Comments