[wanabidii] TAARIFA KWA UMMA Juu ya Taarifa za Msajili wa Vyama vya Siasa Kuingilia Mambo ya CHADEMA

Thursday, July 03, 2014
OFISI YA MKOA MTWARA S.L.P 446 MTWARA 

TAARIFA KWA UMMA Juu ya Taarifa za Msajili wa Vyama vya Siasa Kuingilia Mambo ya Chama na Kudhoofisha Demokrasia 

Utangulizi

Taarifa hii inatolewa na Uongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Mkoa wa Mtwara baada ya kutafakari na kujiridhisha kuwa taarifa zilizotolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Fransis Mutungi, ambazo hajazikana zina lengo hasi kwa ukuaji wa demokrasia nchini na kuwa zinadidimiza kabisa na kudhihaki juhudi na michango ya wananchi wa mkoa wa Mtwara katika kujenga demokrasia hapa mkoani na nchini kote. 

Hoja za Tamko 
1.-Ikumbukwe kuwa hivi karibuni Jaji Mutungi amenukuliwa na vyombo vya habari akikaripia na kuwazuia viongozi wa chama, yaani Mwenyekiti wa Chama Taifa Mhe. Freeman Mbowe na Katibu Mkuu wa Chama Mhe. Dr. Wilbroad Slaa, kugombea tena uongozi kwenye chama kwa madai ya kuvunja Katiba ya Chama huku akidai eti Katiba ya chama imekiukwa. 

2.-Huku akijua kuwa utawala wa serikali umepiga marufuku, kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mikutano ya hadhara mkoani Mtwara na hata shughuli zingine zap kisiasa mkoani na kwenye wilaya zake. 

3.-Jaji Mutungi kuingilia shughuli halali za chama kinyume cha majukumu ya ofisi yake na matarajio ya wananchi katika kujenga demokrasia nchini. 

HIVYO BASI: 
1.-Tunaona msajili wa vyama vya siasa anaingilia mambo ya ndani ya chama na kuacha majukumu ya ofisi yake kwa mujibu wa sheria. Hii ni kutokana na ukweli kuwa tamko la Msajili limekuja kinyume cha Katiba ya CHADEMA ambapo kifungu kinachoweka kizuizi kwa -kiongozi kugombea uongozi kutokana na kuwepo madarakani kwa kipindi fulani hakipo, na kuwa kilifutwa kihalali kwa mabadiliko ya Katiba yaliyofanywa tangu 2006; - 

2.-Katiba ya CHADEMA ilitungwa upya mwaka 2006 na hivyo sio tu baadhi ya vifungu viliandikwa upya bali Katiba yote iliandikwa upya na kuwa taarifa hizi zilishafikishwa ofisi ya msajili, inakuwaje leo aje kudai mabadiliko huku akijua sio kweli? Cha kushangaza zaidi Msajili aliandikia barua Ofisi ya CHADEMA Makao Makuu tangu Januari 2014 na kupata ufafanuzi juu ya kile kilichofanyika mwaka 2006 katika uandikaji wa Katiba mpya ya CHADEMA.

Huku tukiendelea kuwaunganisha wapenda demokrasia na mabadiliko nchini kuendelea kujenga demokrasia na kuenzi upatikanaji haki kwa njia za kidemokrasia, tunaamini mbinu hizi za wasiopenda demokrasia ZITASHINDWA. Mhe. Mutungi asiwe mmoja wa watu hao, na hivyo:- 

1.-Tunamshauri Msajili ajikite kutekeleza majukumu yake kisheria na kwa mujibu wa Katiba ya Nchi. Hii itamjengea uhalali kuwepo lakini heshima pia kwa jamii. Anapofanya mambo yanayoashiria kutumiwa na makundi ya wasiopenda demokrasia ili kuutetea utawala wa chama kilicho madarakani, anajivunjia heshima yeye mwenyewe na jamii; 

2.-Msajili arejee kwenye kutimiza matarajio ya wananchi ikiwemo kusimamia uendeshaji wa michakato ya usajili na uendeshaji vyama vya siasa katika kujenga demokrasia kwa mujibu wa Katiba za vyama vyenyewe. Msajili akumbuke kuwa yeye si mwanachama wa CHADEMA na wala si mahakama; na 3.-Arejeshe ofisi yake kwenye jukumu kuu la kuimarisha demokrasia kwa kuitaka serikali iache mara moja ubakaji wa demokrasia mkoani Mtwara, na hivyo waondoe vizuizi vya mikutano ya wananchi, majumuiko ya wazi na uhuru wa kutoa maoni na kusikilizwa. 

Imetolewa nami, - 

Bw. Kassim Bingwe 

Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Mtwara

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Related Posts

0 Comments