[wanabidii] TANZANIA KUWA JIMBO JIPYA LA CHINA BARANI AFRIKA

Thursday, June 12, 2014
Na Daniel Mbega, Ludewa

ISAAC Haule (65), mkulima mdogo katika Kijiji cha Nkomang'ombe wilayani Ludewa, ana hamu ya kuona miradi ya Mchuchuma na Liganga ikianza kutekelezwa kwa maelezo kwamba inaweza kuleta zama mpya katika sekta ya madini
Baba wa watoto watano na mtumishi wa umma mstaafu, Haule anasema wananchi wana imani na miradi hiyo, lakini anadhani Ludewa inaweza kuwa 'ubalozi' mpya wa China kutokana na kampuni ya Sichuan Hongda kuingia mkataba wa uwekezaji wa Dola 3 bilioni (takriban Shs. 4.8 trilioni) kwenye uchimbaji wa makaa ya mawe na chuma ambao utadumu kwa zaidi ya miaka 100.
"Sahau ubalozi rasmi ulioko Mtaa wa Kajificheni katika eneo la vizito la Oysterbay jijini Dar es Salaam, au masoko yaliyosheheni bidhaa zilizotengenezwa China, lakini 'ubalozi' mpya mkubwa utakuwa hapa Ludewa kwenye miradi hii," anasema.
Hata hivyo, anasema utekelezaji wa miradi hiyo utafungua ukurasa mpya wa uchimbaji madini, hususan chuma huko Liganga ambapo upatikanaji wake utasaidia kukuza sekta ya viwanda vya chuma nchini Tanzania.
"Ukilinganisha na mataifa ya Ulaya Magharibi, kwa maoni yangu, Wachina ni wawekezaji wazuri, tuna imani miradi hii itafanikiwa kwa kuwa hakutakuwa na siasa," anaongeza.
Maoni yake yanaungwa mkono na Pius Ngeze, kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na mbunge wa zamani wa Ngara moani Kagera, ambaye anaona uwekezaji wa Wachina katika miradi hiyo pacha kama muhimu kwa uchumi wa taifa pamoja na kelele zinazopigwa na mataifa ya Magharibi.
"Tangu uhuru China imekuwa ikiisaidia nchi hii, hii si mara ya kwanza, ukilinganisha na Ulaya Magharibi ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikisaidia maendeleo ya Afrika, Wachina wanaaminika. Nina imani hata miradi hii itafanikiwa," anasema.
Ngeze anasema, kwa kadiri utandawazi ulivyo, Ulaya Magharibi haipaswi kuihofia China kutokana na kumwaga fedha nyingi Afrika kwa sababu bara hili nalo linahitaji maendeleo baada ya kuwa nyuma kwa miaka mingi.
"Ukweli ni kwamba mataifa ya Ulaya Magharibi yamenufaika sana na bara la Afrika tangu enzi za utumwa hadi ukoloni, wametuhujumu, wakachukua rasilimali zetu kwa ajili ya kushibisha mahitaji ya viwanda vyao na hawakuwapa Waafrika elimu ya kutosha kujitawala.
"Sasa wameona China imeingia wanaanza kulalamika kwa hofu kwamba hawatakuwa na nafasi ya kutunyonya kwani utaratibu wa China kuwapeleka Waafrika kwenye vyuo vyake utatusaidia kujiendesha wenyewe," anasema.
Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, kampuni za China zimeongezeka kwa kasi kwa kupata mikataba mbalimbali, hususan katika sekta ya miundombinu. Tangu mwaka 2000 China imefadhili miradi mingi nchini Tanzania ukiwemo uwanja wa kisasa wa soka jijini Dar es Salaam ambao uligharibu Dola 34.2 milioni (Shs. … bilioni) huku China ikichangia Dola 19.1 milioni.
Pia China imesaidia kukarabati Uwanja wa Amani mjini Unguja; Ujenzi wa Kituo cha Mafunzo ya Kilimo Dakawa; Ujenzi wa Ukumbi wa Mwalimu Nyerere; Ukarabati wa Miradi ya Maji mjini Dodoma na Chalinze; Miundombinu ya Teknolojia ya ICT; na Ushirikiano wa Ulinzi.

UJENZI WA BARABARA
Kampuni za Kichina zimepata mikataba mingi ya ujenzi. Kwa mujibu wa taarifa kutoka Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, kampuni 14 kutoka China zimeingia jumla ya mikataba 58 ya ujenzi wa kilometa 3,140.85 yenye thamani ya Dola 1.75 bilioni.
Kampuni ya China Henan International Cooperation Group Co., Ltd. (CHICO) ambayo ilipata mkataba wenye thamani ya Dola 206 milioni kutoka Wakala wa Barabara Zambia kujenga barabara ya Mansa-Luwingu yenye urefu wa kilometa 175, peke yake imeingia mikataba 13 nchini Tanzania ya barabara zenye urefu wa kilometa 705.2 zikiwa na thamani ya Dola 490.26 milioni.
Hizi ni pamoja na barabara za Singida-Iguguno; Sekenke-Shelui; Mwandiga-Manyovu; Kigoma-Kidahwe; Bonga-Babati; Tabora-Urambo; Kyaka-Bugene; Dareda-Minjingu; Kidahwe-Uvinza-Ilunde; Isaka-Ushirombo; Kilwa Road Phase III; Nyanguse-Musoma; na Kagoma-Lusahunga kwa ubia na kampuni ya CRSG.
China Sichuan International Cooperation Co., Ltd (SIETCO) inajenga barabara zenye urefu wa 283.9km zenye thamani ya Dola 123.03 milioni ambazo ni Isuna-Singida; Tarakea-Rongai-Kamwanga; Iringa-Migori; na Migori-Fufu Escarpment, wakati kampuni ya CICO inajenga barabara ya Nangurukuru-Mbwemkuru yenye 95km kwa thamani ya Dola 23.82 milioni.
Kampuni ya China Geo-Engineering Corporation International Ltd (CGC INT'L) inajenga barabara zenye urefu wa 525.9km zikiwa na thamani ya Dola 151.2 milioni. Barabara hizo ni Shelui-Nzega; Kyamorwa-Buzirayombo; Manyoni-Isuna; Arusha-Namanga; Chalinze-Tanga Phase I na ndiyo iliyojenga Daraja la Mkapa (Daraja la Umoja) linalounganisha Tanzania na Msumbiji.
Katika orodha hiyo, ipo kampuni inayomilikiwa na serikali ya China, Hydropower Engineering and Construction Company (SINOHYDRO) ambayo ilipata mikataba 12 nchini Tanzania ya ujenzi wa barabara zenye urefu wa jumla ya 779.95km zenye thamani ya Dola 434.36 milioni. Barabara hizo ni Sengerema-Usagara; Buzirayombo-Geita; Geita-Sengerema; Dodoma-Mayamaya; Manyoni-Itigi-Chaya; Puge-Tabora; Handeni-Mkata; Korogwe-Handeni; Katesh-Dareda; Singida-Katesh; Tanga-Horohoro; na Peramiho Junction-Mbinga.
CHIKO ilijenga barabara ya Sam Nujoma jijini Dar es Salaam yenye urefu wa 4km kwa thamani ya Dola 7.9 milioni, China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) ilipata mikataba minne ya kujenga barabara zenye urefu wa 145.6km kwa thamani ya Dola 95 milioni. Barabara hizo ni Magole-Turiani; Tabora-Urambo; Dumila-Rudewa na Jangwani Depot kwa ajili ya mradi wa mabasi yaendayo kasi Dar es Salaam (BRT).
China Communications Construction Company (CCCC) ina mikataba mitano ya ujenzi wa barabara za urefu wa 273.5km zikiwa na thamani ya Dola 178.333 milioni ambayo inahusisha barabara za Mbeya-Lwanjilo; Lwanjilo-Chunya; Mwigumbi-Maswa-Bariadi-Lamadi; Nzega-Tabora na Fufu Escarpment-Dodoma.
Beijing Construction Engineering Group Co., Ltd. (BCEG) ilishinda zabuni katika mradi wa BRT kuanzia Stendi ya Mabasi Ubungo; Kariakoo na Kivukoni, wakati China Henan ndiyo iliyojenga Daraja la Ruvu kwa Dola 2.69 milioni.
Kampuni nyingine za China na miradi yao kwenye mabano ni, Jiangxi Geo-Eng (75km Sumbawanga-Kanazi), China Hunan Construction Engineering Group Corporation - CHCEG (76.6km Kanazi-Kizi-Kibaoni), China Railway 15th Bureau Group Corporation - CR15G (112km Sumbawanga-Matai-Kasanga), na China Newera (64.2km Ikana-Laela).
Kampuni za Kijapani ambazo katika miaka ya 1980 na mwishoni mwa 1990 ndizo zilikuwa zikishindana na kampuni kutoka Ulaya, katika kipindi hiki zilifanikiwa kupata mikataba sita tu ya kujenga barabara za urefu wa 204.4km yenye thamani ya Dola 106.09 milioni wakati kampuni kutoka Ulaya zilikuwa 12 ambazo zilijenga barabara zenye urefu wa 1,688.91km na thamani ya Dola 667.25 milioni.
Enoch Ugulumu, mkuu wa Idara ya Mipango na Uchumi katika Chuo Kikuu cha Iringa (zamani Chuo Kikuu cha Tumaini), anasema China imekuwa ikifanya biashara barani Afrika kwa miaka mingi na sasa nchi hiyo imegeukia kwenye Uwekezaji wa Nje kutazama maeneo muhimu ya kuwekeza kama sekta ya madini.
"Watanzania wengi wanatumia bidhaa za Kichina – kuanzia mijini hadi vijijini – tunazo simu za mikononi, nguo na pikipiki maarufu kama 'Boda-Boda'. Lakini miradi hii pacha hakika inaonyesha uwepo wa Wachina kwa miaka mingi hapa nchini kwa kuwa tunaambiwa kwamba inaweza kudumu kwa zaidi ya miaka 100," anasema Ugulumu ambaye amekuwa akifuatilia kwa karibu uwekezaji huo.

WACHINA HAWAULIZI MASWALI
Hata hivyo, Ugulumu ana imani na uwepo wa Wawachina katika madini, akisema ikiwa utekelezaji wa miradi hiyo pacha utaanza kutakuwa na uhakika kwani China haina kawaida ya kuingilia siasa za ndani za washirika wake wala haishinikizi mabadiliko ya kidemokrasia au serikali.
"Nchi nyingi za Afrika, kwa mfano; Malawi, Zambia, Tanzania na Afrika Kusini zinayavutia Mataifa ya Magharibi kidemokrasia, lakini tazama wananchi wake wanavyoogelea katika umaskini na ukosefu wa ajira. Wacha Wachina waje jamani," anafafanua.
Akizungumzia uwazi katika uwekezaji wa moja kwa moja (FDI), Ugulumu anasema China iko wazi kulinganisha na mataifa ya Magharibi kama Marekani, akitoa mfano kwa nchi kama Zimbabwe, Uganda, Libya, Chad, Gabon, Msumbiji na Guinea ambako mataifa hayo mawili yalikuwa yamewekeza lakini Marekani ikadaiwa kushindwa kutoa takwimu sahihi.
Japokuwa China imewekeza mabilioni ya dola barani Afrika katika sekta ya madini ili kupata mali ghafi kwa ajili ya uchumi wake unaokua kwa kasi, zikiwemo kilometa za mraba 23 katika Bonde la Mui nchini Kenya lenye hazina ya zaidi ya tani 400 milioni za makaa ya mawe yenye thamani ya Dola za Marekani 38.123 bilioni kupitia kampuni ya Fenxi Mining Group, lakini miradi pacha ya Mchuchuma na Liganga ndiyo mikubwa zaidi kwa nchi hiyo.
Shirika la Taifa la Maendeleo NDC) na SHC walisaini mkataba wa ubia mnamo Septemba 21, 2011 na kuunda kampuni ya Tanzania China International Mineral Resources (TCIMR) ambayo, pamoja na mambo mengine, itajenga mtambo wa kufua umeme katika eneo la Mchuchuma wilayani Ludewa ambao utazalisha umeme wa Mega Watts 600, kiwango ambacho kinakaribia kabisa Mega Watts 623 zinazozalishwa kwa mwaka nchini.
Chini ya makubaliano hayo TCIMR itajenga migodi ya makaa ya mawe na chuma, mtambo wa kufua umeme wa makaa ya mawe, na mtambo wa kuyeyusha chuma huko Liganga. Mradi huo pia utajenga njia ya umeme ya 220 kV kutoka Mchuchuma hadi Liganga na njia ya 400 kV kutoka Mchuchuma hadi Mufindi ili kuunganisha kwenye gridi ya taifa.
SHC ilishinda zabuni ambayo ilishuhudia karibu kampuni 48 zikishindana, miongoni mwao tatu zilitoka Australia, nne kutoka India, mbili za China, na nyingine kutoka Singapore, Marekani, Korea Kusini na Malaysia.
Baadhi ya kampuni hizo zilikuwa China Huadian Engineering Company Limited, Nava Bharat Pte Limited (Singapore), Sarda Energy and Minerals Limited (India), AES Corporation (US), STX Corporation (Korea), Rio Tinto (Australia), BHP Billiton (Australia), CANHAM Mining International (Australia), Indria Berhad (Malaysia), Tata Steel Corporation (India), Global Steel Holdings (India) na Ispat Industries (India).
Mgodi wa Mchuchuma umeonyesha kuwa na hazina ya zaidi ya tani 536 milioni za makaa, wakati eneo la Liganga linakadiriwa kuwa na hazina ya chuma ghafi kati ya tani 200 hadi 1,200 milioni, huku tani 45 milioni zikiwa zimethibitishwa katika uchimbaji. Inakadiriwa kwamba tani milioni tatu za makaa zitachimbwa kwa maka, zikidumu kwa zaidi ya miaka 100 na tani 2. milioni za chuma zitachimwa kila mwaka kwa zaidi ya miaka 90.
Kwa Watanzania wengi, SHC inaonekana kama ndiye mkombozi katika mgawo wa umeme wa mara kwa mara pamoja na kupanda kwa gharama za nishati hiyo ambazo wanalipa sasa, hali inayowapa shida wengi wao kutokana na kuwa na kipato cha chini ya Dola moja ya Marekani kwa siku.
"Gharama za umeme ziko juu mno, hatuwezi kuzimudu. Bora kiwepo chanzo kingine cha umeme pengine gharama hizi zitashuka," anasema Mathias Malimi, mfanyabiashara na mkazi wa Iringa.
Madaha Juma Madaha, Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, ana matumaini makubwa kwamba miradi hii ni dhahiri na kwamba Watanzania zaidi ya 8,000 watapata ajira.
"Chini ya Wachina tunaweza kuvuna chochote katika rasilimali zetu, lakini tunapenda wazawa ndio wanufaike kwanza," anasema Madaha.
Mbunge wa Ludewa, Deo Haule Filikunjombe (CCM), anasema makubaliano baina ya SHC na serikali yanaweza kuzaa matunda, lakini akaonya kwamba serikali inapaswa kuhakikisha kwamba wanufaika wa kwanza ni wakazi wa Ludewa.
"Tusingependa eneo hili likumbwe na maandamano kama yaliyotolea Mtwara," alisema Filikunjombe, akifananisha na kilichotokea mkoani Mtwara wakati wa mvutano wa bomba la gesi kwenda Dar es Salaam.
"Ukilinganisha na miradi mingine ya madini, walau hapa serikali imefanya jambo kubwa kwa kupata asilimia 20 kwenye ubia ambazo zinaweza kuongezeka kadiri uzalishaji unavyoongezeka," alisema, akiongeza kwamba Watanzania walishirikishwa katika kila hatua katika mchakato wa mkataba huo.
Imekubaliwa kwamba viwanda vya makaa na chuma vitajengwa Ludewa hivyo wakazi wa huko hawana haja ya kuwa na hofu.
Septemba 2012 wavuti ya All Africa iliripoti kwamba Stanbic Bank Tanzania ilikuwa imepata fursa ya kufadhili miradi hiyo kwa thamani ya Dola 2.914 bilioni ikishirikiana na benki ya ICBC ambapo benki hizo mbili tayari zilikuwa zimesaini makubaliano na TCIMR.

MATARAJIO YA MIRADI PACHA
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Zuberi Kabwe (Chadema) amekaririwa mara kadhaa akisema ubia katika miradi hiyo ni wa uwazi na kwamba uzalishaji wa 600MW unaweza kuikomboa Tanzania katika mgawo wa mara kwa mara wa umeme.
"Mara mtambo wa kufua umeme utakapoanza uzalishaji, kuna uhakika kwamba karibu 1500MW zitazalishwa kutoka Kusini mwa Tanzania kwani mgodi wa Mchuchuma ni miongoni mwa migodi mitatu mikubwa katika eneo hilo inayosimamiwa na NDC," anasema Zitto.
Meneja Uhusiano wa NDC, Abel Ngapemba, amekaririwa akisema kwamba serikali itavuna Shs. 51.8 bilioni kama mirabaha ka mwaka kwenye miradi hiyo.
Bei ya tani moja ya makaa, kwa mujibu wa Ngapemba, inatarajiwa kuwa Dola 86.201 na mapato yatakayotokana na mauzo ya umeme yanakadiriwa kuwa Dola 285.981 milioni kwa mwaka wakati Dola 971.28 zitazalishwa kwa mwaka kwa mauzo ya chuma, Dola 424.935 milioni katika mauzo ya titanium na Dola 114.125 kwa mauzo ya vanadium.
Wakati mataifamengi ya Magharibi yanaiona Afrika kama bara lililotandwa na umaskini, China inaliona bara hilo kuwa na fursa zisizokwisha za biashara. Haikushangaza wakati Machi 25, 2013 China na Tanzania ziliposaini jumla ya mikataba 17 jijini Dar es Salaam yenye thamani ya Dola 13.355 bilioni ambayo serikali ya Tanzania ilisema sehemu kubwa ya fedha hizo itagharamia maeneo ya kimkakati ya uchumi na itasaidia moja kwa moja kwenye bajeti walau kwa miaka miwili ya fedha.
Mikataba hiyo ni pamoja na ujenzi wa bandari mpya ya kisasa Bagamoyo ambayo imelenga kusaidia nchi za Maziwa Makuu ambayo ilipangwa kukamilika mwaka 2017. Bandari hiyo mpya ya Bagamoyo itakuwa na uwezo wa kupokea makontena 20 milioni kwa mwaka, kulinganisha na makontena 500,000 yanayopokelewa kwa mwaka kupitia bandari ya Dar es Salaam.
Wachunguzi wanasema China ndiyo itakayonufaika zaidi na bandari hiyo ambayo itasaidia kusafirisha madini kutoka nchi za bara kupitia Bahari ya Hindi. Inakadiriwa kwamba bandari hiyo mpya inaweza kuipiku hata ile ya Mombasa ambayo inapokea makontena 600,000 kwa mwaka, hivyo kuleta ushindani mkubwa.
Mwaka 2013 China ilitarajiwa kutoa Dola 500 milioni kwa ajili ya kuanza ujenzi huo, ambao ungehusisha ujenzi wa barabara ya urefu wa kilometa 34 kuunganisha Bagamoyo na Mlandizi na reli ya urefu wa kilometa 65 kuunganisha Bagamoyo na Tazara pamoja na Reli ya Kati. Miaka miwili iliyopita, China ilitoa mkopo kwa Tanzania wa Dola 1.3 bilioni kwa riba ya asilimia tatu ili kufanikisha ujenzi wa bomba la gesi lenye urefu wa kilometa 524 kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.
Mwezi Mei 2013, Tanzania ilisaini mkataba wa maridhiano na kampuni ya China Merchants Holdings kwa ajili ya ujenzi wa bandari mpya, eneo maalum la biashara na mtandao wa reli ambao utagharimu zaidi ya Dola 9.53 bilioni.
Mnamo Oktoba 2013 Tanzania ilisaini mikataba kadhaa yenye thamani ya Dola 1.639 bilioni na kampuni za Kichina kujenga mitambo ya umeme na majengo, mikataba ambayo inadhihirisha namna China inavyozidi kujisimika nchini Tanzania.
Sherehe za utiaji saini mikataba hiyo, ambazo zilishuhudiwa na Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda, zilifanyika jijini Guangzhou, China, na ilihusisha mkataba wa Dola 667.755 milioni kwa kampuni ya Tebian Electric Apparatus Stock kwa ajili ya ujenzi wa njia ya umeme wa 400 kV, na mkataba mwingine wa Dola 667.755 milioni na kampuni ya China Railway Jianchang Engineering Company na China Poly Group Corporation ili kujenga maghorofa ya makazi na biashara.
Ikiwa nchi ya pili kwa utajiri duniani, China imejenga imani kwa Tanzania na mataifa mengine ya Afrika kiasi kwamba yamepuuza madai yanayotolewa kwamba China ina kiu ya kuvuna malighafi kutoka Afrika.
"Wawekezaji wamejizatiti katika kuchochea maendeleo kwenye miundombinu ya usafirishaji na hii itasaidia kujenga njia mpya na kuimarisha ile ya sasa katika uzalishaji wa umeme," Dk. Chrisant Mzindakaya, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa NDC, alisema wakati wa kusaini mkataba wa uwekezaji kwenye miradi pacha mnamo 2011, akaongeza: "Mategemeo yangu ni kwamba, makubaliano yenu leo hii yatakuwa katika hali ya kila mmoja kunufaika (win-win situation) siyo tu kwa taasisi zetu mbili, bali kwa ustawi wa mataifa mawili rafiki."
Mwenyekiti wa SHC, Lin Conglong, alisema uamuzi wa kampuni yake kuwekeza Tanzania ulichangiwa, pamoja na mambo mengine, na uhusiano wa jadi baina ya Tanzania na China kupitia kwa Mwalimu Julius Nyerere na Mwenyekiti Mao Tse Tung.
Ushirikiano wa China na Tanzania ulianza miaka ya 1960 na umeendelea mpaka sasa na inaelezwa kwamba Tanzania ndiyo mpokeaji mkubwa wa misaada kutoka China kuliko nchi zote za Afrika.
Mpaka sasa, kuna ushirika wa China na Tanzania katika maeneo nane nchini Tanzania, miongoni mwayo ni kiwanda cha nguo cha Urafiki (ambacho hata hivyo kimesinzia kwa sasa).
Kwa mujibu wa takwimu kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania, hadi kufikia Agosti 2012, kulikuwa na kampuni 300 za Kichina zilizowekeza nchini Tanzania katika maeneo ya miundombinu, kilimo, viwanda na ujasiriamali mdogo na wa kati (SME) zote kwa pamoja zikiwa na mtaji wa zaidi ya Dola 971.28 milioni.
Hata hivyo, Rais Dk. Jakaya Kikwete alikaririwa akisema kwamba angependa kuona miradi yote ya viwanda, hususan Mchuchuma na Liganga, ikianza kazi kabla hajaondoka madarakani. Aliwahakikishia Watanzania kwamba miradi hiyo itaanza kabla ya mwaka 2015 na kwamba angetumia uwezo kama rais kuhakikisha hayo yanawezekana.
"Serikali imeazimia kuibadili NDC kama kichocheo cha mapinduzi ya viwanda nchini. Miradi ya viwanda kutegemea matumizi ya chuma cha Liganga na mkaa wa Mchuchuma, ambao umekuwa ukizungumzwa kwa miaka mingi, lazima ianze kabla sijang'atuka," alikaririwa akisema.
Rais Kiwete alirudia tena ahadi yake hiyo mwezi Oktoba 2013 wakati alipozuru Liganga, akisema miradi hiyo itaanza muda siyo mrefu.
Inaelezwa kwamba kuanza kwa miradi hiyo kutategemea kukamilika kwa kibali cha Tathmini ya Athari za Mazingira na Jamii (ESIA) baada ya kazi ya awali kufanywa na Mbunge wa zamani wa Ludewa, Profesa Raphael Mwalyosi. 


* Makala haya yalifadhiliwa na Jukwaa la Waandishi wa Habari za Uchunguzi Afrika (Forum for African Investigative Reporters – FAIR) na WITS China-Africa

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments