Tunawasalimu watanzania wote kwa salamu inayoashiria mabadiliko na uwazi.
ACT-Tanzania, tunapenda kuyatolea majibu maswali mbali mbali yaliyoulizwa na watanzania ambayo tulikuwa bado hatujayajibu, au ambayo majibu yake hayakueleweka sawa sawa.
Swali: Je! ACT-Tanzania ipo katika mitandao tu? Au mbona hatuioni sehemu nyingine zaidi ya mitandaoni!
Jibu: ACT-Tanzania haipo mitandaoni. ACT-Tanzania imo katika jamii, ndio maana ilifanikiwa kupata wanachama zaidi ya 2000, waliohakikiwa kutoka mikoa 10 nchini, na wanachama wengi tu kutoka mikoa mingine ambayo haikuhakikiwa na ukweli ni kwamba hadi sasa ACT-Tanzania ina wanachama zaidi ya 20,000 wenye kadi na wanachama zaidi ya 100, 000 ambao wanasubiri kadi.Hata hivyo ni kweli kwamba ACT-Tanzania bado haijafika maeneo mengi, hivyo ni jukumu letu sote kufanya kila tuwezalo kuhakikisha chama kinafika kila mahali na sote tuna wajibu katika hili.Kuhusu uwepo wa chama mitandaoni, tunapenda kuwafahamisha tu kwamba, mitandao ni miongoni mwa njia ambayo tunaitumia kufikisha habari zinazohusiana na chama kwa watanzania.Njia nyingine tunazotumia ni pamoja na barua pepe na simu.
Swali: Mbona hatuoni ofisi zenu mkoani/wilayani/mtaani kwetu?
Jibu: Ni kweli kwamba bado hatujaweza kufungua ofisi za chama katika maeneo mengi kwa sababu mbali mbali ikiwemo ukosefu wa rasilimali fedha (kwani chanzo cha mapato ya chama kwa sasa, ni michango ya wanachama wenyewe pekee).Hata hivyo tayari tuna ofisi maeneo mbali mbali.Ukitaka kufahamu kama kuna ofisi huko uliko, unaweza kuwasiliana na uongozi na utafahamishwa.Kuhusu maeneo ambayo hayana ofisi; ni jukumu letu sote kushirikiana na kuhakikisha ofisi zinakuwepo kwenye maeneo hayo, na kwa kuwa tuna wajibu katika jamii yetu, kwa nini tusisaidiane kuhakikisha kunakuwa na ofisi mtaani kwenu badala ya kulaumiana! Sote tutekeleze wajibu wetu ili tuweze kudai haki zetu.
Swali: ACT-Tanzania ninyi mnasema ni wawazi, mbona hamjatuletea ripoti ya kwamba mlitumia shilingi ngapi katika zoezi la uhakiki na hela hizo mlizipata wapi?
Jibu: Kwa kuwa swali hili limegusa moja kwa moja moja ya msingi muhimu wa chama cha ACT-Tanzania , tutalijibu peke yake.
Swali: ACT-Tanzania mtaanza lini kufanya mikutano ya hadhara baada ya kupata usajili wa kudumu kwani watanzania wanapenda kuwaona na kuwasikia!
Jibu: Mikutano ya hadhara ya chama chenu cha ACT-Tanzania, itaanza hivi karibuni na mtatangaziwa ratiba.Hata kama haitawezekana kufanya mikutano nchi nzima, angalau mikutano itafanyika katika baadhi ya mikoa kwa kuanzia.Mikutano itakapotangazwa, mnashauriwa kuhudhuria kwa wingi.
Swali: Mbona sisi tumekikubali chama na tunataka kadi na bendera lakini hatuzipati? Na kwa nini hatuoni bendera za chama zikipepea maeneo mbali mbali! Nini shida?
Jibu: Ukweli ni kwamba mahitaji yanakuwa makubwa kuliko uzalishaji na hii ni kwa sababu, wakati fulani, tunakumbwa na ukata wa fedha kwa kuwa mapato ya ACT-Tanzania yanategemea michango ya wanachama wa ACT-Tanzania wenyewe, na wana ACT-Tanzania ni watu wa kipato cha chini. Hata hivyo tunayofuraha kuwafahamisha kwamba tumeagiza kadi na bendera milioni kadhaa (hatuwezi kusema milioni ngapi maana tunaweza kuwastua sana watani wetu) lakini karibuni tutazipata na kila mtu atapata kadi bila shida yeyote.Tunawasihi muendelee kututumia mawasiliano yenu ili kurahishisha zoezi.
Swali: Hivi nyie ACT-Tanzania mna matatizo gani! Mnatuambia wawazi halafu hiyo katiba yenu mnaificha ficha ya nini?
Jibu: Chama kinatambua shauku waliyonayo watanzania ya kutaka kuiona, kuipitia na kuichambua rasimu ya katiba ya chama. Kwa kutambua hilo, chama kilikusudia kuitoa kwa umma mwanzoni mwa mwezi huu wa Juni 2014, hata kabla haijapitishwa na vikao vya ndani ili watu wote waweze kuijadili na ikibidi kushauri, lakini tumeshindwa kufanya hivyo kwa sababu kubwa mbili;-
1.Wanasheria wa chama wameshauri kwamba kusambaza rasimu ya katiba ya chama kwa umma, kabla ya kupitiswa na vikao vya ndani, kunaweza kuleta mgogoro wa kisheria.Kwa kuwa ACT-Tanzania inaheshimu ushauri wa wataalam, imeamua kusubiri kwanza hadi rasimu hiyo itakapopitishwa na vikao muhimu vya chama.
2.Gharama: kwa kuwa rasimu ya katiba ya chama si lazima ipitishwe na vikao vya chama kama ilivyo bila mabadiliko, na kwa kuwa kupiga chapa kunahitaji gharama kubwa, imeonekana itakuwa si sawa kupiga chapa za rasimu na kuisambaza halafu baada ya pengine mwezi mmoja, vikao vikaamua kuwe na mabadiliko kidogo na machapisho ya mwanzo yakawa hayana kazi tena.Hayo yatakuwa ni matumizi mabaya ya fedha zinazotokana na michango ya wananchi.Hata hivyo tovuti yetu ikiwa tayari hivi karibuni, tutaiweka rasimu ya katiba ya chama katika tovuti ya chama.
Mwisho , Chama kinawahamasisha watanzania wote wazidi kuuliza maswali ikiwa kuna jambo lolote linalohitaji ufafanuzi.Vile vile tunawasihi watanzania wazidi kukikosoa chama pale wanapoona chama kinaenda kusikostahili, kwani ACT-Tanzania inaamini kwamba kwa kukosolewa inaweza kuwa imara zaidi. Vile vile chama kinapenda kuwasihi kuwa; kwa yale mambo yanayohitaji utendaji, kila mtu atumie fursa alizo nazo kuhakikisha anakieneza chama kokote aliko, na kwa kufanya hivyo, atakuwa ametimiza wajibu wake.
ACT – TANZANIA………………………..Taifa kwanza leo na kesho
Mabadiliko na uwazi…………………….Chukua Hatua!
Nimeitoa wanabidii
Unapokea Email hizi kwa sababu umejiunga na Jukwaa la 'Mabadiliko'.
Kuchangia mada tuma kwenye Email hii: mabadilikotanzania@googlegroups.com
For more options, visit this group at:
http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania?hl=en?hl=en
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Mabadiliko Forum" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to mabadilikotanzania+unsubscribe@googlegroups.com.
To post to this group, send email to mabadilikotanzania@googlegroups.com.
Visit this group at http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania.
To view this discussion on the web visit https://groups.google.com/d/msgid/mabadilikotanzania/CACMr6QgPzVaU441MXFt59J%3DVBJ%3DBYOLy01pR0uEMg8v06nBwCw%40mail.gmail.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 Comments