HII NI SEHEMU MUHIMU SANA YA TAARIFA YA KAMATI YA TAMISEMI KUHUSIANA NA BAJETI YA OFISI YA WAZIRI MKUU, TAMISEMI:
3.11 Aidha, agizo kwa halmashauri zote kutenga asilimia isiyopungua sitini (60%) ya fedha itokanayo na makusanyo ya ndani (own source) kutekeleza miradi ya maendeleo halikutekelezwa kikamilifu na baadhi ya halmashauri. Kamati itazidi kuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa suala hili linakuwa sehemu ya mipango ya bajeti za halmashauri zote nchini na itakagua utekelezaji wa miradi hiyo.
Kamati yetu inaamini kwamba, lengo la Ugatuaji wa Madaraka kutoka Serikali Kuu kwenda Serikali za Mitaa, yaani 'Decentralisation by Devolution (D by D)',lilikuwa kupeleka si tu maamuzi na usimamizi karibu zaidi na wananchi, lakini pia kuzielekeza Halmashauri zetu kuanza harakati za kujitegemea katika utendaji wake kwa kukusanya mapato yao wao wenyewe. Na ilitegemewa kuwa Serikali Kuu atabaki kuwa mlezi wa kudumu wa Halmshauri hizi kwa kuzipa Sera na Miongozi mbali mbali ya kutekeleza majukumu yake, na pia kupeleka ruzuku ya misharahara na ya miradi ya maendeleo kwa kipindi fulani. Kila mtu, kati yetu wale tunaoamini na tunaopenda nyongeza ya mamlaka zaidi ya wananchi na ushirikishwaji wa karibu zaidi katika kujiletea maendeleo yao, tulidhani huu ni uelekeo sahihi, na tulijua ipo siku mchango wa Serikali Kuu utakuwa ni mdogo sana kwenye Serikali za Mitaa. Leo hii hali ni tofauti na haileti matumaini kabisa. Sura ya Mipango na Maumbile ya Bajeti za Halmashauri za Wilaya kwa kiasi kikubwa, katika kipindi cha miaka miwili hii ya kuanzishwa rasmi kwa Kamati Yetu na Utekelezaji wake wa majukumu, tumejifunza na kubaini uwepo wa wa hali ya juu wa "dhana ya utegemezi'' uliokithiri kwa Serikali Kuu, badala ya Serikali za Mitaa kuanza kujifikiria zaidi katika uelekeo sahihi wa "kujitegemea".
Mheshimiwa Spika, Utegemezi huu, kwa bahati mbaya sana, haujawahi na kamwe hautokuja kuzisaidia Halmashauri zetu kwenye eneo la miradi ya maendeleo; na sababu ziko wazi kabisa: kwamba, kama Taifa tuna utegemezi mkubwa sana kwenye mikopo ya kibiashara "concessional loans" kutoka kwa marafiki zetu ama michango ya wahisani kwenye bajeti, hivyo ikitokea kuwa wahisani hawajaleta fedha hizi ama wameleta nusu, kwa hakika, mpango wetu wa bajeti hautotekelezeka kama tulivyotaka. Lakini tunaamini kuna miradi midogo midogo ya wananchi, ambayo, kwa kiasi kikubwa haihitaji 'mapesa mengi' kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya ruzuku kwa Serikali za Mitaa. Miradi ya aina ya kumalizia majengo ya madarasa, majengo ya zahanati na vituo vya afya, nyumba za walimu, nyumba za wauguzi vijijini, mabarabara ya vijijini, kuchimba visima n.k., inaweza kabisa kutekelezwa kwa fedha zinazotokana na mapato ya ndani!
Mheshimiwa Spika, hili la kunyimwa mikopo ama wahisani na wabia wetu wa maendeleo kuacha, kupunguza kiwango ama kuchelewesha fedha kwa ajili ya kutusaidia kutekeleza mpango wetu wa bajeti, lina maana moja kubwa; kwamba,'tumepigiwa simu ya kutuamsha kutoka kwenye usingizi mzito (wake-up call!)' kuwa tuanze kufikiria ''kujitegemea'' kwenye bajeti yetu, na kwamba ni ngumu sana kutegemea kuleta maendeleo ndani ya nyumba yetu kwa kutegemea msaada wa rafiki ama jirani. Mheshimiwa Spika, miaka takriban 20 iliyopita, Prof. Abdulrahman M. Babu aliliona hili na aliandika kwenye kitabu chake kinachojulikana kama "An Economic Strategy for the Second Liberation of Africa " kilichopigwa chapa na Mkuki na Nyota Publishers Ltd, Mwaka 1994, kuwa, na ninaomba nimnukuu:
"The situation is so bad that no "reforms", whether inspired by the World Bank or IMF (International Monetary Fund), or initiated locally, can get us out of the mess. For what is needed is not reform but a different outlook which calls for a decisive change of direction, a change of the primitive colonial structure of the economy to a national economy; above all, a change in the structure of production. This entails a change from an outward-motivated to an inward-motivated development strategy, whose guiding principle must be based on the recognition that external causes are only a condition of change, whereas internal causes are the basis of change.''
Ambayo inatafsirikia, kwa tafsiri isiyo rasmi kama:
"Hali ni mbaya sana kiasi kwamba hakuna 'mabadiliko' yatakayofanyika, ama kwa kuhamasishwa na Benki ya Dunia au Shirikia la Fedhaa la Kimataifa, au mabadiliko yatakayoanzishwa kutokea ndani, yanayoweza kutunasua kutoka hapa tulipo. Kwa kuwa kinachohitajika siyo mabadiliko bali mtazamo mpya kabisa ambao utahitaji uamuzi mahsusi wa kubadili uelekeo, kubadili muundo wa uchumi wa kikoloni kwenda kwenye uchumi wa kitaifa; na juu ya yote, mabadiliko kwenye muundo wa uzalishaji. Hii inamaanisha mabadiliko kutoka kwenye mkakati wa maendeleo unaotokea nje kwenda kwenye ule unaotokea ndani yetu wenyewe, ambao msingi wake mkubwa unaoongoza ni lazima uwe umejikita kwenye kutambua kwamba sababu za nje ni masharti tu ya mabadiliko, wakati sababu za ndani ni msingi wa mabadiliko."
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ni kwa misingi hii, Kamati iliamua, kwenye vikao vya Bajeti mwaka jana, kupendekeza kuondoa utaratibu wa kufanya kazi kwa mazoea, yaani 'Business as usual' ili kuendana na dhana ya ugatuaji wa madaraka na kufanikisha uwepo wa Halmashauri na uendeshaji wake unaolenga kufuata misingi iliyozianzisha badala ya kuendesha Halmshauri kwa mtindo wa kizamani usioendana na matakwa ya mfumo huu mpya.
Katika vikao vya Bajeti ya mwaka 2013/14, Kamati iliazimia kuiagiza Wizara ya TAMISEMI kuziagiza Halmashauri zote nchini, kwanza, kuongeza ubunifu na jitihada kwenye ukusanyaji wa mapato mbalimbali ya Halmashauri, pili, kutenga asilimia 60 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo. Agizo hili lilionekana gumu na kwamba halitekelezeki, visingizio vilikuwa vingi, Kamati, hata hivyo haikutetereka, imeendelea kushikilia msimamo wake kwa faida ya nchi na wananchi wake. Kwa sababu tunaamini kabisa kuwa tukiboresha Serikali za Mitaa tutayagusa maisha ya watu wote. Maana hakuna aliye nje ya Serikali za Mitaa!
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 Comments