[wanabidii] SAFARI YA UKAWA KUELEKEA IKULU:NGUVU YAO NA CHANGAMOTO ZINAZOWAKABILI.

Thursday, May 08, 2014

 
Tarehe 28 mwezi wa Aprili,2014 nikiwa napitia taarifa mbalimbali za kisiasa nilikutana na kichwa cha habari kilichokuwa kinasema "UKAWA kusimamisha mgombea mmoja wa Uraisi".Kwangu mimi haikuwa taarifa ya kushtua sana bali ilinifanya nitafakari kuhusiana na uhalisia wa tamko hili walilolifanya.Swala lililonitafakarisha zaidi halikuwa tu hoja yenyewe iliyotolewa bali pia majira(season) ambapo taarifa hii imetolewa.Wanasaikolojia husema-"Usitoe ahadi nzito aidha wakati umefurahi sana au umekasirishwa sana".Sababu ya msingi ni kuwa mara nyingi katika mazingira hayo utatoa ahadi bila kuwa na muda mzuri wa kufanya uchambuzi wa ndani wa ahadi unayoitaka.Na 

nikajiuliza,wametoa ahadi hii baada ya kutafakari sana au ni kuwa wamekasirishwa sana au kufurahi sana
Lakini hadi hatua hii unaweza ukawa unajiuliza swali,kwa nini kichwa changu cha makala yangu kinaeleza hatima ya UKAWA na kuelekea IKULU na sio kuelekea KATIBA MPYA?.Ni muhimu kulieleza hili kwa sababu ni ukweli ulio wazi kabisa kuwa umoja huu wa katiba ya wananchi unaofupishwa kwa jina la UKAWA umeendelea kuonyesha ajenda zaidi ya Katiba katika muelekeo wake.Kama ambavyo Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa mheshimiwa Freeman Mbowe alivyoeleza katika mkutano huo na hapa nina nukuu-"Hivi sasa kwa swala la sisi kuungana kwa maana ya kuwa na nguvu ya pamoja halikwepeki.Siasa ni dynamics(zinabadilika).Fikra za jana ni tofauti na fikra a leo,kwa hiyo ni ukweli usiopingika kwamba tunahitajiana kwa manufaa ya watu wetu na nchi yetu" Tamko rasmi la UKAWA kuelezea lengo lao la kusimamisha mgombea mmoja katika uchaguzi mkuu nafasi ya urais na pia kuwa na mgombea mmoja katika nafsi za ubunge,ni ishara wazi kuwa lengo lao la kupata katiba linaweza kufunikwa na lengo la kushinda uchaguzi.Na hili si jambo la kushangaza hata kidogo kwani lengo la kwanza la chama chochote cha siasa ni kuchukua dola.Kama wakifanikiwa kuunganisha nguvu yao,bila shaka uhaguzi ujao utakuwa na ushindani mkubwa ambao haujawahi kutokea.

Wapo wanaowakosoa UKAWA na kusema kuwa maazimio kama haya yalishawahi kusemwa huko nyuma lakini hayakufanikiwa.Na wengine wanasema ni urafiki wa kinafiki hasa kati ya CUF na CHADEMA ambao walionekana kuwa maadui wa waziwazi ilipofika wakati CHADEMA walipoamua kutowahusisha CUF katika kambi yao rasmi ya upinzani bungeni.Wapo wanaosema pia kuwa UKAWA haina usajili kama chama cha siasa au kama wanataka kuwa na coalition(muungano) katiba yetu hairuhusu kufanya hivyo.Hizi ni changamoto za kweli lakini ni nyepesi sana kuzikabili na kuzitatua kwa watu weye malengo thabiti kisiasa.Katika changamoto ninazoziona mbele yao hizi si changamoto za muhimu kabisa.

Nikianza na hoja ya wale waanaosema kwamba walishawahi kufanya maazimio kama haya na uadui wa CUF na CHADEMA.Kwenye siasa husemwa hakuna adui wala rafiki wa kudumu ila kuna malengo ya kudumu.Ni kawaida sana maadui wa kisiasa wa jana ukawakuta ni marafiki wa kudumu sana wa leo.Nani alijua kama Steven Masato Wasira aliyegombea kwa chama cha upinzani na kumshinda waziri mkuu mstaafu Jaji warioba hata baada ya kufunguliwa kesi,leo hii yuko ikulu katika sehemu nyeti ya nchi;hiyo ndiyo siasa.Nchi jirani ya Kenya imethibitisha hilo baada ya mahasimu wakubwa wa siasa Rais Uhuru Kenyata na Makamu Wake William Ruto kuuunganisha nguvu kwa swala la kuchukua nchi.Huu unaweza usiwe mfano madhubuti(perfect example) hasa kwa kuzingatia Uhuru na Ruto walitumia nguvu ya makabila yao lakini kwa mafunzo ya jumla ni mfano muhimu wa kisiasa wa jinsi maadui wa jana wanavyweza kugeuka kuwa marafiki wa karibu wa kesho. Kwa ufupi ni kwamba kwenye siasa tofauti za jana zinaweza zisiwe na nguvu sana katika maamuzi ya leo ya wanasiasa na hii ndio maana CHADEMA wametangaza kuwajumlisha CUF na NCCR katika kambi ya upinzani katika majira haya ya kujijenga kisiasa.
Swala la kuwa UKAWA haina usajili wa kudumu nayo ni hoja isiyoweza kuwa kizuizi cha kudumu kama kweli wana dhamira ya dhati.Inawezekana sheria isiweze kuruhusu kwa sasa vyama hivi kuwa na muungano(coalition) lakini sidhani kama ni jambo lisilowezekana hasa kwa kuzingatia kuwa tuko katika wakati strategic wa wao kuweza kulifanikisha hilo wakati joto la mabadiliko ya katiba liaendelea.
Kuna mambo mawili ambayo UKAWA wameamua kuyafanyia timing ya kisiasa.Moja ni Fursa ya kisiasa-wameamua kutumia mjadala wa katiba kujiimarisha kisiasa kwa kutafuta hoja wanayoamini itakubaliwa zaidi na wananchi na itakuwa chanzo cha wao kuungwa mkono katika harakati za uchaguzi mkuu ujao.Mjadala huu unawapa uhalali wa kufanya mikutano na kuelezea malengo na sera yao kwa wananchi,kwa maneno mengine wanapata nafasi ya kueleza ilani zao ingawa bado si rasmi.Ingawa bado wanakabiliwa na changamoto katika hoja yao ya katiba hasa katika mfumo wa serikali kama nitakavyoeleza hapo chini,bado kisiasa ni wakati muafaka kwao kutumia vuguvugu hili wakati wananchi wanatamani sana kusikia kinachoendelea.Pili wameamua kuwaonyesha wananchi kuwa lengo lao kuu ni kuitakiwa mema nchi bila kujali tofauti zao,hii ndio maana wameamua kuungana pamoja.Hatua hizi zote zinalenga kuongeza imani yao kwa wananchi kuelekea uchaguzi mkuu.Na ni ukweli usiopingika kuwa lipo kundi kubwa la wananchi watakaokaa upande wao kwa kujiuliza-kama wameamua kuweka tofauti zao zote hizi kisiasa lazima watakuwa na nia njema na nchi yetu.Au haiwezekani vyama vyote hivi viwe na lengo baya lazima CCM ndiyo itakuwa ina nia mbaya katika hili.Haya ni mawazo yenye maana sana katika hatima ya chama au wanasiasa wowote wale katika kuelekea kushinda uchaguzi.

Pamoja na fursa za UKAWA bado naziona changamoto nyingi ambazo si rahisi sana(sijasema haiwezekani) kuzishinda kwa muda mfupi hasa kwa kuzingatia malengo yao ya kushinda uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Changamoto ya kwanza ni nani atasimama kama mgombea Urais kati yao?Hili si gumu sana kwa baadhi ya vyama lakini ni swala la muhimu kati ya CHADEMA na CUF.Kwa NCCR-Mageuzi wanaweza wakawa tayari kukubali mgombea mmoja kirahisi hasa kwa kuzingatia ukweli kwamba katika chaguzi zilizopita ukiacha ule wa mwaka 1995,nguvu ya NCCR imeendelea kupungua kitaifa na hata katika ubunge wakibakiza nguvu yao Kigoma tu na hasa inayotokana na umahiri wa wagombea na sio uthabiti wa chama chenyewe.Pengine wangesimamisha mgombea aliyesimama katika chaguzi uliopita Mh.Hashimu Rungwe,lakini kura alizopata wakati ule zilikuwa ni 26,388 sawa na asilimia 0.31 ,hii ni idadi ndogo sana kuonyesha ushawishi wake.Hata hivyo Hashimu Rungwe akiwa na Hassan Mmbwana aliyekuwa Kamishina wa NCCR Mageuzi wa Mkoa wa Tanga walitangaza kuhamia Chama cha Ukombozi wa Umma(CHAUMA) wakitupia lawama ya kukosekana kwa demokrasiaa ndani ya NCCR-Mageuzi.Pengine aliyebakia angekuwa ni Mwenyekiti wa chama Taifa,James Mbatia,lakini swali kubwa linabaki kama alishindwa kupata ushindi katika uchaguzi wa ubunge jimbo la KAWE ,je ataweza kuleta ushawishi ngazi ya taifa?hesabu za kisiasa zinakataa.Hizi ni sababu tosha kwa NCCR kuwa tayari kutosimamisha mgombea katika uchaguzi mjao katika umoja wao na badala yake kuwaachia CHADEMA na CUF waamue hili.Lakini kwa kufanya hivyo ni ukweli usiopingika kuwa NCCR watabaki kuwa ni wadau wasio na nguvu katika umoja huu.
Kwa aliyekuwa mgombea wa CHADEMA Dr.Wilbroad Slaa alipata 2,271,941 ambazo ni sawa na silimia 26.34 huu kwakwe ni mtaji mkubwa hasa ukizingatia mambo mawili.Kwanza tofauti yake na mshindi wa kwanza Rais Kikwete aliyepata kura 5,276,827(61.7%) ikiwa ni tofauti ya kura 3,004,886.Nadhani mkakati wa chadema ulikuwa ni kuongeza idadi ya kura ili kushinda uchaguzi ujao au kuendelea kujijengea nguvu yao ya kisiasa,na hii ndio sababu inayoifanya chadema kushiriki kila uchaguzi hata ule ambao kwa uwazi inaonekana hawatashinda,nia wakati mwingine si ushindi bali ni kujitambulisha zaidi na kuvutia wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi ujao.Kwa upande mwingine tofauti yake na aliyekuwa mshindi wa tatu Prof:Ibrahim Lipumba aliyepata kura 695,667 sawa na asilimia 8.06 ni kubwa sana(significant),tofauti ya kura 1,576,274 hivyo kwa mahesabu inaonekana itakuwa ni vyema kwa Dr.Slaa kusimama kama mgombea wa umoja huo.Lakini je,urahisi wa namba hizi ndio utakuwa urahisi kwa Prof:Lipumba kukubali kutogombea?

Naamini haitakuwa rahisi kwa CUF kukubali kumwachia Dr.Slaa kuwa mgombea hata pamoja na ushawishi wa takwimu hizo.Ukweli ni kuwa CUF kwa bara wana nguvu katika maeneo ya pwani zaidi na maeneo machache yasiyo ya pwani.Lakini kwa sasa CUF ni sehemu ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,hii ni kusema wako kwenye nafasi nzuri kuendeleza nguvu yao katika visiwa hivyo na hata kuwa na matumaini kuchukua nafasi ya Urais katika siku zijazo.Mkutano wa UKAWA uliofanyika hivi majuzi Zanzibar,ni wazi kuwa ulikuwa ni kwa manufaa ya CUF kwa kuzingatia wafuasi finyu wa vyama vingine katika UKAWA.Hata kama tumaini la kushinda uchaguzi wa urasi wa muungano si kubwa sana kwao,bali ili kuendelea kubaki kuwa chama cha nchi nzima na kushikilia ngome zao bado kuna umuhimu mkubwa wa CUF kuendelea kupata kura kwa kumtumia Prof;Lipumba katika kugombea nafasi ya Urais.Tofauti ya CUF ni kuwa ingawa wananguvu kubwa Zanzibar kuliko bara lakini wana viti vya UBUNGE pande zote mbili na  Prof:Lipumba huwa anapata kura kutoka pande zote mbili.Lakini kwa CHADEMA ni tofauti hawana hata mbunge mmoja upande wa Zanzibar.Kwa mantiki nyingine katika nafasi ya Urais wa muungano,CUF inaonekana ni chama cha jumla zaidi kuliko wenzao wa CHADEMA.
 Katika mchakato huu wa katiba mpya,maslahi yanayofanana(common interest) kwa vyama hivi ni kushika dola,lakini maeneo yanayolengwa ni tofauti.Kwa CHADEMA Tanzania bara ni muhimu sana kwa hatima yao ya kisiasa kwani kwa upande wa Zanzibar ni kama imeshindikana kujipenyeza kabisa.Kwa CUF upande wa Zanzibar ni muhimu zaidi kuliko upande wa Tanzania Bara kwani nguvu yao ni dhahiri na imethibibitishwa na ushiriki wao katika serikali ya umoja wa kitaifa(SUK).Kwa mantiki nyingine pamoja na kutaka kuunga mkono matakwa ya wananchi lakini kwa jicho la kisiasa ni kusema kuwa kama serikali ya Tanganyika itapatikana itakuwa ni muhimu kwa ushindi wa CHADEMA kwani kura wanazopata wagombea wa Urais wa CCM zinazopigwa na wazanzibari ni kikwazo sana kwao na kwa upande wa CUF Zanzibar ni muhimu sana kwao kwani bila nguvu ya CCM ya bara Zanzibar ni ngome ya asili ya CUF.Kwa maneno mengine uimara na uhai wa CCM Zanzibar unategemea sana msaada wa karibu kutoka Bara.

Katika kutimiza haja yao ya kuunga mkono rasimu hasa umuhimu wa serikali mbili,UKAWA hawana budi kujikita katika kuulewesha umma hasa kujibu hoja ngumu kwa upande wao ni namna gani gharama za uendeshaji hazitaongezeka kwa kuwa na serikali tatu.Hoja ya gharama ndio hasa ambayo haijaeleweka kwa wananchi,wakifanikiwa kuieleza hii na ikakubaliwa kuungwa mkono katika hoja ya serikali tatu itakuwa ni rahisi sana.Ndani ya vyama vya upinzani nimewahi kusikia maoni yanayotofautiana pia;kuna wale wanaoamini katika marais watatu na kuna wale wanaosema tuwe na rais mmoja ila mawaziri wakuu 2 kila upande wa muungano,hili nalo lazima wakubaliane katika kufanikisha kuungwa mkono na jamii.Nimesikia wakisema kuwa hakuna utafiti wa kisayansi uliofanywa ili kuthibitisha gharama itaongezeka.Lakini ukweli ni kuwa hakuna utafiti uliofanywa wa kuonyesha gharama itapungua ndani ya serikali tatu,kwa nini hawataki wananchi waamini kuongeza idadi ya serikali ni kuongeza gharama?Ili kujenga ushawishi wao katika hili,watafute kampuni inayoaminika ifanye utafiti wa kitaalamu ili watumie taarifa hiyo kuwa kama authority yao katika kuthibitisha kuwa gharama hazitaongezeka.
Kwa upande wa chama tawala naona kuna makosa makubwa yanayofanyika katika kutetea hoja yao.Nguvu kubwa imewekwa katika kushambulia wapinzani na kueleza ubaya wa serikali tatu,ikiwemo mbinu ya kuwawekea hofu wananchi wa vita na kuvunjika kwa muungano.Hoja hizi hazitaleta matunda wanayoyataka,kwa historia zilitumika pia katika kupinga mfumo wa vyama vingi lakini umaarufu wa Mrema ulithibitisha kuwa hoja za kutia hofu haziwezi kushawishi watu wakuunge mkono badala yake watataka kujua zaidi kuhusu unayetaka wamuogope na matokeo yake wanaenda kuwa wafuasi wake.Badala yake,CCM inatakiwa ijikite katika kueleza umuhimu wa serikali mbili na kujibu kwa ufasaha swali gumu kwa upande wao-kama kero zimeshindwa kuisha kwa miaka yote ya muungano  itawezekanaje kuaminini mfumo huu?Pia maoni ya rasimu ni maoni ya wananchi kwa nini wao wanayapinga?Kundi la wanaotaka serikali 2 hizi ndizo hoja za msingi za kujibu na kushawishi umma.

Katika uchaguzi mkuu uliopita idadi ya wapigakura waliojiandikisha ni 20,137,303, waliopiga kura ni 8,626,283 sawa na asilimia 42.84 ya wapiga kura wote waliojiandikisha,hii ni changamoto inayoikabili UKAWA kuwabadilisha WASHABIKI kuwa WAPIGAKURA.Wanaweza wakazunguka nchi nzima lakini kama idadi kubwa ya wafuasi wao si wapiga kura waaminifu hasa maeneo ya mijini,matokeo yatawashangaza itakapofika wakati wa kupigia kura rasimu ya katiba.

Katika kukuza demokrasia haya ni mambo yanayoweza kutarajiwa kila wakati,ila si rahisi kama inavyoweza kuonekana kwa nje.Ni kweli UKAWA wanataka kuingia IKULU,ni muhimu wakazizingatia changamoto hizi zinazowakabili.
MUNGU IBARIKI TANZANIA.
Joel Arthur Nanauka
0688-67 79 68

Share this :

Related Posts

0 Comments