[wanabidii]

Friday, April 18, 2014
UONGO, UNAFIKI, UKASUKU, NA UZANDIKI WA CCM!
 
Inasikitisha kuona kwamba CCM wamekuwa mstari wa mbele kuwadanganya wananchi kwamba uendeshaji wa serikali 3 ni ghali kuliko serikali 2 huku wakiwa hawatoi takwimu za kuonesha ughali huo unakujaje. Swali la kujiuliza ni kwamba ikiwa serikali 3 ni ghali na kama kweli CCM wana nia njema ya kupunguza matumizi ya serikali ni kwa nini basi tusiende kwenye serikali 1? Hapo ndipo unapogundua kwamba Dr Antipas Lissu alipowaambia CCM kwamba wamezoea kuishi kwa uongo hakuwa amekosea hata kidogo. Ndivyo CCM walivyozoea kuishi.
 
Hii hesbau ni rahisi sana. Leo nilikuwa namuuliza mtoto wangu anayesoma chekechea kama 1 na 2 ni ipi kubwa, akaniambia kwamba ni 2! Sasa swali rahisi kama hili kwanini CCM wanashindwa kulitatua wakati mtoto wa chekechea anaweza? Ndani ya CCM kuna maprofesa lukuki lakini wote wameacha taaluma zao na kuchagua kutumikia uongo. Ndugu zangu, wote ni mashahidi na mnafahamu kwamba 1 ni ndogo kuliko 2 ila CCM wameng'ang'ania serikali 2 ambazo ni ghali kuliko serikali 1 kwa sababu zina manufaa kwao kisiasa. Ndio maana wanajenga hoja mufilisi kwamba serikali 3 ni ghali kuliko 2 huku wakisahau kwamba 1 ni nafuu zaidi kuliko 2! Pia serikali 1 zitaimarisha muungano na umoja zaidi kuliko hizi serikali 2 za kulazimishana. Hili hawalioni ila wamebaki kukomaa na serikali 3!
 
Halafu, ni lini CCM walikuwa na huruma kwa wananchi? Sote tunajua na tunafahamu jinsi pesa za umma zinavyofisidiwa watu wa CCM na kutumiwa na serikali kununua na kuendesha magari ya kifahari huku wananchi wakila majani pamoja na kukosa huduma za kijamii kama matibabu, maji, elimu, miundombinu, nk. Hiyo huruma ya CCM imetoka wapi ghafla hadi wafikirie kupunguza idadi ya serikali kwa manufaa ya wananchi? Hiki ni kichekesho cha mwaka.
 
Uongo mwingine wa CCM ni dhana potofu kwamba serikali 3 zitavunja muungano. Hii ni hoja ya kitoto na kizezeta kabisa. Kinachosikitisha na kushangaza zaidi ni pale CCM wanapolazimisha na kuwatia hofu wananchi kwa kuwaaminisha kwamba uwepo wa serikali 3 (serikali ya Tanganyika, Zanzibar na MUUNGANO wa Shirikisho) eti ni kuvunja muungano. Muungano utavunjikaje wakati katika hizo serikali 3 imo serikali ya Muungano (Shirikisho)? Hivi hawa INTARAHAMWE hawana haya? Mtaji wa hawa watu ni ujinga watanzania walio wengi. Kuna wajinga wachache ambao wanakubali uongo huu lakini wengi wetu tunaupuuzilia mbali.
 
Hivi jamani mtu ukiwa na nyumba yako ambayo haikidhi mahitaji, ukiamua kuifanyia renovation au ukaibomoa na kujenga nyumba mpya iliyo kubwa, imara na bora zaidi, tatizo liko wapi? Ni nini hofu ya CCM katika uwepo wa serikali 3 hadi waanze kuwatisha raia kwamba ikiwa serikali 3 zitaruhusiwa jeshi litachukua nchi? Kama ndivyo basi, sisi raia tunaoteseka chini ya utawala wa CCM tunalikaribisha jeshi kwa mikono miwili lije litawale badala ya kuendelea kuishi ndani ya utumwa wa serikali ya CCM.
 
CCM hawahawa waliwaaminisha watu kwamba vyama vingi vikiruhusiwa, nchi itaingia vitani kama ilivyowahi kutokea huko Rwanda. Walifikia hatua ya kutembea nchi nzima wakionyesha video za vita ya Rwanda na intarahamwe ili kuwatisha wananchi kuhusu ujio wa vyama vingi. Ni zaidi ya miaka 20 sasa tangu vyama vingi viruhusiwe nchini lakini hatujawahi kuona nchi ikiingia vitani. Ama kweli CCM wamezoea kuishi kwa UONGO, ukweli hawauwezi! Propaganda zao hizi tumezizoea, hawakuanza leo, jana wala juzi.  Ni uongo wao wa siku nyingi sana.

Share this :

Related Posts

0 Comments