Tafakuri na Shaaban Y.
Kuongoza na kutawala, ni jukumu la serikali. Kutawala ni kama kulinda, kutotawanya, kukusanya na kutoruhusu kutawanyika.
Kulinda binadamu dhidi ya uharibifu na uovu ni jukumu la serikali. Kulinda na kuhifadhi ubinadamu ni jukumu la serikali. Kuongoza ni kuonyesha njia ni wapi taifa linapaswa kuelekea kwahiyo kiongozi ni lazima aweze kutawala na kuongoza kwa pamoja. Serikali haiwezi kukamilika pasipo kuwa na vitu hivyo vyote viwili. Kimoja ikiwa ni dira na kingine kukusanya na kulinda. Ili serikali ifanye kazi vizuri ni lazima iwe na uwezo huo. Lazima ikusanye, ilinde na iongoze.
Mfano mzuri wa kutawala na kuongoza ni mfano wa kondoo na mchungaji. Mchungaji ni lazima akusanye
kondoo katika kundi moja ili awaongoze kwenda malishoni. Na kila aliyetoka nje ya mstari ni lazima amrudishe katika mstari ili kondoo wote wafike na wawe na mwelekeo mmoja. Mchungaji ni lazima ajue anapowapeleka kondoo.Na ili nchi iende sawa kiongozi ni lazima awe na uwezo wa kutawala na kuongoza kwa pamoja. Taifa lolote ni lazima liwe na mwelekeo kukosa mwelekeo ni kukosa uongozi.
Kutawala peke yake hakusaidii pasipokuwepo na dira. Na ili dira iwepo ni lazima watu wakusanywe pamoja katika lengo moja ambalo litakuwa ni ujenzi wa jamii bora zaidi kwa faida ya wote. Akili za wananchi ni lazima zielekezwe katika mwelekeo fulani, akili zilizotawanyika hazitaweza kujenga taifa. Kwa hiyo kiongozi ni lazima awe na maono, na kujua ni wapi anataka kupeleka watu wake na taifa. Ni lazima ajue kuratibu watu wake katika serikali kulingana na maono aliyonayo ili maono ya serikali yawe pia ni ya wananchi. Kwa njia hii pekee taifa huweza kuwa na dira.
Lakini hii inahitaji uongozi wenye roho moja, akili na jitihada za pamoja katika kufanya kazi ili kufanikisha maono na sera ambazo wote ni lazima waziamini. Ni lazima kiongozi awe na timu inayofanya kazi vizuri na kwa pamoja.
Ni muhimu kuwa na viongozi hodari na wanaoamini katika maono na itikadi ambayo kiongozi wao anayo na kusambaza maono hayo kwa wananchi ambao nao kwa upande wao ni muhimu kuyapokea kama ni mazuri kwa mustakabali wa taifa.
Hapa unakuja umuhimu wa chama katika kusaidia itikadi na maono haya kwakuwa serikali peke yake bila kuwa na chama kinachoamini maono hayo serikali haitoweza kufanya kazi vizuri na nchi kwenda mbele. Chama ni muhimu sana katika kutumika kusambaza maono haya ambayo ni muhimu kuwafikia wananchi.Ninapo zungumzia itikadi ni ile nguvu ambayo itatumika kusambaza maono. Kwakuwa naamini maono na itikadi ni vitu viwili tofauti. Maono ni taswira ya kitu ambacho bado hakionekani kiko katika fikra, kitu kinachohitaji kutekelezwa ili kuwa kitu dhahiri. Lakini maono haya yanahitaji nguvu ya utekelezaji wake ni lazima watu wayaamini na wafanye jitihada ya kuyakamilisha ili kujenga kile kitu wanachohitaji na hapo ndipo itikadi inapounganishwa na maono.
Itikadi mara nyingi haitumii akili ni kuamini tu katika kitu, lakini maono hutokana na fikra za kina, lakini hizi fikra zinahitaji msukumo hivyo ni lazima tuunganishe maono hayo na itikadi. Ni lazima vitu hivi viwe na uwiano.
Baada ya kutafakari kwa muda mrefu na kupata uhakika wa jambo na pale fikra zinapojengeka hapo ndipo itikadi inapojengeka, itikadi inapojengeka katika maono hutengeneza dira. Kwahiyo ufanyaji kazi wa kitu chote kinachoitwa taifa ni lazima uendane na maono. Kwahiyo itikadi ni imani katika jambo fulani.
Kuna tofauti kubwa sana kati ya mipango na maono. Ni lazima kwanza uwe na maono alafu ndio uweke mipango na mikakati ya kufikia huko. Kuwa na mipango bila maono ni kukosa mwelekeo. Ni lazima tujue tunafanya nini na kwasababu gani na kama kila tunachofanya kitatufanya kuyafikia maono yetu.
Mfano wa maono na mipango ni kama nyumba na matofali. Maono ni nyumba lakini mipango ni matofali. Kimoja kinakupelekea kufanikishakuwa na kingine. Kwanini tunashindwa kama taifa? Ni kwasababu tunakosa maono ya pamoja na hivyo tunakosa dira. Tuna mipango mingi tu bila maono.
Maono ni picha kubwa lakini mipango ni vitu vidogo vinavyokamilisha picha kubwa. Ili kujenga nyumba kubwa ni lazima uwe na matofali, mbao, mabati, misumari nk…..Hivi vyote navifananisha na mipango. Nyumba nina- ifananisha na maono. Kwahiyo ili kufanikiwa kuwa na nyumba ni lazima tuwe na vyote hivyo. Sisi tunafikiria misumari, mabati, mbao na matofali badala ya kufikiria nyumba.
Kwa mfano ni lazima tujue tunataka kujenga taifa la namna gani, ni lazima tuwe na taswira ya namna ya taifa hilo litakavyokuwa ili tuunganishe nguvu zetu kulijenga. Ni lazima elimu yetu ielekezwe kujenga taifa la namna hiyo. Bila kuwa na mwelekeo huu hatutajenga chochote. Kuna aina mbili za mataifa maskini; Kuna taifa ambalo ni maskini lisilo kuwa na matumaini na kuna taifa ambalo ni maskini lakini lenye jitihada.
Taifa lolote maskini na lenye jitihada ni lazima liongozwe na maono na matumaini ya kufanikisha hayo maono. Kwakuwa wanaamini umaskini sio kitu cha kudumu ni cha kupita. Wanajua utajiri ni zao la akili, busara, jitihada na maarifa. Kuwa maskini na kukosa matumaini hupelekea kuwa na ufukara. Kwahiyo taifa fukara ni lile maskini na watu wake wamekosa matumaini na baadae yao. Hili kamwe halitoendelea. Mataifa mengi ya afrika yapo hapa.Kwetu sisi kama watanzania kuna matumaini kama tutabadili mwelekeo wa fikra zetu wa sasa.
Serikali na jamii, inaunganishwa na kitu kimoja tu haki. Pale serikali inapokiuka misingi yeyote ya haki inaharibu misingi ya uwepo wake. Watu katika taifa hugawanyika na malengo ya pamoja hupotea.Serikali kama dereva na wananchi kama gari, Ubora wa taifa lolote utategemea sana ubora wa viongozi walionao.
Maisha ya nchi ni kama safari ndefu, wote tukiwa tumepanda kwenye basi kubwa na lengo letu likiwa kufika sehemu moja.Ni lazima tutafute dereva makini na bora ili tufike salama na sio dereva yeyote Yule. Tunajua magari hupinduka na gari linapopinguka safari ya watu huishia njiani. Embu tuangalie kwa makini tabia za wasafiri tujifunze kutoka kwao, jinsi wanavyoshirikiana wakiwa safarini, hii ni kwa sababu tu wao ni safari moja.Sisi ni kaka na dada tunaojenga taifa moja. Katika taifa letu kuna nembo ya mwanamke na mwanamme kama nembo ya taifa.
Sisi wote ni lazima tuungane kujenga taifa moja tukijua ni kwakuwa wamoja tu bila kujali uanamke wetu na uanamume wetu ndipo taifa hili litakapo songa mbele ikiwa kila mmoja wetu atashiriki katika ujenzi wa taifa hili kwa moyo wake wote. Iwe katika malezi ya watoto wetu na ujenzi wa uchumi wetu. Au iwe katika kujenga maadili ya taifa.
Nembo yetu ya taifa inasisitiza juu ya uhuru na umoja. Lengo lilikuwa ni kufanya jitihada za kuleta watu wetu pamoja baada ya kupata uhuru wetu. Kwakuwa kama tungepata uhuru bila kufanya jitihada za kufanya watu wetu kuwa wamoja ingekuwa haina maana. Umoja wetu ndio utakaopelekea mwelekeo wetu kama taifa. Ni katika umoja huu ndipo tutaka- poweza kulinda uhuru wetu. Ni umoja huu ndio uliotufanya kupata uhuru wetu kutoka kwa Waingereza.
Lakini taifa letu ni lazima lisiwe taifa la kiimla; watu wetu ni lazima wawe na uhuru wao, wasikandamizwe na serikali kwa namna yeyote ile na ni lazima tuunganishwe kama taifa na haki, wajibu, umoja na uhuru wa mtu. Lakini pia ni lazima tulinde uhuru wa taifa.
Sisi ni wasafiri tunaoongozwa na picha kubwa. Picha kubwa ya aina ya taifa tunalotaka kulijenga, aina za jamii tunazotaka kuzijenga na aina ya familia tunazotaka kuzijenga. Vyote hivi havitawezekana kama hatutakuwa wamoja na tunaoongozwa na picha kubwa.
Kila taifa lazima lijue mwisho wake ni upi. Kila taifa ni lazima liwe na mwelekeo. Hakuna ghorofa litakalo jengwa na kutokuwa na mwisho. Mchora ramani huchora na kujua mwisho wake. Hata pale tunapoangalia asili, mti huchipua hukua na mwisho wake hufa. Vilevile kwa maisha yamekuwa hivi kwa binadamu.
Tofauti na kwa wenzetu sisi bado tuna cha kujenga. Hatujafika kileleni bado. Lazima tuwe na tumaini hili. Mataifa hujengwa kwa juhudi, maarifa, hekima na busara.
Msingi wa majadiliano katika sehemu hii ni serikali, Kama dereva wa jamii na taifa. Kama ilivyo kwa dereva yeyote yule, lazima awe na mwelekeo isipokuwa kama amelewa, gari itayumba na kukosa dira. Na lengo letu sisi ni kufika salama.
Jamii bora na taifa bora hujengwa na serikali makini ambayo akili zao zote ziko katika ujenzi wa Taifa na jamii. Ni kujitolea huku kwa upande wa serikali ndiko kutakakofanya taifa liendelee. Na hili linahitaji nidhamu ya hali ya juu. Na dhamira ya dhati ya kutaka kuona mabadiliko.
Serikali na jamii ni vitu viwili tofauti na wala sio kitu kimoja. Vina asili tofauti. Utapoangalia kwa ukaribu utagundua hili, Kwa serikali ni lazima wawe na uwezo mkubwa wa kiakili na nguvu kuliko jamii ili wawe na uwezo wa kutawala. Vingenevyo jamii haitoweza kulindwa kwasababu asili ya binadamu ni uovu na serikali iko kulinda haki ya kila mmoja. Hakuna serikali yeyote iliyosimama kwa muda mrefu kwa kutenda uovu kwasababu asili yeyote ya serikali ni kulinda haki.
Kwahiyo serikali ni kiini cha Taifa lolote.Serikali imara hutengeneza Taifa imara na kinyume chake. Jamii na serikali sio kitu kimoja kamwe haiwezi kuwa kitu kimoja. Ingawaje serikali ni sehemu ya jamii.Kama kulivyo na bwana mwema na bwana mwovu vile vile kuna serikali ovu na serikali njema.
Ubwana uliopo katika serikali sio ubwana wa kujikusanyia bali ule wa kufanya kazi kwa faida ya umma, wa kuhakikisha jamii inazalisha na kuwa endelevu na wa kuhakikisha haki inatendeka, inalindwa na inaendelezwa. Kuhakikisha pia umoja wa nchi unaendelea kuwepo kama nyenzo ya kuharakisha maendeleo.
Ninapozungumzia umoja sio huu wa kutokuwepo mifarakano miongoni mwa sehemu za jamii zinazounda Taifa. Bali umoja wa kiakili na kimalengo, umoja wenye nia moja. Umoja ulio huru dhidi ya ubinafsi. Umoja unaoleta hisia za utaifa. Unaoleta hisia za mimi ni wa taifa fulani.
Hisia hii ni muhimu kwa ujenzi wa taifa lolote. Pale hisia hii inapoondoka na jamii inaposhindwa kutambua wana wajibu kama walivyokuwa na haki kwa taifa, ile asili ya utaifa huondoka na kuwa kundi la watu wanaoishi pamoja na sio taifa, kila mtu akiongozwa na ubinafsi wake na dhamira yake binafsi na ile hisia ya utaifa huondoka na dhamira ya taifa katika mioyo ya raia huondoka.
Tukizungumzia ya kwamba kwa kutokuwepo kwa vita ndani ya taifa kwamba ni wamoja tutakuwa tunakosea. Umoja wa taifa lolote utaupima katika ushirikiano wa watu wake, na utayari wa watu wake kulitumikia taifa kwa faida ya wote. Watu wanaweza kutofautiana katika taifa lakini ni katika kuboresha taifa na sio katika misingi ya ubinafsi. Msingi wa umoja utauona katika kujitolea kwa watu kwa faida ya umma. Kwahiyo serikali inahusika moja kwa moja katika ujenzi wa umoja wa taifa na kulinda umoja huo. Umoja huu ambao msingi wake ni malengo ya pamoja. Ni lazima umoja huu uangaliwe kwa jicho moja. Ni lazima liwe jipya kila muda unavyokwenda likienda likibadilika kutoka katika picha kubwa ya Taifa na kutokana na hali inavyoenda kwa wakati huo. Picha kubwa ni taswira ambayo taifa limeweka kuifikia. Taswira ambayo ni lazima juhudi zifanyike ili iwe kitu halisi kinachoonekana.
Hatua ya kwanza kwa Taifa lolote kuendelea ni kujitambua kwake. Taifa halitoweza kujitambua pasipo serikali kujitambua na wananchi kujitambua. Na kujua uhusiano wao, uhusiano wa Taifa, wananchi na serikali. Pasipo kujitambua huku, hatutaweza kuendelea na kujitambua huku kutakuja tu kama tukiwa wenye malengo mamoja.
Hisia hii ya mimi ni mtu wa taifa fulani na kujua wajibu na haki zako. Hisia hii ya kumuona mtu mwingine kama sehemu yako, ambaye mna sehemu katika taifa, mna haki na wajibu ndio msingi wa uraia. Kujitambua huku ndiko kutakako tufanya kuwa taifa lililo kamilika, kumuona raia mwenzako kama ndugu yako.
Utaifa hufanyika kwa miaka mingi na msingi wa utaifa hujengwa katika mioyo na akili za watu na ubomolewa pia katika mioyo na akili za watu. Turudi katika fikra nyepesi katika familia. Hisia hii ya kuwa mtu wa familia fulani kila mtu anaijua. Familia ambayo inaundwa na baba, mama na watoto. Familia kama sehemu ndogo ya taifa ambayo baadae inaunda jamii na taifa.
Hisia hii ya utaifa ni sawa na ile ambayo mtu anatakiwa ahisi kama ni mtu wa familia fulani. Hali hii huweza kuharibika na hisia hizi zote za utaifa, ufamilia na hisia za ujamii huondoka. Na mfumo wote wa kijamii kuanguka. Kuanguka kwa hivi vyote hutokana na uongozi mbovu wa kila sehemu husika na upungufu wa nidhamu na maadili katika jamii.
Na taifa kama taifa haliwezi kulindwa pasipo vitu hivyo. Ili kulinda vitu vyote hivyo na jamii iwe na mpangilio mzuri, nidhamu inahitajika. Ni vigumu kwa serikali kutawala pasipo kila kiongozi husika katika ngazi ya jamii, familia na taifa kutimiza wajibu wake. Lakini mzigo mkubwa lazima atwishe viongozi kwasababu wana wajibu wa kuunda na kulinda kile walichounda.
Hii inahitaji kiongozi makini anayejua anachokifanya. Vijana wanazaliwa na wanakua, wanakuta wazee wakiishi, wanategemea uongozi kutoka kwao. Uongozi unaotokana na fikra sahihi. Jinsi gani waishi katika taifa. Lakini hawakuti hilo. walitegemea kupewa muongozo kuhusu utaifa na uzalendo, kutoka kwa watu waliotangulia kabla yao.
walitegemea watakuta dira ya jinsi gani kijana aishi katika taifa lake. Tabia za wazee kwa taifa lao walitegemea ziwe za unyoofu, wawe rula ya kuwajenga vijana katika utaifa. Ni muhimu kufahamu kama wazee waki kengeuka juu ya utaifa na uzalendo na juu ya maadili na nidhamu ya taifa, taifa na jamii itakosa mwelekeo.
Kama wazee wetu wangekuwa na fikra chanya juu ya taifa hili, vijana wangefuata nyuma kama maji yanavyofuata mkondo wake. Vijana wanaokua wanahitaji mfano, na wanapozaliwa na kukua wanategemea kuupata mfano huu kutoka kwa wazee wetu hasa kuhusu suala la kujitegemea kama taifa na juhudu zetu kulifanya taifa hili kusimama, kwani ni juhudi pekee itakayo tusimamisha na kutufanya tusonge mbele kama taifa. Ingekuwa rahisi sana kwetu kama tungekuta msingi mzuri umejengwa ili safari yetu isiwe ngumu sana bali tuwe na majukumu mengine ya kufanya sisemi kama misingi iliyowekwa ni mibaya sana bali sio imara kulifanya taifa hili kusimama kujitegemea kisha kusonga mbele, bado tuko kama mtoto mdogo anayetambaa hatujaweza kunyanyuka na kutembea bado ni tegemezi kwa mambo mengi ni wakati wetu sasa kusimama.
Ni dhahiri kabisa tunapokea taifa lisilo na umoja na uzalendo na ni jukumu letu kuileta nchi pamoja upya.
Ni lazima sasa tujenge uzalendo na uwajibikaji katika taifa ili tuwe na fikra chanya. Katika mtazamo huu, tunaweza kulijenga taifa hili na kurithisha kizazi hata kizazi katika jitihada ile ile na uzalendo ule ule wa kulijenga.
Bila hisia hii ya uzalendo na uwajibikaji kwa taifa hatutaweza kulijenga taifa hili. Hatutaweza kulijenga taifa hili katika ubinafsi.Roho hii ya jitihada za pamoja katika kujenga nchi ni lazima ijengwe. Jitihada za mtu binafsi kujiendeleza lazima ziende sambamba na jitihada za taifa kujiendeleza.
Hili taifa ni lazima liwe na sehemu katika kila moyo wa mwananchi.Wajibu wa mtu wa kujiendeleza mwenyewe na familia yake bila kuingiliwa, wajibu huu usiingiliane na wajibu wa mtu kwa taifa lake. Maslahi ya binafsi na yale ya Taifa ni lazima kuwe na mipaka. Hivi vitu viwili ni lazima viunganishwe. Familia lazima ijue ni sehemu ndogo ya taifa na haki zao zote wanapata kutoka katika taifa kama walivyokuwa na wajibu kwa taifa.
Muunganiko huu ni muhimu sana kati ya familia na taifa. Hisia ya familia kwa taifa lake ni muhimu sana. Kwahiyo tunahitaji kutoa elimu hii ya umma ili tupate kujitambua kama taifa.
Hili tunaweza kufanikisha kama tukiwekeza katika elimu, na kuelimisha watu wetu kuhusu wajibu na haki zao na kama tukitekeleza ipasavyo sheria zilizopo ili kulinda maslahi ya umma. Ni muhimu kujenga roho hii ya watu wetu kuelekea katika taifa.
Bila kujenga roho hii hatutaweza kunyanyua chochote juu ya msingi wa taifa hili.Msingi huu wa wajibu na haki ni muhimu sana. Tusipojenga misingi hii ya wajibu na haki hatutaweza kufika popote kama taifa. Hatutaweza kujenga taifa hili katika misingi ya ubinafsi.
Tutaweza kulijenga taifa hili ikiwa tu tutakuwa na mahusiano mazuri miongoni mwetu. Na kama tukiwa na malengo ya kujenga jamii zetu na taifa letu kwa pamoja na katika mwelekeo sahihi unaotokana na fikra sahihi na kuongozwa na uzalendo kwa taifa letu.
Ni kujitolea huku tu ndio kutakako lipeleka taifa hili mbele. Kujitolea pasipo kuweka ubinafsi mbele.Wengi wetu tunashangaa bunge lilipofikia. Hadhi na nidhamu yake, lakini tunashindwa kuangalia chimbuko lake kwa undani zaidi kwa kuangalia jamii yetu na mfumo wake, ambako wabunge wametokea huko.
Pasipo kuangalia familia zetu na uhusiano wetu miongoni mwa jamii jinsi ulivyo, Upendo wetu kwa majirani na kwa jamii, na mashirikiano yetu. Nidhamu katika familia zetu na katika jamii. Kuwajibika kwetu miongoni mwetu katika ngazi ya chini ya familia, na katika jamii. Heshima yetu na nidhamu yetu kwa jamii ikoje na vitu kama hivyo. Kama tukitafakari kwa makini sana tutaona matatizo haya yameanzia chini kabisa. Kwenye uwajibikaji katika familia na katika jamii na imefikia katika ngazi ya taifa.
Jamii inayowajibika itachagua mtu anayewajibika kwenda kuwa kiongozi wao. Ni vigumu kwa jamii iliyojipanga na inayowajibika kuchagua kiongozi asiyewajibika kuwa kiongozi wao. Kwahiyo matatizo yetu mengi yanatokana na uwajibikaji wa pamoja katika ngazi ya jamii na ya familia.
Uwajibikaji huu wa pamoja kwa faida ya umma ndio hujenga jamii iliyostaarabika na yenye dira. Ni muhimu kujenga jamii ambazo zina mwelekeo mmoja. Jambo hili linahitaji nidhamu. Ni dhahiri watu wenye nidhamu wakimtuma mtu kwenda kuwawakilisha bungeni ni lazima mtu huyo atawaheshimu. Kwasababu ametoka kwenye jamii yenye nidhamu. Jamii isiyochekelea rushwa na ufisadi kwa matendo. Jamii iliyoratibiwa na kupangiliwa, jamii inayojiheshimu, yenye nidhamu na utaratibu na inayoishi kwa ushirikiano ili kuleta maendeleo ya jamii nzima.
Kama nilivyosema awali serikali kazi yake ni kukusanya, kupanga na kulinda kile inachokijenga ili kiwe endelevu. Jambo la kujiuliza je hii nidhamu ilikuwepo kwenye jamii yetu na katika serikali yetu? Kama ilikuwepo na sasa inabomoka ni nini chanzo chake? Na kama pia ilikuwepo ilikuwepo kwa kiwango gani? Ukweli ni kwamba nidhamu hii haikuwepo. Inahitajika kujengwa kwakuwa bila nidhamu hii taifa letu kamwe halitoweza kupiga hatua. Bila nidhamu hii hatutaweza kuweka utaratibu wala kujipanga kama jamii.
Kitu ninachoona tuna mahitaji makubwa ya kutengeneza nidhamu katika taifa letu. Nidhamu hii ni lazima ijengwe kwa jicho la lenzi ili kuleta taifa letu katika mpangilio na uwajibikaji. Kuna mahitaji makubwa ya kuwajenga watoto wetu katika nidhamu na katika wajibu. Ni lazima watambue wanawajibu kwa taifa.
Wazazi wawafundishe watoto wao wajibu huu muhimu. Ili taifa hili liendelee kuwepo ni lazima nidhamu ijengwe. Ni lazima tuwajenge watoto wetu kujitambua wao ni kina nani na wanawajibu gani kwa taifa.Kama wazazi wakishindwa kuwatawala watoto wao itakuwa vigumu sana kwa serikali kutawala nchi. Ni lazima wazazi wawalee watoto wao katika nidhamu ni lazima wawatiishe. Nchi haiwezi kuzalisha chochote bila nidhamu na uwajibikaji. Ni lazima tufanye kazi kama kitu kimoja ili taifa hili liendelee.
Matatizo tunayoyaona sasa hivi yanatokana na uzembe unaofanyika katika ngazi za chini wa kutokutimiza wajibu katika malezi.Baadae yeyote ile ya taifa lolote lile itategemea sana nidhamu , uwajibikaji na elimu ya vijana wake. Na kazi hii ni ya kizazi baada ya kizazi, ni kazi ya kila siku ya ujenzi wa taifa. Huu muunganiko wa sehemu hizi ndogo unaounda taifa utakapo fanya kazi vizuri katika utengamano ndio utakaopelekea taifa hili kuendelea.
Familia ndizo zinazounda jamii na nchi, uhusiano huu kati ya familia na jamii, pamoja na taifa kwa ujumla kama ukiwa wenye dhamira na malengo mamoja utafanya taifa hili kuendelea. Kila kimoja wapo kikitambua uwepo wa mwenzake na umuhimu wake katika kujenga taifa imara. Na serikali ikiwa kama nyenzo ya kuleta maendeleo ya pamoja. Ikiwa sehemu hata moja ya uhusiano wa sehemu hizi ukibomoka ni vigumu kwa taifa kuendelea.
Huu ni mtandao ambao ni lazima ufanye kazi kwa pamoja. Ni lazima kuwe na mipaka kati ya maslahi binafsi na yale ya taifa yanayo tuunganisha kwa pamoja kama taifa.Bila nidhamu hatutaweza kujenga taasisi yeyote ikaimarika na ikaleta tija. Ni lazima tujiangalie upya na hili linahitaji nguvu kwasababu sio jambo la mchezo.
Bila hilo taifa hili halitoweza kuendelea. Na hiki ni chanzo kikubwa cha kutokuendelea kwetu kama taifa.Serikali yeyote duniani hutengeneza nchi na raia wanaofanana na asili ya serikali yenyewe. Serikali isiyo na nidhamu itatengeneza raia wasio na nidhamu. Na kinyume chake ni sahihi.
Kwahiyo tabia ya nchi inategemea sana tabia za viongozi wake. Kwasababu raia wanaangalia viongozi kama mfano. Mzabibu utazaa zabibu kamwe hauwezi kuzaa mapera. Kiongozi mwovu hawezi kuzaa raia wema. Nchi bora hujengwa na viongozi bora. Ni lazima tujenge tabia ya nchi.
Hatuwezi kujenga taasisi yeyote ikaendelea bila kuwa na nidhamu. Tusijidanganye. Wito wangu mimi ni kutaka mabadiliko katika taifa hili. Mabadiliko ya jinsi tunavyofikiri. Ni kutaka kuleta mwamko juu ya masuala ya kimsingi yanayohusu taifa hili. Kwasababu bila uelewa huu hatutaweza kulijenga taifa hili.
Uhusiano wa serikali na raia au wananchi ni lazima uwepo katika wajibu. Raia lazima waione serikali kama mtetezi wao na kama baba yao. Na si kama adui. Hapo ndipo upendo wa wananchi kwa serikali utakapo kuwepo. Ikiwa watu wa serikalini wataona kuwepo serikalini ni njia ya kujitajirisha badala ya kutumikia wananchi ni lazima chuki itakuwepo itakayotokana na hali ya wananchi kuwa duni na ile ya viongozi wao kuwa yenye utajiri na hii italeta matabaka. Kwa serikali kubadilisha mwelekeo wake wa asilia wa kusimamia haki na kuleta maendeleo na kwenda kwenye kujilimbikizia mali kwa viongozi, mali inayotokana na ufisadi, ni hatua ya kwanza ya serikali hiyo kuwa ya kibwanyenye na ya kigandamizaji.
Wataendelea kuridhisha tamaa zao na kukandamiza haki za raia na katika mazingira hayo ni lazima chuki itajengeka kati ya wanaotawala na wanaotawaliwa. Na jamii itavurugika na kuwa ya waovu na watu wabinafsi. Kutokana na serikali kutokujali raia. Serikali inaposahau majukumu yake na kuendeleza anasa ni hatari kwa nchi. Haki haitetendeka. Wakati watu wakifa njaa na wengine kukosa madawa katika hospitali serikali za namna hii hutumia pesa ovyo katika mambo yasiyo na msingi, mambo ya kustarehesha nafsi. Serikali ya namna hii haiwezi kujali raia hata kidogo ni lazima kwanza ijiangalie yenyewe kabla ya raia.
Ni lazima tubadili mwelekeo huu wa fikra kwasababu sio fikra sahihi na zenye tija kwa taifa. Ni lazima tujenge taifa lenye upendo na matumaini kwa wote.Kwahiyo nidhamu ni muhimu sana katika ujenzi wa taifa lolote lile, mahusiano yetu kama jamii yatategemea sana nidhamu hii.
Tukijenga familia zenye nidhamu ni dhahiri tutapata jamii zenye nidhamu na zenye uwezo wa kujiongoza zenyewe. Nidhamu hii ndio kiini cha mashirikiano katika jamii yeyote. Bila mashirikiano yetu hatuwezi kuwa na dira kama taifa. Bila nidhamu hii hatutaweza kuwalea watoto wetu pamoja wala kuwa na malengo ya pamoja kama jamii na kama taifa. Bila nidhamu hii hatutaweza kuzalisha viongozi bora wa kesho.
Nidhamu hii hufanya uongozi kuwa rahisi na kuwa kitu chenye mwelekeo.Nidhamu ni nguvu elekezi ya kiakili, inayomsaidia binadamu kuacha mambo yasiyo na faida na kufuata yenye faida kwa kujizuia ili kupata dira.
Nidhamu ni kujitawala.Nidhamu huleta mwelekeo iwe kwa mtu binafsi au kwa taifa. Kwahiyo ili tupate mwelekeo kama taifa na ili taifa letu liweze kuzalisha na kuwa endelevu, nidhamu hii ni muhimu sana.Tutawezaje kujenga taifa hili pasipo nidhamu? Pasipo watu wetu kuwa na mwelekeo mmoja kama taifa? Tutawezaje kufanikiwa kama taifa katika malengo yetu bila nidhamu hii?. Kama nilivyosema nidhamu huleta dira, bila nidhamu hatutafanikiwa kama taifa. Ni muhimu kuijenga sasa katika kila Nyanja ya maisha yetu kuanzia katika familia, jamii , shuleni na katika serikali yetu. Bila nidhamu hii hatutaweza kujitawala kama taifa.Huu ni ukweli ambao ni lazima tuuzingatie na tufanye juhudi kujenga nidhamu hii muhimu kwa maendeleo ya taifa letu.
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 Comments