Katika siku za karibuni mvua kubwa zimenyesha katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati na kusababisha vifo, upotevu na uharibifu wa mali za wananchi, uharibifu wa miundombinu ya umma na kuvuruga utaratibu wa kawaida wa maisha. Wananchi walioathirika zaidi ni wale wanaokaa mabondeni na waliojenga karibu na mikondo ya maji. Kabla sijaenda mbali zaidi napenda niweke wazi kwamba serikali inahusika kwa kiasi kikubwa katika mafuriko haya pamoja na uharibifu uliosababishwa na mafuriko, hasa kwa miundombinu ya barabara, majengo na madaraja. Kwa sababu gani nasema hivyo? Ninazo sababu nyingi zinazonipelekea niitundike serikali msalabani kwa uzembe, usimamizi duni na utoaji taarifa usio sahihi:
- Kama nilivyotangulia kusema, mvua hizi zimenyesha katika ukanda mzima wa Afrika Mashariki na Kati. Lakini kwanini adhari zake zimeonekana Tanzania tu? Mbona hatujasikia madaraja yakikatika wala mafuriko kutokea huko Kenya, Uganda, Kongo, Rwanda na Burundi? Hii ni kwa sababu ya ujenzi wa miundombinu duni na isiyozingatia ubora unaofanywa na serikali ya Tanzania. Miundombinu yetu imejengwa kiholela na kifisadi bila kuzingatia viwango vya ubora. Hili hasa husababishwa na ufisadi, 10%, usimamizi duni na kutowajibika kwa serikali. Tenda nyingi za ujenzi hutolewa kwa makampuni yasiyokuwa na uwezo wa kujenga miundombinu bora kwa sababu za kifisadi.
Lakini pia usimamizi wa miundombinu haufanyiki inavyopaswa. Mfano mzuri ni ile barabara ya Kilwa iliyojengwa na wachina kutoka Bandarini hadi Mbagala. Barabara ile ilijengwa kwa viwango duni, ambapo kipande kati ya Bandarini na Mtongeni kilipokewa na waziri Kawambwa (wakati huo akiwa Waziri wa Miundombinu), pamoja na kwamba barabara ilikuwa imejengwa chini ya kiwango. Na kipande kati ya Mtongani na Mbagala kilikataliwa na Magufuli kwa sababu alijiridhisha kwamba hakikuwa kimejengwa kwa ubora ubnaotakiwa. Kile kipande kingine kilichopekelewa kifisadi na Kawambwa, pamoja na kwamba hakikujengwa kwa ubora, tayari kimeishaanza kuharibika hata kabla ya kutimiza miaka 3 baada ya kukabidhiwa. Hii inaonyesha kwamba barabara nyingi zilizojengwa, hasa kipindi cha Kawambwa, hazina ubora wowote. Ndio hizi unazoziona zikikatika hovyo na madaraja yake kuzolewa na maji.
- Makaravati yanayopokea maji ya mvua ni membamba sana na yameziba kwa uchafu jambo ambao hupelekea maji kupita juu ya barabara na kusababisha uharibifu na mafuriko pamoja na kubomoa nyumba za wakazi wanaoishi jirani na barabara. Hapa tena suala lile lile la ufisadi linarejea. Wakandarasi hupewa fedha za kujenga makaravati makubwa lakini matokeo yake, wasimamizi (wakimwemo Mawaziri) hula njama za kupokea rushwa kutoka kwa wakanadarasi na kupelekea fedha kupungua. Kwa sababu hiyo pesa ambazo zingetumika kujenga miundombinu sahihi huishia matumboni mwa wajanja na mafisadi wachache. Hatimaye wakanadarasi huishia kujenga makaravati madogo ambayo hayatoshi kupokea maji pindi itokeapo njia kubwa.
- Kuna wananchi ambao kisheria hujenga maeneo ya mabondeni au kwenye mikondo ya maji lakini badala ya kuwazuia serikali huwaacha wajenge na kuendelea kufanya makazi maeneo hayo. Ukitembelea maeneo hayo utakuta ofisi za CCM, mashina na matawi ya chama na utakuta bendera za chama zikipepea. Lakini pia utakuta ofisi za umma na uongozi (kama vile ofisi za Katibu Kata, wenyeviti wa mitaa/vitongoji, madiwani, nk) waliochaguliwa katika chaguzi halali za serikali. Wakati wa kupiga kura, chama na serikali huwatumia sana wakazi hawa na kuona kwamba makazi yao ni halali. Baada ya kuisha kwa uchaguzi na yakishatokea mafuriko ndipo makazi yao hugeuka kuwa haramu. Acheni hizo nyie serikali.
Na jambo la kushangaza zaidi serikali huwasambazia wakazi hawa huduma za kijamii kama vile umeme, maji, barabara, nk. Serikali hukusanya kodi za majengo na biashara katika meneo haya. Pia huwagawia viwanja wakazi hawa kabla ya kujenga. Lakini hata katika yale maeneo ambayo viwanja havijatolewa kwa wakazi, je,serikali inakuwa wapi wakati watu wanajenga na kuanza kuishi katika maeneo hayo haramu? Mimi nilidhani kwamba watu wakijenga maeneo yasiyotakiwa makazi yao huwa haramu na wao pia huwa haramu. Inakuwaje sasa serikali iwapelekee miundombinu na huduma za kijamii na iwatumie watu hao katika siasa?
- Kitengo cha utabiri wa hali ya hewa (TMA) kinafanya kazi sawasawa na waganga wa kienyeji. Ni afadhali hata tungewaajiri waganga wa kienyeji wawe wanatutabiria mvua badala ya kupoteza pesa nyingi za umma kwa kuwalipa watu wasiofanya kazi ipasavyo. Utabiri wa hali ya hewa ni wa ovyo na wa kibabaishaji kabisa. Na udhaifu huu umekuwa ukijirudia kila mwaka. Mpaka mvua hizi zinanyesha na kusababisha uharibifu, idara ya hali ya hewa haijatoa tahadhari yoyote wala kuwaonya raia wanaokaa mabondeni kuchukua tahadhari zinazofaa. Baada ya maafa kutokea ndipo utawaona wakiuza sura kwenye media wakiwataka watu wahame na kulinda mali zao. Wahameje wakati maafa yameishatokea na baadhi yao wamepoteza maisha? Ujinga huu unaofanywa na idara ya hali ya hewa hauvumiliki hata kidogo.
- Usimamizi wa usafi wa mazingira hauzingatiwi. Mifeji hushuindwa kutiririsha maji kwa sababu imejaa uchafu wa kila namna unaotupwa na wananchi huku serikali ikiwa imewafumbia macho. Lakini hasa, uchafu unaoziba mitaro na mifereji ya maji ni ule unaotokana na uzembe wa serikali kutozoa taka kwa kasi inayotakiwa na badala yake uchafu huu huzolewa na maji ya mvua. Madhara yake ni kwamba uchafu huziba mitaro na kusababisha maji kufurika na kuingia kwenye makazi ya watu.
Kwa sababu hizi, na nyingine nyingi ambazo zijazitaja hapa, serikali inahusika moja kwa moja ktk mafuriko haya na madhara yake kwa wananchi. Haiwezekani nchi iendeshwe ovyo namna hii wakti wananchi wakiteseka kila mwaka. Matokeo ya ufisadi, ubinafsi, ugoigoi, ukiukwaji wa sheria na utawala wa ovyo unaofanywa na serikali ndio huletelezea maafa makubwa kama haya ambayo hugharimu roho za raia, upotevu na uharibifu wa mali na kumasikinisha raia. Na tusitarajie kwamba kutakuwa na mabadiliko yoyote ikiwa serikali hii hii iliyofeli itaendelea kuongoza katika nchi hii. Badala ya kukazana kuboresha miundombinu na kuimarisha utawala bora, wanakaa kututisha kwamba jeshi litachukua nchi. Ni afadhali jeshi litawale kuliko hivi wananchi wanavyoishi kama watumwa katika nchi hii ya kifisadi.
0 Comments