[wanabidii] NANI ANADANGANYA WATU ATI TANGANYIKA NI HARAMU NA HAIPO NA HAITAKIWI?

Sunday, April 20, 2014

"NANI ANADANGANYA WATU ATI TANGANYIKA NI HARAMU NA HAIPO NA HAITAKIWI??"

Aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi amejibu baadhi ya hoja za watu wanaopendekeza muundo wa serikali mbili na kusema Serikali ya Zanzibar ndiyo iliyoanza kutaka serikali tatu mwaka 1984."

Aidha, amewashangaa wanaolibeza jina la Tanganyika kutumika serikalini kwa madai kuwa jina hilo siyo haramu kwa kuwa limo ndani ya Katiba ya sasa.

Alisema kuwa wakati huo madai ya serikali tatu yalitolewa na Zanzibar na kusimamiwa na Rais aliyekuwa pia Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaji Aboud Jumbe.

"Hoja ilipelekwa pia kwenye Baraza la Wawakilishi, Brigedia Mstaafu Ramadhan Haji Fakhi (aliyekuwa Waziri Kiongozi), alikuwa akiongea kwa sauti nzito, kama ulikuwa ukimsikiliza, unasema muungano haupo," alisema Profesa Kabudi na kueleza kuwa Fakhi alisema: "Zanzibar siyo koloni la Tanganyika."

Alikuwa akichangia hotuba katika Kongamano la Kujadili Miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, lililofanyika mjini Zanzibar jana. Alieleza kwamba mjadala wa sasa wa muungano siyo mkali kama uliokuwepo mwaka 1983 na 1984.

Hata hivyo, hotuba hiyo ya Profesa Kabudi iliyokuwa ikirushwa moja kwa moja na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1) ilikatishwa kabla mzungumzaji kumaliza hotuba yake.

Akifafanua matumizi ya jina la Tanganyika kwenye Katiba ya sasa, Profesa Kabudi alisema: "Katiba ya Jamhuri ya Muungano ibara ya nne, 34, 64, 102 na 151, inaonyesha kuwa zipo mamlaka tatu. Mamlaka ya masuala ya muungano na mamlaka ya masuala yasiyo ya muungano katika upande wa Tanzania Bara (Tanganyika)."

Alibainisha: "Nataka niwaambie, leo ukienda kwenye Ibara ya 151 ya Katiba, Tanzania Bara imetajwa kuwa iliyokuwa Jamhuri ya Tanganyika, kwa hiyo hata Katiba ya sasa Tanganyika ipo, kwa hiyo Tanganyika siyo jina haramu."

Alisema anaamini kila taifa lina ujinga wake katika kutunga Katiba, lakini ujinga wa kizazi kimoja hauwezi kuwa wa kizazi kingine.

"Ujinga wa kizazi hiki, tusidhani utakuwa ujinga wa kizazi cha kesho, vizazi vijavyo vya Tanzania vitakuwa na ujinga wake."

Alifafanua: "Ni vyema kuwawekea misingi lakini waje kuishi na ujinga wao, kuliko kulazimisha ujinga wako, kwa sababu wewe ujinga wako ndiyo amali yako lakini kwa wengine siyo amali. Ulitegemea Waingereza wangekapigia mizinga kachanga ka siku moja?"

HATI YA MUUNGANO;

Akizungumzia hati ya muungano iliyozua sintofahamu hivi karibuni kwa madai kwamba haikuwepo, alisema msingi wa kikatiba na kisheria wa muungano wowote ni hati za muungano.

Alisema miaka ya 1980, suala lililokuwa linajadiliwa ni iwapo hati za muungano ni sehemu ya sheria za kimataifa au la. Baadaye ilibainika kuwa hati hizo ni mkataba wa kimataifa na kwamba unatawaliwa na sheria za kimataifa.

"Hili suala la kwamba hati zipo au hazipo siyo suala kubwa, suala ziliridhiwa? Ushahidi upo upande wa Tanganyika ziliridhiwa. Kwa upande wa Zanzibar kuna utata na hiyo kesi ipo mahakamani," alisema.

Alisema kutokana na utata huo katika Rasimu, wakapendekeza namna ya kutatua tatizo lililodumu kwa miaka 50 kwa kuandika kuwa hati ya maridhiano ya Tanganyika na Zanzibar kuwa msingi mkuu wa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

"Aya hizi isipokuwa kichwa cha habari nimezinukuu kwenye tovuti ya gazeti la Mwananchi la leo Jumapili 20/04/2014".


--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Related Posts

0 Comments